Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jeremiah Juma: Simba, Yanga waje tu nawasubiri kwa hamu

WAKATI wengi wakimpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya straika wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma msimu huu, lakini mwenyewe amezikataa sifa hizo akisema hajawa na msimu bora kutokana na kutofikia malengo binafsi.

Jeremiah amekuwa na kiwango bora huku akiwa na rekodi ya pekee kwa kuwa mfungaji bora wa muda wote kikosini humo tangu ajiunge 2009 alipohitimu masomo mkoani Iringa.

Katika mazungumzo maalumu na Mwanaspoti, straika huyo amefunguka mengi ikiwamo kudumu kwake Prisons, panda shuka ya timu hiyo, rekodi Ligi Kuu na ishu yake na timu za Simba na Yanga.


MSIMU MBAYA

Jeremiah anasema licha ya timu yake kujinasua nafasi za chini na kuondoa presha kikosini hata kwa mashabiki, lakini alihitaji kufikia au kuvuka rekodi ya msimu wa 2017/18 alipofunga mabao 14 na siyo tisa aliyonayo sasa.

Anasema kutoanza vyema msimu kwa kuwa na matokeo yasiyoridhisha ndio sababu iliyompunguza kasi kutokana na presha kuwa kubwa na muda mwingine kushindwa kufunga alipopata nafasi.

“Siyo msimu bora kwangu. Nilikuwa bora kipindi nimefunga (mabao) 14 na kuitwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ japokuwa ni furaha na faraja kubwa kuona timu inabadilika na kutoka nafasi za chini,” anasema Jeremiah.


KUIKAMIA YANGA

Nyota huyo anasema tatizo kubwa la mashabiki wengi wa soka nchini hupenda kufuatilia zaidi mechi za Yanga na Simba kuliko michezo mingine wanapocheza na timu nyingine.

Anasema Prisons hawana upande wowote na huwa wanapata matokeo kwa timu yoyote inapotokea maandalizi mazuri na mechi kuwakubali.

“Wengi husubiri siku tukicheza na hizo timu kwanini wasiangalie hata zile za Azam na Namungo ambazo huwa tunashinda? Wanasubiri mtandaoni tu halafu baadaye tukicheza na Simba na Yanga ndio wanaibuka na maneno.”


TATIZO PRISONS

Kwa misimu mitatu nyuma Tanzania Prisons imekuwa na matokeo yasiyoridhisha huku ikiponea chupuchupu kushuka daraja ikiwamo msimu uliopita ilipofanikiwa kushinda  mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania kwenye michezo ya mtoano (play off).

Ishu nyingine ni kuwa muda wa kupumzika kama ilivyo hivi sasa chini ya kocha Abdalah Mohamed ‘Baresi’ hawakuupata, jambo ambalo liliwapa wakati mgumu kupata matokeo mazuri.

“Wengi waliokuwa wakisajiliwa wanaishia benchi au hata kutoonekana uwanjani na kutufanya kuendelea kutumika, lakini kwa sasa tunapumzika na kukusanya nguvu mpya.

“Kwa sasa mabadiliko tunayaona ambayo kwa ujumla yanatupa mwelekeo mzuri kwani tunakuwa na muda wa kubadilishana na wengine, na ndio kitu kimetupa ahueni kupata matokeo mazuri,” anasema Juma.


MAFANIKIO YAKE

Kinara huyo wa mabao kikosini anasema anajivunia rekodi ya kuendelea kutesa kwenye ufungaji bora ndani ya timu kutokana na kukosa mshindani.

Anasema kujituma na kufanya kile kocha anachotaka kumekuwa kukimpa uhakika wa namba akisisitiza kuwa wachezaji wanaotua kikosini wanakuwa hawana upinzani.

“Ndio maana mara nyingi utakuta sura ni zilezile uwanjani. Mfano mimi, Samson Mbangula na Jumanne Elfadhir japokuwa pia hata sisi ni kutokana na kujituma kuisaidia timu.”


STARS SASA

Jeremiah anasema hajafikiria kustaafu soka kwani nguvu bado anazo na soka lipo miguuni, isipokuwa anafikiria zaidi kurejea kwenye kikosi cha Stars kulitumikia Taifa.

