Prime
Kutoka Nonda hadi Mayele hii ni Yanga ya kimataifa
Muktasari:
- Mayele ndiye mchezaji pekee katika kikosi hicho anayekipiga kwenye ligi ya Afrika; wengine wote wanacheza ligi za nje ya bara hilo.
KESHO Jumatano, Juni 17, timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo itakuwa na kibarua cha kukabiliana na Ureno katika mechi yao ya ufunguzi wa kampeni za mwaka huu. Ndani ya kikosi hicho yupo mtu wa kuitwa Fiston Mayele, mzee wa kutetema.
Mayele ndiye mchezaji pekee katika kikosi hicho anayekipiga kwenye ligi ya Afrika; wengine wote wanacheza ligi za nje ya bara hilo.
Kikosi hicho cha watu 26 chini ya Kocha Sebastien Desabre kinaundwa na wachezaji kutoka ligi mbalimbali za Ulaya, akiwemo Chancel Mbemba wa Lille na Yoane Wissa wa Newcastle United, huku wengine wakitoka katika klabu za Uturuki, Ugiriki na mataifa ya Mashariki ya Kati. Hiki ni kikosi kilichosheheni nyota, hivyo uwepo wa Mayele ndani yake si jambo la kuchukulia poa.
Mayele ambaye amesaini kuichezea Al-Fateh ya Saudi Arabia akitokea Pyramids ya Misri, alicheza Tanzania kwa misimu miwili, 2021/22 na 2022/23, akiitumikia Yanga. Hali hiyo inamfanya Mayele kuwa mwakilishi wa Ligi Kuu Bara kwenye Kombe la Dunia.
Hapa ndipo Yanga inapoibuka kidedea mbele ya wengine, kwa sababu inakuwa klabu ya kwanza Tanzania angalau kuwa na mchezaji kwenye Kombe la Dunia aliyewahi kuwa wa kwao.
Hii ni historia ambayo haiwezi kubadilika, kwa sababu mafanikio haya ya Mayele yana mchango mkubwa wa Yanga. Itakumbukwa ni Yanga iliyompandisha Mayele kwenye kilele cha ubora Afrika katika msimu ambao walifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hili linaelekea kuwa utamaduni wa klabu hiyo yenye maskani yake kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.
Mwaka 1995, klabu hiyo ilimsajili mchezaji chipukizi kutoka Atletico Olympic FC ya Burundi, Nonda Shaban. Akacheza msimu mmoja kisha kutimkia Vaal Professionals ya Afrika Kusini, baadaye FC Zurich ya Uswisi, Monaco ya Ufaransa na hatimaye Blackburn Rovers ya England.
Akiwa Monaco chini ya Kocha Didier Deschamps, ambaye sasa anaifundisha Ufaransa, Nonda alifanya maajabu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hadi kufika fainali mwaka 2004.
Katika nusu fainali alifunga bao la tatu dhidi ya Chelsea ya England katika ushindi wa mabao 3-1. Monaco ikaenda fainali na Nonda akacheza, japo walipoteza dhidi ya FC Porto ya Ureno chini ya Jose Mourinho.
Wakati huo, Tanzania tulikuwa tunaangalia mashindano hayo kupitia ITV iliyokuwa ikiunganishwa na kituo cha Canal+ cha Ufaransa.
Mtangazaji wa mechi hizo alikuwa akirudia mara kwa mara Nonda Shaban aliwahi kuichezea Yanga ya Tanzania. Nonda Shaban aliipeleka juu sana Yanga.
Na sasa Fiston Mayele anaelekea kuipeleka juu zaidi Yanga.
Wachezaji hawa wote walipandishwa juu na Yanga, na baadaye wao wakaja kuipandisha Yanga.
Nonda Shaban alicheza mechi ya mkondo wa kwanza ya Kombe la CAF (ambalo sasa halipo tena) dhidi ya Vaal Professionals ya Afrika Kusini. Ulikuwa mchezo wa mkondo wa kwanza ugenini, na Yanga wakapoteza kwa mabao 3-2.
Nonda alifunga bao la pili la Yanga katika dakika za mwisho kabisa na Wasauzi wakavutiwa naye na kumng’ng’nia. Nonda hakurudi Tanzania kwa mechi ya mkondo wa pili; akabaki huko huko, na ndipo safari yake ikaendelea hadi Ulaya.
Kama si Yanga kumtambulisha kimataifa, huenda safari yake ingechukua njia nyingine na pengine ingechukua muda mrefu zaidi. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mayele. Baada ya wachezaji hawa kupaishwa na Yanga hadi juu, nao wakarudi kwa namna nyingine kuipaisha Yanga. Nonda akaitangaza Yanga kupitia Ligi ya Mabingwa Ulaya na Mayele anaenda kuitangaza Yanga kupitia Kombe la Dunia.
Hakuna klabu nyingine yoyote Tanzania iliyotoa mchezaji aliyefikia mafanikio hayo; ni Yanga pekee. Na kama Mayele atafunga bao kwenye Kombe la Dunia, itakuwa fahari kubwa sana kwa wananchi.
WANANCHI NA WAKONGOMANI
Yanga ni klabu yenye mahusiano ya kihistoria na taifa la Kongo tangu enzi za Zaire ya Mobutu Sese Seko.
Historia hiyo inaanzia mwaka 1971, pale klabu hiyo ilipomsajili winga wa AS Vita Club ya Kinshasa aliyekuja Tanzania kumfuata baba yake, ambaye alikuwa afisa wa ubalozi wa nchi yake nchini.
Winga huyo aliitwa Fred Mayaula Mayoni, ambaye miaka mingi baadaye aliacha mpira na kuwa mwanamuziki mkubwa Afrika.
Mayaula Mayoni aliitumikia Yanga kwa mwaka mmoja, 1971 na miongoni mwa kumbukumbu zake ni mabao mawili aliyofunga dhidi ya watani wao Simba SC, ambao wakati huo walikuwa bado wanaitwa Sunderland. Yanga ilishinda mchezo huo kwa mabao 2-1, huku bao la Sunderland likifungwa na Omar Gumbo.
Mayaula Mayoni akafungua milango ya Wakongo kwa wananchi, na mwaka 1974 akaja kocha Tambwe Leya. Huyu ni mmoja wa makocha bora kuwahi kuifundisha timu hiyo na aliendeleza mahusiano ya Wakongo na Yanga.
Maisha yaliendelea hivyo, na wengine wengi wakaendelea kuja na kuondoka kwa miaka mingi, hadi sasa tunawaona kina Maxi Nzengeli.
Kila la heri Mayele kwenye mchezo wa kesho. Watangaze wananchi, utangaze Ligi ya Tanzania.