Kwani nyie mnatakaje?

Saturday September 25 2021
New Content Item (1)
By Waandishi Wetu

BAADA ya Yanga kumtambulisha Cedrick Kaze jana jioni kama Kocha Msaidizi na Mwinyi Zahera kama Mkurugenzi wa Ufundi, tambo zilianzia pale klabuni Jangwani huku wakiwatambia wenzao wa Simba kwamba ; “Kwani nyie mnatakaje, tumalize ndani ya dakika 90 au twende kwenye penati?” Lakini Simba wenzao wa Simba wakacheeka na kuwasisitiza; “ Tukutane kwa Mkapa sisi ndiyo wenye nchi. Sisi tuna timu. ” Mambo yote ni leo saa 11 kwenye mechi yao ya Ngao ya Jamii Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kwa kawaida mechi ya Ngao ya Jamii hukutanisha timu inayotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ile inayobeba Kombe la Shirikisho (ASFC), lakini kama ilivyokuwa msimu uliopita Simba ndio iliyobeba mataji yote mawili na kulazimika kukutana na Yanga iliyopasuka kwenye fainali ya ASFC na kumaliza ya pili katika Ligi Kuu Bara kama ilivyokuwa kwa Namungo walipovaana nao msimu uliopita.

Hili linakuwa pambano la nne kwa watani hao kukutana ndani ya mwaka huu wa 2021, lakini ni mechi yao ya saba kwenye Ngao ya Jamii tangu zilipoanza kukutana mwaka 2001.

Simba na Yanga zilikutana kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2021 iliyopigwa Januari 13 na Yanga kuibuka wababe kwa mikwaju ya penalti, kisha zikakutana tena katika pambano la marudiano la Ligi Kuu Bara Julai 8 na Yanga kushinda tena kwa bao 1-0 kabla ya kuvaana tena katika fainali ya ASFC.

Katika fainali hiyo iliyopigwa Julai 25 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma, Simba safari hii iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililowekwa kimiani na kiungo wao kutoka Uganda, Taddeo Lwanga na Jumamosi hii wanakamilisha mechi yao ya nne ndani ya 2021.

Mwanaspoti linakuletea mechi sita na matokeo yake za mapambano ya awali ya watani wa jadi hao katika mechi za Ngao ya Jamii, japo kwa misimu miwili kati ya mitatu yaani 2002 na 2005 fainali ya Kombe la Tusker Cup zilitumika kama Ngao ya Jamii, ikiwamo 2003 Simba ilivaana na Mtibwa Sugar.

Advertisement

Kati ya mechi hizo sita za awali za watani, Simba ndio kinara kwa kushinda mara nyingi dhidi ya watani zao, ikifanya hizo mara nne, huku Jangwani wakishinda mara mbili.


Februari 17, 2001

Hii ndio iliyokuwa mechi ya kwanza kwa watani hao kukutana kwenye Ngao ya Jamii na Yanga kuitambia Simba kwa mabao 2-1 katika mchezo huo mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), jijini Dar es Salaam.

Yanga ilishtukizwa na watani wao kwa bao la kipindi cha kwanza lililofungwa na Steven Mapunda ‘Garrincha’ dakika mbili kabla ya mapumziko yaliyowafanya mashabiki wa Jangwani kunyong’onyea.

Hata hivyo, kipindi cha pili Yanga ilirudi kivingine ikiwa na kasi kubwa na kulisawazisha bao hilo dakika mbili baada ya kipindi hicho kuanza, kupitia kwa winga wao matata, Edibilly Lunyamila na kwenye dakika ya 80, aliyekuwa nyota wa zamani wa Simba, Ally Yusuf ‘Tigana’ alimaliza udhia kwa bao la pili.

Licha ya Simba kucharuka kutaka kusawazisha bao hilo kwa dakika 10 zilizosalia, matokeo yalibaki kama yalivyo na Yanga kuwa mabingwa wa Ngao ya Jamii enzi hizi ikifahamika kama Ngao ya Hisani.


Machi 31, 2002

Simba na Yanga zilikutana tena, lakini safari hii ikiwa ni kwenye fainali ya Kombe la Tusker iliyotumika kama mechi ya Ngao ya Jamii na Wekundu wa Msimbazi walilipa kisasi kwa kuinyoosha Yanga kwa mabao 4-1.

Wafungaji katika mchezo huo ambao ulihudhuriwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, nusura uvunjike dakika ya 32, yalifungwa na Mkenya Mark Sirengo aliyefunga mawili dakika ya 3 na 76, Madaraka Selemani dakika ya 32 na Emmanuel Gabriel aliyetupia bao moja dakika ya 83.

Bao la kufutia machozi la Yanga lililokuwa la kusawazisha, liliwekwa kimiani na Sekilojo Chambua dakika 16 kabla ya Wekundu kucharuka na kuwakimbiza Yanga.

Bao la Madaraka la dakika ya 32 liliibua timbwili kwani Mzee wa Kiminyio huyo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Mwamuzi wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, FAT (sasa TFF).


