JICHO LA MWEWE: Al Ahly wameturudisha shule kwa dau la Luis

LUIS Jose Miquissone atakuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kuuzwa katika historia ya Tanzania kama Simba watamuuza kwenda Al Ahly kwa dau la Dola milioni moja katika dirisha hili la uhamisho barani Afrika.

Hizi ni Shilingi 2 Bilioni za Kitanzania na zinaacha maswali mengi nyuma yake. Kundi kubwa la mashabiki wa Simba nadhani litaafiki staa huyu aondoke pale mtaa wa Msimbazi kwa dau hili la pesa. Kuna kundi dogo la wahafidhina linaweza kupinga.

Wanaopinga watakwambia Simba haiitaji kuuza wachezaji wake bora kwa vile kwa sasa wamekaribia kutwaa ubingwa wa Afrika. Kwamba ni bora wabaki na mastaa hao ili waweze kutwaa taji na kisha kupata fedha.

Ukweli ni kwamba kwa mara nyingine tena Simba wamekaribishwa katika dunia ya pesa za Waarabu au tunaweza kusema wakubwa kwa ujumla. Waliwahi kufanyiwa hivyo na TP Mazembe wakati walipomtaka Mbwana Samatta. Lakini pia waliwahi kufanyiwa hivyo na Etoile Du Sahel wakati walipomtaka Emmanuel Okwi.

Safari hii Simba walichofanyiwa na Al Ahly ni kuondoa mchezo ‘nenda rudi’. Moja kwa moja wamekwenda katika dau ambalo halihitaji sana kuwabembeleza Simba. Hatujawahi kuona mchezaji wa Kitanzania akinunuliwa kwa dau kama hilo, kwanini tubishane?

Al Ahly wanachofanya ni kuikanya Simba kwamba daima samaki mkubwa atamla samaki mdogo. Wakati fulani tajiri wa Simba, Mohamed Dewji aliwahi kukaririwa akidai kwamba Simba haina mpango wa kuuza mastaa wake kwa sababu inasaka ubingwa wa Afrika.

Ukweli ni kwamba baada ya Simba kujitutumua katika michuano hii kwa mara nyingine tena ilikuwa wazi kwamba ingegeuzwa soko la wakubwa. Nahofia sio Luis tu. Huenda wakubwa wengine wakarudi kwa kina Clatous Chama na Joash Onyango au wengineo.

Iliwatokea Leicester City baada ya kutwaa ubingwa wa England mwaka 2016. Wakubwa wakagawana kina N’Golo Kante, Riyad Mahrez, Danny Drinkwater na wengineo. Majuzi hapa Ajax walipofika mbali katika michuano ya Ulaya wakubwa wakaanza kugawana wachezaji wao kina Matthias De Ligt, Frenkie de Jong na wengineo.

Iliwahi pia kutokea kwa Monaco ilipofanya vizuri katika michuano ya Ulaya miaka ya karibuni. Wakubwa wakarudi kugawana kina Kylian Mbappe, Bernardo Silva, Benjamin Mendy, Tiemoue Bakayoko na wengineo.

Katika dunia hii ya biashara ambacho Simba wanapaswa kufikiria ni kiasi gani walitumia kumnasa Luis kutoka alikokuwepo. Ni wazi kwamba watagundua kwamba walitumia pesa kidogo na watatengeneza pesa nyingi wakimuuza kwenda Al Ahly.

Mwisho wa siku, wana uhakika gani kama wakiendelea kuwa na Luis thamani yake itapanda zaidi au kwamba wao watakwenda kuchukua ubingwa wa Afrika ili wapate pesa. Ni kamari ambayo hauwezi kuichezea. Unachukua tu pesa.

Hapo hapo kuna ubinadamu wa kawaida. Al Ahly lazima watakuwa wameongea na wakala wa Luis na kumhakikishia dau kubwa la pesa ya kumsaini ambalo litakwenda katika akaunti ya nyota huyo. Lakini pia itakuwa wamemuahidi mshahara mzuri.

Simba watakuwa na uwezo wa kumuongezea mkataba Luis na kumlipa dau kubwa la mshahara kama ambalo Al Ahly wameweka kwa Konde Boy? Jibu lake litakuwa hapana. Sioni kama Simba wapo tayari kumlipa Luis kiasi kama cha dola 20,000 kwa mwezi.

Ukweli ni kwamba hapa Al Ahly wameikumbusha Simba nafasi yao kwa Luis. Kwa kuanzia ofa ambayo ipo mezani lakini pili wameikumbusha namna gani wao wanafanya ili kutwaa ubingwa wa Afrika mara nyingi.

Kwamba wana uwezo wa kutwaa ubingwa huo lakini bado ikachukua nyota wakubwa wa timu ambazo zilikuwa zinafukuzana nao katika mbio za ubingwa. Walishafanya hivyo katika miaka ya karibuni kwa kumchukua beki wa kimataifa wa Morocco, Badr Benoun kutoka Raja Casablanca na kuwaacha mashabiki wa Raja wakiwa na hasira. Hao ndio Al Ahly.

Lakini dau la Al Ahly kwa Luis nadhani linawakumbusha kuwa na mfumo mzuri wa kuchunguza wachezaji kwingineko ili wawe wabadala pindi mastaa wao wakubwa wanaponunuliwa. Simba wamejiandaaje kama Luis akiondoka? Hili ndio jambo la msingi.

Kitu kizuri watakuwa na pesa mkononi na wataweza kwenda mahala na wao wakatambia akaunti yao. Wanaweza kuchota walau dola laki tatu tu wakaenda kusaka mbadala wa Luis mahala. Tatizo watakwenda wapi? Wamemuona nani ambaye anaweza kuwa mbadala halisi wa Luis?

Tuna shida kubwa katika kusaka wabadala. Haishangazi hata kuona wakati fulani Emmanuel Okwi alikuwa anarudi kila uchao kwa sababu Simba hawakuweza kupata mtu ambaye walidhani angekuwa mbadala wake. Ni mpaka walipokuja hawa kina Luis.

Hata sasa sina uhakika wa moja kwa moja kwamba endapo mtu atakuja kumchukua Chama pale Simba basi tayari Simba watajua wanaenda wapi kumpata Chama mwingine. Hili ndilo tatizo kubwa katika soka letu.

Kitu kingine ambacho Simba wamekumbushwa katika sakata hili ni ujanja wa kuchukua wachezaji wa kigeni wakiwa katika umri mdogo. Ukweli ni kwamba umri wa Luis umesaidia sana kuitamanisha Al Ahly kumnasa staa huyu Mmakonde. Ana miaka 25.

Mara nyingi tumezoea kuona klabu zetu zikileta wachezaji wa kigeni wenye umri mkubwa ambao thamani ya kuuzika tena inakuwa ngumu. mara nyingi wachezaji hawa wanakuwa wamemaliza mikataba yao mahala kwingine. Huwa tunavizia wachezaji wa bure.