Prime
JICHO LA MWEWE: Ya Dube, maandiko yametimia

Muktasari:
- Ijumaa usiku Azam walitema bungo wakati walipotangaza rasmi kwamba wamefikia makubaliano ya kuachana na mshambuliaji wao Prince Dube. Mmoja kati ya washambuliaji wazuri waliotokana na kazi nzuri ya uchunguzi wa kusaka wachezaji ambayo Azam wamefanya miaka ya karibuni. Wazungu wanaita ‘scouting’.
HATA leo usiku Prince Dube anaweza kutangazwa kuwa mchezaji mpya wa Yanga. Hii ni kati ya siri zilizofichwa vibaya katika soka letu. Siri nyingine iliyofichwa vibaya ni ile ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuondoka Yanga kwenda Azam. Hatimaye kisasi kimelipwa. Usingetazamia kama maisha yangekwenda haraka kwa namna hii.
Ijumaa usiku Azam walitema bungo wakati walipotangaza rasmi kwamba wamefikia makubaliano ya kuachana na mshambuliaji wao Prince Dube. Mmoja kati ya washambuliaji wazuri waliotokana na kazi nzuri ya uchunguzi wa kusaka wachezaji ambayo Azam wamefanya miaka ya karibuni. Wazungu wanaita ‘scouting’.
Alitoka kwao akaingia nchini kimya kimya. Hatujui Azam walimuona wapi. Msimu wake wa kwanza tu uliwaacha wakubwa wakitokwa na udenda kutokana na uwezo wake wa kuziona nyavu. Hata hivyo kutokana na utajiri wa Azam haikuonekana kama Dube angeweza kwenda kokote kati ya Simba na Yanga mpaka alipoingia katika mtego wa kukomoana kwa wakubwa.
Nadhani Yanga walijiapiza kwamba kwa namna yeyote ile wangevamia katika kambi ya Azam na kulipa kisasi baada ya kile walichofanyiwa kwa Fei. Na inaonekana Dube mwenyewe alishachoka kukaa Chamazi. Alitamani ‘vibe’ ya timu kubwa za Kariakoo.
Shughuli ya Dube imekwisha. Mzunguko wa kukomoana kati ya Yanga na Azam umefikia mwisho Ijumaa usiku. Wakati ule wa sakata la Fei Toto wote tulijua kwamba Azam walikuwa nyuma ya biashara nzima. Baada ya Mama Samia kushauri Yanga wamalizane na Fei haikuchukua saa 72 Azam walikuwa wanatangaza kumsajili Fei kwa mkataba wa miaka mitatu. Kama usingesukwa mpango ina maana hata Simba wangeingia katika mbio.
Ni kama ambavyo safari hii tulijua kwamba Yanga walikuwa nyuma ya Dube katika sakata zima lililoendelea hapa karibuni wakati mjukuu huyu wa Robert Mugabe alipohaha kuhakikisha mkataba wake na Azam unavunjwa. Simba walijaribu kuweka pua yao lakini waliambulia aibu kwa sababu hawakuandaa mkakati mzima wa kumtorosha Azam halafu wakavamia kitu wasichokijua.
Inatajwa kwamba Azam walikuwa tayari kumruhusu Dube aende Simba kuliko kwenda Yanga. Walipambana kadri walivyoweza kuhakikisha Dube anakwenda Simba lakini haikuwezekana. Tayari Yanga walishaweka mkono wao siku nyingi. Wao ndio walioanzisha filamu nzima wasingeweza kushindwa kirahisi.
Ni kama ambavyo Azam walianzisha vema filamu ya Fei na hata kama Yanga wangemlazimisha Fei kwenda kwingineko bado isingewezekana. Hili ndio tatizo la kuzungukana. Lakini pia ndio tatizo la nguvu kubwa ambayo mwanasoka anayo katika mchezo huu. Akiamua jambo lake hata wakala wake au meneja wake hawezi kumbadili mawazo. Hata timu iliyopo haiwezi kumbadili mawazo.
