Jambazi sugu aliyetawala soka la Kenya

Wednesday January 06 2021
kenya pic

KATIKA historia ya soka la Kenya inayoanzia miaka ya 1970 kumekuwa na wanasoka wengi walioingia dimbani wakakipiga balaa. Uhatari wao ulitishwa. Kwa moyo wao wote mashujaa hao waliitetea bendera ya Kenya.

Tairus ‘Tairero’ Omondi, Dan Miswa, Jaffer Mwidau, Abbas Magongo, Anthony Ndolo, John ‘Zangi’ Okello, Charles Otieno, Sammy ‘Jogoo’ Onyango, Ben Oloo, Hezron Kissinger, Abdalla Shebe, Ahmed Shero, Hesbon Omollo na Joe Kadenge (wote marehemu). David ‘Kamoga’ Ochieng, Henry Motego, Austin ‘Makamu’ Oduor, Peter ‘Bassanga’ Otieno, Mahmoud Abbas, Tobias ‘Jua Kali’ Ocholla, George ‘Fundi’ Onyango, Isaiah ‘Janabi’ Omondi na Peter Dawo ni majina ambayo yanapotajwa soka la Kenya inatabasamu.

Lakini katika miaka ya 1970 na 1980 soka la Kenya lilipokuwa linatawala Afrika Mashariki na Kati kulikuwa na mtu mmoja ambaye hatajwi sana, lakini naye alikuwa ni roho ya timu.

Katika moja ya kurasa za kitabu cha ‘The Life of a Football Legend’ kilichoandikwa na mwanahabari nguli wa nchi hiyo, John Nene, gwiji wa zamani wa soka la Kenya, Joe Kadenge anasimulia maisha ya nyota wa zamani wa Gor Mahia, Nicodemus Arudhi. Huyu alikuwa na sura mbili. Alikuwa na majina mengi pia. Kwa mujibu wa rekodi za 981 kutoka magereza mbalimbali nchini humo, Arudhi aliitwa David Odhiambo, mtoto wa Nicodemus au Daniel Odhiambo au Daniel Nicodemus.

Nyota huyo ambaye aliitumikia Harambee Stars wakati fulani alikuwa kipenzi cha mashabiki na wachezaji wenzake. Aliichezea Stars mara tatu tu dhidi ya Togo, Mali na Cameroon, katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 1972.

Arudhi, kama alivyofahamika na wengi hakuwa mchezaji tu, alikuwa na maisha mengine nje ya uwanja. Mwanasoka huyo aliyezaliwa 1944 mbali na ufundi aliouonyesha mchana uwanjani, giza lilipoingia aligeukia ujambazi. Nje ya soka, Arudhi alikuwa ni jambazi sugu aliyetumia silaha hatari kuwadhulumu wakazi wa Nairobi mali zao. Uwanjani alihofiwa sana na mabeki, lakini matukio ya usiku yalimfanya kuwa mmoja wa watu waliotafutwa zaidi na Polisi katika miaka ya 1990. Baba yake alijulikana kwa jina la Nicodemus Awidhi Arudhi. Familia hii ilijaaliwa vipaji viwili; muziki na soka, lakini Arudhi historia inaonyesha alitumia muda mwingi jela kuliko aliokaa huru.

Advertisement

Marafiki walijua

Hakuna aliyejua kuhusu, sura ya pili aliyojivika Arudhi. Viongozi wa soka, kocha wake na wananchi hawakujua, lakini marafiki zake wa karibu walijua. Wachezaji wenzake walijua kila kitu kuhusu maisha ya siri na hatari. Kama anavyothibitisha Kadenge kwenye kitabu chake, katika wakati ambapo wachezaji walichezea posho na vijizawadi na sio mishahara minono kama ilivyo sasa, Arudhi alionekana na pesa nyingi. Alivaa mavazi ya thamani, alikuwa na koti la thamani la ngozi. “Alikuwa na pesa nyingi. Alivaa nguo za thamani, alikuwa na koti zuri la dhahabu, aakati ambapo wengine walisafiri kwa basi, yeye alikuwa na kawaida ya kupanda gari za kukodi (taxi) za kifahari.”

