Kilichomuua gwiji wa Reggae Jimmy Cliff
Muktasari:
- Akiwa kijana nyota tangu miaka ya 1960 alisaidia kuibua sauti ya Jamaica katika hadhira ya kimataifa kupitia vibao maarufu kama Wonderful World, Beautiful People na You Can Get It If You Really Want.
MWANAMUZIKI mkongwe wa reggae duniani, Jimmy Cliff ambaye jina halisi ni James Chambersalifariki Jumatatu, wiki hii, akiwa na umri wa miaka 81.
Akiwa kijana nyota tangu miaka ya 1960 alisaidia kuibua sauti ya Jamaica katika hadhira ya kimataifa kupitia vibao maarufu kama Wonderful World, Beautiful People na You Can Get It If You Really Want.
Alikuwa pia mwigizaji wa filamu akiigiza kama mwasi aliyebeba bunduki katika filamu ya kihalifu 1972 inayoitwa The Harder They Come. Hii likuwa ni msingi wa sinema ya Jamaica iliyoleta muziki wa reggae ndani ya Amerika.
Mke wa Cliff, Latifa Chambers alitangaza kifo hicho kupitia ukurasa wake wa Instagram. Akiandikiwa kuwa “Ni kwa huzuni kubwa kuwajulisha kwamba mume wangu, Jimmy Cliff, amefariki kutokana na degedege baada ya kuugua nimonia.”
Tasnia ya burudani ulimwenguni ilipokea taarifa hiyo kwa masikitiko. Cliff ambaye alizaliwa Julai 30, 1944 mjini St.James, Kingston, Jamaica, ni mmoja wa wanamuziki bora wa reggae wa kiwango cha Boby Marley, Peter Tosh na Gregory Isaac.
Atakumbukwa kwa mafanikio makubwa ikiwamo tuzo ya Grammy 1985 kupitia kibao chake cha Cliff Hanger na 2013 “Rebirth” ambapo alinyakua tuzo ya album bora ya reggae.
Cliff ndiye mwanamziki bora wa reggae aliyekuwa amebaki aliyepata tuzo ya juu ya heshima ya serikali ya Jamaica ijulikanayo kama The Order of Merit ambayo hutolewa kwa ajili ya mafanikio ya sanaa na sayansi. Kwa wale wapenzi wa klabu za hapa Tanzania zinazopiga ‘Old is Gold’ ikiwamo ya sasa The Mars, na zile za zamani East 24 na Mzalendo Pub za jijini Dar es Salaam, mojawapo wa vibao vyake kilichokubalika ni Reggae Night kilichotoka 1983.
Vilevile ana kibao chenye jina la Kiswahili kijulikanacho kama ‘Hakuna Matata’ ambacho ni wimbo katika filamu maarufu ya katuni ya wanyama ijulikanayo kama The Lion King ya 2019.
Umaarufu wake duniani unabebwa zaidi na nyimbo zake zenye maudhui bora katika maisha ikiwamo Many river to cross, I can see clearly now na You can get it if you really want.
Kuonyesha heshima kubwa kwake tangu Jumatatu kurasa nyingi za mitandao ya kijamii zinapiga nyimbo na kuweka picha zake, huku pia kukiwa na idadi kubwa ya wapakuaji wa nyimbo zake.
Kama ilivyoelezwa sababu ya kifo chake ni kutokana na kuugua homa ya mapafu ambayo kitabibu hujulikana kama nimonia, ambapo ilisababisha kupata madhara ya degedege kitabibu yanaitwa seizure.
SABABU WAZEE KUPATA NIMONIA
Katika jicho la kitabibu mtu mzima mwenye umri wa miaka 81 ni kihatarishi kuugua nimonia kali pamoja na kutokea kwa madhara kama degegede au kifafa. Hii ni kwa sababu umri huo kinga ya mwili kuwa dhaifu.
Nimonia ni maambukizi katika mapafu ambapo vifuko vidogo vya hewa vijulikanavyo kama alveoli hupata shambulizi na kujaa maji kisha huvimba. Hali hii inaweza kusababisha madhara na hatimaye kifo.
