Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachoiponza Yanga chaanikwa hadharani

Yanga Pict
Yanga Pict

Muktasari:

  • Hii tofauti na mpinzani wake, Florent Ibenge, ambaye uzoefu wake katika mechi kubwa, ulimsaidia kuimaliza Yanga kirahisi.

KABLA ya kuingia kwenye mechi ya Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika juzi ambayo Yanga ililala 2-0 nyumbani Kwa Mkapa dhidi ya Al Hilal ya Sudan, kocha mpya wa timu hiyo ya Jangwani ambaye hana uzoefu wa mechi za kimataifa, Sead Ramovic, ameonekana hakujua tatizo sugu la timu hiyo ya Jangwani msimu huu.

Hii tofauti na mpinzani wake, Florent Ibenge, ambaye uzoefu wake katika mechi kubwa, ulimsaidia kuimaliza Yanga kirahisi.

Ramovic ameonekana hakutarajia kama Ibenge angelipanga jeshi lake kimkakati  -- kutoshindana na Yanga katika kupiga pasi. Lakini Ibenge ni mzoefu, alijua hilo lingekuwa kosa kubwa kwake. Kwenda mbele mfululizo kutafuta mabao, kungeacha wazi maeneo makubwa ya viungo waliojaa ufundi na akili ya kumsambaratisha mpinzani kama Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Clatous Chama, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya kuonyesha vipaji vyao vya soka.

YA01
YA01

Badala yake, wachezaji wa Ibenge tangu mapema mwanzoni mwa mechi walionekana kuchelewesha mchezo, hapakuwa na aliyekuwa na haraka ya kufanya jambo lolote. Hata mchezaji wa Al Hilal alipogongana na mwenzake alibaki chini kuhakikisha mpira hautembei ikiwa ni mbinu pia ya kuwatoa mchezoni Yanga.

Hii ni kwa sababu Ibenge ni mzoefu, alijua haraka haraka dhidi ya kikosi kilichojaa wachezaji magalactico kama cha Yanga ilikuwa ni kujipalia makaa.

Wachezaji wa Al Hilal walikuwa watulivu na wavumilivu pale walipowaona Yanga wakipasiana tu. Walichofanya ni kuhakikisha wanaziba maeneo muhimu na kuwaachia Yanga maeneo ambayo sio hatarishi.

Uvumilivu wao na subira vilizaa matunda kwa kutumia mashambulizi mawili ya kushtukiza na kufunga mabao mawili kwa kutumia mashuti mawili pekee waliyopiga langoni mwa Yanga. Mashuti mawili, mabao mawili, ilithibitisha soka la kiwango cha juu cha kufuata maelekezo ya kocha mzoefu wa hizi kazi. 

YA02
YA02

Ibenge alithibitisha uzoefu wake dhidi ya Ramovic.

Ramovic alionekana hakutarajia kwamba timu kubwa kama Al Hilal ingecheza mechi kwa kujaza wachezaji katika eneo la kujilinda na kwenda mbele mara chache kwa kushtukiza.


MABAO 17 YAMEWAPONZA

Hiki ndicho ambacho kimeonekana kuisumbua Yanga msimu huu tangu baada ya kuanza kwa kishindo cha kupiga watu mv-ua za mabao.

Katika mechi nne za mchujo wa kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Yanga ilituma ujumbe wa onyo kwa wapinzani.

Ilifunga jumla ya mabao 17-0 katika mechi hizo nne dhidi ya timu mbili (nyumbani na ugenini) wakizichaza Vital’O ya Burundi na CBE ya Ethiopia.

Na hilo lilifuata baada ya timu hiyo kutoka kushinda ubingwa wa Kombe la Toyota nchini Afrika Kusini ambako iliichakaza vibaya miamba ya nchini humo Kaizer Chiefs kwa mabao 4-0 katika mechi ya fainali.

YA03
YA03

Ushindi huo ulikuja miezi kadhaa baada ya Yanga kucheza kwa kiwango cha juu dhidi ya watawala wa soka la Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita (2023-24), ambako kama sio kukataliwa kiutata kwa bao la Aziz Ki, Yanga ingeing’oa timu hiyo inayoogopeka na kwenda nusu fainali.

Mafanikio hayo yalikuja baada ya msimu uliotangulia wa 2022-23, kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako ilifungwa nyumbani 2-1 lakini ikaenda kushinda 1-0 ugenini Uarabuni katika mazingira magumu dhidi USM Alger huko nchini Algeria.

Mafanikio yote haya yalizishtua timu za Afrika na zikataka kuifahamu vyema Yanga, ambayo ikaanza msimu huu kwa kusajili wachezaji wengine wakali kama Clatous Chama, Prince Dube, Isaka Boka, Duke Abuya na wengine kadhaa, walioifanya timu ionekane pengine timu itatisha zaidi ya ilichokifanya hapo nyuma. Na hicho ndicho kilichomsukuma msanii Harmonize kutunga wimbo maarufu wa ‘Yanga Hii Utaifungaje’.


Y04
Y04

KUFUNGWA UJITAKIE

Kwa makocha wazoefu, kufungwa na Yanga hivi sasa, labda ujitakie na hilo ndilo jambo ambalo limekuwa likiisumbua Yanga tangu msimu huu uanze. Na pengine ndilo lililomgharimu kocha Muargentina Miguel Gamondi, aliyefutwa kazi baada ya Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara (1-0 vs Azam na 3-1 vs Tabora United).

Tangu msimu umeanza, Yanga imekuwa ikipata matokeo ya ushindi mwembamba huku wakihoji vilikoenda vipigo vile vya 17-0 vya mechi za mchujo wa kuingia makundi CAF-CL.

