Prime
Je, unafahamu wachezaji wanavyobeti Ligi Kuu Bara?

Muktasari:
- Kanuni za maadili za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), zinakataza na zimeweka onyo kali kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na viongozi wa soka kujihusisha na ubashiri (betting) wa matokeo ya mechi za mashindano.
UBASHIRI katika mechi za soka umeanza kuwa janga ukidaiwa kuingia kwa kasi, huku malalamiko kutoka katika baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara hususani zile za chini yakianza kuibuka wachezaji wakilalamikiwa kujihusisha au kushawishiwa kujihusisha katika suala hilo.
Kanuni za maadili za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), zinakataza na zimeweka onyo kali kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na viongozi wa soka kujihusisha na ubashiri (betting) wa matokeo ya mechi za mashindano.
Lakini, licha ya kuwapo kwa kanuni hizo za Fifa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo ni mwanachama wa Fifa, limetunga kanuni ya 41(11) inayozuia ubashiri kwa watajwa hapo juu, inayoeleza kuwa: “Mchezaji atakayebainika kupanga matokeo ya mchezo kwa namna yoyote ile atafungiwa maisha kucheza mpira ndani na nje ya nchi.”
Hata hivyo, pamoja na uwepo wa kanuni na miiko inayozuia wachezaji kujihusisha na upangaji wa matokeo, jambo hilo limekuwa likifanywa na baadhi ya wachezaji wa timu tofauti zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa ibara ya 27 (i) na (ii) ya kanuni za maadili za Fifa, ni kosa kwa mchezaji kama mwanafamilia wa mpira wa miguu kujihusisha na ubashiri wa matokeo.
“Watu waliofungwa na kanuni hii watakatazwa kushiriki ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kamari, bahati nasibu au matukio kama hayo au miamala inayohusiana na mechi za kandanda au mashindano na au yoyote yanayohusiana na shughuli za mpira wa miguu.

“Watu waliofungwa na kanuni hii hawatakiwi kuwa na fedha za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja, maslahi (kupitia au kwa kushirikiana na wahusika wengine) katika shughuli, kama vile kuweka dau, kamari, bahati nasibu au matukio kama hayo au miamala inayohusiana na mechi za soka na mashindano.
“Maslahi ni pamoja na kupata chochote kinachowezekana kama faida kwa watu waliofungwa na kanuni hii wenyewe na/au wanaohusiana na vyama,” inafafanua ibara hiyo.
Ibara ya 27 (iii) inafafanua adhabu ambayo mhusika wa ubashiri wa matokeo anaweza kukutana nayo iwapo atabainika kujihusisha na kosa hilo.
“Isipokuwa kwamba mwenendo husika haujumuishi ukiukwaji mwingine wa kanuni hii, ukiukaji wa kifungu hiki utaenda sambamba na faini ya angalau Faranga 100,000 (Sh328 milioni) na kupigwa marufuku kushiriki katika masuala yoyote ya soka kwa muda usiozidi miaka mitatu. Kiasi chochote kinachopokewa kitakuwa kimejumuishwa katika hesabu ya faini,” inafafanua kanuni hiyo.

MCHEZO WENYEWE
Kwa wale wachezaji au maofisa wa benchi la ufundi ambao wanafahamu kuwa ni makosa kujihusisha na ubashiri wamekuwa wakiwatumia ndugu au marafiki zao kuweka mikeka ili wasibainiwe kirahisi na mamlaka za soka nchini.
Uchunguzi na Mwanaspoti na maelezo ya baadhi ya wadau wa soka ni kwamba, wanachokifanya wahusika ni kutafuta watu wa karibu wanaowaamini kama wake, wapenzi, ndugu au marafiki kisha wanawapa pesa - wanawaelekeza aina gani ya matokeo ya kubashiri wanayopaswa kuweka mikeka na baada ya mechi fedha zinazopatikana zinarudi kwa wachezaji husika.
“Mimi mpenzi wangu ni mchezaji na huwa anabeti kupitia simu yangu na huwa anaweka pesa nyingi maana anakuwa na uhakika na mara nyingi huwa anabeti mkeka wa idadi ya magoli.
“Ni wachezaji wengi tu wanafanya hivyo. Mimi zamani sikuwa nafahamu namna ya kucheza, lakini akawa ananielekeza taratibu hadi sasa najua, hivyo siku ya mechi yeye akiwa kambini ananitumia au kuniachia hela halafu mimi nabeti,” anatoa ushuhuda mmoja wa wapenzi wa mchezaji wa timu iliyopo katikati mwa msimamo wa ligi.

