Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIBADENI: Simba ikikaza, inabeba ndoo!

KIBADENI Pict
KIBADENI Pict

Muktasari:

  • Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Simba, Majimaji na Taifa Stars aliiongoza klabu hiyo kucheza fainali hizo akisaidiana na Muethiopia Etienne Eshette na kupoteza nyumbani kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast baada ya mechi yao ya awali kule ugenini kuisha kwa matokeo ya 0-0.

MIAKA imepita, lakini rekodi ya kocha Abdallah 'King' Kibadeni, ya kuwa kocha mzawa aliyewahi kuifikisha Simba katika fainali ya Kombe la CAF 1993 haijavunjwa.

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Simba, Majimaji na Taifa Stars aliiongoza klabu hiyo kucheza fainali hizo akisaidiana na Muethiopia Etienne Eshette na kupoteza nyumbani kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast baada ya mechi yao ya awali kule ugenini kuisha kwa matokeo ya 0-0.

Kwa sasa Simba ipo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, michuano iliyozaliwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa Kombe la CAF na Kombe la Washindi Afrika na Jumapili hii itashuka kwenye uwanja wa nyumbani kurudiana na RS Berkane ya Morocco, ikiwa na deni la mabao 2-0 iliyofungwa ugenini Morocco.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na mkongwe huyo nyumbani kwake eneo la Chanika, pembezoni mwa jijini la Dar es Salaam na kufunguka mambo mengi akikumbushia fainali hizo za 1993 zilivyoikatili Simba kubeba taji la kwanza la Afrika, lakini akiainisha sababu iliyochangia iwe hivyo.

Pia amefunguka jinsi anavyoiona Simba ya sasa na nafasi ya kubeba ubingwa kama itaamua kukaza katika mechi ya Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan, mjini Unguja licha ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 kwa kupindua meza kama ambavyo timu hiyo imekuwa ikifanya kwa miaka ya hivi karibuni.

Kadhalika amemchambua kocha Fadlu Davids aliyeifikia rekodi ya kuifikisha Simba katika fainali ya michuano ya CAF ikiwa imepita takriban miaka 32 tangu yeye (Kibadeni) alipofanya hivyo na kusimulia pia mbinu anazopaswa kuingia nazo uwanjani kuwamaliza Berkane...Endelea naye.

KIBA 07

FAHARI KWAKE

Kibadeni anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee hadi sasa kuwahi kufunga hat trick katika Dabi ya Kariakoo, anasema kitendo cha Simba kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ni fahari kwake kama Mtanzania na Mwanasimba kwani wamesubiri kwa muda mrefu.

Kibadeni anasema kitendo Simba kufika tena fainali huku akiishuhudia baada ya yeye kuiongoza kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo ni furaha kubwa kuliko anavyoweza kujieleza. "Najisikia furaha sana kuona historia inajirudia na mimi bado nipo, tuwaombee Simba na wachezaji wake waweze kutufikisha katika rekodi ambayo hatujawahi kuifikia. Ni miaka mingi sana imepita, vijana wana jukumu la kuhakikisha wanatupa furaha tuliyoikosa wakati ule kwani wana kikosi bora sana."

KIBA 02

KIKOSI CHA SASA

Kibadeni anasema kwa kikosi kilichopo anaamini lolote linaweza kutokea na historia ikaandikwa, licha ya Simba kupoteza ugenini wikiendi iliyopita kwa kufungwa mabao 2-0 ugenini na RS Berkane.

"Kwanza tumuombe Mwenyezi Mungu atuwezeshe kushinda, sio kwa ujanja wa mtu au uhodari wa mtu, hapana, kila mmoja amlilie kwa kumuomba atujalie tupate ushindi kwa sababu tuna kiu sana ya muda mrefu, tumevumilia sana, kwa hiyo ninachotaka kukisema ni kwamba kikosi cha Simba kipo vizuri," anasema Kibadeni anayemiliki taasisi ya kuibua na kukuza vipaji vya KISA.

"Siwezi kusema nani na nani wacheze au wafanye nini, wao wenyewe watajua wanafanya kitu gani maana kocha ni mzoefu anajua, ukisemasema hovyo utamchanganya, lakini kubwa ninachokiomba kwamba wajue Watanzania hasa wapenzi wa Simba tunahitaji kitu gani, viongozi, kocha na wachezaji wajue tuna kiu kubwa tunataka kushinda, watengeneze mipango yao yote watakayoweza kupanga kuhakikisha kwamba tunataka tusheherekee kikombe hapa nyumbani.

