JESCA: Hivi ndivyo tulivyoumizwa Sauzi

Muktasari:

  • Bondia huyo anayepigana katika uzani wa fly ambaye kwa sasa rekodi yake ikionyesha amecheza jumla ya mapambano tisa akishinda matano kati ya hayo moja ni ushindi wa ‘KnockOut’ KO, amepigwa mara tatu na moja kati ya hayo ni KO huku akiambulia sare mara moja.

HUENDA bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Jesca Mfinanga hana hamu tena na Afrika Kusini kutokana na mikasa mikubwa aliyokutana nayo, ingawa hakutarajia kutokana na shauku kubwa aliyokuwa nayo awali ya kufika kwenye taifa hilo.

Bondia huyo anayepigana katika uzani wa fly ambaye kwa sasa rekodi yake ikionyesha amecheza jumla ya mapambano tisa akishinda matano kati ya hayo moja ni ushindi wa ‘KnockOut’ KO, amepigwa mara tatu na moja kati ya hayo ni KO huku akiambulia sare mara moja.

Juni 22, Mfinanga pamoja na bondia mwengine wa kike katika ngumi za kulipwa nchini, Egina Kayange walikuwa na kibarua kizito cha mapambano ya ubingwa Afrika nchini Afrika Kusini na Mfinanga alikuwa akiwania mkanda wa ubingwa wa Afrika dhidi ya Simangele Hadebe wa Afrika Kusini ambaye alikuwa akiutetea.

Wakati Egina alichezea mkanda wa ubingwa huo lakini kwa upande wa nchi za Kusini mwa Afrika yaani ABU Sadic dhidi ya Monica Mukandla kutoka Zimbabwe.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Mfinanga na ameelezea mambo mazito ya manyanyaso waliopitia nchini humo kutoka kwa wenyeji wao kabla ya Balozi wa Tanzania nchini humo, James Bwana kuingilia kati kuwatetea na kurejea nchini baada ya wiki moja ya mateso waliyopata.

Walivyozinguliwa

Mfinanga anasimulia katika safari yao waliondoka jumla ya watu watatu yaani wao mabondia wawili pamoja na mtu aliyewatafutia pambano hilo lililopigwa Juni 22, mwaka huu Johannesburg, wakala Innocent Evarist.

Bondia huyo ambaye ni binti wa mwamuzi wa kimataifa, Pendo Njau, anasema mateso yao yalianza mara baada ya kuwasili na kupelekwa katika hoteli waliyokuwa wamepangiwa na promota wa pambano hilo, Sifiso Shongwe kupitia promosheni yake ya Fantastic 2 Boxing Promotion.

Mfinanga anaeleza kwa kuwa pambano lake lilikuwa la uzani wa fly alilazimika k utumia muda mwingi kukaa bila ya kula kwa lengo la kulinda kilo kutokana na pambano lake kuwa ni la ubingwa.


Utata wa kupima kilo

“Unajua sheria za ubingwa zinakutaka bondia ili uchukue ubingwa lazima upigane kwenye kilo husika au chini yake lakini ukizidi huwezi kuchukua ubingwa hata ukishinda pambano, hivyo nikajitahidi kulinda uzito kwa kukaa bila kula.

“Sasa baada ya kufika niliomba mzani kwa promota kwa ajili ya kukagua kilo kila wakati kabla ya kwenda kupima lakini tulivyoenda siku ya kupima ndiyo matatizo yalipoanzia kutoka kwa mmoja kati ya maofisa waliokuwa wakisimamia zoezi na ndiyo alikuwa mwamuzi wa pambano langu.

“Baada ya kupima niliambiwa kilo zangu zimezidi lakini niliwabishia kwa kuwa mzani wao walionipa wenyewe ulikuwa unaonyesha nipo sawa, tulibishana kabla ya kukubaliana nao kupunguza kilo kwa mazoezi ili zifikie wanapotaka.

“Lakini baada ya kwenda kukimbia tena nikiwa na njaa ambayo nilitoka nayo Tanzania nilivyorejea, bado kukawa na utata wa pointi kufikia kilo walizotaka, wakakubaliana wanaume watoke ili nivue nguo kupima tena.

“Binafsi hiyo hali ilinikwaza nikaweka ngumu mwanzo lakini baada ya muda nilikubali ila nikaomba hata mabondia wengine wa kike waliokuwepo eneo la kupimia watoke nje, tukabakia na yule anayesimamia uzito na kuna bondia wa kike kutoka Malawi na mwenzangu Egine.

“Nilivua nguo zote nikabakiwa na nguo za ndani nilivyopima yule dada bado aligoma akata nipime nikiwa mtupu haikuwa jambo jepesi kwangu ila nililazimika kuvua zote, kisha nikapima ndiyo zikapatikana kilo ambazo walihitaji, akapiga na picha zile kilo kuwaonyesha wengine.

“Kwake ilikuwa furaha lakini kwangu iliniumiza ingawa nilikuwa naelewa ni mbinu ya kutaka kunitoa mchezoni, baada ya hapo tulipelekwa kula kisha tukarejeshwa hotelini na pale hotelini tulikuwa na ruhusa ya kunywa kahawa tu.

Mambo yazidi kumchanganya

“Lakini kawaida siku ya kupima uzito ya mapambano ya ubingwa wa ABU huwa kunakuwa na kikao cha mabondia na maofisa wa ABU kwa ajili ya kusomewa sheria na kujua ‘gloves’ zitakazotumika kwa kila upande kuweka saini yake pamoja na malipo yetu kuwa kwa msimamizi wa pambano kutoka ABU ila kwetu hayakufanyika kabisa.

