Kumbe Msuva anaipa madini Yanga

Thursday September 09 2021
msuva pic
By Khatimu Naheka

BAADA ya kuona sehemu ya tatu ya mahojiano na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva kuhusu maisha yake na mchumba wake ambaye ameishi naye kwa miaka 10. Sasa tunaingia sehemu ya mwisho ya mfululizo huu. Twende pamoja.


MAISHA NA KIBABAGE

Msuva akiwa Difaa kabla hajajiunga na klabu yake ya sasa ya Wydad Casablancaalijikuta akikutana na beki kinda wa kushoto, Nickson Kibabage ambaye hata hivyo ameshaondoka Morocco akirudi nyumbani. Hapa anaeleza maisha yao yalivyokuwa ndani ya nchi hii.

“Maisha yetu na mdogo wangu Kibabage yalikuwa mazuri sana, ilikuwa ni kama kaka na mdogo wake wa familia moja. Ni mchezaji mzuri sana ambaye atakuja kuwa na faida kubwa kwa taifa. Ana kipaji sana na anajua mpira, lakini bado anahitajika kuendelea kutafuta uzoefu zaidi,” anasema Msuva.

“Alipofika huku alikuwa amepewa nyumba, lakini baadaye nikamwambia atoke kule aje tukae wote kwangu wakati huo nikiwa Difaa, ila nilimwambia ile nyumba asiirudishe sababu ya kufanya hivi ni kwamba muda mrefu nilikuwa naye pamoja, tunaamshana kwenda mazoezi binafsi.

Advertisement

“Kibabage ana kipaji, lakini pia kitu kilichonivutia mpaka nikaamua kukaa naye ni usikivu wake, isingekuwa usikivu nisingekaa naye. Nilikuwa namuamsha alfajiri twende tukafanye mazoezi, mwanzo alikuwa anaona ngumu analalamika kaka Saimon unajua bado sijapumzika namwambia achia shuka tuondoke mpaka alizoea. Nilikuwa namkumbusha jinsi ya kuishi kwa malengo na kujituma.

“Baada ya mimi kuondoka Difaa naye aliondoka akaenda klabu nyingine ya hapa kwa mkopo, bahati mbaya nako hakuwa anapata nafasi sana, kuna wakati mbaya zaidi hata benchi hakai wakamrudisha timu ya vijana chini. Sasa hizo changamoto kutokana na umri wake alishindwa kupambana nazo.

“Nilikuwa namuita nakaa naye na hapa namfariji, nampa moyo, tunabadilishana mawazo kwa kuwa hiyo klabu na hapa kwangu sio mbali sana. Ni kama umbali wa nusu saa tu - akija hapa analia nikaona itampa shida akawa na mawazo ya kurudi nyuma, yaani arudi nyumbani akajipange tena hata kwa mwaka mmoja nikaona sio kitu kibaya.”


AVUNJA MKATABA

Msuva anasema maisha yake na Kibabage yalivutia kutokana kila mmoja kuwa hodari katika kupika chakula chake, lakini beki huyo alikuwa balaa katika upishi wa mboga.

“Maisha yangu na Kibabage nitayakumbuka sana. Nilikuambia awali kwamba mimi sijui kupika sana, nilikuwa najua kupika ugali na wali kidogo, lakini mwenzangu alikuwa anajua sana kupika wali na zaidi dogo alikuwa anapika sana mboga,” anasema.

“Tukawa tunagawana mimi nikipika ugali, basi yeye anapika mboga na akipika mboga unafurahi unasema ndio hii ni mboga iliyopikwa, kwa hiyo maisha yetu yalikuwa na sura flani hivi ya ushirikiano kama kaka na mdogo wake. Sasa amerudi nyumbani, kuna kitu nikuambie watu wasimdharau mtu aliyeamua kurudi nyumbani hawajui amekutana na changamoto zipi, kitu cha muhimu ni kujua unarudi nyumbani ukiwa na malengo gani.

“Kibabage baadaye alivunja mkataba wake na Difaa na nasikia alirudi kujiunga na KMC. Sio kitu kibaya jambo la msingi anatakiwa kwenda kuishi kwa malengo. Kama ambavyo nilikuambia jambo zuri bado yuko katika timu za taifa za vijana na wakubwa na atakuwa karibu na makocha watamuona kama ataheshimu malengo yake, akitambua kilichomkwamisha sasa atakuja tena huku au zaidi ya huku.”