Makocha wa upinzani wameonekana kuistukia Yanga. Ni wachache sana ambao wako tayari kujivika mabomu na kushindana nayo katika kupiga pasi.

Watu walimkosoa kocha wa Azam, Rachid Taoussi kucheza kwa ‘kupaki basi’ licha ya Yanga kubaki 10 uwanjani baada ya beki wa timu hiyo ya wananchi, Ibrahim Bacca kutolewa kwa kadi nyekundu mapema kipindi cha kwanza.

Lakini Taoussi alijua – kushindana pasi na Yanga kulimgharimu ajira mtangulizi wake, Youssouph Dabo, ambaye alikula 4-1 na timu yake ilidhalilishwa vibaya katika mechi ya fainali ya michuano ya kufungulia msimu ya Ngao ya Jamii. Taoussi, akaiachia Yanga ikae na mpira, yeye abaki na ushindi, akailaza 1-0 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu kati ya timu hizo.

Hili lilifanywa pia na Tabora United. Licha ya mabeki wote wanne wa kikosi cha kwanza cha Yanga (Bacca, Dickson Job, Yao Kouassi na Boka) kukosekana katika mechi hiyo ya ligi kutokana na sababu mbalimbali na hivyo Yanga kuwachezesha viungo wawili katika safu ya ulinzi (Dennis Nkane na Aziz Andabwile na baadaye Khalid Aucho), bado Tabora iliimaliza Yanga kwa mashambulizi ya kushutukiza na ndicho kilichotokea juzi pia dhidi ya Al Hilal.

Kwa staili hii ya kuiachia Yanga ikae na mpira, kujaza wachezaji katika eneo la ulinzi huku ukiziba tu maeneo muhimu na hivyo kuwatamanisha hadi mabeki wa timu hiyo ya Jangwani wavutike mbele kushambulia na kuacha maeneo makubwa wazi katika nusu yao ya uwanja, ni ishara kwamba Yanga itaendelea kupata matatizo makubwa kama haitabadilisha inachokifanya sasa.


YA05
YA05

KUTIMUA MAWINGA/ USAJILI

Kiasili Yanga ni timu ambayo imekuwa ikitumia mawinga na mara nyingi mastaa wakubwa wa timu hiyo ya Jangwani wamekuwa wakicheza katika nafasi hizo za pembeni za ushambuliaji.

Edibily Lunyamila, Said Maulid ‘SMG’, Mrisho Ngassa, Simon Msuva na wengineo ni mifano ya namna ambavyo Yanga ilikuwa ikitumia sana mawinga wakali katika kurahisisha mambo.

Lakini Yanga ya sasa, imeachana na mawinga baada ya kutoridhishwa na viwango vyao ikiwatema watu kama Jesus Moloko, Tuisila Kisinda, Bernard Morrison,

Mahlatse Skudu Makudubela na wengineo ikimbakisha Dennis Nkane, ambaye sasa anachezeshwa kama beki wa kulia.

Baada ya mafanikio makubwa, Yanga imeonekana kutamani mafanikio zaidi, ikaacha kuutanua uwanja na kujaza washambuliaji wa kati Jean Baleke, Dube, Clement Mzize na Kennedy Musonda ambao wote wanawania nafasi moja pale mbele kati.

Na nguvu kubwa ikatumika kujaza viungo wa ushambuliaji huku eneo la kiungo cha ulinzi na lile la mabeki yakiwa na upungufu.

Kukosekana kwa mrithi wa kiungo wa ulinzi mwenye ubora wa kushindana na Aucho pia ni tatizo jingine.

Barcelona iliyoundwa na kina Lionel Messi, Xavi, Iniesta, Sergio Busquets, Luis Suarez na Neymar, ilitwaa mataji yote na ilikuwa ngumu kushindana nayo kwa pasi. Timu zikagundua mbinu za kuwaachia mpira na kuwafunga kwa kaunta. Wapinzani wa Yanga wanaonekana wamegundua mbinu hii. Barca imerejea katika makali yake msimu huu baada ya kubadili mfumo na kuwatumia mawinga wenye ufundi mkubwa wa soka, Lamine Yamal na Raphinha na sasa ni Barcelona inayoshinda mechi kwa mabao mengi ya kaunta, sio tena yenyewe inayofungwa mabao mengi ya kaunta. Kupanga ni kuchagua.

Kutokana na hali hiyo, kumemuibua nyota wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ ambaye amesema matokeo hayo mabaya viongozi wanapaswa kujitafakari na siyo kumlaumu kocha moja kwa moja.

“Yanga kwa kiwango walichofikia nilitarajia makubwa sana katika michuano ya kimataifa, sasa unapoanza kwa kupoteza nyumbani nadhani ni kitu kimoja kibaya sana. Ukiangalia wachezaji wa Yanga walivyocheza sio kwa kiwango tulichokizoea.

“Kwa matokeo haya sasa viongozi nao wajitafakari, kama waliliondoa benchi la ufundi kwa matatizo mbalimbali, nao wajitafakari tatizo gani linaitafuna timu kwa sasa inashuka. Ukiangalia robo tatu ya wachezaji viwango vyao kila siku vinazidi kushuka. 

“Hapa mwalimu huwezi kumlaumu kwa sababu ni mechi yake ya kwanza, nilitarajia baada ya Miguel Gamondi kuondolewa angalau Yanga ingepata mechi hata moja ya kimataifa ya kirafiki ili kocha awaangalie wachezaji wake lakini haikuwa hivyo, ni wazi wachezaji ndio wamemuangusha mwalimu,” alisema mkongwe huyo.