Prime
Lamine Yamal anavyowapoteza wengi kwenye umri wake

Muktasari:
- Hilo la kuwa bora kwenye historia ya soka linaweza kuzua kelele nyingi, lakini ukitazama kile Yamal alichofanikiwa hadi sasa kwenye umri alionao, si wachezaji wengi walifanikiwa kufanya hivyo hata ukiwajumuisha wale magwiji wanaohesabika kuwa manguli zaidi kwenye mchezo huo walipokuwa na umri kama wake.
BARCELONA, HISPANIA: KINDA na fundi wa mpira wa Barcelona, Lamine Yamal pengine ni mchezaji bora kabisa kwenye umri wake kwenye historia ya soka.
Hilo la kuwa bora kwenye historia ya soka linaweza kuzua kelele nyingi, lakini ukitazama kile Yamal alichofanikiwa hadi sasa kwenye umri alionao, si wachezaji wengi walifanikiwa kufanya hivyo hata ukiwajumuisha wale magwiji wanaohesabika kuwa manguli zaidi kwenye mchezo huo walipokuwa na umri kama wake.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 17 hivi karibuni aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kwenye soka la Ulaya kufikisha mechi 100 za kimashindano huku ndiyo kwanza kiwango chake kikizidi kunoga.
Kwenye ishu ya kumfanya Yamal kuwa mchezaji bora zaidi kwa wakali waliochini ya umri wa miaka 18 kwenye historia ya mchezo wa soka, imefanya kuangaziwa wengine wale waliotoboa na kutambulika kama magwiji, walifanya nini kwenye mchezo huo wa soka walipokuwa na umri kama wa mkali huyo wa kimataifa wa Hispania.
Yamal amevunja rekodi zote zilizowekwa na wachezaji vijana kwenye kikosi cha Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, baada ya kuanza kuzichezea timu hiyo akiwa na umri wa miaka 15 na siku 291 kwenye klabu na miaka 16 na siku 57 kwenye timu ya taifa, kikosi cha La Roja. Hakuwa na mchango kwenye ubingwa wa La Liga 2022-23, lakini kinda huyo alikuwa akifanya mazoezi na kikosi cha wakubwa wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Xavi.
Yamal msimu wake wa kwanza Barcelona ulimalizika bila ya taji, lakini aling'ara kwenye majira ya kiangazi mwaka jana akiwa na kikosi cha Hispania na kubeba ubingwa wa Euro 2024 na alikuwa bado na umri wa miaka 16, wakati alipofunga bao matata kabisa kwenye nusu fainali dhidi ya Ufaransa. Ndiyo kwanza alitimiza umri wa miaka 17, wakati alipoasisti bao la Nico Williams kwenye mechi ya fainali dhidi ya England.
Sasa amejipambanua kama mmoja wa wachezaji bora kabisa Barcelona na ndiyo mchezaji muhimu. Alikuwa staa kwenye mechi zote mbili dhidi ya Real Madrid, ambazo waliangusha kipigo kizito, huku akiwa mfalme mpya wa Ulaya kwenye kukokota mipira na kuwavuka wachezaji wa timu pinzani kama anavyotaka, akiongoza Barcelona ya kocha Hansi Flick kwenye kufukuzia mataji matatu makubwa msimu huu.
Hadi kufika sasa, kinda huyo amefunga mabao 20 na kuasisti 26 katika mechi 92 alizochezea Barcelona, huku mabao manne na asisti tisa amefunga katika mechi 19 alizoitumikia Hispania. Atafikisha umri wa miaka 18, Juni.
Lakini, walifanya nini magwiji wa soka walipokuwa na umri kama wa Yamal ili kumwondolea kinda huyo kibali cha kuwa mchezaji bora wa umri wake kwenye historia ya soka. Magwiji hawa walifanya nini walikuwa U18?

- Kylian Mbappe; Kinda Kylian Mbappe aliibukia akiwa kwenye kikosi cha AS Monaco kabla ya kutua Paris Saint-Germain na baadaye kwenda kushinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa wakati huo umri wake ukiwa miaka 19.
Fowadi huyo mfaransa alikuwa kwenye kiwango bora wakati anaibukia, lakini hakuwa hatari na takwimu kama hizo za kinda Yamal. Hakucheza Les Bleus hadi alipofikisha umri wa miaka 18. Mechi yake ya kwanza kucheza Monaco alikuwa na miaka 16 na siku 347 na hapo alivunja rekodi ya Thierry Henry. Lakini, hakuwa na maajabu sana hadi alipofikisha umri wa miaka 18. Alifunga mabao manne na asisti tano tu katika mechi 21 za Ligue 1, alipokuwa na umri wa Yamal.

