Ballon d’Or 2025 ipo kwa watu hawa

Muktasari:
- Baada ya kushuhudia mshindi mpya kwa mwaka 2024, wakati kiungo wa Manchester City, Rodri alipombwaga Vinicius Jr na kunyakua tuzo hiyo, mwaka huu ushindani umeripotiwa kuwa mkali kwelikweli. Bahati mbaya, Rodri, amekosa fursa ya kutetea tuzo yake baada ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na kwa majeruhi, lakini jambo hilo limewaibua wakali wapya wanaochuana.
LONDON, ENGLAND: KAMA ulidhani ushindani wa Ballon d'Or haupo tena baada ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kuondoka utakuwa umejidanganya sana, tuzo hiyo haijawahi kudoda.
Baada ya kushuhudia mshindi mpya kwa mwaka 2024, wakati kiungo wa Manchester City, Rodri alipombwaga Vinicius Jr na kunyakua tuzo hiyo, mwaka huu ushindani umeripotiwa kuwa mkali kwelikweli. Bahati mbaya, Rodri, amekosa fursa ya kutetea tuzo yake baada ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na kwa majeruhi, lakini jambo hilo limewaibua wakali wapya wanaochuana.
Msimu wa 2024-25 hauna michuano mikubwa ya soka la kimataifa, hivyo tuzo ya Ballon d'Or itatolewa kwa kuzingatia viwango vya wachezaji walivyovionyesha kwenye klabu zao.
Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya mastaa 10 wenye nafasi kubwa ya kunyakua tuzo hiyo kwa mwaka huu na kuondoka na Mpira wa Dhahabu.

10. Robert Lewandowski (Straika, Barcelona)
Msimu huu 2024-25: Mabao 42, asisti 5
Baada ya Lewandowski kutokuwamo kwenye orodha ya wanaowania Ballon d’Or kwa mwaka 2024, ilionekana zama za mchezaji huyo kufanya kweli na kushinda tuzo hiyo ya Mpira wa Dhahabu zimefika ukingoni, lakini mwaka huu kila kitu kimebadilika na kuwamo kwenye orodha ya wanaoweza kubeba tuzo hiyo. Barca kwanza imeshachukua ubingwa wa Copa del Rey na Supercopa de Espana na kwa msaada wa mabao yake na asisti, klabu hiyo ya kocha Hansi Flick ipo kwenye nafasi nzuri ya kunyakua taji la La Liga, kitu ambacho kitampa nafasi kubwa straika huyo mwenye umri wa miaka 36 kuweka historia ya kunyakua tuzo hiyo ya Ballon d’Or huku kutolewa kwa Barca kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kumemtibulia sana mipango.

9. Lautaro Martinez (Straika, Inter)
Msimu huu 2024-25: Mabao 25, asisti 8
Siku chache zilizopita, Inter Milan ilikuwa kwenye uwezekano wa kushinda mataji matatu msimu huu baada ya kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Coppa Italia na ilikuwa ikiongoza msimamo wa Serie A. Lakini, baada ya vipigo vitatu mfululizo, Inter iling’oka kileleni na kuwaachia Napoli kwenye kinyang’anyiro cha kuwana taji la Scudetto msimu huu, huku kwenye Coppa ilitupwa nje na mahasimu wao AC Milan. Jambo hilo lilimtibulia Lautaro Martinez kwenye mchakamchaka wa kuwania tuzo ya Ballon d’Or, licha ya Inter kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuisukuma nje ya michuano hiyo Barcelona kwenye hatua ya nusu fainali. Endapo kama kikosi hicho cha Simone Inzaghi kitashinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Lautaro atajiweka pazuri.

8. Kylian Mbappe (Straika, Real Madrid)
Msimu huu 2024-25: Mabao 36, asisti 5
Supastaa Kylian Mbappe hakuanza maisha yake vizuri Real Madrid msimu huu tofauti na mashabiki walivyotarajia, lakini ndani ya uwanja amekuwa akifunga mabao kama anavyotaka. Alifunga hat-trick dhidi ya Manchester City, Februari mwaka huu na amefunga mabao ya kutosha akiwa na kikosi hicho cha Bernabeu na kumfanya kuwa kwenye orodha ya mastaa ambao wanaweza kushinda tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu. Endapo kama Real Madrid itamaliza msimu huu ikiwa imebeba taji la La Liga, hilo litamfanya Mbappe aanze kufikiriwa kwa ukaribu na wapiga kura kwenye tuzo hizo za Mpira wa Dhahabu, huku jukumu lake alilonalo mbele yake ni kuhakikisha Madrid inashinda El Clasico.

7. Harry Kane (Straika, Bayern Munich)
Msimu huu 2024-25: Mabao 41, asisti 12
Hatimaye, straika Harry Kane amemaliza gundu la kubeba taji kubwa kwenye maisha yake ya soka baada ya kunyakua ubingwa wa Bundesliga akiwa na kikosi cha Bayern Munich msimu huu. Kane amekuwa straika hatari sana kwenye kufunga mabao, lakini kwa kipindi chote hicho pamoja na kuwa balaa kwa kufunga mabao, alikuwa hajawahi kushinda ubingwa wowote hadi hapo Bayern Munich ilipompa hadhi ya kuwa bingwa msimu huu. Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, mambo hayakuwa matamu kwa wababe hao wa Ujerumani baada ya kukomea kwenye hatua ya robo fainali mbele ya Inter Milan, lakini kiwango chake cha uwanjani kunampa nafasi ya kuwa kwenye orodha ya wanasoka wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda Ballon d'Or mwaka huu.