DANSA BONGOFLEVA

Kama ulikuwa hufahamu, Msuva aliwahi kuwa dansa katika kundi la madansa Bongo na hapa anaeleza kwamba bado anafuatilia kipaji hicho, ingawa sasa hafanyi sana labda awe anajichezea mwenyewe nyumbani.

“Asili ipo haiwezi kutoka kirahisi, unajua nilifanya kwa muda kidogo. Bado nakumbuka kucheza muziki, lakini hata sarakasi si unajua nazo nilicheza sana huko nyuma. Bado najaribu kuzikumbuka, huwa kama najikuta nina mawazo basi nitafanya kimoja kati ya hivyo,” anasema.

“Nitasikiliza muziki au nitacheza na wakati mwingine nitatoka hapo nje nitaruka sarakasi zangu maisha yanaenda.”

Katika mahojiano na Mwanaspoti muda wote televisheni yake ilikuwa inapigwa ngoma kali za Bongofleva kudhihirisha kwamba jamaa hasahau kile anachokipenda na hapa anaeleza anavyofuatilia muziki huo wa nyumbani.

“Unajua muziki upo katika damu yangu, nafuatilia muziki wa nyumbani kama kawaida. Shida yangu napenda muziki, lakini sio mpenzi wa kwenda disco, huwa napenda kusikiliza na wakati mwingine kucheza kidogo, bado nawasiliana na wanamuziki wengi wa nyumbani kina Jux hawa tunachati,” anasema.

“Wananipa moyo niendelee kupambana. Kuna wakati wakitoa wimbo mpya wananijulisha au mimi mwenyewe nakutana nazo tu mitandaoni. Nafurahi kuona wanazidi kupiga hatua nawafuatilia sana kina Rayvany, Rich Mavoko, Mbosso, Bilnass, Lavalava, Aslay, Diamond, Ali Kiba hadi kinadada hawa Lina na wengine kiukweli nafarijika kuona vijana wenzangu wakifanya kitu wanachokipenda.”


VIPI KUHUSU JAMES?

Saimon ana mdogo wake anayecheza soka anaitwa James Msuva ambaye hajafanya makubwa kama ilivyo kaka yake na hapa anaeleza kinachomsibu.

“James buana anajua mpira sana, sema amekosa bahati. Hapa kati amepotea sana alikumbwa na majeraha ya nyama, unajua huu ndio ugonjwa mgumu kupona na bahati mbaya zaidi umemuanza akiwa bado mdogo. Nilihangaika naye sana kuna wakati nilikuja naye mpaka huku ila amepona ingawa bado hajakaa sawa,” anasema.

“Ukipata tatizo la nyama unatakiwa upumzike sana na ndicho alichokifanya, naamini baada ya muda watu watamuona James mpya mwenye juhudi mpya uwanjani. Bado anatakiwa kujituma zaidi haitakuwa rahisi kung’ara ila akipambana watu wataona kipaji chake.”


ANAIPA YANGA VITU

Msuva anamalizia kwa kuelezea anavyoshirikiana na viongozi wa Yanga kuwashauri mambo mbalimbali baada ya kupotea katika ramani ya soka la Afrika, lakini pia akiwapongeza Simba kwa kutisha miaka minne Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu.

“Yanga unajua ni klabu ambayo nimetoka na viongozi wao wananithamini. Naongea nao wengi, wanaomba ushauri na nawashauri. Kuna hasa naongea sana na Mhandisi Hersi alipokuja hata hapa alinifuata na tukaongea, kuna mambo alitaka nimshauri nikafanya hivyo,” anasema.

“Naona sasa wamefanya usajili mzuri, naamini safari hii watarejea na nguvu katika mashindano ya Afrika. Nafuatilia sana ligi ya Tanzania hata Simba nawapa pongezi sana wamekuwa na timu bora sana miaka hii minne wamechukua mataji ya ndani na hata Afrika wanafanya vizuri, Azam nao naongea nao yule Popat (Abdulkarim) naongea naye sana, nafuatilia ligi.”


ASANTE YANGA

Akiizungumzia zaidi Yanga, Msuva anaishukuru kumfungulia njia.

“Mwisho wa siku juhudi zangu zililipa mashabiki walewale ndio waliokuja na viroba vya mchele na pesa kunipongeza nilipofanya vizuri, nilifanyia kazi kipi makocha wananiambia na nilitambua mashabiki wao wanataka kitu kizuri. Kufika hapa lazima niishukuru sana Yanga, iliniokoa maisha yangu kufika kwangu hapa, ni matunda ya maisha yangu na Yanga,” anasema Msuva.

Advertisement