KESSY: Nilizushiwa kifo, turubai likafungwa

SAFARI ya soka na maisha ya beki wa KMC, Hassan Kessy kwa ujumla yamejaa kicheko, simanzi lakini hakuwahi kukata tamaa kupambania ndoto zake.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, yaliyochukua takribani saa tatu, kuna wakati simanzi ilitawala pale beki huyo alipokuwa akisimulia mapito yake ikiwamo kuchomwa moto miguu yake ili asicheze soka.
Anavuta pumzi kisha anaanza kufunguka; “Katika maisha yangu nilipitia mambo ya kustaajabisha, ila kama Mungu hajapanga uondoke hapa duniani, hauondoki.”
KELELE ZILIVYOMWAMSHA USINGIZINI
“Nilisumbuliwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, nikawa natumia dawa tu. Kuna muda ulifika nikachoka na kuamua kurudi nyumbani ambapo nilikuwa naishi na bibi yangu,” anasema Kessy anasema na kuongeza;
“Kuna siku sikuwa sawa nilikuwa najihisi vibaya sana nilimuomba bibi yangu asiende shambani ili akae pamoja na mimi kwasababu hali yangu haikuwa nzuri, nashukuru alinielewa tulikaa pamoja, usiku ulipoingia nilichukua simu yangu na kumpigia mama yangu nilimweleza kuwa sipo sawa kiafya chochote atakachosikia kuhusu mimi asishtuke.”
Kessy anasema kauli aliyoisikia kutoka kwa mama yake ni kuambiwa kwamba hawezi kufa.
Alilala kwa muda na ilipofika alfajiri ya siku inayofuata alisikia kelele bila kutambua ni nini kinaendelea alipoamka na kutoka nje alikuta maturubai yamefungwa na watu wengi wamejazana.
“Nilihoji mbona mnanipigia kelele mimi nimelala naumwa bibi yangu alishtuka na kunirudisha ndani akiniambia walijua nimefariki, nilishtuka sana, huwezi amini pamoja na kudhoofu, nguvu zilinijia na kuamua kutoka ndani na kwenda kijiweni,” anakumbuka.
“Nilivuka hadi upande wa pili wa barabara ambapo kulikuwa na kijiwe cha kutengeneza baiskeli, nilikuwa mtu mwenye nguvu na ujasiri, licha ya watu kunishangaa kwa jinsi nilivyodhoofu.”
ACHOMWA MOTO KISA SOKA
Kessy ambaye amecheza kwa mafanikio Simba, Yanga na Nkana FC ya Zambia amefunguka changamoto alizozipitia hadi kufikia alipo sasa.
“Nacheza soka hadi sasa kwasababu ndio kitu nilikiamini na kukipa nafasi kwani nilishatenganishwa na baba yangu mzazi kutokana na kuamini katika mpira zaidi ya shule,” anasema Kessy na kuongeza;
“Baba yangu miaka ya nyuma alikuwa ni mchezaji hakuna alichokipata kutokana na soka alipobaini nami nataka kufuata nyayo zake za kucheza, hakutaka hilo litokee kwa kunisisitiza nisome kwanza na nilikuwa na akili sana darasani, lakini kipaumbele changu kilikuwa ni mpira.”
Kessy anasema baada ya kushindwa kumsikiliza mzazi wake ndipo mzee huyo alipofanya tukio la kushangaza ambalo liliwashangaza wengi na hawakulitarajia la kumchoma moto miguu ili asiweze kutimiza ndoto zake za kucheza soka na ndio ukawa mwanzo wa kutenganishwa na baba yake.
“Bibi yangu mzaa mama aliamua kuokoa jahazi, akanichukua ili nikaishi naye. Huwezi amini nilikuwa nalala chumba kimoja naye, kulikuwa na vitanda viwili mmoja kushoto mwingine kulia,” anasema.
KIFUA KIKUU
“Nimekumbana na mambo mengi ya maisha yangu ya soka. Nakumbuka nikiwa Mtibwa Sugar nilikutana na suala hilo ambalo liliniweka nje ya uwanja mwaka mmoja na nusu,” anasema na kuongeza;
“Nakumbuka tulikuwa tunajiandaa na mechi, tulikalishwa kwa ajili ya mipango kuelekea mchezo huo, nilijisikia kiu nikatoka nje kunywa maji, nilianza kukohoa kikohozi kisichokata, nikawa napambana tu na hali yangu kwa kuendelea kucheza, ilifika muda nilijisikia vibaya na kuomba kupata matibabu,” anasema.
“Niliongea na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Mtibwa Sugar Jamal Byser kuomba kufanyiwa vipimo kutokana na hali ya kikohozi kuniletea maumivu makali, alikubalia na ndipo nilipopelekwa Dar es Salaam kwaajili ya vipimo, nilipimwa kila kitu siku ya kwanza hawakugundu a kitu,” anaongeza.
