Prime
Kwaheri Fabrice Ngoma, nyakati zilipishana

FABRICE Ngoma ameaga pale Simba kupitia ukurasa wake wa instagram. Ukweli ni kwamba mambo yamefika mwisho kati ya Ngoma na Simba. Inaonekana Simba wameamua kutompa mkataba mwisho Ngoma.
Na nimesikia Ngoma ana ofa zake mkononi. Nimeambiwa Waarabu pia wanaisaka saini yake na itakuwa rahisi kwake kwa sababu atakuwa mchezaji huru.
Kwa nilichosikia sidhani kama umekuwa mwisho mzuri kwa Ngoma na Simba. Ilipaswa kuwa na mwisho mzuri zaidi.
Taarifa za mwisho kabisa zinadai kwamba Ngoma alikuwa ameongoza mgomo na wachezaji wenzake kuelekea katika pambano dhidi ya Yanga wakidai bonasi zao kabla ya kuchezwa kwa pambano hilo.
Sishangazwi sana na hilo kwa sababu Ngoma anaonekana kuwa kiongozi ndani na nje ya uwanja. Ungeweza tu kuona hata ugomvi wake na kupa Moussa Camara pale Unguja ulitokana na uongozi wake mkubwa uwanjani ambao nadhani hata kina Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ hawauwezi. Ni vile tu kwamba nahodha wake timu kubwa huku kwetu lazima awe mzawa.

Kudai chake ni tatizo? Sio tatizo. Nadhani Simba na Ngoma hawakutakana. Kama Ellie Mpanzu angekuwa amedai stahiki zake na mkataba wake umefika mwisho sidhani kama wangeamua kuachana naye. Ni vile tu kwamba Ngoma na Simba hawakuhitajiana sana katika mida hii ya majeruhi huku hali ikiwa tete.
Ingekuwa ni Mpanzu kungekuwa na mbio nyingi za kukimbizana mida hii kwa ajili ya kutanua mkataba wake. Ni kama ambavyo wakati ule kulikuwa na mbio nyingi za kutanua mkataba wa Clatous Chama wakati ulipokaribia. Hata hivyo, kwa Ngoma walijua kwamba bado kulikuwa na hatihati nyingi za kuendelea kukaa naye.
Walipishana nyakati. Baada ya mbwembwe nyingi za kudai kwamba walikuwa wamempora Ngoma Uwanja wa Ndege ukweli ni kwamba Ngoma alifika nchini, huku miguu ikiwa imemsaliti. Akili ilikuwa nyingi kichwani lakini kasi haikuwa kubwa sana. Alituonyesha ni kwanini alikuwa amepita katika klabu mbalimbali kubwa hapa Afrika.

Na Simba yenyewe aliikuta imemsaliti. Alipishana na kizazi kizuri cha Simba. Zaidi ni kwamba alikuwa katika nyakati ngumu ambazo mtani wao alikuwa juu hivyo maisha siku zote yalikuwa ya kulinganishana.
Ngoma huyu sio wa AS Vita. Amekuja nchini maji ya jioni. Lakini na Simba yenyewe alipishana nayo. Haikuwa Simba ile ya kina Jose Luis Miquissone, Clatous Chama, Larry Bwalya, Serge Wawa Pascal, Josh Onyango na wengineo. Akaja katika Simba ambayo ilikuwa inajitafuta, huku yeye mwenyewe akijitafuta kukimbizana na umri.
Wachezaji wazuri wanapenda kucheza na wachezaji wazuri ili waendelee kuwa wazuri. Ni kama ambavyo naamini huenda Khalid Aucho umri umeenda, lakini anafurahia kucheza na wachezaji wazuri kwa sababu wanamlinda kama ambavyo naye anawalinda. Ngoma hakupata bahati hiyo. Fikiria kama Ngoma angekuwa anacheza kikosi cha sasa cha Yanga. Mambo yangekuwa mazuri zaidi kwake.

