Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JIWE LA SIKU: Safari ya Chama  ilianzia katika 5-1

Muktasari:

  • Chama amejiunga na Yanga akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake wa miaka miwili na Simba kufikia tamati, Juni 30 mwaka huu na klabu hiyo kuamua kutomuongezea mkataba kiungo huyo mshambuliaji wa Zambia.

BAADA ya muda mrefu wa kuhusishwa kwa muda mrefu kusajiliwa na Yanga, hatimaye mapema Jumatatu, wiki hii Clatous Chama alitambulishwa rasmi na klabu hiyo kama mchezaji wao mpya.

Chama amejiunga na Yanga akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake wa miaka miwili na Simba kufikia tamati, Juni 30 mwaka huu na klabu hiyo kuamua kutomuongezea mkataba kiungo mshambuliaji huyo wa Zambia.

Karibu katika kila dirisha la usajili, Chama alikuwa akihusishwa na kutua Yanga hadi ikazua msemo kwamba "Chama ndiye mchezaji pekee ambaye kila msimu anasajiliwa na Yanga lakini anachezea Simba."

Kulikuwa na maneno mengi mtaani wengine wakidai kwamba Chama alikuwa akiitumia Yanga kuboreshewa maslahi yake na Simba.

Ilidaiwa kila mkataba wa Chama ulipomalizika ama ulipokaribia kumalizika, zilianzishwa kwa makusudi tu stori za kwamba Mwamba wa Lusaka anajiandaa kutua Yanga.

Jambo hilo likatajwa kama gia nzuri kabisa ya Chama kuongezwa mkataba mpya mnono zaidi wa kiwango kile alichotaka kwa sababu kutokana na ubora wake uwanjani, alikuwa ameshikilia mpini na klabu ya Simba ilikuwa imeshika kwenye makali. Kwa hali kama hiyo ungetarajia kabisa Chama kuwa mshindi, ushindi ambao ungemfanya kuwa mchezaji anayelipwa kibosi kabisa.      

Mara hii imekuwa tofauti. Kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja tetesi za Chama kuhusishwa kujiunga na Yanga zilikuwa zikisambaa kwa kasi zaidi ya wakati mwingine wowote katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii huku ikitajwa kwamba Simba haikuwa na mpango wa kumpa mkataba mpya.

Unamzungumzia Chama, mchezaji aliyejenga jina na heshima kubwa ndani ya Simba huku akiwa kipenzi cha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo tangu alipojiunga nayo mwaka 2017 akitokea Zesco United ya Zambia.

Ni mchezaji aliyefanya makubwa ndani ya Simba na hilo linathibitishwa na takwimu ambazo ameacha katika mechi alizoichezea kwenye michuano ya ndani ya kimataifa.

Kwa mujibu wa takwimu, Chama katika michezo 179 ya Ligi Kuu na mashindano ya klabu Afrika, amehusika na idadi ya mabao 102 akifunga mabao 42 na kutoa asisti za mabao mengine 60.

Uamuzi wa Wekundu wa Msimbazi kuachana na Chama umechochea minong'ono ya muda mrefu ambayo ilikuwa ikiendelea ndani ya Simba ya kutokuwa na imani na kiungo mshambuliaji huyo akituhumiwa kuwa na uhusiano uliopitiliza na upande wa pili na kusababisha kuathiri kiwango chake ndani ya uwanja.

Ni kwa misimu mitatu mfululizo, viongozi na mashabiki wengi walikuwa wanamtazama Chama kama mtu ambaye amepoteza mapenzi ndani ya timu yao na anaitumikia kwa sababu ya fedha tu hivyo uzi baina yao ulikuwa unazidi kuwa mwembamba na kamba ilikuwa inaelekea kukatika.