Kessy anasema baada ya marudio ndio walibaini ana TB na baada ya kusikia hivyo alishtuka na kumuuliza mama yake mzazi ugonjwa huo unasababishwa na nini na kuhoji kuna ndugu aliwahi kuugua akaambiwa hakuna.
“Nilikaa nje ya uwanja mwaka mmoja na nusu kama sijakosea nilikuwa nimepewa utaratibu wa kutumia dozi kwa kufuata kila baada ya wiki moja,” anasema.
Pia anaongeza kuwa akiwa Nkana FC pia alikutana na tukio jingine lililomshangaza baada ya kupewa kiatu ajaribu kama kinamtosha na baada ya hapo alijikuta mguu unavimba.
“Tulikuwa tumetoka mazoezini nilikuwa na wechezaji wengine akatokea mmoja ambaye tunacheza nafasi moja akanipa kiatu nijaribu baada ya kufanya hivyo tu mguu wangu ukaanza kuvimba,” anasema.
MILIONI 70 ZILIMPELEKA NKANA FC
Kabla ya Kessy hajatajwa kwenda Nkana, alihusishwa kuongeza mkataba na waajiri wake Yanga lakini haikuwa hivyo hadi alipoamua kujiunga na timu ya Zambia kwa mkataba wa miaka miwili.
“Ni kweli nilifanya mazungumzo ya Yanga ili kuongeza mkataba lakini baada ya kupata ofa ya NkanaFC nilishindwa kujizuia kuungana nayo kutokana na ofa kubwa waliyonipa,” anasema na kuongeza;
“Niliwekewa milioni 70 mezani wakati Yanga walitaka wanipe Sh45 Milioni ata ungekuwa wewe nafikiri ungefanya kama nilivyofanya mimi.”
BENCHI MECHI 5
Licha ya kusajiliwa kwa dau kubwa Nkana bado hakuwa na namba kikosi cha kwanza baada ya kukutana na mchezaji Mussa Mohammed, raia wa Kenya ambaye hakumpa nafasi ya kucheza hadi mechi tano.
“Mechi yangu ya kwanza baada ya kukaa benchi mechi tano ilikuwa ni dhidi ya Kabwe Warriors tulipata matokeo kwa kushinda mabao 2-0 wafungaji alikuwa ni Idris Mbombo na Walter Bwalya,” anasema na kuongeza;
“Kwenye mchezo huo nilionyesha kiwango kizuri na kufanikiwa kuibuka mchezaji bora wa mchezo hapo ndio ulikuwa mwanzo wa kuaminiwa nilicheza kikosi cha kwanza hadi tunatwaa taji.”
NKANA FC, SIMBA NA YANGA
Anasema kuna tofauti kubwa sana kati ya Ligi Kuu ya Zambia na Tanzania kwani kule hakuna matabaka ya timu kama ilivyo huku Simba na Yanga zinavyoonekana ni kubwa zaidi ya nyingine.
“Nimecheza Simba na Yanga, hizi timu zina mashabiki wengi wenye mapenzi makubwa ukicheza vizuri mechi yoyote mashabiki wanaweza kukutunza chochote na ukaondoka mzito,” anasema na kuongeza;
“Zambia timu zote zipo sawa hakuna utofauti wowote kama huku, kule mechi zikichezwa na ukafanya vizuri timu ndio inaandaa fungu la kutoa na sio mashabiki,” anasema na kuongeza;
“Bonasi kule ukishinda ni dola 250 mechi ya nyumbani, ugenini ni dola 300. Mashabiki wa kule ni kuhukumu tu, matokeo mabaya nakumbuka mechi yetu na Power Dynamos tulifungwa nyumbani ndio mashabiki wakaanza kutushambulia kwa kuturushia mawe.”
Anasema waliwatuliza baada ya kupata matokeo ugenini lakini ile siku hawakuwa na amani kwani mashabiki wao walikuwa hawana imani tena na timu hadi walipopata matokeo mazuri ugenini.
