JICHO LA MWEWE: Machozi ya Nabi katika mwisho wa kiume wa Yanga Algeria

MWISHONI kabisa tulimwona Kocha Nasreddine Nabi akitoa machozi. Ni nadra kwa mwanamume kulia. Tunaambiwa tulie kwa ajili ya kuipa mioyo yetu nafuu lakini hatufanyi hivyo. Nabi alilazimika kufanya hivyo.

Alijua ameshindwa kumalizia kipande kidogo cha historia kilichokuwa kimebakia. Matokeo ya jumla kati ya Yanga na USMA Alger yalionyesha mechi hizi mbili za fainali zimemalizika kwa sare. Yanga alifungwa 2-1 pale Temeke na alishinda 1-0 pale Algeria. Tofauti ya Afrika na Ulaya ni huku Afrika bado bao la ugenini linahesabika. Ingekuwa Ulaya pambano lingeenda katika matuta.

Yanga walipambana sana juzi katika uwanja uliojaa harufu ya mauti. Ilianzia siku moja kabla ya mechi wakati mashabiki wa wapinzani walipokwenda kufyatua fataki katika hoteli ambayo Yanga walifikia. Baadaye mazingira hayo yakahamishiwa uwanjani. Kikubwa zaidi ni hotelini Yanga walivamiwa na wahuni wachache, lakini uwanjani wakakutana na umati mkubwa uliojaa chuki dhidi yao.

Hapa ndipo ninapowasifu Yanga. Namna walivyoweza kutuliza vichwa vyao na kuicheza fainali hii. Halikuwa jambo rahisi. Walipambana hasa. Ndani ya uwanja, Nabi alituletea kikosi tofauti kidogo. Aliwaanzisha Wacongo wawili katika mbavu za kulia na kushoto. Kulia alimpanga Djuma Shaban, kushoto akampanga Joyce Lomalisa.

Katikati alianza na mabeki watatu kutoka Morogoro, Tanga na Zanzibar. Dickson Job, Bakari Mwamunyeto na Ibrahim Bacca. Mbele yao akawaweka Mudathir Yahya na Sure Boy. Yanga walikuwa wagumu kupitika, lakini walikuwa wazuri katika kupeleka timu yao mbele kuwasaka Tuisila Kisinda, Kennedy Musonda na Fiston Mayele.

Awali Nabi alilaumiwa katika pambano la kwanza kwa kuwaacha nje Djuma na Lomalisa. Inawezekana waliomlaumu walikuwa sahihi. Mabeki hawa wa kupanda na kushuka wenye uzoefu mkubwa hawakuonekana kutetereka hata katika masuala ya ulinzi tofauti na hofu ya Nabi iliyomlazimu awaache nje katika pambano la awali.

Yanga, zaidi ya kila kitu ni namna ambavyo walicheza bila ya hofu wakati wakiwa na mpira. Kelele za Waarabu zingeweza kukuondoa mchezoni kama usingekuwa na weledi kama mchezaji wa kulipwa. Walifanya kila kitu sahihi mpaka walipopata bao la kuongoza la mpira wa penalti.

Sifa ziende kwa mwamuzi kwa kutenda haki. Mayele alisukumwa kizembe katika boksi na beki mmoja wa USM Alger. Katika dunia nyingine mwamuzi angeweza kuacha hasa unapochezesha mechi katika shinikizo kama lile. Hakufanya hivyo. Alituliza akili na kuipatia Yanga penalti ambayo ilikaribia kuwasogeza Yanga katika ubingwa.

Mara kadhaa Mayele amekuwa akikosa penalti za Yanga. Huwa anapewa kwa ajili ya kujiongezea idadi ya mabao. Safari hii Yanga hawakufanya utoto. Wakampa penalti, Djuma Shaban ambaye ni mmoja kati ya wapigaji wazuri wa penalti katika soka la Tanzania. Haikuwa penalti rahisi. Fikiria, dhidi ya umati ule, ugenini, huku akimulikwa usoni na tochi maalumu za kumkosesha umakini. Djuma aliiweka penalti mahala panapostahili.