Kaka wa mmoja wa wachezaji anat-hibitisha kwamba amekuwa akitumi
wa katika kubeti.
“Mara nyingi tu huwa nafanya hivyo na huwa natumiwa pesa siku moja au mbili kabla. Kuna wakati anatuma hela ili nimbetie yeye peke yake lakini mara nyingine hadi wachezaji wenzake huwa wanafanya hivyo.
“Mechi ikiisha na mkeka ukawa umetiki, naenda kutoa hela kwenye kibanda cha simu au nawatumia kwenye simu zao na mimi napata kamisheni yangu,” anasema shuhuda huyo.
WANAJITOA MUHANGA
Wapo wachezaji ambao wanabeti wao wenyewe moja kwa moja na wanachokifanya ni kubeti kwa kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina tofauti na yale yao ya kawaida lakini pia kuna ambao wamekuwa wakibeti moja kwa moja kupitia kupitia laini za simu ambazo zimesajiliwa kwa majina yao.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa yupo mchezaji wa timu moja iliyopo katika nafasi nne za juu ambaye alifanikiwa kupatia ubashiri wa mechi alizobetia, lakini kampuni ambayo aliitumia kubetia ilizuia fedha hizo na mchezaji husika akaogopa kudai kwa kuhofia kwamba angebainika anafanya ubashiri wa matokeo ya michezo hivyo angekumbana na adhabu kubwa.

Kiungo ambaye hakupenda jina lake kuandikwa aliliambia Mwanaspoti kuwa mwanzoni alikuwa anabeti kwa kutumia simu yake lakini kwa sasa hafanyi hivyo.
“Zamani nilikuwa nabeti kama kawaida kwa kutumia simu yangu, sikuwa najua kama kufanya hivyo ni kosa lakini baada ya kuambiwa kwamba inaweza kuniletea shida nikaamua kubadilisha, sasa natumia simu ya mpenzi wangu,” anafichua kiungo huyo.
MAMBO KWA USHAHIDI
Mchezaji mmoja wa nafasi ya ulinzi anafichua kuwa mwishoni mwa msimu uliopita, wachezaji wa timu yake ya zamani na nyingine ambazo zilikutana siku hiyo, walifanya ubashiri kwa kushirikiana.
“Mimi sikuwa nafahamu kinachoendelea, sasa wakati mchezo unaendelea huku tukiwa tunaongoza kwa mabao 3-0, mchezaji mwenzangu akawa ananiomba tuwaonee huruma wapinzani nao wapate hata bao moja mimi nikawa sielewi.
“Baadaye mchezaji mmoja wa wale wapinzani wetu akawa anatuambia jamani kama kutufunga mmeshatufunga basi tuachieni tupate hata goli moja na cha ajabu wachezaji ambao niko nao timu moja wakawa wanawekea msisitizo kuwa tuwaachie wasije kukosa hela.
“Wakati mchezo unakaribia kumalizika, kipa wetu alifanya kosa la kizembe ambalo ni kama aliwaachia jamaa wapate bao na jambo la ajabu wachezaji wenzangu na wale wa timu pinzani wakawa wanafurahia, mpira ulipomalizika, nawauliza wakaniambia kuwa walibeti ‘GG’ kwamba kila timu itapata goli na hivyo mkeka wao umetiki,” anasema mchezaji huyo.

MAKIPA WATIMULIWA
Bosi mmoja wa klabu moja iliyopo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, anaeleza kwamba waliwahi kuwasitishia mikataba makipa wawili kutokana na mikasa ya mambo ya kupanga matokeo kutokana na makosa ambayo wameyafanya kwenye mechi.
“Kipa wa kwanza (anamtaja raia wa kigeni), huyu kama mnakumbuka msimu uliopita alitupa shida sana kuna mabao unaona kabisa ameukamata mpira vizuri, lakini akiruka akishuka chini anauachia mtu anafunga au unaona makosa yake kama vile anachukua rushwa. Sisi tulidhani anahongwa kutufungisha, lakini kumbe mwenzetu anabeti.
“Kilichokuja kutuaminisha kuna mabao rahisi aliyaachia kwenye mchezo wa timu ndogo ambayo hata sisi tunaizidi kiuchumi. Tulipokuja kufuatilia tukabaini anabeti mechi zetu na unajua hizi betting zinatoa nafasi tofauti, kwamba hata mabao mangapi ya kuruhusu kwa mechi au mapumziko, tulipombana meneja wake akatuambia, tukaona tumfukuze.
“Nimeona bado wanamlalamikia kwenye klabu nyingine alizokwenda, itakuwa bado anafanya mambo yake yaleyale, waambieni wamchunguze kwa kina maana huku kwetu yalitushinda.
“Kipa mwingine tulimfukuza msimu huu, kuna mechi ilitutibua sana, huyu tulikuwa naye kwa mkopo tulipokutana na klabu moja (anaitaja) aliachia mabao rahisi sana, yaani sisi tunafunga yeye anaachia kumbe mwenzetu anashirikiana na kiongozi wake mmoja wa zamani kubashiri matokeo na ile mechi ilitakiwa imalizike kwa sare kwa mujibu wa matokeo waliyobashiri, kila tukipata bao yeye huku nyuma anaachia tena kirahisi.
“Mchezo ulipomalizika kweli tulikasirika sana, lakini kwa kuwa ni mzawa tukasema tumvutie pumzi. Wakati huo tulikuwa hatujamlipa ada yake ya usajili anatudai tena kabla ya mechi alitukumbushia fedha zake, mchezo ulipopita siku tatu mbele akatujia na gari mpya ameinunua baada ya mechi.
“Kumbuka aliyekuja na gari nzuri, sio ya chini ya Sh23 milioni, ni mtu anayekudai tena hujamlipa hata mishahara yake, hilo lilitushtua tukasema sisi wenyewe watoto wa mjini tulifuatilia na kujua mpaka kampuni iliyomuuzia gari, tukaambiwa aliyekuja kulipia hiyo gari sio kipa huyo ni kiongozi wa klabu moja kubwa tena akimtuma msaidizi wake.

