Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwaheri Ally Star, utabaki nembo ya taarabu

KWAHERI Pict

Muktasari:

  • Wiki hii, tasnia hiyo imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Ally Star, muimbaji na mtunzi mahiri wa Tanzania One Theatre (TOT).

SEKTA ya muziki wa burudani nchini Tanzania, hususan taarabu, inaendelea kupoteza nguzo zake muhimu mmoja baada ya mwingine, hali inayowaacha wasanii wachanga wakiwa na maswali mengi juu ya mustakabali wa fani hiyo nyeti na ya kihistoria.

Wiki hii, tasnia hiyo imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Ally Star, muimbaji na mtunzi mahiri wa Tanzania One Theatre (TOT).

Ally Star alifariki dunia Jumanne ya Februari 3, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa wiki kadhaa. Jana Jumatano Januari 4, 2026, mwili wake ukasafirishwa kwenda Kilosa Kichangani mkoani Morogoro, kwa ajili ya mazishi.

Kifo chake kimeacha huzuni kubwa kikitikisa mioyo ya wadau wa sanaa, wanamuziki, waandishi wa habari na mashabiki wa taarabu kote nchini.

Nawakumbuka waimbaji na watunzi waliobeba hadhi ya taarabu ndani ya TOT na bendi nyingine za taifa, waliotumia muziki kama chombo cha kuelimisha, kuburudisha na kuonya jamii. Ally Star alikuwa miongoni mwa safu hiyo ya wasanii waliothamini neno, mizani na maana ya muziki kuliko makeke ya jukwaani.

Alikuwa msanii aliyefahamu kwamba taarabu ni utambulisho wa utamaduni, historia na busara za jamii ya waswahili.

Akiwa ndani ya TOT, Ally Star alijitambulisha kupitia nyimbo alizoimba na kutunga zikiwemo Natanga na Njia, Zumbukuku, Hauvumi Lakini Umo na Limbukeni. Nyimbo hizi hazikuwa tu za kuburudisha, bali zilikuwa masomo ya maisha.

Kupitia mashairi mazito na uimbaji wa hisia, Ally Star aliweza kuigusa jamii na kuwafanya wasikilizaji wajitafakari. Alikuwa msanii aliyefanya hadhira isikilize kwa makini, ifikiri, na wakati mwingine ijione ndani ya simulizi la wimbo.

Nilimfahamu Ally Star kupitia maonesho ya TOT katika kumbi mbalimbali za burudani, hususan jijini Dar es Salaam na katika ziara za mikoani. Alikuwa mtu wa utulivu mkubwa nje ya jukwaa, mwenye heshima na nidhamu ya hali ya juu, mtu wa vichekesho, lakini aliposhika kipaza sauti, alibadilika na kuwa msimulizi mahiri wa hadithi za jamii. Huo ulikuwa upekee wake, hakupaza sauti kwa nguvu, bali kwa maana.

TOT kama bendi ya taifa imekuwa shule kwa wasanii wengi, na Ally Star alikuwa mmoja wa walimu wasio rasmi ndani ya taasisi hiyo. Wasanii wachanga walijifunza kwake kuhusu nidhamu ya jukwaa, heshima ya mashairi na namna ya kuwasilisha ujumbe bila kumkosea hadhira. Alikuwa mtu wa busara, aliyeshauri kwa upole na kufundisha kwa mfano.

Taarifa za kuugua kwake zilianza kusikika kwa tahadhari, na wengi waliendelea kumuombea afya njema. Hata hivyo, mapenzi ya Mwenyezi Mungu yametangulia.

Kifo chake kimeiacha TOT na tasnia ya taarabu kwa ujumla ikiwa na pengo kubwa, pengo la sauti, kipaji na hekima.

Kwa kweli Ally Star alikuwa zaidi ya mwimbaji; alikuwa mlezi wa utamaduni wa taarabu, alielewa mizizi ya muziki huo na aliuheshimu, hakukimbilia mitindo ya muda mfupi, bali alilinda ladha ya asili huku akiupa uhai wa kizazi cha sasa, ndiyo maana nyimbo zake zitaendelea kusikilizwa na kutajwa hata baada ya yeye kutangulia mbele ya haki.

Jana Jumatano aliposafirishwa kwenda Kilosa Kichangani kupumzishwa katika maskani yake ya milele, jamii ya sanaa inabaki na maswali mengi, nani atachukua nafasi ya Ally Star? Nani atalinda mashairi, mizani na roho ya taarabu ndani ya TOT na nje yake?

Japo kifo ni sehemu ya maisha ya binadamu, lakini msiba wa Ally Star ni pigo lisilo na kifananisho kwa wapenzi wa taarabu, ameondoka kimwili, lakini urithi wake utaendelea kuishi kupitia nyimbo, kumbukumbu za jukwaani na wasanii aliowagusa.

Kwa kweli, kama ilivyo kwa magwiji wengine waliotangulia, Ally Star atabaki kuwa nembo ya taarabu ndani ya TOT na katika historia ya muziki wa Tanzania, hata baada ya kifo chake.

