Miaka 20 ya Kagera Ligi Kuu Bara, yashuka daraja ikiwa sebuleni

Muktasari:
- Ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Pamba iliyorejea katika Ligi Kuu baada ya miaka 23 tangu iliposhuka mwaka 2001 ulihitimisha maisha ya Wana Nkurukumbi, ambao walijiweka pabaya Jumatatu usiku walipokubali kichapo cha bao 1-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Mashujaa.
MWENDO imeumaliza. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu Kagera Sugar, baada ya kuhitimisha miaka 20 ya kuichezea Ligi Kuu Bara kwa kushuka daraja ikiwa sebuleni ikilifuatilia pambano la KenGold na Pamba Jiji zilizokuwa zikiumana juzi kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Pamba iliyorejea katika Ligi Kuu baada ya miaka 23 tangu iliposhuka mwaka 2001 ulihitimisha maisha ya Wana Nkurukumbi, ambao walijiweka pabaya Jumatatu usiku walipokubali kichapo cha bao 1-0 wakiwa nyumbani dhidi ya Mashujaa.
Kagera imeungana na KenGold, iliyopanda msimu huu kutoka Ligi ya Championship sambamba na Pamba na kutangulia mapema na kumuandikia rekodi ya kipekee kipa wa zamani wa kimataifa wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Juma Kaseja kushuka daraja na timu hiyo akiwa kama kocha mkuu.
Ushindi wa Pamba, uliishusha daraja Kagera ikiungana na KenGold, licha ya kuwa na mechi mbili mkononi, baada ya kucheza mechi 28, ikishinda tano, sare saba na kupoteza 16, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 40, ikishika nafasi ya 15 kwa pointi 22.

Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki 2005, imeondoka katika ligi hiyo bila kuwahi kutwaa ubingwa, lakini ikiweka rekodi kadhaa zilizoifanya iwe moja ya timu ngumu na zilizokuwa zikiongozwa na vigogo, Simba na Yanga.
Klabu hizo kongwe zilikuwa hazina uhakika wa kuifunga Kagera, iwe nyumbani kwao Kaitaba au kokote ikizifuta ugenini kutokana na kuwa na wachezaji wapambanaji, waliotetemesha mabeki na makipa wa Simba na Yanga, rekodi zikionyesha hivyo kabla ya msimu huu kuwa wepesi mno.
MOTO ULIANZIA HAPA
Kagera Sugar ilianza kushiriki Ligi Kuu Bara mwaka 2005 baada ya kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Kwanza 2004 ambako ilipanda sambamba na Ashanti United ya Ilala ambayo ilishuka daraja baada ya kucheza kwa msimu mmoja tu.
Kagera iliingia na mguu mzuri kucheza msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu 2005 kwa kumaliza katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 46, baada ya kushinda mechi 13, sare saba na kupoteza nane tu kati ya 28 iliyocheza.
Mwaka huo, Yanga ndio ilikuwa bingwa ikiwa na pointi 61, juu ya Moro United ya Morogoro iliyomaliza ya pili kwa pointi 58, ikiziwa tatu tu na kikosi hicho cha Jangwani, huku nafasi ya tatu ikitwaliwa na Simba iliyomaliza na pointi 56.
Safari ya matumaini kwa Kagera Sugar ikaendelea 2006, ilipomaliza katika nafasi ya nne tena ikivuna pointi 50, nyuma ya Yanga tena iliyomaliza kinara kwa pointi 70, ikifuatiwa na Simba (ya pili kwa pointi 62), huku Mtibwa Sugar ikiwa ya tatu kwa pointi 58.
Mwaka 2007, ambapo ilikuwa ikichezwa Ligi ndogo, Kagera Sugar ilikuwa Kundi C, ambapo ilimaliza nafasi ya tatu kwa pointi 10, ikishinda mechi mbili, sare nne na kupoteza mbili, nyuma ya vinara, Mtibwa Sugar iliyoongoza kwa pointi 15.
HOMA YA VIPINDI
Kwa msimu wa 2007-2008, Kagera Sugar ilimaliza Ligi Kuu Bara kwa kushuka kutoka ndani ya Top 4 ilipoanza kupazoea na kumaliza ya tano ikiwa na pointi 38, ikishinda mechi 10, sare nane na kupoteza pia nane kati ya 26 iliyocheza, huku mabingwa wakiwa ni Yanga waliomaliza na pointi 49.