Ni mwendelezo wa ghafla wa wachezaji wetu kupambana kukatisha mikataba yao baada ya kukutana katika mikutano ya siri na klabu nyingine bila ya ruhusa ya klabu zao. Alifanya Fei na sasa amefanya Dube. Wote wamefanikiwa. Nani anafuata? Ni jambo linalofikirisha kwa kiasi kikubwa. Labda klabu zitashtuka kwa kiasi kikubwa na kuweka mikataba migumu kwa wachezaji wake.
Hili pia linatokana na ukweli kwamba klabu zetu hazina utamaduni wa kuuziana wachezaji. Mchezaji wa kwanza na wa mwisho kununuliwa kihalali kabisa katika klabu hizi kubwa alikuwa Mrisho Ngassa. Azam walipeleka ofa yao Yanga ikakubaliwa na Mwenyekiti, Imani Madega akamuuza kwa dau la Sh50 milioni. Zilikuwa nyingi wakati huo.
Vinginevyo baada ya hapo klabu zimekuwa zikitamani wachezaji wa wapinzani wao na sasa wameona njia bora zaidi ya kumnasa mchezaji wa timu pinzani mwenye mkataba ni kuhakikisha wanamfuata nyuma ya pazia na kumtengenezea njia za fitina za kugombana na waajiri wake ili ahame kwenda kwa wapinzani.
Nilidhani walau njia bora zaidi ni kumshawishi mchezaji wanayemtaka na aliye na mkataba asisaini mkataba mpya wakati mkataba wake utakapokuwa unakaribia kukata roho. Hili ni rahisi hasa unapozingatia kwamba wachezaji wetu wana mikataba ya muda mfupi tu. Wachezaji wetu wengi wanasaini mikataba ya miezi 24 tu. Kwanini usitengeneze fitina hii?
Matokeo yake wachezaji hawa Fei na Dube waliziacha timu zao wakati msimu ukiendelea huku wao wakiwa chaguo la kwanza katika klabu zao. Fei aliwaacha Yanga pabaya akaenda zake Forodhani Zanzibar kula urojo huku Yanga wakipambana kuitafuta fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kama angekuwepo Yanga ingetisha zaidi na zaidi.
Na sasa Dube yupo Yanga. Nini kinafuata? Yanga wanaenda kuimarika zaidi. Kama wakimpata Clatous Chotta Chama inaweza kuwa ‘dream team’. Timu yenye Dube, Chama, Pacome Zouzoua, Aziz Ki na Maxi Nzengeli katika eneo la ushambuliaji inabakia kuwa miongoni mwa timu bora za ukanda huu.
Kama kila mtu atacheza kwa ubora wake, halafu wakacheza kitimu zaidi na katika kasi zaidi basi Yanga watakuwa tishio. Wakiwa na wachezaji hao halafu wakacheza kama walivyocheza kwa misimu mitatu iliyopita basi wanaweza kuwa hatari zaidi kutokana na uwezo binafsi wa wachezaji wake.
Hata hivyo, sio mara zote timu ya namna hizi zinafanya kazi. Wakati mwingine timu inahitaji wachezaji waliotofautiana uwezo kwa ajili ya kutumikiana. Kumbuka Real Madrid ya Zinedine Zidane, David Beckham, Luis Figo na Ronaldo De Lima. Timu yao ilikosa balansi. Wachezaji wengi walijikuta na uwezo wa kuchezea mpira lakini hawakuwa bora wakati hawana mpira.
Kitu kizuri kuhusu Dube, na kama Chama atacheza Yanga, basi watakuwa wamewapata wachezaji ambao wamezoea mpira wetu na mazingira. Itakuwa wanajua vilivyo presha ya kucheza katika timu hizi kubwa ambazo hazihitaji chochote zaidi ya ushindi. Hata sare tu inakuwa kama kichapo. Inanikumbusha Simba ilipowasomba kwa pamoja John Bocco, Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe kutoka Azam.