KAGERE: Mfalme mwenye rekodi tamu Bara
Muktasari:
- Nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya na Simba anayekipiga kwa sasa Namungo ni kama simba aliyelowa, kwani huwezi kumfananisha na nyani.
KABLA ya mechi ya jana mchana kati ya Fountain Gate na Namungo, Meddie Kagere ‘MK 14’ a.k.a The Terminator’ hakuna bao lolote katika Ligi Kuu Bara, lakini hiyo haimfanyi mshambuliaji huyo mkongwe kuendelea kukumbukwa na mashabiki wa soka kwa rekodi alizoziandika tangu alipotua nchini mwaka 2018.
Nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya na Simba anayekipiga kwa sasa Namungo ni kama simba aliyelowa, kwani huwezi kumfananisha na nyani.
Mkongwe huyo raia wa Rwanda mwenye asili ya Uganda wakati anaondoka Msimbazi alikuwa na rekodi tamu kwa mastaa wa kigeni katika Ligi Kuu Bara ambayo imeendelea kuishi hadi leo, kwani licha ya wachezaji wengi waliokuwa bora na wazoefu kucheza ila wameshindwa kuifikia.
Kagere alitua Simba akitokea Gor Mahia msimu wa 2018-2019 na kufunga mabao 23 na kuipiku rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ya wachezaji wa kigeni kufunga mabao mengi msimu mmoja alipofunga 21 msimu wa 2015-2016.
Msimu wa pili kwa staa huyo akiwa na Simba pia, alifunga mabao 22 na kutetea tuzo ya mfungaji bora ikiwa pia ni rekodi kwani, haikuwahi kutokea kwa mchezaji yeyote iwe mzawa au wa kigeni kutwaa tuzo ya ufungaji bora mara mbili mfululizo.
Nyota wengine waliotwaa tuzo ya mfungaji bora japo kwa msimu tofauti tangu mwaka 2000 ni Simon Msuva, Tambwe na John Bocco.
Bocco alitwaa msimu wa 2011-2012 enzi akiwa na Azam FC alipofunga mabao 19 akairudia tena 2020-2021 alipokuwa na Simba akifunga 16 huku Tambwe akiinyakua 2013-14 akiwa Simba alipofunga 19 kisha akaichukua alipokuwa Yanga 2015-2016 akifunga 21.
Kwa upande wa Simon Msuva alichukua tuzo hiyo akiwa na Yanga akifanya hivyo msimu wa 2014-2015 alipofunga mabao 17 kisha akairudia tena msimu wa 2016-2017 wakati alipofunga 14 sambamba na aliyekuwa nyota wa Ruvu Shooting, Abdulrahman Mussa.
Rekodi hiyo ya Kagere ya kuibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo imeendelea kuwatesa washambuliaji kwani hata msimu uliopita tulishuhudia kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI akiibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21.
Aziz Ki alishinda vita hiyo katika michezo ya mwisho ya msimu baada ya kushindana na nyota wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyemaliza na mabao 19, jambo linalosubiriwa kuona kama ataweza kuifikia rekodi ya Kagere iliyowashinda wengi. Lakini hadi unaposoma makala haya Aziz Ki alikuwa amefunga bao moja tu na asisti nne, kuonyesha ana kibarua kizito kuifikia rekodi hiyo ya Kagere ya kutwaa tuzo back 2 back katika Ligi Kuu Bara.
Msimu wa mwisho wa Kagere akiwa Msimbazi ulikuwa wa 2021-2022 ambapo katika Ligi Kuu alicheza michezo 25, sawa na dakika 1286 akichangia mabao tisa ya timu hiyo baada ya kufunga saba na kuasisti mawili tu.
Baada ya hapo ‘MK14’ akaachana na kikosi cha Simba na kujiunga na Singida Big Stars msimu wa 2022-2023 ambapo aliendelea kuonyesha kiwango bora kufuatia kufunga mabao manane, kisha msimu uliopita akaichezea Namungo na kufunga mabao mawili.
Kwa sasa nyota huyo anaandamwa na ukame wa mabao kwa sababu mchezo wake wa mwisho kufunga bao ulikuwa Februari 24, 2024, dhidi ya KMC FC, ambapo kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’ kikicheza ugenini kilitoka sare ya kufungana kwa mabao 2-2.
Licha ya ukame huo, ila bado Kagere ni moja ya washambuliaji bora wa kigeni wanaocheza Ligi Kuu Bara ambapo rekodi zake zinaendelea kuishi, hususani ile ya kuibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo ambayo hadi leo hii imeshindwa kufikiwa.
Rekodi zinaonyesha katika misimu saba aliyocheza Ligi Kuu, amefunga jumla ya mabao 75 akilingana na Amissi Tambwe aliyefunga idadi kama hiyo, lakini katika misimu nane akiwa na timu za Simba, Yanga na Singida BS.
MSIKIE NGAWINA
Kocha Msaidizi wa Namungo, Ngawina Ngawina anasema bado wana matumaini makubwa kwa mchezaji huyo na suala la kutokufunga kwake hadi sasa ni jambo la kawaida kwa mshambuliaji, huku akieleza changamoto hiyo imewakumba wengi na sio yeye pekee.
“Msimu umekuwa mgumu sana na sio yeye pekee ambaye hajafunga wapo wengi tu, sisi kama benchi letu la ufundi tutaendelea kumjenga kimwili na kiakili kuhakikisha anarudi katika ubora wake, atakapofunga ataanza kutengeneza hali ya kujiamini,” anasema