Msimu wa 2008-2009, Kagera ilimaliza Ligi Kuu ikiwa nafasi ya sita na pointi 29, baada ya kucheza mechi 22, ikishinda nane, sare tano na kupoteza tisa, ikifunga mabao 18 na kuruhusu 21, huku Yanga ikiibuka bingwa tena kwa msimu huo.

Msimu wa 2009-2010, Kagera ilimaliza Ligi Kuu ikiwa nafasi ya saba kwa pointi 24, ikishinda mechi tano tu, sare tisa na kupoteza nane, ikifunga mabao 13 na kuruhusu 20, ambapo Simba iliibuka bingwa baada ya kukusanya pointi 62.
Msimu wa 2010-2011, timu hiyo ilirudi kivingine na kumaliza katika nafasi ya tano kwa pointi 35, ikishinda mechi tisa tu, sare nane na kupoteza tano kati ya 22 ilizocheza, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 18, huku mabingwa wakiwa ni Yanga waliomaliza na pointi 49.
Baada ya hapo, ikamaliza nafasi ya saba kwa pointi zake 32 msimu wa 2011-2012, ikishinda mechi saba, sare 11 na kupoteza nane, ikifunga mabao 27 na kuruhusu 28, ambapo ubingwa wa taji hilo ulienda kwa Simba iliyomaliza kinara kwa pointi 62.
Msimu wa 2012-2013, ikamaliza nafasi ya nne kwa pointi 44, ikishinda mechi 12 tu, sare nane na kupoteza sita, ikifunga mabao 28 na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara 20, ambapo ubingwa msimu huo ulienda kwa Yanga iliyomaliza na pointi 60.
Msimu wa 2013-14, ilimaliza katika nafasi ya tano kwa pointi 38, sawa na Simba iliyokuwa ya nne ila zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, ambapo Kagera ilishinda mechi tisa, sare 11 na kupoteza sita, nyuma ya mabingwa wapya, Azam FC.
Baada ya hapo, msimu wa 2014-2015, ilimaliza ya sita na pointi 32, ikishinda mechi nane, sare nane na kupoteza 10 kati ya 26 ilizocheza, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 26, huku mabingwa wa Ligi Kuu wakiwa ni Yanga waliomaliza na pointi 55.
Msimu wa 2015-2016, ikaepuka na janga la kushuka daraja baada ya kuponea katika ‘play-offs’, kufuatia kumaliza katika nafasi ya 12 kwa pointi 31, ikishinda mechi nane, sare saba na kupoteza 15, ikifunga mabao 23 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 34.
MSIMU BOMBA
Baada ya hapo, msimu wa 2016-2017, ikajipanga vizuri na kumaliza ya tatu kwa pointi 53, ikishinda mechi 15, sare nane na kupoteza saba, nyuma ya Simba iliyomaliza ya pili kwa pointi 68 sawa na Yanga iliyochukua taji kwa tofauti ya mabao. Huu ndio uliokuwa msimu bora zaidi kwa Kagera katika Ligi Kuu Bara, kwani haikuwahi kumaliza tena katika nafasi hiyo hadi inapojiandaa kuiaga rasmi.
Msimu wa 2017-2018, ilimaliza ya tisa kwa pointi 37, ikishinda mechi nane, sare 13 na kupoteza tisa, ikifunga mabao 23 na kuruhusu 27, nyuma ya mabingwa Simba iliyomaliza kinara na pointi 69, ikifuatiwa na Azam ya pili kwa pointi 58.
Msimu wa 2018-2019, ikadondokea tena ‘play-offs’, na kuepuka kushuka daraja baada ya kumaliza katika nafasi ya 18 kwa pointi 44, sawa na Mwadui FC iliyokuwa ya 17, ikishinda mechi 10, sare 14 na kupoteza pia 14, ikifunga mabao 33 na kuruhusu 43.

Msimu wa 2019-2020, ikamaliza katika nafasi ya nane kwa pointi 52, ikishinda mechi 15, sare saba na kupoteza 16, ikifunga mabao 44 na kuruhusu 41, ambapo mabingwa wa Ligi Kuu Bara walikuwa ni Simba waliomaliza na pointi 88.
