JICHO LA MWEWE: Metacha amejisogeza karibu na mlango wa kutokea Jangwani

Tuesday June 22 2021
metacha pic
By Edo Kumwembe

METACHA Mnata, kipa namba moja wa Yanga ameingia katika mtego ambao haujui na wala hautamuacha salama. Mtego wa kujiingiza katika chuki na mashabiki wa timu yake. Bahati mbaya kwake unaweza kujiingiza katika chuki na mashabiki wa timu yoyote duniani lakini sio Yanga.

Mwaka 1976 Yanga waliwahi kuingia katika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza duniani kufukuza wachezaji wake wote halafu ikaanza upya. Mwaka 1994 Yanga walifukuza wachezaji wao karibu wote wa kikosi cha kwanza. Waakanza upya kwa kupandisha makinda wao wa kikosi B.

Metacha alianza kwa kuandika baadhi ya maneno ya mafumbo katika mtandao wake wa jamii wa Instagram miezi michache iliyopita. Ilikuwa ni kama vileewaaga mashabiki wa timu hiyo. Mashabiki wakajikuta wameduwaa. Ghafla akafuta alichoandika.

Kwanini Metacha alifanya alichofanya wakati huo? Utoto tu. ukosefu wa weledi. Baada ya kugundua kwamba Yanga pengine wanamuamini zaidi yeye kuliko kipa mwingine wa kimataifa wa Kenya, Faroukh Shikalo nadhani amekuwa na utoto mwingi bila ya kujua tabia za Yanga.

Hiki ndio kilikuwa chanzo cha chuki. Bahati mbaya zaidi ni kwamba mashabiki wa Yanga wakaanza kuhisi kwamba Metacha anataka kwenda Simba. Hakuna kitu kibaya katika timu hizi, hasa Yanga, pale wanapokulalia milango wazi.

Ukiwa katika hali hii, kosa lako linaonekana kubwa zaidi kuliko mema yako. Kwa mfano, wiki chache zilizopita Shikalo alifungwa bao la kizembe na Prince Dube wa Azam. Hakukuwa na mashabiki wa Yanga waliomtukana Shikalo. Kwanini? Kwa sababu hawasumbui.

Advertisement

Wanaamini Shikalo anacheza kwa moyo mmoja ingawa sio kipa bora. Wanaamini kwamba Metacha ana kitu na Simba. Wanaamini labda anatumika. Na ndio maana hawaangalii kiasi gani anaokoa, hapana, wanaangalia kiasi gani anakosea.

Kuna wakati Simon Msuva aliwahi kuishi maisha kama ya Metacha pale Yanga. Hasa wakati ule ambao mechi dhidi ya Simba zilionekana kumshinda kwa kile ambacho binafsi naamini kwamba alikuwa anajikuta katika presha kubwa.

Tofauti ya Msuva na Metacha ni kile kilichotokea majuzi katika pambano la Yanga na Ruvu Shooting. Msuva aliendelea kukaa kimya hata pale alipotukanwa matusi ya nguoni na mashabiki. Metacha kaamua kuwatukana mashabiki.

Duniani kote mashabiki wamepewa uhuru mkubwa na vyombo vya soka kuliko wachezaji. sijajua kwanini hasa lakini ni wazi kwamba mashabiki wanaheshimika kama watu wenye mpira wao. Wao ndio utukana, ukejeli, uponda lakini ni ngumu kwao kufungiwa.

Mchezaji ukijibu mapigo tu basi unafungiwa. Kama sio na klabu yako kama ambavyo Yanga wamefanya kwa Metacha basi utafungiwa na Shirikisho. Siku zote mashabiki ni Wafalme. Lakini kumbuka kwamba wao wako wengi. Hauwezi kuwafungia mashabiki elfu kumi wanaotukana. Ni ngumu. Kumfungia mchezaji mmoja ni rahisi.

Kwa wenzetu mara nyingi wachezaji wanaelewa hali hii. Hali ya kudharauliwa na mashabiki, kutukanwa na mengineyo lakini wanajua kwamba wao ni wachezaji wa kulipwa (Professional players) na hawapaswi kujibu mapigo kwa namna yoyote ile.

Unapojibu mapigo papo kwa papo au kupitia mitandao unaweza kujikuta katika hali ngumu zaidi au unaweza kusababisha machafuko katika mechi. Fikiria kama mashabiki wa Yanga wangehamaki zaidi na kulitupia mawe basi la Yanga wakati wakimsaka Metacha wamtoe nje na kumuadhibu?

Ndio maana wachezaji wa kulipwa wanashauriwa kuwa ‘wapumbavu’ kwa ajili ya kuokoa athari kubwa inayoweza kutokea kutokana na vitendo vyao ndani na nje ya uwanja.

Katika magomvi haya ya mchezaji dhidi ya mashabiki unaweza kukosea katika kila timu lakini sio Yanga. Hawa watu ndio maana wanaitwa wananchi. Ni watu wenye hisia kali na timu yao na ni vigumu kwao kusamehe.

Kinachofuata kwa sasa ni Metacha kuondoka Yanga. Kuna mambo mawili. Kwanza kabisa kabla hata ya tukio lenyewe Yanga ina matatizo makubwa katika eneo lake. Sio yeye wala Shikalo ambao unaweza kudai kwamba ni makipa unaowaamini. Viwango vyao ni vya kawaida.

Mara ya mwisho mwisho Yanga kuwa na makipa bora ambao wangeweza kucheza katika lango lolote katika timu kubwa nchini kama vile Simba na Azam ni pale walipokuwa katika mikono salama ya Yaw Berko.

Lango la Yanga halipo salama kwa sasa. Bila ya tukio la juzi ni wazi kwamba Yanga wanahitaji makipa wawili wa nguvu kuliko walionao. Alichofanya Metacha ni kuhalalisha tu ujio wa makipa hao hasa wakati huu ambapo naambiwa kwamba mkataba wake unaelekea ukingoni.

Lakini pia sioni kama Metacha ataweza kujenga daraja la mahusiano kati yake na mashabiki. Yanga wanaweza kuwa walimsamehe kiurahisi Saido Ntibanzokiza alipoomba kutolewa baada ya kufunga bao la tatu dhidi ya Gwambina wiki chache zilizopita.

Kilikuwa kitendo cha utovu wa nidhamu lakini Yanga hawakujali sana kwa sababu mchezaji huyo alikuwa amefunga. Alikuwa amewasaidia kuuweka salama ushindi wao. Tatizo la Metacha ni kwamba alikuwa amefungisha na alikuwa ameuweka rehani uongozi wao dhidi ya Ruvu Shooting.

Akiondoka nini kitafuata? Ni swali gumu. Baada ya hapo unajiuliza kama anaweza kwenda Azam.

Advertisement