Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna cha kujifunza kwa kina Mukoko, Bangala

Kuna cha kujifunza kwa kina Mukoko, Bangala

UNAMKUMBUKA kocha wa zamani wa Azam FC, Mbrazil, Neidor dos Santos?

Kocha huyu aliwahi kuinoa Simba na baadaye Azam FC aliwahi kukaririwa akisema katika soka la Tanzania, kuna wachezaji wana namba zao za kudumu.

Alisema hivyo, akiwatolea mfano Wabrazili wawili waliokuwa wakiitumikia timu ya taifa ya nchi yao, Ricardo Izecson dos Santos Leite maarufu kama Kaka na Juninho Pernambucano.

Kaka alikuwa akimweka benchi, Juninho katika timu hiyo. Neidor dos Santos alisema siku Kaka akipata dharula na Juninho kupewa nafasi basi mchezaji huyo hatapata tena nafasi mpaka pale Juninho naye atakapopata dharula.

Kocha huyo alifafanua wachezaji hao hawakai benchi kizembe. Wanajiandaa kusubiri nafasi itokee ili waonyeshe kile walichonacho miguuni mwao.

Ikitokea yule anayepata nafasi akakosa mchezo mmoja, basi atakuwa kuwa na kibarua kigumu kumtoa aliyechukua nafasi yake. Kwani ataitendea haki nafasi hiyo kwa kiwango stahiki.

Kiwango chake kitampumbaza kocha na kuamini aliyeko uwanjani ndiye anayestahiki kuitumikia timu hiyo.

Jambo kama hilo tumeliona kwa wachezaji wawili wa Yanga ya Dar es Salam, Yanick Bangala na Mukoko Tonombe. Kumbuka Mukoko alimaliza msimu akiwa na kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya straika wa Simba, John Bocco katika mchezo wa Fainali wa Azam Sports Federation Cup kule Kigoma.

Kadi hiyo ilimfanya akose mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya NBC wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na michezo mingine miwili ya ligi hiyo.

Ndipo Bangala aliyesajiliwa kuja kucheza kama beki wa kati akitarajiwa kuwa pacha wa Mwamnyeto akasogezwa juu kucheza kama kiungo mkabaji kuziba nafasi ya Mukoko. Hapo Dickson Job akacheza kwenye nafasi yake ya beki akiwa pacha na Mwamnyeto.

Hawa wote watatu, Bangala, Job na Mwamnyeto walijua kuwa kurudi kwa Mukoko baada ya kumaliza adhabu yake kutahatarisha nafasi zao. Hakuna aliyefanya makosa na kuja kuwa mhanga wa mchezaji huyo wa kimataifa wa DR-Congo. Viwango walivyovionyesha vilimfanya hata Kocha wa Yanga, Nasrudeen Nabi kushindwa kumrudisha Mukoko kwenye nafasi yake.

Na hakuna hata shabiki mmoja wa Yanga aliyelalamika kwanini Mukoko hachezi! Achana na maneno ya mashabiki wa mpira wetu (Simba na Yanga), kuwa eti Mukoko alikosa namba kwa kuwa alihujumu mechi ya Simba na Yanga kule Kigoma kwa kumchezea rafu ya makusudi Bocco. Eti ndio sababu iliyomfanya akose namba kikosini. Sio ya kweli hayo.

Hebu jaribu kuvaa viatu vya Nabi, nani ungemuacha benchi kati ya Bangala, Job na Mwamnyeto ili Mukoko acheze? Hakuna mtu yeyote anayeweza kuja na jibu tofauti na la Nabi ikiwa wenzake hao watatu wako katika utimamu wa mwili.

Jaribu kujiuliza tena, kwanini kati ya wachezaji hao watatu mmoja alipokosekana pengo lake halikuzibwa na Mukoko? JIbu liko wazi, mchezaji mzuri ni yule anayekubali kujifunza kwa yule anayemuweka benchi.

Hapa namkusudia Zawadi Mauya ambaye amekuwa chaguo la pili inapotokea nafasi kati ya wachezaji hao watatu yaani Bangala, Job na Mwamnyeto kama mmoja wapo atakosekana.

Kama atakosekana Mwamnyeto au Job, Kocha Nabi atamshusha Bangala kuchukua nafasi ya mmoja wapo na Mauya atacheza kiungo wa chini.

Mauya bado hajafikia asilimia 100 ya uchezaji wa Bangala ambao umeleta utulivu ndani ya Yanga baada ya kuondoka wachezaji Athumani Idd ‘Chuji’ na Papy Kabamba Tshishimbi.

Uwezo wa Bangala wa kunyang’anya mipira, kuificha na kupiga pasi fupi na ndefu unaifanya Yanga kuwa timu yenye utulivu katikati katika msimu huu. Bahati mbaya sana Mukoko hakuwa na vitu kama hivi zaidi ya kunyang’anya mipira.

Mukoko hakuweza kuifanya Yanga iwe na utulivu katikati ya uwanja msimu uliopita. Kwa ligi kama yetu yenye idadi maalumu ya wachezaji wa kigeni, ndipo Kocha Nabi alipoamua kutumia akili ya kiufundi kwa kumtengeneza Mauya kama mbadala wa Bangala.

Hapo ndipo ilipomlazimu Mukoko kuondoka kwa maslahi ya Yanga kuepuka kukaa benchi akiwa mchezaji wa kigeni akisubiri dharula itokeee. Uamuzi huo pia ni kwa maslahi ya Mukoko ambaye amekuwa akiitwa katika Timu ya Taifa ya DR Congo.

Nini cha kujifunza kwa wachezaji wetu? Tuchukulie mfano, Kiungo wa Simba, Jonas Mkude anaumia. Kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anaumia na kuna watu wanacheza nafasi zao. Hata wakipewa kucheza nafasi hizo, hawawezi kuvaa viatu vya wachezaji hao.

Mashabiki nje wanapiga kelele kwa wachezaji waliongia kama mbadala wa wachezaji hao wakiona tofauti kubwa kati yao.

Mbaya zaidi, kocha anaomba wachezaji walioko kwenye majeraha warudi awapange kwenye nafasi zao. Ndipo pale Kocha wa zamani wa Azam FC, Neidor dos Santos akasema Tanzania kuna wachezaji wana namba zao.

Rejea pale Msimbazi, Clatous Chama aliondoka Simba kwenda RS Berkane ya Morocco akiwa mchezaji wa kikosi cha kwanza.

Akiwa huko alikutana na changamoto zilizomlazimu arejee nchini. Kwelie akarudi na kutua tena Simba katika namba ile ile aliyoiacha wakati anaondoka.

Chama ameendelea kuwa mchezaji tegemeo wa Simba, yaani ndani ya miezi sita hakukuwa na mchezaji aliyefikia kiwango chake. Kifupi ni kwamba hakukuwa na mbadala wa Chama, ndio maana mabosi wa Msimbazi walipambana kumrejesha tena kikosini na sasa wala hawajilaumu.