Marafiki zake, licha ya kuona utofauti mkubwa ikiwemo kuwa mtu wa kukaa pekee yake na wakati mwingine kuonekana na bastola hawakuwa tayari kuongea. Kuna kipindi inadaiwa aliiba suti kwenye duka moja jijini Paris, Ufaransa mwaka 1976.

Kuchezea Harambee

Arudhi ambaye jina lake halisi ni Daniel Odhiambo alianza kuichezea timu ya taifa akiwa na miaka 20, silaha yake kubwa ikiwa ni nguvu ya miguu ya kupiga mashuti na kasi. Licha ya kaka yake pia kuwahi kuichezea Stars, jina la Arudhi lilipata umaarufu zaidi.

Kwenye ligi, Nicodemus Arudhi aliichezea Luo Union baada ya timu yake hiyo, alijiunga na Luo Stars, Februari 17, 1968, matokeo yake Gor Mahia ikazaliwa. Kwa mashabiki, Arudhi alikuwa zaidi ya mchezaji. Kwa Gor Mahia alikuwa ni ‘Joe Kadenge’ wao.

Kwa mujibu wa rekodi za Shirikisho la Soka duniani (Fifa), Arudhi aliichezea Harambee Stars mara tatu dhidi ya Togo, Mali na Cameroon kwenye Kombe la Afrika (1972. Japo alicheza kwenye mchezo wa Ghana, sambamba na Ouma Chege, Arudhi aliwanyanyasa mabeki atakavyo. Ndiye aliyefunga bao pekee lililoipatia Harambee ushindi dhidi ya Mali katika mchezo mkali wa Afrika uliopigwa Februari 26, 1972 akiwa na miaka 28 wakati huo.

Kenyatta amtoa Jela

Hata hivyo, maisha yake ya uhalifu hayakuzuia kuiteka mioyo ya wana Gor Mahia. Miguu ya Nicodemus Arudhi iliiteka mioyo ya mashabiki wa soka nchini humo akiwemo Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta. Ni kawaida kwa Rais akiongozwa na sheria za nchi kuwaachia huru wafungwa, lakini kilichofanyika kwa Arudhi haikuwa kurudishiwa uhuru wake, bali kuwekwa huru kwa sababu maalumu. Mwaka 1965, Kenya ilikuwa na mchezo muhimu dhidi ya Ghana ulipiogwa Uwanja wa Nyayo na kutokana na uzito wa mchezo, Rais Kenyatta alitoa amri kwa mkuu wa Gereza la Kamiti kumuachia huru mfungwa huyo kwa ajili ya kuichezea Harambee.

Arudhi alipewa msamaha wa siku moja. Uwanja wa City ulizingirwa na askari wa magereza, ishara kuwa kuna mfungwa uwanjani. Hakumuangusha Rais, alifunga bao la kusawazisha, mchezo ukamalizika kwa sare ya 1-1. Baada ya mchezo alirudishwa gerezani. Baadaye sana aliachiwa huru alipomaliza kifungo.

Kifo chake

Mhalifu huyu mzoefu hakuwahi kuacha kazi yake ya ujambazi. Juni 21, 1981 inadaiwa kuwa Arudhi alijisalimisha polisi huku akiahidi kuwapeleka alikoficha bunduki. Hata hivyo, walipofika katika eneo husika aliamua kutimua mbio.

Hakufika mbali, walimpiga risasi. Katika maelezo yao inadaiwa kuwa polisi walisema walipata silaha nyumbani kwa nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia. Simulizi hiyo haingii kichwani kwa sababu mara kwa mara Arudhi alikuwa ndani (nyumbani) na nje ilikuwa ni jela mbalimbali nchini.

Kwa sababu alikuwa mtu hatari aliyetafutwa na polisi kuna wakati alikamatwa kwa shtaka la mauaji. Kwa maana hiyo, ni ngumu kwa mtu kama huyo kuhifadhi silaha nyumbani kwake. Miaka 20 ya kucheza soka la uhakika na ujambazi wa kutisha ilimalizwa kwa risasi.

Alikuwa na miaka 37 tu wakati wa kifo chake. Miaka 16 baada ya Rais Kenyatta kumfungulia ili aokoe jahazi la Harambee, Arudhi alipoteza uhai wake mtaani Shauri Moyo katika usiku wa giza. Inadaiwa alipigwa risasi mgongoni na askari.

Imeandikwa na FADHILI ATHUMANI

Advertisement