Sababu wenye umri mkubwa kupata nimonia kali ni kuwa na kinga dhaifu, kuugua magonjwa sugu mengine ikiwamo sukari, magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya kushambulia na kuziba njia ya hewa.
Umri wa miaka 65 + mwili ni kawaida kushindwa kupambana na maambukizi na kadiri umri unavyoongezeka ndivyo pia hatari ya kuugua nimonia na kupata madhara inavyozidi kuwa kubwa.
Watu wenye umri mkubwa huwa ni kawaida kushindwa kumeza vyema na hii inaweza kusababisha nimonia ya kupokea, ambapo chakula au kioevu huingia kwenye mapafu badala ya njia ya chakula.
Sababu za nimonia zinaweza kuainishwa kwa njia mbili ikiwamo kupata baada ya kuwepo katika mazingira ya hospitali na pia kutegemeana aina gani ya kijidudu kinachosababisha ugonjwa.
Vimelea kama bakteria na virusi ndivyo mara kwa mara husababisha tatizo hilo kwa watu wenye umri mkubwa. Ingawa zaidi ni bakteria ndio mara kwa mara husababisha nimonia kwa wazee.
Utafiti wa hivi karibuni nchini MarekanI ulikadiria karibu watu wazima milioni moja wenye umri wa miaka 65 au zaidi hulazwa hospitali wakiwa na nimonia kila mwaka.
CHANZO CHA DEGEDEGE
Inaelezwa Cliff alipatwa na degedege. Hali hiyo huwa ni ongezeko la ghafla la shughuli za umeme kwenye ubongo. Huweza kudumu kwa dakika kadhaa na kusababisha mabadiliko ya muda katika mwenendo, tabia, ufahamu au hisia.
Ingawa degedege mara moja linaweza kusababishwa na mambo kama vile ugonjwa au jeraha. Kwa degedege la kujirudia na kwa muda mrefu hujulikana kama kifafa.
Dalili hutofautiana na zinaweza kuanzia kupinduka macho, kukakamaa, kutetemeka bila kudhibitiwa na kupoteza fahamu.
DALILI ZA NIMONIA KALI KWA WAZEE
Zipo dalili zisizo dhahiri au zisizo maalumu zinaweza kuchelewesha utambuzi na matibabu. Dalili hizo ni kama vile kukosa utulivu, kuweweseka au kuchanganyikiwa. Pia kuwa dhaifu au kuanguka mara kwa mara, homa au joto la mwili kushuka.
Vilevile upungufu wa pumzi au kupumua kwa kasi, kikohozi chenye kohozi, mikoromo wakati wa kupumua, kichomi, maumivu ya kifua hasa wakati wa kupumua. Dalili zingine ni pamoja na kuhara, kukosa hamu ya kula na kushindwa kudhibiti mkojo.
KIPI KIFANYIKE KUZUIA
Je, nini kifanyike kuzuia nimonia kali kwa wazee?
Kwanza ni kuuhakikisha watu wote wanapata chanjo ya kuzuia nimonia na mafua makali ya virusi. Hii itawafanya kuwa na kinga imara.
Kufanya mazoezi mepesi ambayo ni rahisi ikiwamo kutembea, kukimbia kidogo kidogo au mazoezi ya viungo ya nyumbani.
Lishe bora ili kuepuka uzito uliokithiri au unene, wale zaidi mboga mboga na matunda mara kwa mara, wanga usiokobolewa, kuepuka vyakula vyenye sukari nyingi na chumvi nyingi.
Kuwa na miendendo na mitindo mizuri kimaisha ikiwamo kuepuka unywaji wa pombe na matumizi ya tumbaku. Hii itamuepusha na magonjwa yasiyoambukiza.
Kuishi katika mazingira bora yenye hewa yasiyo na msongamano wa makazi wala uchafuzi wa hewa.
Ikumbukwe nimonia inawapata wanapokuwa wamelazwa muda mrefu katika huduma za afya. Hivyo ni muhimu kulinda afya ili kuepuka kuumwa na kulazwa.
Angalau wafanye uchunguzi wa jumla wa afya mara moja kwa mwaka ili kubaini matatizo ya kiafya na kuyadhibiti mapema kabla ya kuleta madhara makubwa.