Thabit: Mchango wa Ally Star TOT haupimiki
Muktasari:
- Thabit ameliambia Mwanaspoti kuwa, kwa Ally Star alikuwa anajifunza vitu vingi ikiwemo utunzi na upigaji kinanda kwani alikuwa makini kila alipokuwa akitoa nyimbo anamsikiliza.
Tasnia ya taarabu nchini imepoteza kipaji kikubwa kufuatia kifo cha mwimbaji na mtunzi, Ally Star, ambapo mkongwe wa muziki Thabit Abdul ameelezea huzuni yake na jinsi alivyojifunza kutoka kwake .
Thabit ameliambia Mwanaspoti kuwa, kwa Ally Star alikuwa anajifunza vitu vingi ikiwemo utunzi na upigaji kinanda kwani alikuwa makini kila alipokuwa akitoa nyimbo anamsikiliza.
"Ally Star alikuwa mtu wa kucheka na kila mtu. Ukikaa naye dakika mbili lazima ucheke, lakini pia alikuwa mshauri mkubwa wa wasanii wengi. Mimi nimejifunza sana utunzi kupitia nyimbo zake, na upigaji wa kinanda, kutoka kwake," amesema Thabit.
Amesema pengo lililobaki baada ya kifo cha Ally Star ni gumu kuliziba, lakini bado kuna wasanii wanaoweza kuiga yaliyomo ndani ya kipaji cha mwanamuziki huyo.
"Pengo la Ally Star kuliziba ni ngumu, lakini bado tunaweza kupata wasanii wenye kipaji cha aina hiyo, ingawa si rahisi kama yeye," amesema.
Ameongeza kuwa ndani ya TOT Ally Star atabaki kuwa nguzo muhimu ya mafanikio yao, huku akiwaachia ucheshi, urafiki na ushauri vitu alivyokuwa navyo.
Mwanamuziki huyo alifariki dunia jana, Januari 3, 2026 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na leo anasafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao Kichangani, Kilosa mkoani Morogoro.