Kigonya: Huyu Bocco na Kaseja waacheni tu

KIPA namba moja wa Yanga na wa kimataifa wa Mali amejiunga na Yanga. Ni Djigui Diarra ambaye inaelezwa kuwa ukiachana na ubora wake golini alikuwa kiungo fundi. Kutua kwake Jangwani kumeamsha mijadala kila kona na hasa akisifiwa kwa rekodi zake.

Kwa sasa yupo Yanga kuongeza nguvu baada ya wababe hao kuwatema makipa wawili waliokuwa tegemeo kina Farouk Shikhalo na Metacha Mnata.

Hata hivyo, sio kipa wa kwanza wa kimataifa kuwadakia mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, wapo wengi na baadhi waliwapa mafanikio huku wengine wakichemka na kusepa.

Pamoja na kusifiwa kwa kipa huyo, Azam pia imeingia mkataba na Mathias Kigonya kipa ambaye pia inaelezwa kwamba alianzia kucheza ndani kama mshambuliaji, hivyo kuunganishwa kwenye mjadala wa Diarra kutokana na wote kuanzia kucheza nafasi za ndani.

Kigonya amezungumza na Mwanaspoti na kufunguka mambo mbalimbali huku akiweka wazi kuwa dabi ya Kenya wakati akikipiga Sofa Paka walicheza na Gor Mahia ambapo ilimjengea kujiamini na hadi sasa anajiamini akiwa golini.

Kipa huyo namba moja wa Azam sasa, alichukua mikoba ya Razak Abalora katikati ya msimu kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na amekuwa akiaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara huku akiwapiga chini wazawa kina Ahmed Salula, Wilbol Maseke na David Mapigano ambaye hata hivyo yupo Namungo FC kwa mkopo.


USHAMBULIAJI HADI KUDAKA

Kigonya, Watanzania wengi wanamfahamu kama kipa, lakini mwenyewe amefunguka sababu zilizomfanya asimame golini na sio kucheza ndani ya uwanja kama alivyokuwa anafanya mwanzo akiwa mshambuliaji.

“Nilikuwa mshambuliaji, lakini baada ya kupata majeraha ambayo yalinifanya nikae nje miaka miwili nilitamani kuacha soka, kwani niliambiwa sitakiwi kufanya kazi ngumu kwa muda, lakini kutokana na kupenda soka nilijikuta narudi tena dimbani,” anasema kipa huyo.

“Nilichanika nyama za paja ndio ziliniweka nje miaka hiyo miwili. Nakumbuka kulikuwa na mechi baada ya mimi kuamua kurudi uwanjani, bahati mbaya kwa mchezaji aliyeumia ikawa nzuri kwangu, kwani kocha aliamua kunipanga langoni na nilifanya vizuri ndio ukawa mwanzo wa kufanya hivyo.”


BOCCO TISHIO

Kipa huyo pamoja na ubora aliotamba kuwa nao, ndiye kipa pekee aliyeruhusu mabao mengi raundi mbili za Ligi Kuu zilizochezwa hadi sasa baada ya kufungwa mabao matatu, lakini anasema hilo wala sio shinda.

Pamoja na yote anasema yeye ni bora zaidi ya makipa wote wanaocheza Ligi Kuu akianza, huku wengine wanafuata, lakini anamtaja straika wa Simba, John Bocco kuwa ni mmoja wa washambuliaji wasumbufu nchini.

“Sitaki kumtaja majina kwa sababu washambuliaji wote ni bora na wanajiandaa kwa ajili ya kufunga, lakini Bocco ni mmoja wa washambuliaji makini na wasumbufu,” anasema.


HAKUNA KAMA ONYANGO

Katika timu ya taifa lake, Uganda the Cranes, Kigonya anasubiri akimtaja mkali wake kikosini katika kusimamia milingoti ya goli.

“Ni ndoto za kila mchezaji anayecheza mechi za ushindani - ndoto yake ni kulitumikia taifa kwa kupata nafasi ya kucheza timu ya taifa. Kwa upande wangu nina ndoto hiyo, lakini sioni nafasi ya kulitumikia kutokana na ubora wa kipa aliyepo,” anasema Kigonya.

“Uganda ni nchi ambayo inazalisha makipa bora na imekuwa bora eneo hilo, timu ya taifa inaita makipa watatu kila ikipata mashindano, lakini namba moja ni Onyango. Ni bora kweli sio utani natamani siku moja nifikie uwezo wake na kupata nafasi ya kulichezea taifa langu.”

Kigonya anasema kukosekana kwa kipa huyo labda aumie, lakini hakuna kipa mwingine bora ambaye anaweza kumpokonya namba huku akisisitiza kuwa ana imani na uwezo wake ipo siku ataitwa hata kukaa benchi.


YEYE NI EDERSON

Moja kati ya golikipa anayemvutia ni Ederson Santana de Moraes wa Manchester Ciy kutokana na aina ya uchezaji akianzisha mashambulizi kuanzia langoni.

“Mimi sio shabiki wa Manchester City, ila napenda aina ya uchezaji wake. Nimekuwa nikimuangalia kila ninapokuwa sipo kwenye majukumu yangu ya kazi, basi nakaa naangalia video zake ili kuendelea kujifunza. Naamini kwenye upambanaji wake,” anasema kipa huyo msomi wa shahada ya uongozi kutoka Chuo Kikuu cha Kampala nchini Uganda.


