Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa Terence Crawford… Changamoto imegeuka fursa

Muktasari:

  • Alilelewa katika eneo hatari linalojulikana kwa umaskini, uhalifu na vurugu, ambayo ilifanya iwe vigumu kwake kusafiri katika ujana wake. Familia ya Crawford mara kwa mara ilikabiliwa na changamoto za kifedha, mara nyingi ikijitahidi kumudu mahitaji ya kimsingi.

OMAHA, MAREKANI: TERENCE Crawford, kijana kutoka Omaha, Nebraska Marekani akiwa mtoto pekee wa Terence Sr na Debbie, ameamua kustaafu mchezo wa ngumi huku akiacha gumzo kubwa kutokana na historia ya maisha yake hadi kupambana na mabondia mbalimbali wenye majina makubwa na chipukizi na kuwashinda.

Alilelewa katika eneo hatari linalojulikana kwa umaskini, uhalifu na vurugu, ambayo ilifanya iwe vigumu kwake kusafiri katika ujana wake. Familia ya Crawford mara kwa mara ilikabiliwa na changamoto za kifedha, mara nyingi ikijitahidi kumudu mahitaji ya kimsingi.

Katika umri mdogo, mara nyingi alihusika katika ugomvi na alifukuzwa kutoka shule tano tofauti kwa sababu ya tabia hiyo. Kwa vile baba yake alikuwa katika Jeshi la Wanamaji la Marekani, hakuwa nyumbani muda mwingi, alimuacha mke wake amlee peke yake.

Mara nyingi alimpiga kwa mkanda na hata kujaribu kuwalipa watoto wa jirani ili wampige, ingawa hakuna aliyefaulu kumbadilisha tabia hiyo.

Changamoto hizo na nyingine nyingi alizokutana nazo katika maisha yake hadi kufikia wakati mama yake kumwambia hana uwezo wa kushinda pambano, kwake aliitumia kama fursa ya kujiimarisha na kuja kuwa bondia asiyepigika.

Mpiganaji huyo wa kiwango cha juu kabisa katika historia, ambaye kwa kweli ndiyo kwanza alikuwa ameingia kwenye kilele cha mafanikio ya kifedha, ametangaza kustaafu akiacha takribani Dola 100 milioni mezani.

Usimtilie shaka kabisa Terence Crawford. Kumbuka shaka iliyokuwepo kwake ndiyo iliyomsukuma miaka yote hii. Ndiyo iliyomfanya awe bingwa asiye na mpinzani (undisputed) katika uzani wa Pauni 140, 147 na 168. Ndiyo iliyomfanya awe mpiganaji bora zaidi duniani (bila kumdharau Oleksandr Usyk, ambaye naye ana nafasi ya kuwa hapo).

Akiwa na miaka 38, Crawford aliyekaa zaidi chini ya Pauni 147, hakuwa chochote alipopangwa kupambana na Canelo Alvarez, Septemba mwaka huu.

Canelo hakuwa tu bingwa asiye na mpinzani wa Pauni 168 wakati huo, bali pia kivutio kikubwa zaidi kifedha kwenye ndondi.

Hata hivyo, ushindi wa kihistoria wa Crawford ulikuwa wa upande mmoja zaidi kuliko inavyoonekana kwenye matokeo ya majaji ya kauli moja.

Kwa kizazi cha wapiganaji, baadhi yao bora sana, ingawa si wakubwa kupigana na Canelo kulimaanisha bahati ya maisha kwa Crawford.

“Hilo ndio pambano pekee ninalotaka,” Crawford alimwambia Turki Alalshikh, mwenyekiti wa mamlaka ya burudani ya jumla ya Saudi Arabia, aliyefadhili pambano la Canelo.

Wakati huo, Alalshikh alikuwa anapendelea zaidi kumkutanisha Crawford na Jaron “Boots” Ennis au Vergil Ortiz Jr., wote wakiwa nyota wasioshindwa wa pauni 154. Crawford hakukubali hata kidogo.

“Boots si pambano kubwa. Vergil Ortiz si pambano kubwa. Hii ni mwisho wa kazi yangu. Watasema ‘Ulitarajiwa kushinda.’ Ninamtaka Canelo Alvarez,” alisisitiza Crawford.

Kama hukuamini kwamba angeweza kumshinda Canelo wakati huo, labda sasa utabadilisha mawazo.

Kabla ya Canelo, kulikuwa na waliodhani hatamshinda Errol Spence Jr, ambaye kimsingi alimaliza kazi yake. Kulikuwa na waliokuwa kwenye kampuni yake ya zamani ya uhamasishaji, Top Rank, ambao kwa haki walimsajili wakati hakuna promota mkubwa aliyemtaka, lakini baadaye wakaanza kufikiri asingewahi kuwa kivutio kikubwa.

Crawford alitiliwa shaka katika kila uzani, hata tangu akiwa mwanamichezo wa kulipwa (amateur). Ingawa ukitazama nyuma, unajiuliza kwa nini ukizingatia ushindi wake wa amateur dhidi ya kijana mwenye kipaji kama Mikey Garcia. Crawford alitiliwa shaka kwa kuwa anatoka Omaha, Nebraska, ambayo haikuwa kwenye ramani ya ndondi hadi yeye alipoiweka.