Kama Simba ingempata Ngoma katika ubora wake angekuwa wa moto zaidi. Tatizo ni kwamba kuanzia watani wao hadi kwao wenyewe tatizo linakuwa kuwapata wachezaji hawa katika umri sahihi. Bei zao zinakuwa ghali kupitiliza. Wakati wa ubora wao kina Ngoma ndio walikuwa wanauzwa dola 500,000 na kuendelea. Hadi leo hatuna ubavu wa kununua wachezaji wa bei hizo.
Hata hivyo, ameisaidia Simba katika kipindi hiki cha mpito. Nadhani Simba wanahitaji kiungo mwingine ambaye ataipeleka timu juu ya Ngoma. Ndio maana sijashangaa sana kuona Simba haijapambana kumbakiza. Angekuwa Ngoma yule Simba wangepambana kwa machozi, jasho na damu kumbakiza. Lakini kwa sasa wataangalia kwingineko.
Inanikumbusha kwa watani zao wakati ule walipoanza kujenga timu wakiwa na Mukoko Tonombe. Wakamsifu sana, lakini wakagundua inabidi wapande daraja zaidi kwa kuwachukua kina Khalid Aucho na Yannick Bangala. Simba wanajua kwamba Ngoma amewapitisha katika kipindi fulani muhimu, lakini ili wawashike watani zao Yanga walipo basi wanahitaji moto mwingine juu ya Ngoma.

Tatizo lililopo ni Simba kukosea kusajili. Kama sio kukosea kusajili basi kuna bahati mbaya ambayo inawaangukia kwa baadhi ya wachezaji kutofanya vema. Mfano ni Augustine Okajepha. Alipaswa kuja Msimbazi na kumpora namba Ngoma. Matokeo yake ameshindwa hata kuchukua nafasi ya Yusuf Kagoma ambaye ni mzawa.
Matokeo yake Simba watakuwa na jukumu la kuziba nafasi ya Ngoma pamoja na kuvunja mkataba wa Okajepha. Mchezaji ambaye ataendelea kuwepo katika kiungo cha chini ni Kagoma peke yake. Pesa inabidi iteketee lakini lazima pia tukubali kwamba itaendelea kujengwa upya kwa mara nyingine.
Ngoma anaweza kuwa wa kwanza miongoni mwa mastaa wengi ambao wanachomoka katika dirisha hili. Sina uhakika na kina Joshua Mutale, Leonel Ateba, Steven Mukwala na wengineo. Simba inaweza kujikuta inajengwa upya tena na tena. Bahati nzuri kwa watani zao ni kwamba tayari timu ya msingi wanayo.

Kwaheri kwa Ngoma. Licha ya umri wake, lakini ameipa Simba kitu. Utulivu uwanjani pamoja na uongozi wake ndani na nje ya uwanja. Binafsi namkumbuka pia kwa uwezo wake mkubwa wa kupiga mipira ya vichwa. Bado mambo hayakwenda sawa na hakucheza na mafundi, lakini angeweza kufanya mambo makubwa zaidi kama angekutana na kina Chama.
Ameivusha Simba kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine na sasa ni zamu ya mabosi wa Simba kuwaridhisha mashabiki na wanachama kwa kumleta kiungo mwingine ambaye ataichukua timu kutoka hatua moja kwenda nyingine zaidi. Hii ndio changamoto kubwa kwa sababu mashabiki wa Simba wamejihisi kudhalilika kupita kiasi katika misimu hii minne iliyopita ambayo mtani ametamba
Ngoma hajatwaa taji lolote muhimu na Simba, lakini sio kosa lake. Ni makosa ya mabosi wake na hakuna kificho kwa sababu hata mashabiki na wanachama wa Simba sasa hivi wamejua. Baada ya vichapo vitano mfululizo kutoka kwa mtani huku pia mtani akitwaa mataji mawili muhimu huku na huku mara nyingi wamejua kuna pengo lipo na Ngoma hakusaidiwa.