JICHO LA MWEWE: Tunapompa mgongo Mbappe na kumtazama Mayele Ligi Kuu

KOMBE la Dunia limenikumbusha namna gani Yanga na Simba inabidi ziwe klabu tajiri sana. Juzi nilikuwa Morogoro mahala fulani nikitazama mechi ya Yanga na Mbeya City. Halafu hapo hapo pambano la Ufaransa dhidi ya Denmark lilikuwa linaendelea pale Qatar. 

Watu walilipa mgongo pambano la Ufaransa dhidi ya Denmark wakaligeukia pambano la Yanga. Dunia imejaa sana maajabu. Hapo kulikuwa na mambo kadhaa ambayo niliyatafakari. Namna ambavyo Watanzania huwa wana jambo lao linapofika suala la Simba na Yanga.

Nilitafakari kwamba Watanzania walikuwa wamechagua kutazama pambano la bingwa wa mtetezi wa Ligi kuu ya Tanzania bara kutoka Afrika Mashariki dhidi ya pambano la mabingwa wa Kombe la Dunia wakitetea taji lao dhidi ya Denmark. Kati ya hawa waliokuwa wanatazama pambano la Tanzania kulikuwa na Simba waliokuwa wanataka Yanga ifungwe na Yanga wenyewe waliokuwa wanataka timu yao ishinde.

Katika lugha nyingine ni kwamba walikuwa wamechagua kumtazama Fiston Mayele badala ya Kylian Mbappe ambaye anaitingisha dunia kwa sasa. Zaidi ya Mbappe kulikuwa na mastaa wengi wa kuwatazama katika kikosi cha Ufaransa lakini watu waliamua kumtazama Mayele na mastaa wa Yanga.

Nenda katika vibanda umiza au baa wakati Simba au Yanga inapocheza halafu pambano la Kombe la Dunia linapoendelea. Mashabiki wanachagua kutazama pambano la nyumbani. Inakuwa hivi katika mechi za Ligi Kuu ya England. Nilidhani katika Kombe la Dunia soka letu lingepoteza mvuto. Nilikosea.

Hii ina maana kwamba klabu zetu kubwa zinapendwa sana. Baada ya kupendwa kiasi hiki zinapaswa kuwa tajiri. Nashukuru kuna mambo ambayo wameanza kuyaona na sasa wanatumia kupendwa huku kwa ajili ya kupata pesa. Kwa kuanzia wanalipwa pesa nyingi katika suala la matangazo ya mechi zao pamoja na vipindi vyao vya televisheni. 

Kama watu wanaweza kukipa mgongo king’amuzi kinachoonyesha Kombe la Dunia na kisha kutazama pambano la Simba au Yanga basi ni mafanikio makubwa ya kibiashara kwa king’amuzi kinachoonyesha mechi zetu za ndani. Inathibitisha kwamba Azam wanastahili kuzilipa Simba na Yanga mabilioni ya pesa kama wanavyofanya sasa.

Fursa nyingine ambayo tunaweza kuwasifu ni namna kwa sasa wanavyoingia mikataba ya hela nyingi na wadhamini wakuu wa klabu hizo. Wanaotaka kukaa kifuani ni wazi kwamba wanalipa pesa nyingi kwa sasa kwa Simba na Yanga pengine kuliko wakati wowote wa historia zao.

Nakumbuka zamani wakati Wafadhili wa hizi klabu walipokuwa wanatangaza bure bidhaa zao katika jezi za Simba na Yanga. Rafiki zangu kina Abbas Gulamali na Azim Dewji walitumia ujanja mwingi kutangaza bure katika klabu hizi na ilikuwa inaonekana kama hisani tu kumbe walipaswa kulipa mabilioni ya fedha.

Fursa nyingine ambayo naamini Simba na Yanga wamekuwa wakiitumia vema katika miaka ya karibuni ni mauzo ya jezi zao. Kwa sasa wamekaa vizuri katika idara hiyo na wanastahili sifa. Zamani ilikuwa jambo la kawaida kwa shabiki wa Yanga kuvaa jezi ya Brazil akiamini kwamba inawakilisha Yanga 

Ilikuwa kitu cha kawaida kuona shabiki wa Simba akivaa jezi nyekundu ya Arsenal au Manchester United na kuhisi alikuwa akiwakilisha klabu yake ya Simba. Tangu mpira wetu uende kwa baadhi ya watu wenye mawazo ya kibiashara nadhani tumetumia vema fursa.

Eneo lililobaki ambalo limeanza kuzisumbua Simba na Yanga ni suala la mashabiki kujitokeza kwenda uwanjani kuzitazama mechi zao hasa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Siku hizi Simba na Yanga zinajaza kwenye viwanja vya mikoani tu na sio Uwanja wa Taifa. Tatizo liko wapi hasa? Nadhani inabidi wajichunguze.

Inasemwa kwamba tatizo lilikuja baada ya mechi zao kuanza kuonyeshwa katika televisheni. Sio kweli. Ulaya mechi zinaonyeshwa katika televisheni lakini bado viwanja vinajaa. Kuna mahali ambapo Simba na Yanga wanakosea. Miaka ya karibuni Simba ilikuwa inajaza uwanja katika mechi zake za kimataifa na bado mechi zilikuwa zinaonyeshwa katika tevisheni.

Eneo jingine ambalo Simba na Yanga wanapaswa kupambana ni kufanya vizuri katika mechi za kimataifa. Kwa namna ambavyo wana mashabiki wengi na wanapendwa inashangaza kuona kwamba bado wamejiwekea hatua kama ya nusu fainali kuwa mafanikio makubwa.

Endapo Simba na Yanga zitafanya vema katika eneo hilo zinaweza kuanza kupata mikataba katika kampuni za kimataifa moja kwa moja na sio lazima kwa kampuni ambazo zina matawi yake nchini. Mfano majuzi tuliona klabu ya Club Africain ikiitangaza kampuni ya Emirates. Inakuonyesha ukubwa wao.

Kina Al Ahly wamekuwa wakitangaza kampuni kubwa za kimataifa ambazo makao yake makuu hayapo Misri. Simba na Yanga zimeshatawala soko la ndani na ni wakati sasa zikaanza kujaribu kutawala soko la nje. Hata hivyo, wadhamini wa kimataifa hawawezi kuja kama na wao hawataanza kutawala soka la nje.

Hii yote itatokana na klabu kuanza kuongozwa na watu sahihi katika mifumo sahihi. Kikwazo kikubwa ambacho Simba na Yanga wanaweza kukumbana nacho katika suala la wao kuimarika ni namna Ligi yetu inavyoendeshwa. Kuna pengo kubwa kati ya wao na Azam halafu dhidi ya timu nyingine. Kuna tofauti kubwa ya kiuchumi na kiuwezo.

Kwanza walipaswa kupata ushindani sahihi kabla ya kufikiria ushindani wa nje. Walipaswa kupata mechi ngumu kwa ajili ya kuwaandaa wachezaji wao kwa mechi za kimataifa. Kwa sasa hali imekuwa tofauti na mechi zao nyingi zimekuwa hazina upinzani mkubwa wa kuwaandaa kimataifa.