Prime
Kinachoendelea kwa watoto wa wanasoka maarufu Rooney, Ronaldo

Muktasari:
- Wao ni Rooney na Ronaldo Part 2. Staili zao wanazocheza kwa namna fulani zinakaribia kulingana na wazazi wao.
LONDON, ENGLAND: WANASEMA mtoto wa nyoka ni nyoka. Na hicho ndicho tunachokisubiri kwa watoto wa masupastaa wa mpira wa miguu, Wayne Rooney na Cristiano Ronaldo.
Wao ni Rooney na Ronaldo Part 2. Staili zao wanazocheza kwa namna fulani zinakaribia kulingana na wazazi wao.
Wakikua kwenye misingi mikubwa ya soka, wote Kai Rooney na Cristiano Ronaldo Junior wameibukia na kuwa moja ya vipaji vichanga matata kabisa kwenye mpira wa miguu.
Hivyo, watoto hao wanaweza kurudisha ule upinzani wa soka la kimataifa waliokuwa nao baba zao, ikiwamo lile tukio lilitokea kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006.
Watoto wao Rooney na Ronaldo wanapiga hatua nzuri kisoka na kuhakikisha wanafikia viwango vya juu kabisa mchezo wa soka.
Jumanne iliyopita, Ronaldo Jnr akicheza timu ya vijana ya klabu anayochezea baba yake huko Saudi Arabia, Al-Nassr aliitwa kwenda kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kwa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 15.

Baba yake kwa furaha kubwa aliandika kwenye mtandao wa kijamii: “Najivunia wewe mwanangu!”
Wakati huo, Kai alifunga bao kwenye dakika za nyongeza kuipa ushindi Manchester United dhidi ya Manchester City kwe-nye michuano ya Kombe la Ligi Kuu England kwa timu za vijana walio chini ya miaka 15 wiki iliyopita.
Baba yake, Wayne aliandika kwenye mtandao wa kijamii: “Najivunia @kairooney.10. Tukio la kibabe la kupindua meza la timu yake na siku zote kufunga bao la ushindi kwenye dakika za nyongeza hiyo ni kitu spesho. Piga kazi mwanangu.”
Hilo limekuja baada ya Kai hivi karibuni kufunga pia bao la jitihada binafsi kwenye kikosi cha Man United chini ya umri wa miaka 17 kilipocheza dhidi ya Real Sociedad ya Hispania licha ya yeye kuwa na umri wa miaka 15 tu.

Hiyo inaonyesha baba zao wote wawili wanaguswa kihisia na vitu vizuri vinavyofanywa na watoto ndani ya uwanja. Changamoto inayowakabili Kai na CR jr ni kukwepa kucheza soka chini ya vivuli vya baba zao, ambao walikuwa hatari na ni magwiji wa soka. Wataweza?
Na sasa wale mashabiki waliokuwa wakiimba “kuna Cristiano Ronaldo mmoja tu” wanapaswa kuacha hilo mara moja baada ya mshindi huyo mara tano wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kuamua kumwinua mwanaye wa kwanza wa kiume wajina wake.
Ronaldo Jnr 14, amekuwa akifanana na baba yake na hata mazoezi pia amekuwa akifanya kama anayofanya mzazi wake huyo ili naye awe na mwenendo wa kibabe.Akizaliwa na mwanamke mmoja wa Kimarekani mwaka 2010, baba yake ambaye ni staa wa zamani wa Real Madrid, Man United na Juventus hajawahi kumtaja hadharani mama mzazi wa mtoto huyo.

Kipindi hicho, Ronaldo aliposti kwenye X: “Ni furaha kubwa na kwa hisia kubwa ningependa kuwapa taarifa kwamba nimekuwa baba wa mtoto wa kiume. Kama nilivyokubaliana na mama wa mtoto, ambaye ameomba utambulisho wake ufichwe na ubaki kuwa siri, mwanangu ataishi chini ya usimamizi wangu.”
Kama ilivyo kwa baba yake, ambaye amepita kwenye klabu kubwa kabisa za Ulaya, mtoto Ronaldo Junior naye atatamani kupitia kwenye nyayo hizo na kuwa mwanasoka mkubwa.
Kwenye chaneli yake ya YouTube mwaka jana, Ronaldo aliposti video iliyokuwa na kichwa cha habari Cris v Cris, ambapo wawili hao walikuwa wakishindana kupiga mipira ya friikikiki kwenye goli na kuweka maelezo, “Nani amepiga vizuri?”
CR7, kama linavyofahamika jina la utani la baba huyo, pengine ni mmoja wa wanasoka bora kabisa wa muda wote, lakini kwenye shindano hilo la kupiga mipira ya friikiki, mtoto Ronaldo alionekana kuwa matata zaidi.

Licha ya kutimiza umri wa miaka 40 tangu Februari mwaka huu, Ronaldo Snr hivi karibuni alikiri kwamba angependa sana kucheza soka la kulipwa sambamba na mwanaye.
“Ningependa sana,” alisema Ronaldo na kuongeza. “Sio kitu kinachoninyima usingizi, lakini ngoja tuone.”
Akifahamika kama Cristianinho ikiwa na maana ya Cristiano mtoto mwanaye Ronaldo alikuwa kwenye timu ya watoto ya Juventus huko Italia.
Kisha, wakati baba yake aliporudi kujiunga na Man United kwa mara ya pili mwaka 2021, mtoto huyo aliungana na baba yake na kwenda kuandikishwa kwenye akademia ya Old Trafford. Cristianinho alipofika kwenye akademia ya Man United, katika kikosi cha wachezaji chini ya umri wa miaka 12 alikutana na mtoto mwenzake fundi wa mpira anayeitwa Kai Wayne Rooney aliyezaliwa Novemba 2009.