“Ilituumiza sana kichwa tukasema tusiishie hapo tuichimbe zaidi tukaja kugundua kwamba kumbe zile fedha ni mgao wa matokeo ya mchezo ule na sio kwamba alikula rushwa hapana aliambiwa akiachia mabao mawili kwenye ule mkeka atapewa milioni 28 na aliyetuambia haya ni rafiki yake mkubwa ambaye ndiye aliyekwenda naye pale kuchukua gari tulimuita na kumuahidi fedha akatuweka wazi.
“Baada ya kupata uhakika huo tukamuita akawa analia tu kwenye kikao kizima mara anasema tunamuonea mara tumsamehe eti anasema zile fedha amesaidiwa na ndugu zake ili awe na gari ya kutembelea, changamoto inakuja sisi ni klabu ndogo na huyu aliyehusika kutuharibia na hata kumshawishi kipa huyu kufanya yale ni mtu mkubwa, tukasema tuyaache lakini yule kipa tulimtimua na tukasajili kipa mwingine.”
MAREFA WANAHUSIKA
Kuna madai mengine yametolewa kwa gazeti hili yakiwahusisha waamuzi wa soka ambao wameona ubashiri ni kama fursa ya kupata fedha kupitia utoaji wa kadi au mabao kwenye mechi ambazo wanaziamua, hali ikiendelea kuonyesha namna soka nchini linavyozidi kusakamwa na mtandao wa ubashiri.
Mwamuzi mmoja ambaye kwa sasa hapewi mechi nyingi za kuchezesha anasema ingawa yapo mambo ya rushwa kwa waamuzi, lakini kando ya kashfa hiyo lipo suala la kubeti ambapo waamuzi wamekuwa wakizuia mabao au hata kuruhusu mabao yasiyo halali hali kadhalika utoaji wa kadi na penalti.
“Kuna wenzangu ambao wamekuwa wakishirikiana waamuzi watatu yaani yule wa kati na wasaidizi wake, kuamua matokeo ya mechi hasa hizi timu ndogondogo.
“Unajua kutabiri matokeo ya Simba au Yanga wakati mwingine ni ngumu. Hizi ni timu ambazo zinaweza kumfunga mpinzani mabao mengi, lakini hizi timu ndogondogo mambo ni rahisi, kuna mechi zimekuwa zikitengenezwa sare ambazo zinatoka kwa waamuzi. Mnakaa mnaangalia mpira mechi ngumu mtu kawaida tu anaweka tuta (penalti), hapo ujue mambo yalikuwa yanatakiwa yawe sare.
“Kuna siku nilicheka sana, waamuzi walitaka mechi iishie kwa bao 1-0 sasa ikatokea dakika za mwisho kabisa jamaa akasawazisha, sasa yule mwamuzi (anamtaja), mechi ilipokwisha nikampigia kumsalimia nikaona anamlaumu sana kipa wa wapinzani kwa kumharibia akisema kanichania mkeka yule ‘mpuuzi’ akiwa analaani sana,” anasimulia mwamuzi huyo.
“Eneo jingine ni kadi. Kuna kadi zinatoka unaona kabisa huyu mchezaji anaonewa. Kuna mechi kiungo mmoja wa Yanga na hata Azam waliwahi kupewa kadi za njano rahisi sana ambazo zinatokana na mwamuzi (anamtaja), alibeti kwamba mechi hiyo mpaka mapumziko inatakiwa kuwa na kadi mbili za njano. Sasa yule kiungo wa Yanga alishangaa tena anatoka Zanzibar, nilimuonea huruma alikuwa mpaka anashangaa kosa ambalo limempa kadi.
“Huyo wa Azam naye ilikuwa hivyohivyo timu yake imeamuliwa ipigwe adhabu kwenda kwao yeye anakwenda kukaa kwenye ukuta akamuuliza kitu mwamuzi, basi akalimwa kadi, alilalamika lakini ndio masharti ya mkeka yalitaka kadi ziwe nne mpaka mpira unaisha na wakati tunakwenda mwisho wa mchezo zilikuwa tatu tu, anafanyaje akampa huyo huyo.