Julai 02, 2005

Kama ilivyokuwa mwaka 2002, Simba na Yanga zilikutana tena kwenye fainali ya Kombe la Tusker iliyopigwa Kirumba na TFF iliamua kuutumia mchezo huo kama Ngao ya Jamii na Vijana wa Jangwani wakapasuka kwa mabao 2-0.

Simba ilipata mabao yake yote yakifungwa kipindi cha pili na Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ katika dakika ya 60 na Mussa Hassan ‘Mgosi’ akapigilia msumari wa mwisho dakika ya 72 na kwenye mchezo huo, Victor Costa ‘Nyumba’ alilimwa kadi nyekundu dakika ya 54 na mwamuzi, Othman Kazi, huku nyota wengine wanne wa timu hizo, Saidi Swedi, Boniface Pawasa kwa Simba na Benito John, Fred Mbuna kwa upande wa Yanga walionyeshwa kadi za njano kila mmoja.


Agosti 18, 2010

Baada ya michuano hiyo kutochezwa tangu fainali ile ya Jijini Mwanza, Simba na Yanga zikakutana tena msimu mmoja baada ya michuano hiyo kurejeshwa upya 2009 ambapo Vijana wa Jangwani walipoteza mbele ya Mtibwa Sugar.

Yanga ikiwa na machungu ya kukosa Ngao kwa Walima Miwa wa Manungu, mwaka huo wa 2010 ilivaana na Simba wakiwa na machungu, lakini goma likaisha kwa suluhu na kuamuriwa kupigwa mikwaju ya penalti na Vijana wa Jangwani wakatakata kwa kushinda mikwaju 3-1.

Nyota waliokwamisha penalti zao kwa upande wa Yanga ni Geofrey Bonny, Stefano Mwasyika na Isaac Boakye, huku Ernest Boakye akikosa, huku Mohammed Banka alikwamisha mkwaju wa Simba, ilihali wenzake Emmanuel Okwi, Uhuru Suleiman na Juma Nyosso wakikosa.


Agosti 17, 2011

Baada ya Simba kupasuka kwenye Ngao ya Jamii 2010, Wekundu hao walirudi kivingine msimu uliofuata wakikutana tena na watani wao Yanga na wababe hao wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, kwenye mchezo huo mkali uliopigwa Uwanja wa Taifa. Mabao ya washindi hao yaliwekwa kimiani na Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 15 kabla ya Mzambia Felix Sunzu kumaliza kazi kwa bao la dakika ya 39 na Yanga kutoka uwanjani vichwa chini.


Agosti 23, 2017

Simba na Yanga zikakutana tena mwaka 2017 na mchezo huo kama uliokuwa wa mwaka 2011 ambao ulikuwa wa mwisho kwa watani hao kukutana, uliisha kwa suluhu na kuamriwa kwa penalti na Wekundu wa Msimbazi, kuibuka na ushindi kwa mikwaju 5-4.

Simba ilipata penalti zake zote kupitia Method Mwanjali, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim, huku za Yanga zilifungwa na Papy Kabamba Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Ibrahim Ajibu na Donald Ngoma, huku penalti ya kwanza ya Kelvin Yondani ikidakwa na kipa Aishi Manula.


Sept 25, 2021

Leo sasa. Hapo kwa Mkapa. Timu hizi zikikutana kwa mara ya saba katika mechi za Ngao ya Jamii, kila moja ikiwa na kikosi kipya sambamba na makocha wasaidizi wanaojua vyema soka la Tanzania na kashkashi za Kariakoo Derby.

Ndio, Simba iliyo wenyeji wa mchezo huo, inaivaa Yanga ikiwa na jeshi ya wachjezaji 32, wakiwamo wapya 12 waliosajili msimu huu. Nyota wapya ni makipa Jeremiah Kisubi na chipukizi, Ahmed Feruz, mabeki Henock Baka ‘Varane’ na Israel Mwenda, viungo wakiwa Abdulswamad Kassim, Pape Ousmane Sakho, Peter Banda, Sadio Kanoute na Duncan Nyoni, huku washambuliaji wakiwa ni Yusuf Mhilu, Jimmyson Mwanuke na Denis Kibu.

Huku benchi lao likiwa na makocha wapya wawili, Thierry Hitimana anayekuwa msaidizi wa Didier Gomes, huku Fareed Cassem aliyekuwa mtaalamu wa viungo wa Yanga akitua pia Msimbazi.

Kwa upande wa Yanga, ingizo jipya ni Kocha Msaidizi, Cedric Kaze aliyeenda kuimarisha benchi la ufundi lililo na Nasreddine Nabi, huku kwa upande wa wachezaji kuna majembe mapya zaidi ya 10 akiwamo straika Heritier Makambo, Fiston Mayele na Yusuf Athuman. Pia kuna makipa Erick Johola na Diarra Djigui, mabeki wakiwa ni David Bryson, Yannick Bangala na Djuma Shaban, huku viungo wakiwa ni Khalid Aucho na Jesus Moloko. ENDELEA KUTUFUATILIA MWANASPOTI LEO TUTAKUWA Live KWENYE MITANDAO YETU YA KIJAMII KUKULETEA MATUKIO YA MECHI YA WATANI

Advertisement