Wawili hao walikuwa gumzo baada ya wote kufunga kwenye mechi ya watoto wenzao dhidi ya West Bromwich Albion mwaka 2022.
Mashabiki wa Man United walivuta kumbukumbu ya miaka ya dhahabu, wakati Rooney na Ronaldo walipokuwa wakijitokeza sana kwenye mbao za watikisa nyavu kwenye mechi za miamba hiyo ya Old Trafford.
Baba zao, walibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu England mara tatu wakati walipokuwa pamoja kwenye kikosi cha Man United chini ya kocha Sir Alex Ferguson.
Lakini, mwaka 2006, katika ya pacha yao matata ya uwanjani kulitokea tukio ambalo liliwaingiza wachezaji hao wa timu moja kwenye mgogoro mkubwa. Hiyo ilikuwa wakati England ya Rooney na Ureno ya Ronaldo zilipokutana kwenye robo fainali ya Kombe la Dunia huko Gelsenkirchen, Ujerumani.

Dakika 61 ubao wa matokeo ukisomeka 0-0 Rooney alichezeana rafu na Ricardo Carvalho wa Ureno, ambaye kipindi hicho alikuwa beki wa Chelsea. Rooney alionekana kumkanyaga Carvalho, jambo lililomfanya Ronaldo kumfuata mwamuzi Horacio Elizondo na kumshawishi amwonyeshe kadi nyekundu Rooney.
Rooney alimsukuma mchezaji mwenzake huyo wa klabu moja mbali na mwamuzi, lakini kwa wakati huo refa Elizondo alishafanya uamuzi wa kumwonyesha kadi nyekundu Wazza. Kwenye tukio hilo, Ronaldo alitoa ishara ya kukonyeza kwenye benchi la Ureno kwamba alichokuwa akikitaka kimetimia, Rooney kuonyeshwa kadi nyekundu.
Rooney alitoka uwanjani na kwenda vyumbani, akiicha England na wachezaji 10 uwanjani ikienda kutupwa nje ya michuano kwa mikwaju ya penalti. Sasa, Rooney, 39, aliyewahi kukipiga pia Everton kwa awamu mbili tofauti, alisema tukio hilo ndilo lenye kumbukumbu mbaya zaidi alilowahi kukabiliana nalo kwenye soka.
Hata hivyo, wakati wapo Man United walimaliza tofauti zao ndani ya uwanja na kuendelea kushirikiana kufunga mabao kwenye fowadi ya miamba hiyo chini ya kocha Ferguson.
Kisha Ronaldo aliondoka Man United. Aliporejea tu, bifu lilirudi upya dhidi ya Rooney. Kipindi hicho, Rooney, alikuwa kocha Plymouth Argyle na kufutwa kazi, Desemba 2024. Rooney alimkosoa mchezaji mwenzake wa zamani CR7 baada ya kugomea kufanyiwa mabadiliko kwenye mechi.
Ronaldo kwenye mahojiano yake na Piers Morgan 2022 alisema kuhusu Rooney: “Sijui kwanini amekuwa akinikosoa vibaya sana . . . bila shaka kwa sababu amemaliza maisha yake ya soka na mimi bado nacheza kwenye viwango vya juu. Sitaki kusema kwamba nina mwonekano mzuri kuliko yeye ambao ndio ukweli.”
Kisha Ronaldo alielezea kushangazwa na maneno ya Rooney kwa sababu pacha wake huyo wa zamani kwenye safu ya ushambuliaji ya Man United alimtembelea nyumbani kwake kumchukua mwanaye.
CR7 alisema: “Alikuja hapa nyumbani kwangu, aliwachukua wanaye na kumwalika Cristiano (Junior) waende nyumbani kwake kucheza mpira.
“Huwa siwaelewi watu wa aina hiyo. Au kama wanataka wawe kwenye kurasa za juu kwenye magazeti au wanataka kazi mpya au vinginevyo.”
Je, Ronaldo Jnr na Kai siku moja wanaweza kurudisha bifu kali la uwanjani kama ilivyokuwa kwa wazazi wao wakati England itakapokipiga na England?
Kama ilivyokuwa kwa Ronaldo, Kai naye amekuwa na kiwango bora uwanjani. Mashabiki wa Man United walipendezwa na aina ya bao alilofunga dhidi ya Real Sociedad, ambapo shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa kijamii: “Anacheza kama baba yake, ni msumbufu na anatumia nguvu.”
Mama yake Kai, mrembo Coleen, 39, alifichua kwamba kuna ugumu fulani kuwa baba mwanasoka maarufu. Inaelezwa kwamba Kai amekuwa akichukizwa pindi makipa wa timu pinzani wanapomtolea maneno kuhusu mambo ya nje ya uwanja ya baba yake. Kutokana na hilo, kwa mujibu wa Coleen ni kuwa Kai amemzuia baba yake kwenda kwenye mechi zake za soka la watoto ili kumpa uhuru na kutokana na hilo, Wayne huwa hatazami mechi anazocheza mwanaye.”
Mwaka jana Kai alisaini mkataba wa udhamini wa Puma na baadaye alionekana kwenye picha ya tangazo la nembo hiyo ya viatu sambamba na Dua Lipa na Kyle Walker. Kama ilivyo kwa Ronaldo Jnr, Kai naye atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanalifikisha soka kwenye anga za juu kabisa kama ilivyokuwa kwa baba zao. Wataweza?