Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lamine Yamal avunja rekodi iliyomshinda Messi Barca

Muktasari:

  • Kabla ya Yamal kufikisha mabao hayo 40, rekodi hiyo ilikuwa imedumu tangu mwaka 1915 na hata Lionel Messi alishindwa kuivunja.

BARCELONA,  HISPANIA: HABARI ndo hiyo. Lamine Yamal amekuwa mchezaji mdogo zaidi katika historia ya FC Barcelona kufunga mabao 40 katika mashindano yote akiwa na klabu hiyo yenye maskani yake Camp Nou.

Kabla ya Yamal kufikisha mabao hayo 40, rekodi hiyo ilikuwa imedumu tangu mwaka 1915 na hata Lionel Messi alishindwa kuivunja.

Hapa chini ni orodha kamili ya wachezaji watano waliofikia mabao 40 wakiwa na umri mdogo zaidi katika historia ya Barcelona.


1. Lamine Yamal

Baada ya hivi karibuni kufunga bao lake la 40 katika ushindi wa Barcelona wa 3-0 dhidi ya Mallorca, Yamal sasa ndiye mchezaji mdogo zaidi kabisa kufikia hatua hiyo.

Akiwa na umri wa miaka 18, bado ana miaka mingi bora mbele yake katika soka, lakini tayari amejiandikia jina lake katika vitabu vya historia ya Barcelona.

Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, alimzungumzia Yamal hivi karibuni alisema: “Bado ni mdogo sana kuendelea kuboresha kiwango chake, ana uwezo mkubwa wa kufikia ngazi nyingine. Nadhani hilo litatokea.”


2. Paulino AlcAntara

Paulino alianza kuchezea Barcelona mwaka 1912 akiwa na umri wa miaka 15, na hadi leo bado ndiye mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika klabu hiyo.

Alifunga bao lake la 40 rasmi mwaka 1915 akiwa na umri wa miaka 19 pekee. Cha kushangaza, rekodi yake ilisimama kwa zaidi ya miaka 100, hadi Yamal alivyoivunja mwaka huu.

Paulino alitumia sehemu kubwa ya maisha yake ya soka akiwa Barcelona kabla ya kustaafu mwaka 1927 akiwa na umri wa miaka 31. Baada ya kustaafu, alisomea udaktari na pia aliwahi kuwa mkurugenzi wa klabu.


3. Ronaldo Nazario

R9 alitumia msimu mmoja tu Barcelona, lakini ulikuwa msimu wa kipekee.

Kwa jumla, alicheza mechi 49 katika mashindano yote na kufunga mabao 47 katika msimu wa 1996–97.

Alipofunga bao lake la 40 akiwa Barcelona, Ronaldo alikuwa na umri wa miaka 20 na siku 204, na hivyo kuwa mchezaji wa tatu mdogo zaidi kufikia idadi hiyo katika historia ya klabu.

Kama angeanza soka lake Barcelona badala ya PSV, huenda angevunja rekodi hiyo ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mabao 40 ya michuano yote akiwa ndani ya uzi wa Barcelona.


4. Bojan Krkic

Aliitwa “Messi mpya” wakati anaibukia kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona. Bojan alionekana kuwa na mustakabali mkubwa sana kwa siku za baadaye katika kikosi hicho cha miamba ya kutandaza soka la ardhini.

Alifunga bao lake la 40 mwaka 2011, akiwa na umri wa miaka 20 na siku 204.

Mwisho wa msimu wa 2010–11, Bojan aliondoka Barcelona akitafuta nafasi ya kucheza mara kwa mara na kujiunga na AS Roma ya Italia.

Alipata mafanikio makubwa zaidi baada ya Barcelona alipokuwa Stoke City, ambako alijijengea umaarufu mkubwa kwa mashabiki, wakati timu hiyo ilipokuwa ikikipiga kwenye Ligi Kuu England.


5. Lionel Messi

Messi alikuwa na umri wa siku 38 zaidi ya Bojan alipofikia mabao 40, jambo linalomweka nafasi ya tano kwenye orodha hii.

Ikilinganishwa na Yamal, Messi alihitaji mechi 98 tu kufunga mabao yake 40 ya kwanza, ikiwa ni mechi 38 chache kuliko Yamal alizohitaji.

Hata hivyo, kwa kuzingatia umri wao wakati huo, Messi alikuwa na umri wa miaka miwili zaidi kuliko Yamal, ndiyo maana anashika nafasi ya tano kwenye orodha hii na kushindwa kuvunja rekodi ya Paulino Alccntara, licha ya kwamba aliibukia kwenye akademia ya La Masia.

Kwa upande wa orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa Barcelona, rekodi ya Messi bado iko salama kwa sasa, huku Yamal akiwa nyuma kwa mabao 632 kufikia mafanikio ya mkali huyo wa Kiargentina na mshindi mara nane wa Ballon d’Or.