2. Lionel Messi; Wakati Ronaldinho anapokea tuzo ya Ballon d'Or alisema: “Tuzo hii inasema mimi ni bora duniani, lakini mimi si bora hata Barcelona tu. Kuna mtu anaitwa Lionel Messi. Ni kama mdogo wangu, yeye ni Muargentina, mimi ni Mbrazili, lakini nimekuwa nikimlea. Atakuja kuwa balaa sana.”
Hayo yalikuwa maneno ya Ronaldinho kuhusu Messi na mwaka huo alitimiza umri wa miaka 18. Huko La Masia, mwanzoni mwa miaka ya 2000 yeyote ungemuuliza kuhusu Messi angekujibu, akiwamo Cesc Fabregas, lakini kwenye soka ndani ya uwanja, supastaa huyo wa dunia hakuwa ameonyesha kitu cha maana kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, Juni 2005. Kabla ya hapo, Messi alikuwa amecheza mechi 10 tu na hakufunga wala kuasisti.

3. Cristiano Ronaldo; Hadithi yake ni kama ya mpinzani wake wa miaka mingi, Messi. Kwa wale walioibukia au kucheza dhidi ya Ronaldo mdogo huko Sporting CP walikuwa na ushuhuda wa kusema atakuja kuwa mchezaji mahiri duniani. “Niliona Ronaldo ubora wake siku ile. Alicheza dhidi ya John O’Shea. Sheasy alihitaji msaada wa kidaktari wakati wa mapumziko kutokana na kizunguzungu alichosababishiwa na Ronaldo,” alisema Roy Keane baada ya kumshuhudia Ronaldo kwenye mechi ya pre-season na hapo Manchester United ilishawishika kumsajili.
Lakini, Ronaldo alikuwa ametimiza umri wa miaka 18 miezi sita kabla ya mechi hiyo ya pre-season mwaka 2003. Kabla ya kufikisha miaka 18, Ronaldo alifunga mabao matano na kuasisti manne katika mechi 20 alizocheza Sporting CP.

4. Wayne Rooney; Bado anatambulika kama nembo ya Ligi Kuu England baada ya kuibukia akiwa mdogo kabisa na kufanya mambo makubwa. Rooney aliibuka kwenye ligi hiyo akiwa na miaka 16 huko Everton. Lakini, takwimu za Rooney kabla ya kufikisha umri wa miaka 18, haziingizi kabisa mguu kwa Yamal anachokifanya kwa sasa Barcelona. Katika umri wa miaka 16, kitu kinachokumbukwa kuhusu Rooney ni bao lake shuti kali alilofunga dhidi ya Arsenal.

5. Pele; Huyu ndiye anayetajwa kuwa mfalme wa soka duniani. Alishinda Kombe la Dunia akiwa na umri wa miaka 17 na hakuna aliyevunja rekodi hiyo. Staa wa Ufaransa, Just Fontaine alifunga mabao 13 kwenye fainali za Kombe la Dunia 1958 zilizofanyika Sweden, lakini baadaye alisema: “Nilipomwona Pele akicheza, nilijihisi napaswa kuacha mpira.” Rekodi za Mbrazili huyo bado hazijavunjwa.

6. Diego Maradona; Kuna mtu mmoja anaitwa Francisco Cornejo, kocha aliyemnoa Maradona utotoni, alisema hivi: “Wakati Diego alipokuja Argentinos Juniors kufanya majaribio, nilishtushwa na kipaji chake, ilikuwa ngumu kuamini alikuwa na umri wa miaka minane.” Aliongeza: “Niliomba kitambulisho chake ili nione, alijibu hana.”
El Diego hakupata mafanikio makubwa kama kushinda Kombe la Dunia akiwa na umri wa miaka 17, lakini jina lake lilifahamika mapema sana duniani kote kutokana na ubora wake uwanjani. Mechi yake ya kwanza Argentinos Juniors alicheza siku 10 kabla ya kutimiza umri wa miaka 16.