Januari ya Simba, Yanga

Januari ya Simba, Yanga

Muktasari:

TAKWIMU za matokeo ya mechi zilizopita za Ligi Kuu Bara zilizochezwa mechi Januari zinailazimisha Yanga kufanya kazi ya ziada ili iweze kuwapiku watani wao Simba na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

TAKWIMU za matokeo ya mechi zilizopita za Ligi Kuu Bara zilizochezwa mechi Januari zinailazimisha Yanga kufanya kazi ya ziada ili iweze kuwapiku watani wao Simba na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa na pointi 44, imekuwa haina takwimu nzuri za kimatokeo katika mechi za Ligi Kuu zinazochezwa Januari kulinganisha na Simba ambao wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 35 huku wakiwa na mechi tatu za viporo mkononi.

Takwimu za misimu mitano iliyopita zinaonyesha kuwa Simba imekuwa ikifanya vyema zaidi katika mechi za Ligi Kuu zinazochezwa katika mwezi huo huku Yanga wakiwa wanakumbana na ugumu mara kwa mata.

Mwanaspoti inakuletea tathmini ya jinsi Yanga inavyoteseka na mechi za Ligi Kuu zinazochezwa Januari kulinganisha na Simba ambao huwa moto wa kuotea mbali.

Ushindi

Katika kipindi cha misimu mitano iliyopita, Yanga imecheza jumla ya mechi 14 za Ligi Kuu katika kipindi cha mwezi Januari wakati Simba yenyewe imecheza jumla ya mechi tisa.

Uwepo wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi kuanzia mwanzoni mwa Januari hadi tarehe za katikati za mwezi huo pamoja na ratina ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni sababu mbili zilizopelekea timu hizo zisiwe na idadi sawa ya michezo ya Ligi Kuu katika mwezi huo.

Kwenye mechi 14 ambazo Yanga imecheza mwezi Januari katika misimu mitano iliyopita, imeibuka na ushindi mara nane (8) ikiwa ni sawa na 57.14% wakati katika mechi tisa ambazo Simba wamecheza kwenye mwezi huo ndani ya misimu mitano iliyopita, wameibuka na ushindi mara sita ikiwa ni sawa na 66.67%

Sare

Timu zote mbili zimepata matokeo ya sare katika idadi sawa ya mechi pindi zilipocheza katika mwezi Januaro ambapo kila moja imetoka sare mara mbili katika mechi za misimu mitano iliyopita zilizochezwa mwezi huu.

Idadi hiyo ya mechi ambazo Yanga imetoka sare mwezi Januari ni sawa na 14.29% wakati kwa Simba ni sawa na 22.22%

Vipigo

Katika kipindi hicho cha misimu mitano iliyopita, Yanga imepata idadi kubwa ya vipigo katika mechi za Ligi Kuu zilizochezwa Januari tofauti na Simba ambayo haijaonja sana ladha ya kupoteza mechi.

Idadi ya michezo ambayo Yanga imepoteza katika mechi za misimu mitano iliyopita ambayo ilicheza Janauri ni minne (4) ambayo ni sawa na 28.57% wakati Simba yenyewe imepoteza mchezo mmoja tu kati ya tisa iliyocheza Januari ambao ni sawa na 11.11%

Mabao ya kufunga

Kutofanya vizuri kwa Yanga katika mechi za Ligi Kuu za Januari hazijaishia katika pointi ilizokusanya bali pia hata kwenye mabao ya kufunga huku Simba wakionekana ni tishio.

Katika mechi 14 ambazo Yanga imecheza Januari, timu hiyo imepachika jumla ya mabao 20 ikiwa ni wastani wa bao 1.43 katika kila mchezo.

Hali ni tofauti kwa Simba ambayo yenyewe imekuwa haitaki mchezo hata katika kufumania nyavu kwani katika mechi tisa ilizocheza mwezi huo, imefunga jumla ya mabao 19 ikiwa ni wastani wa mabao 2.11 kwa kila mchezo.

Mabao ya kufungwa

Simba ina wastani wa kufungwa mabao machache katika mechi za Ligi Kuu ilizocheza Januari katika misimu mitano iliyopita kulinganisha na Yanga ambayo ina wastani wa kuruhusu mabao mengi.

Januari ya Simba, Yanga

Katika mechi 14 ilizocheza ndani ya Januari kwenye misimu mitano iliyopita, Yanga imeruhusu jumla ya mabao 12 ikiwa ni wastani wa bao 0.86 kwa kila mchezo wakati Simba yenyewe katika mechi tisa, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba (7) ikiwa ni wastani wa bao 0.78% kwa kila mchezo.

Wadau

Kocha wa Simba, Sven Vandebroeck alisema kuwa hadhani kuwa historia hiyo ni kigezo cha kuamua bingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

“Katika mpira wa miguu kila siku tunaangalia zaidi kilicho mbele na sio kile kilichopita. Hicho kilichofanyika nyuma hakiwezi kutusaidia chochote kwa sasa na tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha tunapata ushindi ambao ndio utatufanya tutimize malengo yetu,” alisema Sven

Kauli hiyo ya Sven iliungwa mkono na beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ambaye alisema msimu huu timu hiyo inaonekana imeimarika.

“Ukiangalia Yanga ya sasa imebadilika na ina kikosi cha wachezaji wazuri wanaoonyesha ushindani na hata ile ari ya upambanaji iko juu na ndio maana unaona hadi sasa haijapoteza mchezo hivyo watu hawapaswi kukariri,” alisema Malima.