"Wawaambie wachezaji kwamba Watanzania wana kiu ya aina gani tena sasa hivi utakuta kuna wachezaji pengine wapya wanakuwa wageni wanaweza kuwa watano, sita au saba pamoja, lakini zamani ilikuwa mtu wa nyumbani unampigia hata kwa baba yake unamwambia, ebu mwambie mwanao asifanye kitu fulani," anasema Kibadeni.

Kibadeni anasema kwa kikosi kilichopo na jinsi kilivyocheza mechi zote hadi kufika hapo, anaona ni timu yenye nafasi kubwa ya kufanya maajabu, licha ya ukweli Berkane kama timu nyingine za Afrika Kaskazini ni ngumu na zinajipanga kiakili kwenye hatua kama hizi za kuwania ubingwa.

KIBA 01

NGUVU YA SIMBA

Kibadeni anasema nguvu ya Simba ya kuwapa mafanikio ipo katika kila idara, kwani imejitosheleza, lakini nguvu zaidi ipo eneo la kipa hadi eneo la kiungo cha ukabaji, akisema wanacheza vyema na kwa akili sana.

"Sasa hivi ukitazama utaona timu iko vizuri, upande wa nyuma kwa kipa hadi watu wa nyuma wale watano wanaocheza nyuma sisemi nani na nani, lakini wale wanaocheza nyuma kwa sasa hivi wako vizuri.

"Nawaona kabisa wanacheza mpira mzuri, halafu wanakwenda kushambulia na nafasi zinapatikana, tunaweza kushinda tukapata bao, lakini kunatokea mambo ya namna mbili moja mtu anakuwa mchoyo kumalizia kumpa hata mwenzie amalize inakuwa kwake ngumu na wakati mwingine mtu anapata nafasi anapoteza."

KIBA 03

FADLU KOCHA WA AINA GANI

"Kwa kweli mwalimu kafanya kazi nzuri sana na kipimo chake utaona matokeo yake kafika mwisho wa mashindano. Kama ingekuwa hafanyi vizuri wala tusingefika hata raundi ya tatu, mimi nasema tumuombee na yeye mwalimu (Fadlu Davids) MwenyeziMungu amuwezeshe.

"Hata yeye anataka malengo yatimie ili na yeye achukue kombe, kwahiyo malengo yake Mungu amruhusu aweze kupata hili kombe na yeye aweke rekodi yake (Fadlu hajawahi kutwaa kombe la Afrika akiwa kocha mkuu).

"Siwezi kusema tu nani na nani acheze siruhusiwi kitaaluma, yeye mwenyewe anajua, zamani tulikuwa tunapata tabu, unaweza kupanga timu, mwenyekiti wa klabu akaja akakwambia Kibadeni tuambie timu yako inayocheza leo kisha ukaambiwa, 'huyu hapana usimchezeshe'.

"Tunaanza kugombana lakini sasa hivi mtu ana uhuru wa kupanga anavyotaka kupanga, anapata ushauri pengine kwa wasaidizi wake, anaweza kuchukua, lakini kuna mwalimu mwingine hakubali anataka kufanya mwenyewe lakini kiujumla ukimuangalia mwalimu anavyokwenda yuko vizuri."

KIBA 05

MATOLA WA BAADAYE

"Nafikiri Matola amepata nafasi kubwa muda mrefu yuko na timu na kila mwalimu mgeni anavyokuja anakuwepo kama msaidizi na yeye azidi kumuomba Mungu tufanikishe kufikia malengo, ikiwa tofauti itakuwa sawa na uwepo wake unakosa faida.

"Najua kwamba uwezo anao na ameshapata uzoefu mkubwa inamtosha, amekaa na walimu wa aina mbalimbali, kama itawezekana safari hii akimaliza kama kusoma akaongeze elimu ili abaki na yeye kuwa kocha mkuu.

"Tusilete hawa wageni kila mara, maana kuna wakati inatupa tabu kidogo, wakija wanashindwa kuunda vijana wa kwetu, sisi tunategemea kwenda kuchukua DR Congo, tukachukue wachezaji Burundi, sisi tunataka watoke hapahapa Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, kwa hiyo yeye (Matola) atusaidie kuhamasisha, tunataka na yeye awe kocha mkuu huko mbele, vinginevyo tutakuwa tunaishia hapahapa na hili ni tatizo, tusipokuwa na makocha wazawa wazuri tutapata tabu kidogo."


HISTORIA NA SIMULIZI YA 1993

Kibadeni alizaliwa Oktoba 11, 1949, katika Mtaa wa Kiburugwa, Mbagala jijini Dar es Salaam. Jina la Kibadeni lilitokana na jina la utani alilopewa na watoto wenzake akiwa Shule ya Msingi Habib Punja, likimaanisha "kitu cha baadaye".