ANAVYOZUNGUMZWA

Mkurugenzi wa Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), Khadija Kopa anasema kifo cha Ally Star ni pigo kwa kundi kwani limempoteza mwasisi mwingine.

TOT ilianzishwa miaka ya mwanzoni mwa 1990 ambapo mmoja wa waanzilishi wake na mkurugenzi wa kwanza wa kundi hilo alikuwa Kapteni mstaafu hayati John Komba.

Kopa anasema alimfahamu Ally Star tangu alipojiunga na kundi hilo 1992, na ni mmoja wa waanzilishi, hivyo walifanya kazi kwa karibu kwa miaka mingi.

“Ally Star alikuwa mtu wangu wa karibu sana. Tulianza kazi pamoja TOT tangu 1992, alikuwa msanii mwenye nidhamu, kipaji na mapenzi makubwa kwa sanaa,” anasema Kopa.

Anasema mwanamuziki huyo alianza kuumwa mbavu na kifua Julai 2025, tatizo walilolihusisha pia na ajali waliyowahi kupata.

Kopa anasema hali hiyo ilianza taratibu kabla ya afya yake kuzorota zaidi kadri muda ulivyokuwa unaenda.

Anaongeza kuwa, baadaye Ally Star alipata kiharusi kidogo na kuwalazimu kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa mujibu wa Kopa, baada ya siku chache akiwa hospitali hali yake ilianza kuimarika kidogo, jambo lililoipa familia matumaini pamoja na wasanii wenzake.

“Alikuwa anaendelea vizuri kidogo tukapata matumaini, lakini ghafla akapatwa na mauti. Tumelipokea hili kama mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” anasema.

Kopa anasema kifo hicho kimeacha pengo TOT, akisisitiza mchango wa msanii huyo kama mwanzilishi, mwimbaji na mtunzi utaendelea kukumbukwa kupitia nyimbo, maadili na historia ya bendi hiyo.

Mmoja wa wakongwe wa muziki nchini, Thabit Abdul anaelezea huzuni yake na jinsi alivyojifunza kutoka kwa Ally Star ambapo anabainisha kuwa miongoni mwa yale aliyojifunza ni utunzi na upigaji kinanda kwani alikuwa makini kila alipokuwa akitoa nyimbo anamsikiliza.

“Ally Star alikuwa mtu wa kucheka na kila mtu. Ukikaa naye dakika mbili lazima ucheke, lakini pia alikuwa mshauri mkubwa wa wasanii wengi. Mimi nimejifunza sana utunzi kupitia nyimbo zake, na upigaji wa kinanda, kutoka kwake,” anasema Thabit.

Amesema pengo lililobaki baada ya kifo cha Ally Star ni gumu kuliziba, lakini bado kuna wasanii wanaoweza kuiga yaliyomo ndani ya kipaji cha mwanamuziki huyo.

“Pengo la Ally Star kuliziba ni ngumu, lakini bado tunaweza kupata wasanii wenye kipaji cha aina hiyo, ingawa si rahisi kama yeye,” anasema.

Anaongeza kuwa ndani ya TOT Ally Star atabaki kuwa nguzo muhimu ya mafanikio, huku akiwaachia ucheshi, urafiki na ushauri vitu alivyokuwa navyo.

Kwa upande wa msanii wa muziki wa taarabu na Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), Abdul Misambano amezungumzia kifo cha Ally Star akisema alikuwa msanii aliyependa furaha na aliyeleta mwanga ndani ya bendi, hali iliyomfanya aheshimiwe na kupendwa na wengi.

Anasema pamoja na utani na ucheshi wake, Ally Star alikuwa mtu wa nidhamu na aliyeheshimu kazi na jukwaa la sanaa.

Msanii huyo anasema dalili za kugua Ally Star zilianza kabla za kampeni uchaguzi mkuu 2025, ambapo alianza kulalamika kuhusu hali yake ya afya. Hata hivyo, baada ya kampeni kumalizika, afya yake ilizorota zaidi kiasi cha kuhitaji matibabu kutoka kwa wataalamu wa afya.

“Ally Star ameanza kuumwa miezi minne iliyopita kabla hata ya kampeni za uchaguzi, hivyo katika kampeni hatukuwa naye. Tumemaliza kampeni mkurugenzi wa TOT Khadija Kopa alinipigia simu twende tukamuone,” anasema Misambano.

“Tulipofika nyumbani kwake hatukumkuta na hali nzuri ndipo Khadija Kopa akasema tumpeleke katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu. Muhimbili amekaa wiki tatu na nusu ndio amefariki jana (juzi).”

Misambano anasema alimfahamu Ally Star tangu mwaka 1993 alipojiunga na Bendi ya TOT na tangu wakati huo alionyesha mapenzi makubwa katika muziki wa taarabu akijituma kwa dhati kuitumikia sanaa hiyo.