Kisubi hana hofu Simba, bao la Ajibu bado lamtesa

UMAHIRI wa kipa Jeremiah Kisubi, ndio sababu ya viongozi wa Simba kunasa saini yake ili kuongeza changamoto kwa makipa wao wengine Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim.

Simba imemsajili Kisubi kutoka Tanzania Prisons, alikokuwa kipa namba moja na anakutana na mwenyeji wake, Manula ambaye ni panga pangua kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Didier Gomes.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na kipa huyo, ambaye amefunguka mengi namna alivyojipanga kuleta ushindani ndani ya kikosi hicho.


USHINDANI SIMBA

Anasema hajajiunga kwa bahati mbaya Simba, anatambua ni timu yenye ushindani kila idara na kazi yake ni kucheza, hivyo amekwenda kuwajibika na sio jambo lingine.

“Najua kuna ushindani, sio jambo geni kwangu, kazi yangu ni kucheza na nimekuja kufanya kazi, ushindani unainua viwango, hivyo ni jambo zuri kushindana,” anasema.

Anasema hajawahi kuwa na hofu kwenye majukumu yake, anaamini anachokifanya na anatambua Simba yupo kwa ajili ya ushindani.

Mbali na hilo, anasema Simba ina presha zaidi kuliko Prisons, lakini hashindwi kukabiliana na mazingira ya aina mbalimbali katika kazi zake.

“Prisons ni timu yenye ushindani mkubwa ila haina presha, Simba presha yake inatokana na mashabiki, sina budi kuendana na hali halisi ya timu,” anasema.


AJIBU AMFUNGA BAO BORA

Bao bora lililobaki kwenye kumbukumbu zake, akiwa kipa wa Ndanda FC msimu wa 2017/18, anasema alifungwa na Ibrahim Ajibu akiwa Yanga.

“Ajibu alinifunga bao la akili sana, mpira ulipigwa na Juma Abdul asingegusa mtu ungepaa juu, Ajibu akalenga pasi iliyozitikisa nyavu zangu, kiukweli ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana,” anasema.


BAO LA KIZEMBE

Anasema msimu wa 2018/19 akiwa Kagera Sugar, alifungwa bao la kizembe na aliyekuwa straika wa Azam FC, Donald Ngoma aliyepiga pasi nyepesi aliyoshindwa kuiokoa.

“Nina kawaida ya kuangalia marudio ya kazi zangu, ndipo niligundua nilifungwa kizembe, kwani nilikuwa najaribu kumpiga chenga Ngoma nikafeli, ndipo akatumia nafasi hiyo kuniadhibu, hilo lilinifunza kuongeza umakini zaidi,” anasema.


SOKA LIMEMPA MWANGA

Anasema japokuwa hawezi kuyaweka wazi mambo yake, ila soka limempa mwanga kutokana na baadhi ya maendeleo aliyoyafanya yametokana na kazi hiyo.

“Yapo mambo niliyoyafanikisha kupitia soka, ingawa siwezi kutaja kimoja baada ya kingine, licha ya kwamba bado soka naendelea kulidai,” anasema.


ATASOMEA UCHUNGAJI

Kitu anachotamani kukifanya baada ya soka ni kwenda kusomea uchungaji ili kupata mwongozo wa kuifanya kazi ya Mungu.

“Mkoani kwetu Kigoma nilikuwa nahubiri neno la Mungu, baada ya soka nitakwenda kusoma uchungaji na Mungu anisaidie maana ni kila kitu kwangu,” anasema Kisubi na anaongeza;

“Katika kazi zangu, Mungu ni wa kwanza, naomba ndipo nakwenda kufanya majukumu yangu, nimeona ukuu wa Mungu kwenye maisha yangu kwa ujumla,” anasema.


KINACHOMUUMIZA

Anasema kama kuna kitu kinachomuumiza ni kupoteza wazazi wake wote, kuna nyakati anazowakumbuka katika mambo mbalimbali ikiwemo ushauri.

“Mama yangu alifariki miaka mitano iliyopita, baba yangu kafariki mwaka huu, jambo hilo linaniumiza kila ninapowakumbuka, kwani upendo wao ulikuwa mkuu sana,” anasema.


NENO LA WADAU

Kocha wa makipa wa KMC, Fatuma Omary anasema timu yenye ushindani kila idala inakuwa na uhakika na matokeo.

“Ushindani wa makipa ndani ya kikosi cha Simba unafanya wachezaji kuwa makini kila wanapopewa nafasi ya kucheza, kila mmoja anatakiwa kupambana kwa nafasi yake bila kuhofia mtu mwingine,” anasema.

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Ally Pazi Samatta anasema ushindani unajenga timu kuwa imara, kupata matokeo na kujilinda, anachokishauri kwa makipa hao ni kila mmoja ajitume kwa kadri anavyoweza. “Penye ushindani pana kiwango kikubwa, makipa waliopo Simba wanatakiwa kushindana kwa kadri wawezavyo ili kumpa kazi kocha kuamua nani amuanzishe ama mmoja anapopata dharura pengo linazibwa na mwingine,” anasema.