King Kibadeni alijiunga na Simba SC akiwa na umri wa miaka 20, wakati huo ikiwa inajulikana kama Sunderland. Mwaka 1974, akiwa mchezaji wa Simba, aliipeleka timu hiyo nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika akifunga bao muhimu dhidi ya Hearts of OAK ya Ghana.

Julai 19, 1977, aliandika historia katika mechi ya watani wa jadi kati ya Simba na Yanga kwa kufunga mabao matatu (hat-trick) kwenye ushindi wa 6-0, rekodi ambayo haijavunjwa hadi leo. Umahiri wake wa uchezaji ulimfanya apate jina la "King", akifananishwa na mfalme wa soka duniani, Pele.

Baada ya kustaafu uchezaji, Kibadeni alijiingiza katika ukocha na alifundisha timu mbalimbali, ikiwamo Simba SC, Kilimanjaro Stars, Kagera Sugar, na JKT Ruvu. Alikuwa pia mkurugenzi wa ufundi katika kituo cha KISA kilichopo Chanika, Dar es Salaam.

Mwanaspoti limefunga safari hadi Chanika kukutana na Kibadeni ambaye anatoa simulizi nzima ya mechi ya fainali za Kombe la CAF iliyofanyika mwaka 1993 akiwa kocha wa Simba ilipopoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Stella Adjame kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.

"Mimi sikuanza mwanzo na Simba, alikuwapo kocha mwingine, lakini nikapewa nafasi hiyo baada ya timu kutoka Msumbiji, msaidizi wa kocha alitoka Ethiopia, sasa ile mechi ya kwanza walitoka sare ya 1-1, kuja huku ikawa suluhu.

"Simba walivyoona vile wakasema hawawezi kuendelea naye, wakaamua kunichukua ili niwe kocha mkuu na tukaanza mechi ya pili dhidi ya Waswaziland tukashinda mabao 3-0 nyumbani, kwao tukafungwa 1-0.

"Kulikuwa na maandalizi mazuri viongozi na wachezaji walinisikiliza sana, niliambiwa nifanye lolote au msaidie mchezaji chochote kwa sababu hela tunazo.

"Kwa hiyo nilikuwa na uwezo wa kumpa mchezaji pesa yoyote kama ana matatizo ya kifamilia au lolote ili tu watulize akili kwenye mashindano, nilibahatika kupata wachezaji wasikivu na wote napafahamu hadi kwao, kwa hiyo hawakuwa na pakunikimbia.

KIBA 04

KIKOSI CHA WAZAWA

"Sikupata shida kupanga kikosi licha ya kuwa na wachezaji wengi wa kiwango cha juu, hii ni kazi yangu na wachezaji wote nawafahamu.

"Kwangu haikuwa tabu, nilikuwa nao mazoezini na hata katika mechi nilikuwa nawaona kwa hiyo nilikuwa najua nani nimpange na yupi kutokana na uwezo wao.

"Nilikuwa nawapanga mwenyewe, wakati mwingine walikuwa wanajua kabisa nani atacheza kuanzia namba 1-11, kulingana na walivyokuwa wakicheza huko nyuma, na walikuwa wanapambana ili nisiwabadilishe."


AHADI ILIVYOWACHANGANYA

"Bosi wa wakati huo aliahidi kabisa kama tukishinda kila mchezaji atampa gari aina ya KIA, yalikuwa kama mabasi ya kubebea abiria sasa ukipata itakusaidia usipate tabu.

"Kwa hiyo kila mmoja alipambana, licha ya kukosa ubingwa ila akatupa magari madogo, akasema 'mcheza kwao hutunzwa', tulikuwa tukifika uwanjani tunayapanga hapo ilikuwa raha kweli.


MWENDO WA KIBABE

"Kwa kweli mechi zote tulizocheza, ilikuwa mimi mwenyewe mipango yangu kwamba tukiwa nyumbani basi tupambane kiasi cha kutosha kama kushinda tupate ushindi mkubwa kuanzia bao tatu au nne, ukizipatia nyumbani ukienda kule kwa mechi ya marudiano inawezekana kwamba mtu asikufunge tatu anaweza akakufunga moja au mbili.

"Sasa sisi mipango yetu Mungu alitusaidia, ilikuwa tukicheza nje tunaweza kushinda nje hukohuko au tukicheza nyumbani tunashinda sio chini ya bao hizo tatu. Hii ilitusaidia kucheza vizuri nyumbani, ukiacha mechi ile ya fainali (na Stella)."