“Siku ya pambano tulikaa bila ya kuletewa chakula hadi muda wa pambano unakaribia hatukuwa tumekula kitu na ajabu baada ya kufika ukumbini tuliambiwa tujiandae mbaya zaidi mabondia wageni wote wakawa wametuweka kwenye eneo la chumba kimoja.


Wadhulumiwa wazi wazi

“Ukweli wote tukapigwa TKO za kudhulumiwa hasa upande wangu ndiyo iliumiza kabisa kwa sababu mwamuzi alikata pambano wakati nashambulia.

“Wakati huo yule mwamuzi tulishakuwa na ugomvi wa siku ya kupima, siku ya pambano nilivyokuwa nimefunga bendeji yeye akaja kunifungua akidai nimekosea hata nilipofunga tena kabla ya kuja mtu ambaye aliombwa na Mtanzania mwengine kuja kutupa sapoti.

“Lakini upande wa Egine wakawa wamerusha taulo ambalo liliibiwa na mtu wa Afrika Kusini katika chumba ambacho tuliweka vitu vyetu wakati tunajiandaa akapigwa kwa mtindo huo.

“Upande wangu kabla ya pambano wakati najiandaa kuweka mwili sawa, kikinga mdomo changu wakati wa kupigana niliweka kwenye kiti ila muda wa kupigana ulivyofika nilikuta kimewekwa na karatasi iliyochorwa maneno ya Kiarabu.


Malipo yazua balaa

“Sasa kabla ya kupanda ulingoni tulimuuliza wakala wetu aliyetupeleka juu ya malipo yetu, akatuambia ameshapewa na promota ila hawezi kutupa pale kwa kuwa Afrika Kusini siyo salama maana tukishajulikana tumepewa pesa tutavamiwa na majambazi na wakati mwengine kufa, hivyo wakala akatuambia hadi tufike uwanja wa ndege siku ya kuondoka.

“Basi tukarejea hotelini wakati huo bado utata wa matokeo ya pambano haujaisha na wakala akaongopa mambo mengi ambayo baadaye hayakuwa na ukweli hasa upande wa pesa.

Wafukuzwa hotelini

“Siku ya pili baada ya pambano, wahudumu walitufuata kuondoa mizigo wakitumbia pesa yetu imeisha na wakati huo promota alimtuma mdogo wake kuja kutuondoa pale kutupeleka Soweto ingawa wakala alidai tunapelekwa hoteli nyengine.


Hofu ya Soweto

“Hiyo Soweto kiukweli haikuwa sehemu salama kwa sababu watu kuuliwa, wizi, uvutaji wa dawa za kulevya unaofanyika mtaani ndiyo tukapelekwa huko kwenye nyumba ya huyo jamaa ambaye alikuwa mganga wa kienyeji wenyewe kule wanaita Sangoma.

“Awali tulijua tunapumzika kumbe ndiyo pale yakawa ndiyo makazi ya siku moja kabla ya kurudi Tanzania, ila ndiyo tuligundua wakala alitudanganya suala la malipo yetu kwa sababu promota alidai tuondoke kisha atatumia, nilikataa nikawaeleza siwezi kuondoka hadi nilipwe pesa yangu.


Ujanja wawatoa Soweto, wahamia kwa balozi

“Baada ya hapo ndipo nilituma video kwa waandishi ikionyesha yale mazingira ya ile nyumba ya mganga ilivyokuwa ingawa wakala na yule bondia mwenzangu walikuwa hawataki niwaambie watu.

“Meneja wangu, Abdul Ally na wadau wengine walishirikiana kuongea na balozi wetu Afrika Kusini, James Bwana aliyelazimika kutufuata mwenyewe kule Soweto, kutuondoa hadi ubalozini na kisha tukaenda kukaa nyumbani kwake.


Balozi aingilia kati

“Balozi kabla ya kuja Soweto alituma viongozi wa Watanzania na kisha akaja mwenyewe ingawa pia kulikuwa na Mtanzania mwengine Seif Zugo ambaye alitusadia pakubwa sana hasa kufika Soweto ambako hata watu wa chakula cha kutuma walikataa kuja.

“Lakini tunashukuru balozi alitusaidia sana japo kuwa tulimwambia hatuwezi kuondoka hadi tutakapokuwa tumelipwa pesa zetu tulizokuwa tunadai kwa promota.

“Balozi alichokifanya, akamtafuta yule promota kwa simu yake jamaa alipoona anaongea na balozi akamwambia ukweli hakuwa na uwezo wa kutulipa ila anafanya mpango kukopa pesa ili atulipe akaomba siku mbili lakini bado alishindwa kutulipa na hata alivyopigiwa simu hakupatikana kabisa.

Wadai chao hadi kieleweke

“Sasa kutokana hali hiyo balozi akatuchukua hadi kwenye chama cha ngumi cha Afrika Kusini ambao walikubali kutulipa wao na sisi tukarejea nchini.

“Nilikuwa nadai siyo chini ya milioni 10, nashukuru kwa msaada wa ubalozi nimepata haki yangu. Jambo la msingi kwa mambondia wanaokwenda huko wafike katika ubalozi wa nchi yako kwanza ili kuepuka yaliyotukuta sisi.

“Unajua kama siyo juhudi za wadau waliomtafuta balozi basi kiukweli hali yetu ilikuwa mbaya sana kwa sababu sisi tulingia Afrika Kusini bila ya kuujulisha ubalozi, hivyo walikuwa hawajui chochote kuhusu sisi kuwepo ndani ya taifa lile,” anasema Mfinanga.