Prime
Kutana na mchezaji mfupi zaidi duniani anayetembea na rekodi

Muktasari:
- Wapo watu ambao kwao kandanda ni burdani kubwa na kila wanapokuwa na nafasi baada ya kazi mchana huenda kuangalia mchezo huo au hufungua kituo cha runinga chenye kuonyesha mchezo au habari zake.
WIMBO mmoja maarufu wa taarabu wa kikundi cha Nadi Akhwan Safaa (Ndugu wapendanao) cha Malindi mjini Unguja unasema "macho hayasemezeki kwa kitu ukipendacho." Hali hiyo pia inathibitika katika mchezo wa kandanda. Ukichunguza utaona kila anayependa kandanda huwa na sababu mbalimbali zinazomfanya kuangalia mchezo kwa kwenda uwanjani au kupitia katika televisheni.

Vilevile wapo watu ambao huhakikisha wanafika uwanjani kila timu wanayoishabikia ikicheza ili kuiunga mkono. Katika baadhi ya michezo wapo mashabiki ambao hufika kufuatilia wachezaji wanaowavutia kuwaona namna wanavyocheza na ikiwa timu
zinazocheza hazina mchezaji wa aina hiyo huamua kukaa pembeni.
Hadi miezi michache iliyopita alipokuwa Saudi Arabia kabla hajarudi Brazil na kujiunga na Clube de Brasil ya mji mdogo wa ukanda wa pwani wa Trapichao alikuwa kivutio kikubwa cha watazamaji. Alipoamua kurudi nyumbani mashabiki wengi wa kandanda walifika uwanja wa ndege kumuaga na kumpa zawadi.
Mchezaji huyo ni Elton Jose Xavier Gomes maarufu kama Elton Arabia au Elton ambaye amekuwa kivutio kikubwa cha watazamaji. Kila wakati klabu yake ya Al-Fateh ilipokuwa ikicheza uwanja ulifurika watazamaji hasa watoto kumuangalia. Hii inatokana na kuaminika kuwa ndiye mtu mfupi kabisa kuliko mchezaji yeyote duniani anayechezea klabu zinazoshiriki ligi katika nchi mbalimbali.
Urefu wake huyu jamaa ni futi 5 na inchi 0.63, lakini kinachoshangaza ni kwamba anaweza kuruka juu na kufanikiwa kupiga kichwa mpira anapokuwa katika kinyang’anyiro cha mpira na wachezaji wenye urefu wa zaidi ya futi 6. Haikushangaza kuona baadhi ya waandishi wa habari za michezo kumpa jina la utani la mwewe.
Mchezaji huyo aliyetokea Klabu ya Bucuresti ya Romania 2007 alikuwa mfungaji bora wa Alqasidiya ya Saudi Arabia na kuiwezesha kupata mafanikio makubwa. Kila alipocheza alikuwa anashangiliwa tangu anapoingia uwanjani na kila anapokuwa na mpira. Siku hizi klabu yake katika mji wa kwao Brazil, kama ilivyokuwa alipokuwa anachezea za Ulaya na baadaye Uarabuni ndio inayovutia watazamaji wengi kuliko nyingine yoyote.

Sababu kubwa ni kwamba mashabiki hufurika uwanjani kwenda kumuona mchezaji huyo mfupi anayecheza kama kiungo mshambuliaji. Kutokana na kuona Elton amekuwa kivutio kikubwa cha watazamaji na kuiingizia klabu mapato mazuri ya viingilio vya watazamaji na biashara, imeamua arudi Arabia na mwaka juzi ilialika wachezaji wafupi na warefu sana ambao ni maarufu kutoka nchi mbalimbali kwa michezo ya maonyesho.
Katika michezo hiyo wachezaji wafupi waliunda timu yao na warefu wakawa na yao. Timu hizo mbili zilikuwa na michezo ya kirafiki katika miji mbalimbali ya Saudi Arabia na kutoa burdani nzuri kwa mashabiki wa kandanda. Miongoni wa wachezaji wafupi walioalikwa na kwenda kucheza Saudi Arabia ni Daniel Alberto Villalva Barrios mwenye urefu wa mita futi 5 na inchi 0.63 wa Argentina ambaye inasemekana ni namba mbili kwa kuwa mchezaji mfupi zaidi duniani ambaye anaichezea River Plate.
Wachezaji wengine walikuwa ni Daniel Alberto Barrios wa Ureno ambaye alistaafu mwaka jana, Jafal Rashed Al-Kuwari aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Qatar na aliwahi kuichezea AC Milan ya Italia, Marcin Garuch ambaye kwa miaka mingi alikuwa katika timu ya taifa ya Poland na Levi Porter wa England aliyechezea klabu mbalimbali vya nchi hiyo na nje.
Katika michezo ile ya wachezaji maarufu wafupi na warefu duniani waamuzi ni wale ambao ni wafupi au warefu sana.
Mwamuzi wa katikati anapokuuwa mfupi, basi wale wasaidizi wake wa pembeni wanakuwa ni warefu na anapokuwa mrefu sana basi wasaidizi wake wa pembeni wanakuwa wafupi.
Waamuzi wote walikuwa ni wale wa kimataifa. Kivutio kingine katika michezo ile ya maonyesho ya aina yake ni kwamba palikuwepo aina tofauti ya viwango vya malipo vya kuangalia mchezo. Watoto wale ambao urefu wao ulikuwa ni wa chini ya futi 5 na inchi 4, waliozidi futi 6 na watu wenye ulemavu walilipa nusu ya viingilio kuangalia michezo ile.
Michezo hii maalumu ya maonyesho ilivutia watazamaji wengi kutoka nchi za nje na hasa zile zilizokuwa jirani na Saudi Arabia. Hivi sasa Qatar inafikiria kufanya mashindano kama hayo ya wachezaji warefu na wafupi. Huu ni ubunifu mwingine katika kuufanya mchezo wa kandanda kuwa wa kupendeza na kuvutia mashabiki wengi.

Baadhi ya kampuni zimetengeneza filamu maalumu ya michezo ile ya aina yake ambayo ilikuwa ya kwanza kufanyika duniani.
Kampuni mbalimbali za kimataifa pia zinajiandaa kudhamini michezo ya wachezaji wafupi wa kimataifa wanaotaka kuunda chama chao cha kandanda ili kusaidia wachezaji wenzao wafupi katika nchi masikini.