ASAINI MKATABA KWA MKAPA
Achana na tukio la kuvishwa jezi ya Yanga akiwa bado haja-maliza mkataba na waajiri wake wa zamani Simba na hatimaye kupelekea kulipishwa faini, unaambiwa beki huyo alisainishiwa mkataba kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
“Baada ya kuvishwa jezi ya Yanga na maneno mengi kuibuka, uongozi ulinisainisha mkataba siku hiyo hiyo kwa Mkapa ndipo nilipoamua kwenya Morogoro kuendelea na mapumziko maana nakumbuka nilikuwa nimefungiwa mechi tano kwa madai kwamba nimeigharimu timu,” anasema na kuongeza;
“Kitendo cha kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Toto Africans mchezo uliomalizika kwa Simba kupoteza kwa bao 1-0 hiyo ndio ilikuwa sababu ya mimi kusimamishwa, hawakuchukulia kama sehemu ya mchezo waliamini niliigharimu timu,”
AVAMIA KAMBI UTURUKI
Unashangaa Kessy kuvishwa jezi ya Yanga akiwa bado hajamaliza mkataba na waajiri wake Simba? Basi unaambiwa hiyo ni trela tu, picha kamili ni kwamba kumbe beki huyo ya alijinoa na timu hiyo ya Jangwani mwezi mzima wakati Yanga ilipokuwa imeweka kambi Uturuki kujiandaa na msimu mpya wa ligi.
“Nakumbuka nilikuwa na adhabu ya kusimamishwa kwa muda na Simba wao wakiwa kwenye mashindano ya Mapinduzi Zanzibar mimi niliungana na Yanga Uturuki kwa siri bila picha zangu kupigwa nilifanya mazoezi na timu hiyo ikiwa chini ya kocha Hans Pluijm msimu wa 2016,” anasema.
NGOMA NUSU AMSTAAFISHE SOKA
‘Kampa Kampa Tena’ ulikuwa ni msemo maarufu wa tambo za mashabiki wa Simba kwamba soka lao ni pasi nyingi, lakini ghafla uligeuka kuwa kebehi kwa klabu hiyo ya Msimbazi ambayo haikuutaka tena baada ya Kessy kumrudishia mpira kipa wake, Vincent Angban kwa pasi fupi na kunaswa na mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma aliyeukwamisha mpira nyavuni katika mchezo baina ya timu hizo uliofanyika Machi mwaka na Simba kufungwa mabao 2-0.
Msemo huo ukageuzwa na msahbaiki wa Yanga wakisema “Kampa, Kampa Ngoma”.
“Sikufanya makusudi siku ile, ilikuwa bahati mbaya nilirudisha mpira kwa kipa, pasi haikuwa na nguvu, Ngoma akaiwahi, nikajikuta naiponza timu, sikulala siku hiyo. Siku iliyofuata niliomba kwenda kwetu Morogoro kupumzika,” anasema na kuongeza;
“Ni tukio ambalo sitakaa nikalisahau lilinivua nguo kwani nilitupiwa matusi ya kila aina hadi mashabiki walipata namba yangu na kuanza kunipigia na kunitukana nikazima simu na kujipa mapumziko ya muda.”
KABURU ALIVYOMRUDISHA UWANJANI
“Tukio la Ngoma lilinifanya niuchukie kabisa mpira nakumbuka kwenye mkataba wangu wa mwaka na nusu nilikuwa tayari nimeutumikoa mwaka nilibakiza miezi sita nikaomba wanikate mshahara nisimalize muda uliobaki,” anasema na kuongeza;
“Aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geodfrey Nyange ‘Kaburu’ alinipigia simu na kunisisitiza nirudi kumalizia mkataba matukio kama hayo huwa yanatokea kwenye mpira nilirudi kulikuwa na mechi ya ligi dhidi ya Mbeya City tukafungwa lawama zikawa upande wang.”
Kessy anasema baada ya matokeo kikaitishwa kikao anakumbuka alikuja muigizaji Chuma Suleiman ‘Bi Hindu’ na Mzee Kilomoni waliwasema sana yeye pamoja na Hamis Kiiza.
Anaongeza kuwa hayakuishia hapo walipata nafasi ya kucheza tena na Toto African alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo alizidi kujichimbia kaburi.
“Hiyo siku tukio wala halikuwa la kadi nyekundu lakini mwamuzi alifanya hivyo basi Haji Manara alinishambulia sana na ndio ukawa mwanzo wa kunisimamisha nisiwe pamoja na timu,” anasema.
Kessy anasema alisimamishwa akiwa amebakiza miezi mitatu kwenye mkataba wake ndipo alipoanza mazungumzo na Yanga.
MECHI SABA MIAKA MIWILI
“Nilipandishwa kutoka timu ya vijana nakumbuka nilicheza mechi saba tu kwenye mkataba wa miaka miwili niliyosainishwa baada ya kupanda baada ya hapo nilikaa nje ya uwanja mwaka mmoja na nusu,” anasema na kuongeza;
“Sababu kubwa ya mimi kukaa nje ni ugonjwa nilioupata ambao hata sikufahamu ulitokana na nini lakini naushuru uongozi wa Mtibwa chini ya Byser walikuwa na mimi nyakati zote bila kujali ninayoyapitia.”
Usikose mwendelezo wa makala haya Kessy akizungumzia mengi zaidi ya kumhusu.