JICHO LA MWEWE: Morrison angeweza kutamba timu za SADC

UNAPOANGALIA ukweli wa mambo ni namna gani mataifa ya ukanda huu yapo mbali na kucheza Kombe la Dunia unajikumbusha tu mchezaji kama Bernard Morrison ‘BM3’ yupo nyumbani kwake Mbezi akiwa hakaribii kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ghana.

Kuna Waghana elfu moja mezani kabla kocha hajaliwaza jina la Morrison aliyeko Tanzania. Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa licha ya utukutu wake usioisha. Ukweli kwamba Morrison angeweza kucheza timu nyingi za ukanda huu.

Morrison angeweza kuitwa Taifa Stars. Angeweza kuitwa kikosi cha Malawi. Angeweza kuitwa kikosi cha Botswana. Angeweza kuitwa kikosi cha Zambia. Angeweza kuitwa katika kikosi cha Msumbiji. Angeweza kuitwa katika kikosi cha Zimbabwe. Angeweza kucheza Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Ukanda huu Morrison asingekosa nafasi. Kuna mahala ambako angeanza mechi moja kwa moja na kuna kwingine ambako asingeshindwa kuingia katika orodha ya wachezaji 25 walioitwa na kocha wa timu ya taifa.

Kwa hapa nchini namuona kabisa Morrison akianza mechi. Kuna wachezaji ambao amewazidi vipaji lakini kwa sasa wapo Benin wakituwakilisha katika pambano dhidi ya Benin jana baada ya kuchapwa Alhamisi.

Katika kikosi kama cha Zambia, Morrison angeweza kuanzia benchi lakini siamini kama asingeitwa kabisa katika kikosi hiki hasa baada ya kiwango chake katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ambapo Simba walifika robo fainali.

Hii inakupa picha ya haraka haraka ya kwanini timu hizi hazijawahi kushiriki Kombe la Dunia. Pengo kati ya wakubwa wa Afrika Magharibi na sisi ni kubwa. Pengo kati ya sisi na wale wa Afrika Kaskazini ni kubwa. Kuna wachezaji wengi wa Afrika Magharibi ambao hawajawahi kugusa katika vikosi vyao vya timu ya taifa na wangeweza kuingia moja kwa moja katika vikosi vyetu.

Mfano mwingine ni beki kama Sergi Wawa Pascal. Ni namna gani asingeweza kucheza katika kikosi cha timu ya taifa? Nadhani angekuwa mlinzi tegemeo kwa muda mrefu sasa lakini timu ya taifa ya Ivory Coast anaisikia redioni tu.

Katika ukanda huu wa Kusini ni Afrika Kusini tu ndio iliyowahi kushiriki Kombe la Dunia. Imeshiriki mara mbili huku mara ya pili wakicheza kama wenyeji. Vinginevyo hakuna timu kutoka katika ukanda huu ambao imewahi kushiriki michuano hiyo.

Tatizo ni nini? Wote tunaweza kufungua mjadala lakini ukweli ni kwamba wachezaji wetu hawachezi katika viwango vya juu Ulaya. Sio sisi tu, hata wachezaji kutoka katika mataifa haya wanaishia kucheza timu za kawaida tu Ulaya.

Jaribu kufikiria kwamba mpaka sasa Kenya na Uganda hazijawahi kutoa mshambuliaji aliyecheza katika Ligi Kuu ya England kama ambavyo Tanzania walimtoa Mbwana Samatta. Wakenya walijikongoja kwa kiungo Victor Wanyama.

Zambia wanajikongoja kwa sasa. Wana mastaa wawili wanaocheza Ligi Kuu ya England. Enock Mwepu anayecheza Brighton na Patson Daka anayecheza Leicester City. Wengine ni hawa akina Clatous Chama wanaocheza Morocco kama ambavyo sisi tuna akina Simon Msuva kule Morocco.

Umewahi kusikia kuna mchezaji wa Malawi ambaye anacheza katika Ligi Kubwa Ulaya? Vipi kuhusu Zimbabwe? Zamani walikuwa na akina Peter Ndlovu lakini sasa hivi hakuna kitu. wachezaji wao wameishia kutamba zaidi Afrika Kusini.

Safari ya ukanda huu kwenda kombe la dunia bado ni ndefu. Ukiachana na wachezaji wenyewe, hata Ligi za ndani hazina ushindani mkubwa wa kuweza kuwatengeneza wachezaji waweze kufuzu kombe la dunia. Mpaka sasa majirani zetu wameanza kuhisi kuna utamu kucheza Tanzania kuliko kwingineko katika maeneo haya.

Binafsi naamini kwamba hata wale Benin wangekuwa timu tishio katika ukanda huu. Sawa hatuwezi kuwalinganisha na mataifa mengine ya Afrika Magharibi kama Ivory Coast, Cameroon au Nigeria lakini ni wazi kwamba kama wangekuwa katika ukanda wetu si ajabu wangekuwa timu tishio.

Hata hivyo Benin bado hawajawahi kufuzu kombe la dunia. Na Napata ukakasi kama kuna timu yoyote kutoka katika kundi letu ambayo itakuwa na ubavu wa kwenda kombe la dunia. Hawa walio juu yetu DR Congo na Benin ni wachovu tu lakini labda tunazidiana katika uchovu.

Kama wakisimama juu ya kundi letu na kupenya nahisi wataenda kutolewa nishai na mataifa kama Senegal, Ivory Coast, Misri, Tunisia, Nigeria na wengineo. Huu ndio ukweli mchungu kuhusu kundi letu ambalo mechi zake ziliendelea jana.

Kuna kazi kubwa ya kufanya katika ukanda huu kuweza kwenda kombe la dunia. Kuna kazi kubwa pia ya kufanya kuweza kutwaa ubingwa wa Afrika ngazi ya klabu. Ukiangalia kwa haraka haraka watu wa Afrika Magharibi na wale wa Afrika Kaskazini wamegawana mafanikio.

Wale wa Afrika Kaskazini wanatamba zaidi katika vilabu huku wale wa Afrika Magharibi wakitamba zaidi katika timu za taifa. Haishangazi kuona Enyimba ikiwa ni timu ya mwisho kutoka Afrika Magharibi kutwaa ubingwa wa Afrika. inakaribia miaka 20 sasa tangu walipofanya hivyo mwaka 2003.