Baada ya hapo, msimu wa 2020-2021, ilimaliza katika nafasi ya 12 kwa pointi 40, ikishinda mechi 10, sare pia 10 na kupoteza 14, ikifunga mabao 34 na kuruhusu 38, ambapo ubingwa wa Ligi Kuu Bara ulienda kwa Simba tena iliyomaliza na pointi 83.
Msimu wa 2021-2022, Kagera ilimaliza katika nafasi ya sita kwa pointi 39, ikishinda mechi tisa tu, sare 12 na kupoteza pia tisa, ikifunga mabao 20 na kuruhusu 25, ambapo msimu huo ubingwa wa Ligi Kuu ulienda kwa Yanga iliyomaliza na pointi zake 74.
Msimu wa 2022-2023, ilimaliza katika nafasi ya 11 kwa pointi 35, ikishinda mechi tisa, sare nane na kupoteza 13 kati ya 30, ilizocheza, ikifunga mabao 23 na kuruhusu 36, huku ubingwa wa Ligi Kuu Bara ukienda kwa Yanga iliyomaliza na pointi 78.
Msimu uliopita 2023-2024, Mtibwa ilimaliza ya 10 ikiwa na pointi 34 sawa na Tanzania Prisons iliyomaliza ya tisa ila zikitofautiana kwa mabao tu ya kufunga na kufungwa, ambapo Kagera ilishinda mechi saba, sare 13 na kupoteza 10 kati ya 30 ilizocheza.
Msimu huo, Kagera ilifunga mabao 23 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 32, ambapo Yanga ilichukua ubingwa kwa pointi 80, ikifuatiwa na Azam FC na Simba zilizomaliza katika nafasi ya pili na tatu zikilingana pointi 69, ila zikitofautiana kwa mabao tu.
Msimu huu wa 2024-2025, ndio umehitimisha rasmi safari ya Kagera Sugar ya miaka 20 katika Ligi Kuu, baada ya kutokuwa na mwenendo mzuri tangu mwanzoni, huku ikisaliwa na mechi mbili mkononi ikiungana na KenGold iliyokata tiketi hiyo mapema.
UGENINI AIBU
Kwa msimu huu Kagera imekuwa moja ya timu zilizochemsha katika mechi za ugenini, kwani imecheza 13 na haikuonja ushindi hata moja, ikitoka sare tatu tu na kupoteza 10 ikiwa nafasi ya pili baada ya KenGold iliyocheza mechi 14 ikipoteza 12 na kuambulia sare mbili tu. Kagera ugenini imefunga mabao matano na kufungwa 21, ikiwa ndio timu dhaifu kabisa kufumania nyavu kwenye viwanja vya ugenini.
Kwa nyumbani ilicheza mechi 15 na kushinda tano, nne ikitoka sare na kupoteza sita ikifunga mabao 17 na kufungwa 19, ikiwa ni klabu ya 12 kati ya 16 zilizofanya vizuri nyumbani, lakini matokeo ya ugenini yamewaangusha na kuwa shimo la kuwashusha daraja wakipishana mlangoni na ‘ndugu’ zao wa Mtibwa Sugar waliorejea katika Ligi Kuu sambamba na Mbeya City. Mtibwa ilishuka msimu uliopita.
TAJI MOJA TU
Tangu mwaka 2005, moja ya mafanikio makubwa ya Kagera Sugar ni kuchukua ubingwa wa Tusker mwaka 2006, ilipoichapa Simba mabao 2-1, kwenye muda wa nyongeza katika fainali ya michuano hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Agosti 20, 2006.
Hilo ndilo taji pekee la maana kwa Kagera katika umri wa miaka 20 ya kucheza Ligi Kuu Bara, kwani kwa upande wa ligi hiyo yenyewe haijawahi kutwaa taji wala kupata uwakilishi wa nchi kwenye michuno ya kimataifa.
Katika mechi hiyo ya fainali, Omar Changa ndiye aliyeizamisha Simba kwa kufunga mabao yote mawili ya dakika za lala salama, wakati Emmanuel Gabriel aliifungia Simba bao la kufutia machozi katika dakika ya 80.