Pia anaamini kabisa anastahili kuwapo kikosi cha Taifa Stars, akibainisha kuwa hata namba akiaminiwa anaweza kufanya makubwa.

“Kwanza sibahatishi nikiwa uwanjani. Kazi naipenda na kuifanya kwa moyo, hivyo naona kabisa nastahili kuwapo Taifa Stars na kama nimeaminiwa naweza kupata namba na kufanya wanachotaka,” anasema.

Mchezaji huyo anasema kutoitwa Stars kumekuwa kukimpasua kichwa licha ya kufanya vizuri, huku akiwaona baadhi ya nyota wakijumuishwa kutokana na anachoamini kuwa ni ukaribu walionao na viongozi.

“Unakuta wengine wanaojumuishwa ni wenye mawakala ambao wapo karibu na uongozi huku wewe unafanya vizuri. Kwa ujumla hili linanipa sana maumivu.”


SIMBA, YANGA FRESHI

Mwamba huyo anasema kutokana na kazi yake zaidi kuwa mpira iwapo Simba na Yanga zitatokea kuhitaji huduma yake yupo tayari kuvaa uzi wowote.

Anakiri kuwa hata hivyo miamba hiyo ya soka nchini kwa nyakati tofauti imewahi kumsaka, japokuwa hakuna dili lililofanikiwa, lakini hata kesho mojawapo ikiwa siliasi ataungana nayo.

“Wote waliwahi kunitafuta ila kulitokea mambo ambayo sikujua haraka, dili likaishia njiani, ila wakirudi hata sasa hivi niko tayari kucheza popote na namba naweza kupata,” anasema.


SIMBA YAMCHEFUA

Mojawapo wa mambo anayodai yalimuacha na huzuni na maumivu ni kipigo kizito cha mabao 7-1 walichopata dhidi ya Simba msimu huu kwenye Ligi Kuu katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.

Jeremiah anasema katika mchezo huo waliingia uwanjani wakihitaji pointi tatu, lakini walijikuta wakiloa kwa kipigo ambacho kiliwapagawisha kwa kiasi kikubwa kikosini.

“Kilikuwa ni kipigo ambacho hatukufahamu kama kitatutokea, licha ya kujipanga kushinda, nadhani kuna sehemu tulifeli kimbinu kwa sababu tulienda mapumziko tukiwa sare ya 1-1,” anasema.


SIRI YAKE NA PRISONS

Jeremiah anasema kudumu kwa Wajelajela hao ni kutokana na falsafa ya taasisi hiyo kuwajali na kuwathamini raia wa kawaida uwanjani hususan kwenye maslahi.

Anasema kuwa katika kuitumikia timu hiyo inapotokea fursa huwa haimuchi mtu mwenye kiwango bora na nidhamu kazini, kwani lazima impe ajira ya kudumu na akijitolea mfano baada ya kujikuta akivaa gwanda.

“Kwanza hiyo ni taasisi ambayo imewekeza zaidi kwa askari uwanjani, lakini hata raia wa kawaida wanaocheza huwa inawajali na kuwathamini. Ikitokea fursa huwa haimuachi hivihivi.

“Lakini hata kwenye maslahi huwajali sana raia. Ndio maana unakuta mchezaji akifika Prisons kama hajawa na tatizo lolote atatamani kubaki hapo. Muda mwingine huuzwa timu nyingine,” anasema Juma.


MSIMU UJAO TOP FOUR

Nyota huyo anatamba kuwa licha ya kutokuwa na mwanzo mzuri, lakini wanashukuru kwa mabadiliko yaliyojitokeza na sasa hawana hofu tena ya kupambana kushuka daraja.

Anasema wanaanza kufikiria msimu ujao zaidi ili kuhakikisha wanarejesha heshima  ambayo kwa kiasi fulani ilikuwa imepotea kuanza kupigania nafasi nne za juu.

Jeremiah anasema kutokana na ushirikiano na usajili bora utakaofanyika Prisons inakwenda kuleta ushindani Ligi Kuu kwani ishu ya kupambania kukwepa kushuka daraja itabaki historia.

“Tunasubiri kumaliza msimu kwa mechi mbili zilizobaki kuhakikisha tunashinda na kumaliza vyema msimu, kuanza mipango mingine mipya tunahitaji msimu ujao nafasi nne za juu,” anasema staa huyo.