KASEJA NA MANULA

Pamoja na kujitaja kuwa yeye ni bora, hasiti kuwataja makipa wazawa ambao anaamini kuwa na wao ni bora na ndio wanaomfuata kuwa ni Juma Kaseja kipa wa KMC na Aishi Manura namba moja wa Simba.

“Kwenye namba moja hapakosekani mbili na tatu. Basi kwa wazawa makipa wangu bora na wanaonipa ushindani ni hao wawili msimu wa 2021/22, natarajia kuwa bora kwa sababu tunaanza msimu pamoja tofauti na uliopita nilisajiliwa katikati ya msimu,” anasema.


TUKIO LA FURAHA

Kila binadamu hukoshwa na matukio mbalimbali, lakini hata kwa Kigonya kuna tukio ambalo hatalisahau kamwe.

“Nakumbuka wakati nipo shule tulikwenda kucheza michuano ya Copa CocaCola 2010. Timu yetu ilikuwa na wachezaji 11 pekee na kipa nilikuwa mimi tu. Kwenye siku ya mwisho ya michuano nilichukua tuzo tatu ya kwanza ilikuwa kipa bora wa michuano, beki bora na mchezaji bora. Nafikiri hili ni jambo lililonifurahisha zaidi kwani nilicheza namba tofauti hasa pale kulipokuwa na pengo mahali,” anasema.

Kigonya anasema ana uwezo wa kucheza zaidi ya maeneo matatu awapo uwanjani kuanzia beki, winga na straika ndio maana haimpi shida kwenye kudaka kwani huisoma akili ya mshambuliaji kabla hajafanya uamuzi.


TUKIO LA HUZUNI

Msimu uliopita kwenye mashindano ya Kombe la Azam katika mchezo dhidi ya Simba hatua ya nusu fainali ambapo walikubali kipigo cha bao 1-0 lililosababishwa na faulo na kupigwa haraka haraka na Bernard Morrison na kufungwa na Luis Miquissone ambaye ametimkia AL Ahly.

“Tulifanya vizuri dakika zote 90, lakini kosa moja tu la kizembe lilitugharimu. Hilo tukio sitalisahau ilikuwa Juni 26 kwenye Uwanja wa Majimaji nilifungwa bao la kizembe ambalo timu nzima hatukulitarajia,” anasema.


MKWANJA WA KWANZA

Ukimuuliza kuhusu fedha alizopata katika soka kwa mara ya kwanza, kipa huyo anacheka kisha anasema kwanza hakuwa anajali juu ya pesa kwani hakuwa na ndoto za kuja kuwa mchezaji mkubwa.

“Ilikuwa wakati napandishwa kikosi cha kwanza cha SC Villa mwaka 2010. Nakumbuka nilipewa Dola 500 wakati huo ilikuwa nyingi na kwa kweli sikujua hata nitumie nini zaidi ya kwenda kumpa mama yangu,” Kigonya anasema na kuongeza kwamba baada ya kumpa kiasi hicho mama yake alimpa baraka ambazo hadi sasa anaamini ndizo zinamfanya kuwa kwenye kiwango bora.


TANZANIA NA ZAMBIA

Kipa huyu anasema soka la Bongo na Zambia lina tofauti kubwa kama mbingu na ardhi na kwamba, licha ya kuwa hivyo lakini halimpi shinda yoyote.

“Soka la Tanzania ni la presha sana. Mashabiki wao wanataka matokeo ya haraka, hawana nafasi ya kutoa muda kwa mchezaji, huu ndio utofauti mkubwa niliouona (kati ya Tanzania na Zambia),” anasema.

“Pia soka lao limekuwa bora na linalipa ndio maana wachezaji wengi sasa wanakimbilia huku. Ukitaka kuishi maisha mazuri na ya furaha fanya vizuri mashabiki watakupenda.”


ALIKOTOKA

Kigonya anasema alianza kucheza soka kwenye akademi mbalimbali nchini kwao Uganda kama Jogoo Stars, kabla ya kutua timu ya vijana ya SC Villa wakati huo alikuwa akisoma, hivyo muda mwingi hakujihusisha kucheza soka zaidi kwani alipendelea kusoma.

Anasema alicheza kwa mafanikio zaidi timu za vijana za SC Villa hadi alipopandishwa kikosi cha wakubwa na hapo ndipo timu ya Soana ilimuona.

“Sikucheza mechi hata saba Soana walinihitaji na kusema licha ya umri mdogo niliokuwa nao walikuwa na imani ningewasaidia. Hivyo walinisajili na nilianza kucheza hapo,” anasema na kuongeza baada ya kujiunga na Soana 2013 ndipo maisha yake mapya ya soka yalianza.

Kigonya alidumu katika timu hiyo kwa msimu mmoja kisha alitua Bright Stars FC alikocheza misimu miwili na akiwa hapo 2016 aliitwa timu ya taifa ya Uganda iliyoshiriki michuano ya Chan 2016 na kuishia hatua ya makundi.

Baada ya michuano hiyo iliyofanyika Januari 16 hadi Februari 7 nchini Rwanda mwisho wa msimu alinunuliwa na Sofapaka ya Kenya.

Imeandikwa na CHARITY JAMES, DAUDI ElIBAHATI NA RAMADHAN ELIAS