Crawford alitiliwa shaka na polisi wa eneo lake. Na vijana wa mitaani. Na baadhi ya walimu wake. Lakini zaidi ya yote na kwa umaarufu mkubwa alitiliwa shaka na mama yake mwenyewe, Bi Debra.

Usiku wa kabla ya pambano lake la kwanza la ubingwa miaka 11 iliyopita, Crawford alijikuta akiwa underdog mbali na nyumbani, akimkabili bingwa wa Scotland aitwaye Ricky Burns huko Glasgow. Kabla hajaondoka kwenda Scotland, Bi Debra alimpa hotuba yake ya kawaida kabla ya pambano. “Wewe si kitu,” alimwambia mwanawe. “Utakula kichapo.”

“Nilijua litabaki akilini mwake na ataenda kule akapige watu.”

Na ndivyo ilivyotokea. Mpiganaji asiyejulikana sana akivuka mabara na kushinda kwa uamuzi wa majaji wa kauli moja akiwa ugenini. Hapo ndipo ulipoanza mfululizo wake mrefu wa ubingwa bila kushindwa.

Mike Tyson ana nadharia kuhusu mashujaa wakubwa wa vita, kuanzia Alexander the Great, wote ni watoto wa mama.

“Ndiyo maana Alexander aliendelea kusonga mbele,” Tyson aliwahi kusema.

“Hakutaka kurudi nyumbani na kutawaliwa na mama yake.”

Crawford raia wa Marekani, amestaafu akiwa na rekodi ya kushinda mapambano yote 42 aliyocheza, kati ya hayo 31 yametokana na KO.

Ushindi wake dhidi ya Canelo, umebaki kuwa pambano la mwisho katika taaluma ya Crawford, aliyefungua ukurasa wake wa ndondi za kulipwa mwaka 2008 kwa ushindi dhidi ya Brian Cummings.

Mustakabali wake ulikuwa ukijadiliwa kwa muda mrefu tangu alipomshinda Alvarez na kuwa bingwa wa undisputed wa super-middleweight, akiongeza mafanikio aliyoyapata awali katika lightweight, light-welterweight, welterweight na light-middleweight.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye chaneli yake ya YouTube, Crawford alisema: “Kila mpiganaji anajua siku hii itafika, ila hatujui lini.”

Katika maelezo ya video hiyo kwenye mitandao ya kijamii, aliongeza kuwa hana tena kitu cha kuthibitisha.

“Nilitumia maisha yangu yote kufukuza jambo fulani. Sio mikanda, sio pesa, sio vichwa vya habari, bali ile hisia unayoipata wakati dunia inakutilia shaka lakini unaendelea kujitokeza na kuendelea kuthibitisha wanakosea,” alisema Crawford.

“Mchezo huu ulinipa kila kitu. Nilipigana kwa ajili ya familia yangu, nilipigana kwa ajili ya jiji langu, nilipigana kwa ajili ya yule mtoto niliyewahi kuwa hana chochote zaidi ya ndoto na glavu. Nimeutoa mchezo huu kila pumzi niliyokuwa nayo, kila sparring, kila ushindi, kila chembe ya moyo wangu. Nimepata amani kuhusu kinachofuata. Sasa, ni wakati. Asanteni.”

Crawford ambaye ni mzaliwa wa Omaha, miongoni mwa ushindi wake wa kukumbukwa ni kutwaa mkanda wa WBO welterweight dhidi ya Waingereza Amir Khan na Kell Brook.

Crawford si bondia wa kwanza kutoweka ghafla akiwa katika kilele cha mafanikio. Na ukweli ni kwamba hatakuwa wa kwanza kurejea tena baada ya kustaafu endapo akiamua kufanya hivyo na wengi wanaamini atarejea ulingoni.

Chukulia mfano ni wewe ndiye Terence Crawford, na pambano lako la mwisho likiwa ni ushindi wa kihistoria dhidi ya Canelo Alvarez huku ukiwa haujapewa nafasi yoyote ya kushinda mbele ya watazamaji 70,000 kwenye pambano la wazi mjini Las Vegas, hicho ni kiwango cha juu sana cha mafanikio. Zaidi ya hapo, ni kupata mamilioni ya dola.

Baada ya kupata dola milioni 30, 40 au hata 50, ni vigumu sana kurejea kupigana kwa asilimia 10 ya kiasi hicho, hata kama ni dola milioni 10. Kwa muktadha huo, Dola 10 milioni zinaweza zisionekane kuwa pesa nyingi.

Je, Terence Crawford atarejea ulingoni baada ya kuamua kustaafu? Tusubiri tuone.

Lakini kama ataamua kubaki amestaafu, basi hiyo itabaki kuwa moja ya kustaafu bora zaidi katika historia ya ndondi akiwa na rekodi zake za kutisha.