6. Pedri (Kiungo, Barcelona)
Msimu huu 2024-25: Mabao 6, asisti 8
Barcelona imekuwa tishio ndani ya uwanja msimu huu na sifa nyingi zikienda kwa wakali kama Lamine Yamal na Raphinha, lakini unaambiwa Pedri ndio ubongo wa timu hiyo inayonolewa na kocha Hansi Flick. Akiwa injinia mkuu wa mipango ya Barcelona kutokea kwenye eneo la katikati ya uwanja, Pedri amefanya hilo kwa mifano pia baada ya kufunga mabao sita na kuasisti mara nane, huku akiisaidia timu hiyo kushinda taji la Copa del Rey na lile la Supercopa de Espana. Bahati mbaya Barcelona imekomea kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini endapo kama itafanikiwa kushinda ubingwa wa La Liga hilo litamfanya kiungo huyo wa Kihispaniola kujiweka pazuri kwenye orodha ya wakali wenye uwezekano mkubwa wa kubeba Ballon d’Or mwaka huu.

5. Mohamed Salah (Winga, Liverpool)
Msimu huu 2024-25: Mabao 36, asisti 24
Liverpool haikufanya vizuri sana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu baada ya kutupwa nje kwenye hatua za chini za mtoano, lakini kwa supastaa wao, Mohamed Salah amekuwa na msimu mzuri kwenye michuano hiyo na ile ya Ligi Kuu England. Mabao yake yamekuwa na faida kubwa kwenye kikosi hicho cha kocha Arne Slot na kufanikiwa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu ikiwa bado na mechi kadhaa mkononi. Kitendo cha Liverpool kupoteza mbele ya Newcastle kwenye fainali ya Kombe la Ligi, kisha kukomea hatua ya mtoano ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya imemnyima Mo Salah fursa ya kuwa mchezaji mwenye uwezekano mkubwa wa kwenda kushinda tuzo ya Ballon d'Or ili kuweka rekodi nyingine kwa wanasoka wa kutoka Afrika.

4. Gianluigi Donnarumma (Kipa, PSG)
Msimu huu 2024-25: Clean Sheets 12
Wakati ikifika miaka 62 tangu Lev Yashin alipokuwa kipa wa kwanza kushinda tuzo ya Ballon d’Or, kuna imani kubwa tuzo hiyo mwaka huu ikabebwa na kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnaruma kutokana na kile anachokifanya uwanjani. Kipa huyo tayari ameshaisaidia PSG kushinda mataji ya Ligue 1 na Trophee des Champions msimu huu, huku akiifikisha kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, akifanya kazi kubwa golini. Donnarumma akiiwezesha PSG kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, hilo litamweka kwenye wakati mzuri kabisa wa kuchomoza kwenye mchakato wa tuzo ya Ballon d’Or na kuwa kipa wa pili kuweka rekodi hiyo, endapo kama atashinda.

3. Raphinha (Winga, Barcelona)
Msimu huu 2024-25: Mabao 37, asisti 25
Kuna ambao walikuwa wanapinga mwanzoni mwa msimu, lakini hadi sasa wameshaona kile ambacho Raphinha amekifanya ndani ya uwanja kiasi cha kumfanya awemo kwenye orodha ya wakali wenye nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu. Ukiweka kando mabao na asisti zake zilizoisaidia kwa kiasi kikubwa Barcelona msimu huu, ameiwezesha pia timu hiyo kushinda mataji mawili Copa del Rey na Supercopa de Espana. Kilichopo mbele yake ni kuiongoza timu hiyo kushinda ubingwa wa La Liga ili kujiweka pazuri baada ya timu ya Barcelona kukwama kwenye hatua ya nusu fainali katika mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilipotupwa nje na Inter Milan. Uzuri kwenye mechi mbili za nusu fainali, zote Raphinha ametikisa nyavu.

2. Lamine Yamal (Winga, Barcelona)
Msimu huu 2024-25: Mabao 16, asisti 25
Hakuna mchezaji aliyewahi kushinda Ballon d’Or kabla ya kufikisha umri wa miaka 21 kwa karibu miaka 70 ya kufanyika kwa tuzo hiyo na sasa, staa wa Barcelona, Lamine Yamal anaweza kwenda kuvunja rekodi hiyo. Hadi sasa tayari ameshashinda ubingwa wa Copa del Rey na Supercopa de Espana, hivyo anasaka taji la La Liga baada ya timu anayochezea Barcelona kukomea kwenye nusu fainali katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, ilipotupwa nje na Inter Milan. Yamal ni moja ya wachezaji wanaocheza soka kwa kiwango kikubwa sana msimu huu huku mchango wake wa uwanjani ndio unaompa nafasi ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha kusaka tuzo ya Mpira wa Dhahabu.

1. Ousmane Dembele (Winga, PSG)
Msimu huu 2024-25: Mabao 35, asisti 12
Supastaa huyo wa Ufaransa ameshinda ubingwa wa Ligue 1 na Trophee des Champions. Dembele ni kama amejipata kwa sasa tangu alipohama kutoka Borussia Dortmund kwenda Barcelona. Kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain anachezea kwa sasa, Dembele amekuwa mchezaji muhimu akiipa timu hiyo ubingwa wa Ligue 1 na kuifikisha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ndoto ya PSG msimu huu ni kushinda taji la Ulaya baada ya kuzitupa nje timu ngumu kama Liverpool, Aston Villa na Arsenal na kwenye fainali itakipiga na Inter Milan ya Italia. Taji hilo litampa nguvu ya kutosha Dembele kwenye vita ya kuwania tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu.