JICHO LA MWEWE: Salamu za fundisho kutoka Real Madrid

JICHO LA MWEWE: Salamu za fundisho kutoka Real Madrid

MADRID ndipo nilipo. Na kundi la waandishi mbalimbali kutoka karibu kila kona ya dunia. Uingereza, India, Vietnam, Argentina, Brazil, Mexico, Afrika Kusini na kwingineko. Ile tabia maarufu ya wenzetu nimeiona katika uchunguzi wangu wa haraka haraka.

Tabia gani? Rafiki yangu wa kwanza kutoka Uingereza nilimuuliza timu ambayo anashabikia. Akanijibu’ “Tranmere Rovers”. Binafsi naifahamu timu hii, lakini nafahamu kwamba Watanzania wengi hawaifahamu kwa sababu haijacheza Ligi Kuu kwa muda mrefu. Si ajabu tangu waanze kushabikia Ligi Kuu ya England hawajawahi kuiona.

Rafiki yangu mwingine pia kutoka Uingereza akaniambia anashabikia Wolves. Alikuwa anahaha kufuatilia matokeo ya Wolves dhidi ya Chelsea ugenini Stamford Bridge. Furaha yake ilikuwa kubwa baada ya Wolves kusawazisha bao la dakika za majeruhi katika sare ya 2-2.

Hawa rafiki zangu wanatoka katika miji yenye timu hizi. Ingekuwa Tanzania nadhani wangekuwa mashabiki wa Manchester United, Arsenal, Liverpool au Chelsea. Wangekuwa mashabiki wa timu kubwa. Lakini kwa mfumo wa kwao wamekuwa mashabiki wa timu za kwao.

Rafiki yangu mwingine anatoka Argentina. Nilimuuliza alikuwa anashabikia timu gani nchini humo. Akaniambia anashabikia Racing Club ambayo inashiriki Ligi Kuu nchini humo. Naifahamu timu hii, lakini mashabiki wengi zaidi wanazifahamu River Plates na Boca Junior.

Rafiki yangu mmoja bosi wa La Liga yeye anashabikia Osasuna. Haumwambii kitu. Ni timu ya kwao huko alikotoka. Kuna somo la kujifunza hapa katika mwendelezo wa kujua kwanini soka letu huwa linakwama katika ngazi za klabu. Kuna sababu nyingi, lakini hili la mashabiki wetu kupenda Simba na Yanga linakwamisha klabu zetu.

Hawa rafiki zangu ni wanazi wa klabu za maeneo waliyotoka. Sisi hapo Tanzania wote ni wanazi wa Simba na Yanga. Nchi nzima. Kuanzia Newala hadi Ngara hadi Kasulu. Nchi nzima ni Simba na Yanga. Yaani nchi nzima yenye watu 60 milioni imegawanyika kwa Simba na Yanga tu. Basi.

Leo mikoani watu wanashindana kuzipokea timu hizi kwa mbwembwe. Zinaanza pikipiki kama 60 hivi halafu yanakuja magari madogo mengi kisha linakuja basi la wachezaji. Hauwezi kuamini timu ya nyumbani inajikuta na ukiwa mkubwa. Kisaikolojia inakuwa imeshafungwa mapema.

Kuna mambo matatu hapa. Jambo la kwanza ni kwamba tunapoteza timu za asili. Zitazame timu zote za Ligi Kuu za sasa. Ni mpya kasoro Simba na Yanga tu. Zilizobaki zimeanzishwa baada ya mwaka 1990. Wenzetu timu zao zimeanzishwa miaka ya 1940 kurudi nyuma. Ni timu za tamaduni. Ni timu zinazoakisi maisha ya mkoa au eneo husika. Ni timu za tamaduni za watu.

Timu ambazo zinaanzishwa na kampuni au mtu binafsi zinaweza kufa. Timu za tamaduni za watu haziwezi kufa kirahisi. Zinaweza kutoka Ligi Kuu mpaka daraja la nne, lakini haziwezi kufa kiurahisi. Kuna mashabiki ambao wanasimama na kuibeba timu.

Na hapa ndipo unapokutana na kitu kingine. Timu zinajikuta na nguvu za kiuchumi kwa sababu mashabiki wanaziwezesha. Mashabiki watanunua jezi, hawatakosekana katika mechi za nyumbani na ugenini na klabu inajikuta inapata mapato.

Wale mashabiki wa Newala United badala ya kutengeneza jezi zao na kuuza, huwa wananunua jezi za Simba na Yanga. Waliokuwa mashabiki wa Tukuyu Stars wameua ile Tukuyu maarufu sasa hivi wanavaa jezi za Simba na Yanga huwa wakizuga kwamba wao ni wanazi wa Tukuyu.

Kwa kiasi kikubwa hii inachangia ukosefu wa ushindani katika soka letu. Maisha ya Simba na Yanga mikoani ni rahisi. Maisha yangekuwa magumu na wangekuwa wanazitolea jasho pointi zao kama watu wa mikoani wangekuwa na timu zao. Hata hivyo mikoani wana timu za za kupita tu. Zinaundwa kwa morali ya kuzileta Simba na Yanga katika Ligi Kuu.

Mfano ni rafiki zangu wa Dodoma City. Unadhani wana maisha marefu? Imeundwa na watu ambao akili zao kubwa zipo Simba na Yanga. Watazugazuga katika Ligi Kuu kwa miaka kadhaa kisha watajiondokea zao. Simba na Yanga zitaendelea kusimama imara katika mioyo yao.

Kitu kibaya zaidi katika hili ni kwamba hakuna tunachoweza kufanya. Asili huwa haitafutwi. Inajitokeza yenyewe. Sidhani kama tunaweza kubadilika kwa sababu hata watoto wetu nao wanapenda Simba na Yanga. Nadhani hata Azam wameathirika na jambo hili.

Rafiki zangu Azam wamewekeza pesa nyingi, lakini imebakia kuwa timu ya familia tu. Tumeshindwa kuiondoa timu katika mikono yao na kuileta mtaani. Kifupi ni kwamba hata hao kina Manchester United walianzishwa na kikundi kidogo cha watu, lakini wananchi wakaipokea na kujikabidhi. Sisi Azam tumewaachia wenyewe.

Ukiniuliza kwanini Azam haifanyi vizuri nitakwambia kwamba haipo katika presha. Haiwajibiki kwa kundi kubwa la watu. Hata waamuzi wanaifanyia dhuluma wakati mwingine kwa sababu hawawi katika presha kama Azam ikipoteza pointi. Mazungumzo yapo katika Simba na Yanga tu pindi mwamuzi akikosea au akipatia.

Mwisho wa siku hizi ndio salamu kutoka Madrid. Kinachoshangaza ni kwamba hizi ndio hoja ambazo wakati mwingine zinakosa suluhisho. Kwa mfano, licha ya mimi kutiririka sana humu, lakini bado sina suluhisho la kile ambacho tunaweza kufanya kuiga wenzetu.

Hata watoto wa viongozi wa timu za mikoani nao wanarithishwa na baba zao kupenda Simba na Yanga. Itakuaje kwa watoto wengine. Simba na Yanga zimebaki kuwa tunu pekee ya maisha yetu kisoka. Inawasaidia lakini pia inaumiza kwingineko.