Inashangaza Kamati ya Saa 72 inavyochukua jukumu la mambo ya uwanjani kuamulia mezani
Muktasari:
- Huo ulikuwa ni uamuzi wa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi maarufu kama Kamati ya Saa 72 baada ya mchezo baina ya wenyeji Dodoma Jiji kuvunjika katika dakika ya sita kutokana na umeme kukatika na kutokuwepo na jenereta ya kutibu tatizo hilo.
KWA kawaida mtandao huchangia kuniondolea msongo pale napokabiliwa na masuala ambayo utatuzi wake unaonekana ni mgumu kufanyika ndani ya muda mfupi. Lakini, kwa takriban siku saba za kukosekana kwa mawasiliano hayo nilikuwa na cha kunipoza akili; kufutwa kwa goli la Dodoma Jiji na Pamba kupewa ushindi wa mezani.
Huo ulikuwa ni uamuzi wa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi maarufu kama Kamati ya Saa 72 baada ya mchezo baina ya wenyeji Dodoma Jiji kuvunjika katika dakika ya sita kutokana na umeme kukatika na kutokuwepo na jenereta ya kutibu tatizo hilo.
Huo ni uamuzi mwingine wa kushangaza na kufurahisha unaoendelea kufanywa na Kamati ya Saa 72 kinyume na utashi, utamaduni na sheria za mpira wa miguu. Ni takriban wiki moja tangu kamati hiyo iamue kumuonyesha kadi nyekundu beki wa Yanga, Ibrahim Bacca baada ya refa kutoona mchezo wake wa hatari dhidi ya mchezaji wa Mbeya City na baadaye kumuongezea adhabu.
Yaani mchezaji anayecheza mchezo wa hatari kama aliofanya Bacca anastahili kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja ambayo kikanuni husababisha akose mechi tatu. Kanuni hizo hizo zinaipa Kamati ya Saa 72 mamlaka ya kumuongezea mchezaji huyo mechi hadi mbili.
Kwa hiyo, licha ya refa kutoona rafu hiyo Kamati ya Saa 72 ikaona kwenye picha za marudio za video na kuamua kuchukua uamuzi ambao ulitakiwa uwe wa refa. Kanuni zinataka uamuzi wa refa uwe wa mwisho na hivyo pale anaposhindwa kuamua vizuri ndiye ambaye hutakiwa kukumbana na adhabu na si aliyefanya tukio ambalo refa hakuliona. Hii ni mara ya kwanza ulimwenguni.
Kamati inaweza kufanya uamuzi kwa matukio yanayotendeka wakati refa amesimamisha mchezo. Ndio maana hata mwamuzi msaidizi wa video (VAR), huwa hafanyi uamuzi wowote iwapo kuna tukio analohisi kuwa la mchezo wa hatari, bali humshauri mwamuzi wa kati aende kwenye runinga pembeni ya uwanja kuangalia kwa karibu na kuchukua uamuzi.
Kama tafsiri yake itakuwa kuwa tukio halikuwa la hatari kiasi cha kustahili kadi nyekundu ya moja kwa moja uamuzi wake utakuwa wa mwisho. Na kama alikosea kushikilia uamuzi wake, basi adhabu itakuwa kwake si kwa aliyefanya tukio. Iweje bila ya teknolojia hiyo ya VAR kamati ichukue mamlaka ya refa?
Hata siku moja haiwezekani kadi ikatolewa kwenye meza ya majadiliano. Halafu meza hiyo hiyo iliyotoa kadi inavua mamlaka iliyojivisha ya refa na kurudi kwenye mamlaka yake ya mezani na kuongeza adhabu ya kukosa mechi mbili. Kamati hiyo hiyo ikafanya uamuzi mwingine wiki iliyopita. Hadi dakika ya sita wakati umeme unakatika, Dodoma Jiji ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0. Lakini bao hilo likafutwa kitu nilichowahi kutabiri, na kamati ikaipa Pamba ushindi wa mabao matatu na pointi tatu. Kisa? Eti Dodoma Jiji ilishindwa kufanya maandalizi sahihi kwa ajili ya mchezo huo.