Kikosi kilichoizamisha Simba kilipangwa hivi; Ben Karama, Martin Muganyizi, Jumanne Rama, Nasib Malila, Bakary Omary, Maregesi Mwangwa, Paul Kabange (Juma Jabu), Yusuf Macho, Omary Changa, Karume Songoro (Mecky Katende) na Vincent Barnabas, (Suudi Ahadi), huku kocha akiwa Silvestre Marsh.
Simba iliyokuwa chini ya Mbrazili, Nelder Dos Santos, ilipangwa hivi: Juma Kaseja, Nurdin Bakari, Sudi Abdi, Kelvin Yondani, Victor Costa, Henry Joseph, Nico Nyagawa, Athumani Idi (Sunday Frank), Mohammed Salum (Suleiman Ndikumana), Sadick Muhimbo (Yahya Akilimali) na Emmanuel Gabriel.
MFUNGAJI BORA
Kagera imeshuka, ikiwa na kumbumbuku ya kutoa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2007-08, pale mshambuliaji wake mahiri wa enzi hizo, Michael Katende alipoibuka kinara akitupia mabao 11, akifunika mastaa wengine wa timu zilizoshiriki ligi msimu huo.
Katende aliyekuwa raia wa Uganda, alikuwa akimpokea Abdallah Juma wa Mtibwa Sugar aliyetwaa tuzo msimu wa 2006 kwa mabao 25, yaliyomfanya nusura aifikie rekodi ya muda wote wa mabao ya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ya mwaka 1998 ya mabao 26 ambayo haijavunjwa hadi leo.

Mbali na Katende, Kagera imewahi kutamba na mastaa wengine waliokuwa gumzo nchini akiwamo, Mrisho Ngassa, Ben Karama, Juma Jabu, Omar Changa, Karume Singoro, Vincent Barnabas, Amri Kiemba, Yusuf Macho, Salvatory Ntebe, Maregesi Magwa, Paul Ngway, George Kavila, Shamte Ally, Obrey Chirwa, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hamis Kiiza ‘Diego’ na wengine.
Pia imepitia mikononi mwa makocha mbalimbali wenye heshima zao kama marehemu Sylvester Marsh, Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’, Jackson Mayanja ‘Mia Mia’ na wengineo kabla ya msimu huu kuonolewa na makocha watatu tofauti, Paul Ntaka, Melis Medo na Kaseja, huku msimu uliopita ilikuwa chini ya Fred Felix ‘Minziro’ anayeinoa Pamba Jiji kwa sasa.
UONGOZI
Baada ya timu hiyo kushuka daraja, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabit Kandoro alinukuliwa akieleza wao kama viongozi wamesikitishwa na hali iliyojitokeza, japo ni changamoto kwao ya kujipanga na kurejea tena wakiwa imara zaidi.
“Kwa nembo na hadhi ya Kagera Sugar kiukweli tumesikitishwa na kilichotokea, kwa sababu ni timu ya kucheza Ligi Kuu na wala sio vinginevyo, msimu umekuwa ni mgumu kwetu lakini umetupa changamoto ya kujipanga tena upya,” anasema Kandoro na kuongeza;
“Mpira wa miguu ni sayansi, ni mjumuisho wa vitu vingi, kama utachelewa kufanya pre-season, itakuja kukugharimu baadaye, kama utapoteza mechi ambazo hupaswi kupoteza nayo itakuja kukugharimu baadaye.
“Kwa hiyo ni mjumuisho wa vitu vingi ambavyo vimetokea na nikiri kwamba sisi kama taasisi tumejifunza vizuri sana kwamba lazima uwe na eneo la ufundi lililo bora, pia eneo la mashindano lililo bora. Unapaswa kuwa na sekretarieti iliyo bora na kikosi bora.
“Unaweza ukaangalia tulikuwa tunacheza halafu hatufungi, hii imetugharimu sana, ukiangalia mpaka sasa tumefunga goli 22, tumefungwa goli 40, sasa kwa klabu inayotaka kuwa nafasi za juu kutoshinda ni changamoto. Kushindwa kushinda nyumbani imetugharimu sana.”

“Kwa mfano mechi dhidi ya Namungo, Tanzania Prisons, KMC, hizi ni mechi ambazo zimetugharimu na tuliliona hilo.
“Kwa hiyo mambo yote hayo ndiyo maana siku ya mwisho yamekuja kutuadhibu. Ajali imetokea, tutajipanga kurudi Ligi Kuu.”