Sio jambo la kificho kwamba kwa muda mrefu, viongozi wa Simba walikuwa wanatamani kuachana na Mwamba wa Lusaka hasa wakichagizwa na uvumi wa ripoti kutoka katika mabenchi yao ya ufundi ambayo mara kwa mara ikadaiwa yalishauri timu hiyo iachane na 'Tripple C' kama inataka kupiga hatua zaidi.

Hata hivyo, uamuzi wa kumuacha Chama ulikuwa mgumu kwa viongozi kwa vile walikuwa wanaogopa presha na lawama kutoka kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo kutokana na mahaba makubwa ambayo walikuwa nayo kwa nyota huyo kutokana na ukubwa wa vitu vyake uwanjani. Kwa sababu Mwamba wa Lusaka ni mwamba kwelikweli. Anarahisisha sana mambo pale mbele la lango la wapinzani. Ndio sababu mara utamuona amehusika katika takriban kila bao la Simba, kama sio kwa kufunga bao kutoa asisti, kama sio asisti basi atampasia mpira yule atakayetoa asisti (yaani pre-asist inakuwa yake). Unamuachaje mtu kama huyu? Hapo ndipo mtihani ulipokuwepo. 

Kulikosekana nyakati au tukio fulani ambalo lingewapa ujasiri viongozi kusimama mbele ya wanachama wao baada ya kuamua kuachana na Chama hadi pale ilipofika Novemba 5, 2023 pale ilipopoteza kwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ni matokeo ambayo kwa kiasi kikubwa yalibadilisha maisha na mitazamo ndani ya Simba na hilo linajidhihirisha katika namna tofauti.

Mahaba ya mashabiki wengi wa Simba kwa baadhi ya nyota ndani ya timu hiyo akiwemo Chama yalipungua wakiamini hawakucheza kwa kujituma katika mchezo huo huku wakienda mbali zaidi na kuwa tayari kuona wakitupiwa virago.

Kana kwamba haitoshi kulikuwa na tuhuma za baadhi ya wachezaji kuihujumu timu katika mchezo huo hadi kupelekea kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao mbele ya watani wao wa jadi.

Lakini kingine mashabiki walianza kuamini kuwa kumbe inawezekana kupoteza mchezo tena kwa idadi kubwa ya mabao hata ukiwa na mastaa wako wote kikosini, hivyo walianza kushinikiza kupewa nafasi kwa wachezaji ambao awali hawakuwa wakiaminiwa na benchi la ufundi mbele ya mastaa hao.

Hiyo ilitengeneza urahisi kwa uongozi wa Simba kuchukua uamuzi mgumu katika dirisha hili kubwa la usajili kwa vile unafahamu kuwa kundi kubwa la wanachama na mashabiki kwa sasa linaimba nao lugha moja tofauti na awali ambapo ingekuwa ngumu kufanya uamuzi ambao ungekuwa hauungwi mkono na mashabiki walio wengi.

Wimbo wa kuitengeneza Simba mpya na kuwapa mkono wa kwaheri mastaa ambao wamedumu kwa muda mrefu ulianza kusambaa na kueleweka kwa kasi vichwani mwa Wanasimba na wengi wakawa wanatamani kuona fagio la haja linapita ili waanze upya.

Kitendo cha kupewa 'Thank You' kwa watu kama John Bocco, Luis Miquissone na Saido Ntibazonkiza ambao walikuwa wachezaji waandamizi kikosini, kilikuwa ni kama kinawaandaa kisaikolojia mashabiki na wanachama kuwa wawe tayari hata kuondoka kwa kipenzi chao Chama.


Tangu Simba ilipofungwa mabao 5-1 na Yanga hadi dirisha la usajili lilipofika mashabiki, wanachama na viongozi wake walikuwa kama wamechomwa ganzi na wasingeweza kusikia maumivu yoyote kwa mchezaji yeyote kuondoka.

Ndio maana haikushangaza kuona licha ya kufahamu mkataba wa Chama unaelekea ukingoni, hawakujihangaisha kumuongezea mkataba mpya na badala yake wakawa wanampambania Kibu Denis abaki.