Kuanzia hapo, Yanga walikuwa wanasaka bao la pili ambalo halikuonekana kuwa mbali. Mpira ukafika mapumziko hali ikiwa hiyo. Kipindi.cha pili mechi ikadhidi kuchezwa katika chuki. Wakati Yanga wakisaka bao la pili Waarabu walikuwa wamedhamiria kupoteza muda. Baadaye wakapata penalti ambayo Djigui Diarra alicheza.

Waarabu wakavurugwa na kuanza kupiga fataki ambazo zilisimamisha pambano mbele ya Rais wa CAF, Patrice Motsepe. Ililengwa kuhakikisha Yanga hawaupati utulivu wa kusaka bao la pili. Hawakuwa timu bora uwanjani kuliko Yanga. Wakati mwingine ungejiuliza kama hawa ndio Waarabu waliofanikiwa kufunga mabao mawili katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa.

Baadaye mwamuzi akamaliza pambano huku Waarabu wakigaragara kwa furaha. Unachotakiwa kufahamu ni yeyote ambaye angechukua kombe hili kati ya Yanga na USMA Alger basi ingekuwa mara yake ya kwanza kutwaa taji hilo. Haikushangaza kuona wakipagawa kiasi kile. Hata kwa Yanga ingekuwa hivyo hivyo.

Baadaye tukashuhudia machozi ya Nabi. Tukashuhudia machozi ya Mayele. Naam, pengine huzuni isingekuwa kubwa kama Yanga wangechapwa mabao matatu au manne katika mechi hii. Hapa walikuwa wameshinda na kusawazisha matokeo ya Dar es salaam. Ambacho hakikuwapa nafasi ya kwenda katika dakika za nyongeza au matuta ni kanuni tu za pambano lenyewe.

Yanga inabidi wapewe sifa. Sijawahi kuona timu ya Tanzania ikishinda mechi nne za ugenini katika michuano ya CAF. Kati ya hizo wamewafunga waarabu mara mbili. Wakati watu wakiamini Fiston Mayele anaweza kuwa mtu wa kwanza kuondoka Yanga kutokana na ubora wake kuongezeka, ukweli ni kumbe Nabi anaweza kuwa mtu wa kwanza kuondoka kabla ya Mayele.

Namna alivyoisuka Yanga hii inastaajabisha kidogo. Kuna mzunguko mkubwa wa wachezaji kikosini na karibu wote wanampa anachotaka. Pia timu ina uwezo mkubwa wa kujibu mapigo katika mazingira mawili. Kwanza ina uwezo wa kujibu mapigo kipindi cha pili katika pambano lolote la soka.

Pili ina uwezo mkubwa wa kujibu mapigo katika mechi ya pili. Ni kama ambavyo walicheza ovyo katika pambano la kwanza dhidi ya Club Africain na pambano kumalizika kwa sare, lakini wakaenda ugenini na kutandaza soka safi kiasi cha kushinda mechi yenyewe. Ni kama walivyofungwa katika pambano la kwanza pale Temeke halafu wamekwenda kushinda Algeria.

Kwa kikosi cha sasa cha Yanga, Rais wao ambaye huwa anasafiri mchana na usiku kwenda kusaka wachezaji nje ya nchi ana kazi ndogo ya kufanya kukiimarisha zaidi kikosi chake. Kwanza aanzie kwa mawinga. Ni muda wa kina Tuisila kuwapisha mawinga wengine wenye kasi na akili kubwa ya mpira uwanjani.

Yanga pia bado haijapata suluhisho la mchezaji ambaye unaweza kusema ni 'Chama wao'. Aziz Ki anaweza kukudanganya na namba zake uwanjani lakini ukweli, anapoteza mipira mingi na hayupo makini uwanjani. Uunganishaji wake wa timu upo chini.

Mwishowe hakuna tunachowadai Yanga. Wamepambana. Wameipa Tanzania heshima. Sio tu kwa mwenendo wote wa michuano, lakini hata namna ambavyo walitupa pambano zuri la fainali huku kombe likiwa uwanjani. Ilikuwa fainali ya kiume. Ulikuwa mwisho wa kiume. Hakuna tunachowadai sana labda kurudi tena katika hatua kama hizi msimu ujao. Inawezekana.A