Ajabu ni kwamba hadi Bodi ya Ligi inakubali Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma utumike kwa mechi za usiku ilishajiridhisha kuwa kuna miundombinu yote inayofaa kwa ajili ya mechi za usiku. Inakuwaje Dodoma Jiji wakaonekana hawakuandaa mechi kadri ilivyotakiwa hadi mchezo unavunjika?
Sheria za mpira wa miguu zinataka mchezo unaovunjika kwa sababu zilizo nje ya uwezo umaliziwe dakika zilizobaki siku inayofuata kuepuka timu kupewa ushindi wa mezani ambao hupoteza ladha ya mashindano. Inawezekana Dodoma Jiji waliambiwa watafute jenereta, lakini jenereta la kuazima au la kukodi si sehemu ya miundombinu ya uwanja iliyokaguliwa na Bodi ya Ligi na huwezi kutegemea kuwa litakalopatikana litafaa kwa wakati huo. Hata msimamizi wa mchezo ambaye ni kamishna alitakiwa kuhakiki mapema kabla ya mchezo kuanza.
Waendeshaji wa mpira wa miguu duniani wanahaha kila kukicha kuhakikisha kuwa mchezo unachezwa kwa dakika zote tisini na kufanyiwa uamuzi stahiki ili kutopoteza ladha ya mpira wa miguu na kuwapa mashabiki kile wanachostahili.
Hata utamaduni wa mpira wa miguu wenyewe unaweka mazingira sawa kwa kila upande kutumia dakika tisini ipasavyo. Ndio maana Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), lilifuta bao la dhahabu. Bao la dhahabu ni lile lililokuwa linafungwa katika dakika za nyongeza za mechi za hatua ya mtoano. Kama timu hazikupata mshindi ndani ya dakika tisini, basi bao linalofungwa wakati wowote mara baada ya dakika 30 za nyongeza kuanza husababisha mchezo kumalizika hapohapo.
Lakini, baada ya tafakari, Fifa ikaona kuwa kanuni hiyo inaondoa haki ya msingi ya timu kutumia dakika 30 za nyongeza ipasavyo na hivyo kulitangaza bao hilo kuwa ni katili na halistahili kuendelea kutumika.
Inakuwaje basi Dodoma Jiji inyimwe haki yake ya msingi ya kutumia dakika zote tisini ipasavyo - tena iporwe bao halali lililofungwa ndani ya muda halali? Kwa kitendo cha Bodi ya Ligi kuwapa mamlaka watu wachache kuamua mezani matokeo ya mchezo uliopaswa kuchezwa kwa dakika tisini ni kuondoa maana nzima ya haki hiyo ya msingi katika mpira wa miguu.
Ni lazima Bodi ya Ligi ijikite katika kuadhibu wale wanaohusika kusababisha matatizo ya mchezo na si kukimbilia kuamua matokeo. Ni lazima jitihada kubwa zifanyike kuhakikisha mpira wa miguu unachezwa kwa dakika zote tisini. Kama ilichukua miezi mitatu kufanya uamuzi wa mechi ya Yanga na Simba msimu uliopita ili mechi kamili ichezwe na si kuadhibu waliohusika kusababisha uahirishwe, imekuwaje rahisi kuamua matokeo ya mechi ya Dodoma Jiji na Pamba iliyovunjika kutokana na tatizo la umeme?
Mwenendo huu wa uamuzi wa Kamati ya Saa 72 unatishia uwezekano wa mechi nyingi zaidi na uamuzi mwingi unaotakiwa kuchukuliwa na waamuzi, kuamuliwa mezani na wachache. Ni budi Bodi ya Ligi ilione hilo na halihitaji kufanya marekebisho katika kanuni kwa kuwa kamati inafanya tafsiri ya kanuni hizohizo.