Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanakuri mwamba aliyemaliza marathoni baada ya miaka 54

Muktasari:

  • Kwa sasa rekodi ya muda bora ya marathon inashikiliwa na Mkenya Kelvin Kiptum aliyoiweka  Oktoba 8, 2023, Chicago, Marekani.

MBIO za marathon zimetoa wakimbiaji wengi maarufu na wameweka rekodi za muda tofauti kwa vipindi tofauti.

Kwa sasa rekodi ya muda bora ya marathon inashikiliwa na Mkenya Kelvin Kiptum aliyoiweka  Oktoba 8, 2023, Chicago, Marekani.

Zipo rekodi nyingi zilizovunjwa na kuingizwa kwenye kitabu cha rekodi za dunia cha ‘World Books of Record’ cha Guiness.

Iliwahi kutokea kwa mwanariadha wa Tanzania, John Stephen Akhwari katika Michezo ya Olimpiki ya Mexico City, Mexico, mwaka 1968 mbio za Marathon Kilomita 42.

Nyota huyo ambaye alibakiza kilomita 19 kumaliza mbio hizo, aliumia na kuonekana angeshindwa kumaliza.

Hata hivyo, alimaliza mbio hizo akitumia saa 3:25:27 wakati mshindi alimaliza kwa saa 2:20:26 (Mamo Wolde wa Ethiopia).

Sasa kwenye suala la kumaliza. Si Akhwarii tu aliyetaka kumaliza licha ya kuumia.

Katika historia ya mbio hizo, kuna mwanariadha aliyefahamika kwa jina la Shizo Kanakuri kutoka Japan.

Mwanariadha huyu aliweka historia ya aina yake alipotumia muda mrefu zaidi kumaliza mbio za marathon na alifanya hivyo kwa takriban miaka 54, miezi nane, siku sita, saa 5:32:20.3.

Ilikuaje? Fuatilia hapa historia ya maisha yake na historia aliyoiandika ya kuanza na kumaliza mbio kwa muda mrefu tangu mwaka 1912 hadi 1967.


KANAKURI NI NANI?

Alizaliwa katika Kisiwa cha Kyushu, Nagomi, Japan, Agosti 20, 1891.

Familia yake iljihusisha na uuzaji wa pombe na mwenyewe alikuwa akisoma shule.

Kila siku, Kanakuri alilazimika kukimbia kilomita sita hadi shule kuwahi masomo.


MAPENZI NA RIADHA

Kanakuri alionyesha mapenzi na mchezo huo tangu akiwa mdogo hadi alipofikisha umri wa miaka 20 mwaka 1911 kuamua kuingia katika shindano la kusaka vipaji vya wakimbiaji watakaoiwakilisha Japan katika michezo ya Olimpiki ya Stockholm mwaka uliofuata 1912.

Katika mbio hizo za kilomita 40, alishinda akitumia muda wa saa 2:30:33 akiweka rekodi.

Walichaguliwa wawili akiwamo yeye kuiwakilisha nchi, lakini kamati ya Olimpiki ya nchi yao, iliwataka wajigharimie nauli kwani haikuwa na hela na gharama ni Dola 12.

 Kwa sababu hiyo, wanafunzi wenzake waliamua kuanzisha harambee ya kukusanya pesa hizo ili kufanikisha safari yao na walipata Dola 10, huku kiasi kilichobaki alipewa na kaka yake mkubwa, Sanetsugu Kanakuri.

Katika harakati za kujiandaa, Kanakuri alikuwa akifanya mazoezi na Kano Jigoro ambaye ni mwanzilishi wa mchezo wa Judo. Kwa wakati huo aliweka rekodi ya kuwa mwanariadha wa kwanza wa Japan kushiriki Olimpiki.


MAUZAUZA YA SAFARI

Baada ya kupata nauli, alianza safari ngumu ya siku 18 kwenda Stockholm, kwanza kwa meli na kisha kwa treni kupitia Reli ya Trans-Siberian na hadi anafika Stockholm alikuwa amechoka sana kutokana na safari ndefu.

Pia alishindwa kulala muda mwingi kwa sababu ya majira ya mwaka na kwa wakati huo ilikuwa ni kipindi cha kiangazi na giza halikuwa likiingia kabisa.

Pia alipata tabu katika chakula cha Sweden, na zaidi kocha wa timu ya taifa, Hyozo Omoro aliwekwa karantini kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu na Kanakuri alishindwa kupata mazoezi ya kutosha kabla ya mbio.


HALI MBAYA, ATOWEKA SWEDEN

Siku ya mbio hizo zilizofanyika katikati ya Jiji la  Stockholm hali ya hewa ilikuwa mbaya na joto kali lilisababisha baadhi ya washiriki walikuwa wakidondoka akiwamo mmoja aliyefariki dunia, Francisco Lazaro akiwa ni mwanariadha wa kwanza kufariki dunia akiwa anashiriki Michezo ya Olimpiki..

Kanakuri pia alikuwa miangoni mwa waliokumbana na hali hiyo kali ya joto na kuwa mchovu baada ya kukimbia kilomita 16.

Alishindwa kuendelea na kuishia njiani na alikuta sherehe moja na kujumuika na kupata juisi ya machungwa ili kujiweka sawa kisha kupumzika kwa saa moja.

Aliona aibu kurudi mashindanoni na kimya kimya aliamua kurudi Japan huku nyuma wasijue alikokwenda na kuzua gumzo wakiamini amepotea.

Hali hiyo iliwalazimu mamlaka za usalama kumweka katika orodha ya waliopototea na jina lake likadumu hapo kwa miaka hamsini.


AIBUKIA MBIO NYINGINE

Huku Sweden wakijua amepotea, aliibukia kwenye mbio nyingine na alichaguliwa kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1916, Ujerumani ingawa haikufanyika kutokana na kuanza kwa vita vya kwanza vya dunia.

Hata hivyo, alishiriki Olimpiki ya mwaka 1920 ya Antwerp, Ubelgiji na kumaliza nafasi ya 16, akitumia saa 2:48:45.4 na  Olimpiki ya mwaka 1924 na alishindwa kumaliza.


ALIVYORUDI SWEDEN KUMALIZIA MBIO

Baada ya muda mrefu kupita, mwandishi mmoja wa habari wa Sweden alipata taarifa Kanakuri ni mzima na yupo kwao Japan.

Mwandishi huyo alifunga safari hadi Japan kujiridhisha na taarifa hizo na alimkuta ni mwalimu wa somo la Jiografia.

Baada ya kumfanyia mahojiano, televisheni ya Sveriges Television ilimpa fursa ya kurudi kumaliza mbio na alikubali.

Alipofika Sweden alianza mazoezi na siku ya mbio, alienda pale pale alipoishia na kuendelea hadi alipomaliza ikiwa ni mwaka 1967. ikiwamo pia mahali aliposimama na kunywa juisi.

 Alisema, “Ilikuwa safari ndefu. Njiani nilioa, nilipata watoto sita na wajukuu 10.”

Kanakuri anajulikana kwa mchango wake katika kuanzisha marathon ya Hakone Ekiden mwaka 1920. Tangu mwaka 2004, zawadi katika mbio hizo zimepewa jina lake kwa heshima yake. Alifariki dunia Novemba, 13, 1983 akiwa na umri wa miaka 92, Tamana, Japan.