KIJIWE CHA SALIM… Sunil Gavaskar: Ameondoka na kriketi yake India
Muktasari:
- Hali hii inawasononesha wachezaji mashuhuri waliokuwa miongoni mwa wachezaji bora duniani miaka iliyopita. Hawa ni pamoja na walioiwezesha India kubeba Kombe la Dunia la mchezo wa kriketi mwaka 1983 na 2011.
INDIA ambayo mpaka hivi karibuni ilikuwa miongoni mwa miamba ya kriketi sasa inadorora kama West Indies ilivyoporomoka baada ya kung'ara kati ya miaka ya 1950 na 1980. Siku hizi India ikifanya vizuri kidogo tu katika mashindano ya kimataifa huonekana kama kipofu kaona mwezi.
Hali hii inawasononesha wachezaji mashuhuri waliokuwa miongoni mwa wachezaji bora duniani miaka iliyopita. Hawa ni pamoja na walioiwezesha India kubeba Kombe la Dunia la mchezo wa kriketi mwaka 1983 na 2011.
Miongoni mwa waliokasirika na kususia kuandamana na kikosi cha India kwenda nje ya nchi kwa mashindano ya kimataifa ni Sunil Manohar Gavaskar.
Mwishoni mwa mwezi Oktoba Gavaskar alipokuwa anakula chakula katika hoteli moja ya Bombay (sasa Mumbai) huku akiangalia mchezo kati ya India na New Zealand alikasirishwa na wachezaji wa India.
Kwa hasira aliirusha sahani ya chakula na kuipigiza ukutani na kuchafua nguo za watu waliokuwa jirani naye.
Gajaskari anatambuliwa na mashabiki wa kriketi waliofuatilia mchezo huu miaka iliopita kwa jina la 'Bwana Mdogo' kutokana na maumbile yake, lakini alifanya makubwa uwanjani.
Aliisaidia India kuwa taifa lenye nguvu katika kriketi na kuacha rekodi ya kupiga kwa ustadi mipira ya kasi na mzunguko na kuwa mchezaji wa kwanza kupiga mipira iliyompatia alama 10,000 na kuweka rekodi ya kupata zaidi ya pointi 100 kwa kila mchezo katika michezo 34 ya kimatifa.
Rekodi hii ilidumu miaka 20 hadi ilipovunjwa na Sachin Tendulkar wa India mwezi Desemba, 2005.
Vile vile ilikuwa tabu kuidaka mipira aliyopiga au kupangua vijiti alivyolinda wakati alipocheza na kusababishwa kufananishwa na kunguru mjanja kwa wepesi wake wa kutegua mtego.
Tafauti na wachezaji wengi wa India, Gavaskar alikuwa mtulivu na alijiamini hata timu yake iliposakamwa.
Mikwaju yake iliyompatia pointi 221 kwenye uwanja wa Oval, 1979 ni rekodi ambayo haijafikiwa na mchezaji yoyote aliyeteremka kwenye uwanja huu maarufu wa Uingereza.
Kwa mtu mfupi kama yeye (futi 4 na inchi 4) kupiga mikwaju iliyopaa na yenye nguvu ni kielelezo cha uwezo mkubwa aliokuwa nao katika kriketi.
Godfrey Evans, wiketi kipa (muangalizi wa vijiti kwa lengo la kuviangusha) wa Uingereza, alisema ili kufidia gharama ni vizuri watazamaji anapocheza Gavaskar wakatoza viingilia vikubwa zaidi.
Hii ni kwa sababu wangekuwa tayari kulipa chochote ili kuona mchezo wake mzuri.
Gavaskar ambaye siku zote alianza mchezo kwa timu ya India alizaliwa Mumbai Julai 10, 1949.
Alikuwa mwanafunzi bora wa kriketi wa India wa mwaka 1966 alipokuwa anasoma katika Chuo Kikuu cha St Xavier's alipopata zaidi ya pointi 200 kwa kuwachakaza wanafunzi wa England waliotembelea India kwa michezo ya kirafiki.
Baada ya kumaliza shule alichezea klabu za Mumbai na msimu wa 1970/71 alikuwamo katika kikosi cha India kilichotemblea West Indies.
Gavaskar alipata pointi 65 katika mzunguko wa kwanza na 67 wa pili katika mchezo uliofanyika Trinidad na kuisaidia India kwa mara ya kwanza kuifunga West Indies.
Baadaye alipata pointi 116 na 64 katika mchezo michezo iliyofanyika Georgetown, Guyana Barbados alifanya vizuri.
Katika msimu wa 1978-79 India ilizuru Pakistan kwa michezo ya kimataifa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 17 kati ya mahasimu hawa wa kisiasa.
Gavaskar alikutana na Imran Khan (aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Pakistani) aliyesifika zama zile ambaye alimueleza kama mchezaji bora kuliko yeyote wa India aliyewahi kukutana naye.
Siku zote Gavaskar alionyesha uzalendo wa hali ya juu na kukipaka kifua chake rangi za bendera ya India.
Ni mtu mwenye kupenda utani, mwenye visa na mikasa ya kumvunja mtu mbavu na ni mtu aliyefurahisha maswahiba zake na wachezaji wenzake kwa kusema: "Watu warefu kama sisi", wakati yeye akiwa ndiye mfupi kuliko wote aliokuwa nao.
Katika miaka ya mwanzo kama nahodha wa India, Gavaskar ambaye pia ni mzuri kudaka michomo ya kimo cha mbuzi, alionekana kuyumba katika kuamua yupi ni mrushaji mzuri wa mipira ya mtetemeko wa timu yake.
Hata hivyo, alijirekebisha na kuiwezesha India kufanya vizuri na kuheshimiwa kama taifa kubwa kwa mchezo wa kriketi.
Kila India ilipofanya vibaya, Gavaskar alibadilishana unahodha na Kapil Dev na kusaidiana naye kushinda Kombe la Dunia mwaka 1983.
Gavaskar alikuwa akianza mchezo pole pole kwa kuchukua pointi moja moja na damu ilipochemka na washabiki kumpigia kelele za "Maro... maro... maro”, yaani piga... piga... piga, ndipo aliposukuma makombora kama vile alikuwa na kisasi na mpira.
Mchambuzi maarufu wa kriketi wa Uingereza, Ted Dexter, alisema mafanikio ya Gavaskar yalichangiwa na kutumia ubao mpana na mzito.
Lakini kilichostaajabisha ni mtu hafifu kimwili kama yeye kumudu kubeba bao zito kwa ustadi na kuutikisa ulimwengu wa kriketi.
Baada ya kuzitesa Pakistani, New Zealand, Australia, Bangladesh na Uingereza, Gavaskar alistaafu mwaka 1987 akiwa na umri wa miaka 39 kwenye Uwanja wa Lords, Uingereza.
Wengi walilia kuona Gavaskar anauaga mchezo na kusema mashabiki wa kriketi wa India wamekuwa mayatima. Gavaskar alipewa tuzo maalum na aliyekuwa Waziri Mkuu wa India, hayati Indira Ghandhi.
Muda mfupi baada ya kustaafu, Gavaskjar aliibuka kuwa mtangazaji wa kriketi kuanzia 1988 na kuandika makala katika magazeti. Vile vile ameandika vitabu vya mchezo huu na juu ya maisha yake.