Kabunda: Kutofunga inaumiza, Simba, Yanga nitacheza tu

Muktasari:
- Licha ya kutopita kwenye klabu za Simba na Yanga, lakini aliwahi kuhusishwa nazo, akiamini kuwa bado muda haujafika, ila ipo siku kitaeleweka tu.
KIUNGO mshambuliaji wa Namungo, Hassan Kabunda ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Ligi Kuu Bara ambao hawajapita mitaa ya Msimbazi na Jangwani.
Licha ya kutopita kwenye klabu za Simba na Yanga, lakini aliwahi kuhusishwa nazo, akiamini kuwa bado muda haujafika, ila ipo siku kitaeleweka tu.
Kabla ya kusajiliwa Namungo msimu wa 2022/23 akitokea KMC hakuwa na msimu mzuri, kwani ndani ya kipindi hicho alitupia kambani mabao manne kwenye mechi 60.
Mwanaspoti lilifanya mahojiano na kiungo huyo, akifafanua mambo mengi ikiwemo mwenendo wa Namungo katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

ISHU YA MASTRAIKA
Msimu uliopita mshambuliaji Pius Buswita ndiye alikuwa kinara wa ufungaji kwa Namungo akimaliza na mabao saba, huku beki Derick Mukombozi akiweka wavuni mabao manne jambo linalowasumbua mastraika kwa sasa kutokana na kufunga mabao ya kutosha.
Kabunda, nyota huyo wa zamani wa KMC anasema hawajisikii vizuri pindi mabeki wanapofunga ilhali washambuliaji na viungo wapo.
Anasema kutokana na mabadiliko ya mifumo kwa sasa kila mchezaji ana kazi ya kufunga na kuisaidia timu kupata matoke mazuri ingawa mabeki wamekuwa na nafasi kubwa ya kutupia mipira wavuni.
"Ni kweli ukiangalia mabeki wanafunga haileti picha nzuri kama washambuliaji. Tunatakiwa kubadilika na hili sio tu kwa timu hizi, bali hata timu kubwa," anasema mchezaji huyo.
Ukimuulizwa kuhusu msimu mzima uliopita kufunga bao moja anajibu, "msimu uliopita nilimaliza na bao moja, sikuwa napata nafasi kubwa ya kucheza. Naamini huu utakuwa bora kwangu."

SIMBA, YANGA NACHEZA
Ni ndoto ya wachezaji wengi ndani na nje ya Tanzania kuchezea klabu kubwa za Simba na Yanga. Ndivyo ilivyo kwa Kabunda.
Anasema ingawa aliwahi kuhusishwa na klabu hizo za Kariakoo miaka ya nyuma, lakini anaamini muda utafika na atacheza Simba na Yanga.
"Afrika hii hakuna mchezaji asiyetamani kucheza Simba na Yanga kutokana na umaarufu wao kimataifa. Naamini muda bado, nitacheza tu siku moja," anasema.
Tangu aanze kucheza Ligi Kuu 2017 akiwa na Mwadui ya Shinyanga hadi sasa mchezaji huyo hajafanikiwa kucheza ardhi nyingine zaidi ya Tanzania.
"Kila kitu ni uvumilivu tu naamini muda ukifika hata kimataifa nitatoboa na malengo yangu siku moja nicheze Ulaya kama Mbwana Samatta au hata zaidi."

KINACHOIKUMBA NAMUNGO
Hadi sasa Namungo imecheza mechi 10 za Ligi Kuu ikishinda tatu, haijatoa sare, lakini ikipoteza mechi saba ikiwa katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi.
Kabunda anasema kama wachezaji hawajisikii vizuri timu inapokuwa na mwendelezo mbaya wa matokeo.
"Ligi imekuwa ngumu sana msimu huu, tofauti na uliopita. Kwa hiyo inaumiza kama timu mnaanza msimu kwenye mechi 10 mnapoteza nyingi kuliko ushindi, lakini bado haijaisha, tunaamini tutafanya vizuri," anasema Kabunda.

FAMILIA YA MICHEZO
Kabunda anasema kwenye familia sio wa kwanza kusaka kandanda kwani baba yake mzazi, Salum Kabunda 'Ninja' aliwahi kukipiga Yanga 1994.
"Sikumshuhudia baba yangu akicheza, lakini mimi sio wa kwanza na naweza kusema familia yetu ni soka, kwani hata wadogo zangu wanaonifuatia wanacheza," anasema
"Ukiachana na ndugu zangu pia mama mzazi alikuwa anacheza netiboli zamani. Kwa hiyo kiufupi ni familia ya wanamichezo."

HISTORIA YAKE
Kabunda anasema, "nilizaliwa Juni 10, 1996 hapa Ilala, Dar es Salaam. Nimesoma Shule ya Msingi Amana. Nilipomaliza masomo nikaanza mambo yangu ya soka na hapo nikachukuliwa na kituo cha kukuza kipaji DYOC cha Kocha Ramadhan Aluko ambao walinisomesha sekondari."
"Nilikuwa pale hadi nilipomaliza sekondari, tulikuwa tunacheza mashindano mbalimbali wakati mwingine tulishiriki mashindano na wazungu.
"Haikuwa muda mrefu tukaanza kuccheza Ligi daraja la tatu na tukawa tunasafiri nchi jirani kama Kenya, Uganda kucheza mechi ambazo zilitujenga ukomavu."
Anasema alianza kucheza mashindano ya Umisseta na wakafanikiwa kubeba ubingwa, na baadaye alipomaliza shule alichukuliwa na timu kutoka Temeke kucheza Copa Cocacola."
Baadaye 2014 alijiunga na timu ya vijana ya African Lyon kwa misimu miwili, kisha akasajiliwa Ashanti alikohudumu kwa msimu mmoja na iliposhuka alitambulishwa Mwadui.
ALIKOPITA
Mwadui, KMC, Namungo, Ashanti United na African Lyon