KIHIMBWA: Ishu ya Yanga na 80,000 ya rasta
Muktasari:
- Kihimbwa jina lake lilikuwa kubwa zaidi alipokuwa Mtibwa Sugar, ambapo aliziumiza kichwa timu kongwe za Simba na Yanga wakati huo zote zikihitaji amwage wino wa kuzitumikia.
SALUM Kihimbwa sio jina geni masikioni mwa wapenzi wa soka kutokana na kipaji alicho nacho akilitumikia vyema eneo la winga, licha ya yeye mwenyewe kudai kwamba anaweza kucheza namba zaidi ya nne uwanjani.
Kihimbwa jina lake lilikuwa kubwa zaidi alipokuwa Mtibwa Sugar, ambapo alihusishwa na kujiunga na Simba na Yanga. Licha ya kutajwa kutua kwenye timu hizo kwa nyakati tofauti, hajawahi kuzitumikia hadi sasa, anakipiga Fountain Gate. “Ni kweli hizo timu mbili za Kariakoo zilinihitaji sana, ila sikufanikiwa kusaini timu hata moja kati ya hizo. Naweza kusema ilikuwa siyo riziki yangu kusaini, ila maongezi tulifanya na kufikia makubaliano vizuri, lakini mwisho wa siku sikusaini mkataba wowote,” anasema.
“Kwenye mchakato wa kuwania saini yangu kwa timu zote mbili nilifanikiwa kuzungumza na viongozi mbalimbali kwa timu zote mbili na wengine nilishakutana nao, maslahi tulipatana vizuri tu.
“Sijawahi kusafilishwa kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam, ila nilishawahi kukutana na kiongozi hotelini kipindi tulipokuwa tunacheza nao mechi. Baada ya mchezo kuisha alinipigia simu nikaongee naye, nikaenda tukaonana na kuongea vizuri shida kilichokuwa kimebaki ni kumwaga wino tu, lakini zoezi hilo halijawahi kukamilika hadi sasa.”
NEYMAR ANAHUSIKA
Ukiondoa ubora wake uwanjani, Kihimbwa ni mmoja wa wachezaji ambao wanatupia pamba kali na kuonekana nadhifu akiwa kwenye mavazi ya nyumbani, na mwenyewe anaeleza kuwa kwake kuvaa ni bora zaidi ya kula.
"Suala la mavazi kwangu ni kipaumbele zaidi ya kula na nimekuwa nikimfuatilia zaidi Neymar Jr. Huyo ndiye staa ambaye nimekuwa nikimtazama 'role model' wangu kwenye uvaaji. Napenda kuwa nadhifu na kuwa tofauti na wengine," anasema.
"Kuhusu gharama ya nguo ninayoitaka huwa sioni kama napoteza (fedha), kwa sababu napenda kuwa na mwonekano. Huwa natoa kiasi chochote bila kujali na siwezi kuweka wazi nguo yangu ya gharama ni bei gani. Kwa mtu yeyote anayefahamu bei za nguo anaelewa navaa kiasi gani ninapotoka."
SILAH WINGA BORA
Kihimbwa humwambii kitu kuhusu Mgambia wa Azam, Gibril Sillah anayemtaja kuwa ni bora kwake.
“Ni kweli wachezaji wengi bora wamepita kwenye eneo ninalocheza sasa, winga, lakini kwa nyota wa kigeni kwa sasa navutiwa na Sillah anafanya vizuri. Ana vitu vingi ambavyo binafsi nimekuwa nikijifunza kutoka kwake.
“Kwa upande wa mchezaji wa ndani navutiwa zaidi na aina ya uchezaji wa Seleman Idd ‘Nado’. Ni winga ambaye pia namtazama na napenda baadhi ya uamuzi wake hasa akiwa ndani ya 18, ni mchezaji ambaye ana jicho la kuona goli,” anasema Kihimbwa ambaye anasema kama sio soka, basi alitamani kuwa Polisi.
KATWILA, MUYA
Mchezaji huyo ambaye amecheza Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons, Mbeya City, Dodoma Jiji na sasa Fountain Gate licha ya kupita chini ya makocha wengi ambao anasema hawezi kuwataja wote, amemzungumzia Zuberi Katwila na Mohamed Muya kuwa ndio makocha wake bora waliomfundisha.
“Naheshimu ubora wa makocha wote niliopita chini yao, lakini nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipomzungumzia Katwila na Muya kwa sababu ndio makocha ambao wamenifanya niwe bora kwenye misimu niliyocheza chini yao,” anasema.
“Kipindi Simba na Yanga zinaniwinda nilikuwa chini ya Katwila. Ni kocha ambaye alikuwa ananiamini na kunipa mbinu za kuwa bora sawa na Muya ambaye kanirudisha kwenye ubora wangu baada ya misimu miwili nyuma kuishia kuuguza majeraha ya mara kwa mara na nilipotua Fountain Gate nimekuwa bora chini yake.”
POPOTE ANACHEZA
“Ni kweli wengi wananifahamu kama winga, lakini naweza kucheza nafasi nyingi uwanjani. Saba, nane, tisa, 10 na 11 na zote naweza kucheza kwa usahihi itategemea na kocha atanipa majukumu gani ya kufanya, lakini ninaweza kucheza kwenye maeneo haya yote.”
KICHWA TU KWA MWEZI 80K
Ukitaka kumtambua kwa haraka mchezaji huyo ni rasta zake kichwani na umbile lake dogo. Kihimbwa amezungumzia umri wa rasta zake tangu aanze kuzifuga akiweka wazi kuwa zina miaka 10 na amekuwa akizihudumia kila baada ya wiki moja.
“Mwezi una wiki nne, basi mimi kila baada ya wiki naenda saluni kuzisafisha na kubadilisha mwonekano kwa Sh20,000, hivyo kwa mwezi natumia Sh80,000. Napenda kuwa nadhifu kuanzia kichwani,” anasema.
Unadhifu wake wa nywele umefanikiwa kuwavutia wengi ambao wanatamani kuwa na mwonekano kama wake, akisema: “Wakianza kwa kuniomba niwapunguzie, lakini sikuweza kufanya hivyo kutokana na kuzipenda nywele zangu na sijawahi kufikiria kuzikata.”
Kihimbwa anamtaja Baraka Majogoro ambaye pia kwa sasa ana muonekano wa rasta kichwani kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao walimuomba awapunguzie rasta zake, lakini hakufanya hivyo lakini sasa amekuwa na mwonekano wa rasta.
MIEZI SITA BILA KUGUSA MPIRA
Mchezaji huyo alipitisha miezi sita bila kugusa mpira wa miguu uwanjani kutokana na kuumia.“Mwaka 2024 niliumia nikiwa na Tanzania Prisons jeraha lililonifanya nikae (nje ya uwanja) miezi sita bila kugusa mpira,” anasema na kuongeza:
“Tangu nimeanza kucheza soka sijawahi kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili, lakini nilipokuwa Prisons nilikutana na jeraha lililoniweka nje ya uwanja kwa miezi sita. Sitakaa nikasahau.” Kihimbwa anasema kuumia kwa mchezaji ni suala la kawaida, nashukuru kwamba ilipomtokea yeye hakukata tamaa.