Ilianza kwa Arusha United, sasa Gwambina FC

MSIMU wa 2019-20 Klabu ya Arusha United FC iliamua kujiondoa Ligi Daraja la Kwanza kutokana na kutochukuliwa hatua kwa matukio mengi yaliyokuwa yakifanywa na timu zinazomilikiwa na taasisi za kijeshi dhidi ya wenyeji hao wa jijini Arusha.

Timu hizo ni pamoja na Rhino ya Tabora, Polisi ya Kilimanjaro na Transit Camp, ambazo mashabiki wake walituhumiwa kuhusika katika vurugu zilizofikia kiwango cha kushambulia wachezaji na hata baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, lakini kila ilipoandika barua Bodi ya Ligi (TPLB) kuomba hatua zichukuliwe, haikuona chochote kikifanyika.

Pia, klabu hiyo ilidai haikuruhusiwa kurekodi mechi zake licha ya Bodi ya Ligi kuipa kibali kufanya hivyo kutokana na viongozi wa mikoa ambayo timu hiyo ilikuwa inacheza, kuzuia wapigapicha wa Arusha United.

Katika baadhi ya matukio, kamishana wa mechi alilazimika kuzuia wachezaji wa Arusha United kuingia vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kuhisi kuwepo harufu kali ambayo walihisi ilikuwa ni dawa iliyopulizwa kudhoofisha wachezaji.

Hata hivyo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya malalamiko hayo wala kufanya uchunguzi kujua kama ni ya kweli, licha ya utaratibu wa Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka (TFF) kuwa na maofisa wake katika kila mechi kwa ajili ya kuziratibu na kufuatilia uchezeshaji pamoja na usalama.

Arusha United ikaamua kujitoa, lakini kwa kuwa uamuzi huo ulifanyika wakati zikiwa zimesalia mechi chache, Bodi ya Ligi ikadaiwa kufanya vituko. Inadaiwa kuwa bodi hiyo ilihakikisha wachezaji – na si timu ya Arusha United — wanafika katika kila kituo kuhakikisha wanaiwakilisha klabu hiyo kucheza mechi zake zote ili uamuzi wa kujitoa usivuruge msimamo wa Kundi B.

Inadaiwa wakati mwingine hadi viongozi wa bodi walihakikisha wanasafiri kufuata mechi za wachezaji wa Arusha FC ili kuhakikisha wanatimu wajibu wa timu hiyo. Kama kawaida yetu, baada ya msimu kuisha, haukufanyika uchunguzi wowote wala tathmini ya kina kujua ukweli wa matukio hayo na kuchukua hatua ambazo zingerekebisha hali hiyo. Arusha United ilishuka na sasa iko daraja la pili.

Sijui kama wale wadau waliokuwa wakiishangilia na kuiunga mkono Arusha United wanaendelea na moyo huo. Kama wapo watakuwa ni wachache sana kwa kuwa ni lazima viongozi wa Arusha United walimwaga sumu mbaya kueleza hali mbaya ya usimamizi wa soka ambayo walihisi ilisababishwa na Bodi ya Ligi kutowajibika ipasavyo.

Ni kitendo cha nadra katika dunia ya leo timu kujitoa kwa sababu kama hizo, halafu kusiwe na hatua zozote za kuliangalia suala hilo kwa kina. Badala yake, unaweza kukuta bodi inanukuu vipengele kwenye kanuni kujilinda bila ya kujali athari zinazotokana na kutochukua uamuzi na pia kutotoa hata ufafanuzi wa kile kilichokuwa kinalalamikiwa.

Nahisi ndicho kinachoendelea hivi sasa kwa Gwambina. Mamlaka hazitaki kukubali kuwa imejiondoa kwa sababu kitendo hicho kitaathiri msimamo wa ligi hata kama kinachoendelea ni kinhyume na kanuni. Mamlaka zinajificha kwenye kanuni kwamba hazijapata taarifa rasmi ya kujitoa kwa Gwambina. Hivyo kinachofanyika ni kuipokonya pointi katika mechi zote ambazo haifiki uwanjani na si kufuta matokeo yake yote. Hapa kuna ujanjaujanja.

Kwangu haikuwa habari ya kushangaza wakati mmiliki wa Gwambina FC, Alexander Mnyeti alipotangaza kuiondoa timu hiyo kwenye ligi zote, akidai hataki kuendekeza tabia ya kukidhi mahitaji ya pembeni ya maofisa wa Bodi ya Ligi.

Kwa taarifa ambazo nilikuwa nazipata kwenye maongezi, ukijumlisha na kauli ya miaka kama miwili nyuma ya Mnyeti, sikuona ajabu kwamba hatimaye mmiliki huyo amefikia hatua ambayo aliwahi kutishia huko nyuma kuwa angeichukua.

Awali alikuwa akilalamikia uendeshaji mbovu wa ligi, waamuzi kuchezesha kwa maelekezo na vitendo vingine na akafikia hatua ya kusema amewekeza sana katika soka kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya michezo na kama hali ingeendelea hivyo hangeona tatizo kugeuza Uwanja wa Gwambina kuwa shamba la kulishia mifugo yake.

Wakati huo niliandika katika safu hii kuwa tishio lake halifai kupuuziwa kwa kuwa ni bahati mbaya sana washiriki wakubwa wa soka Tanzania hawana viwanja, tofauti na nchi zilizoendelea. Kwetu viwanja vingi vinamilikiwa na serikali, CCM, Halmashauri au watu binafsi wachache sana kama Azam FC.

Katika mazingira kama hayo, wamiliki wa viwanja ni lulu kwa mpira wetu kwa kuwa ndio wadau wakubwa. Leo Mnyeti amevunja timu na huenda kesho akaamua uwanja utumike kwa shughuli nyingine. Vipi kuhusu vijana wa eneo hilo? Vipi ligi za wilaya, za mkoa na hata mechi za mabingwa wa mikoa? Vipi mashindano mengine ya vijana?

Hatua ya mmiliki wa Gwambina haiwezi kushughulikiwa kwa kukaa ofisini na kunukuu kanuni zinazohalalisha uwanja kuzuiwa kutumika kwa mechi za Ligi Daraja la Kwanza, bali kwa mazungumzo ya kiungwana.

Ni wiki iliyoisha tu, mechi zilizotakiwa kufanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa zilisogezwa mbele kwa kuwa mmiliki amepanga shughuli nyingine! Hapo TFF na Bodi ya Ligi hawastuki tu! Vipi wamiliki wengine wakiamua kutumia viwanja vyao kwa shughuli nyingine na mechi za ligi zikalazimika kusubiri?

Huenda ni kweli kabisa kwamba Gwambina Complex ina upungufu, lakini ukweli mmiliki ametoa tuhuma za kuombwa rushwa, ni suala zito; halifai liishe juujuu. Ni muhimu kufanya uchunguzi wa kina kama nilivyodokeza hapo juu kuhusu ule uwanja ambao haukukaguliwa na bado ukapitishwa.

Kama viwanja vinapitishwa halafu baada ya raundi tatu tu vinazuiwa, basi kuna tatizo kubwa. Inawezekanaje uwanja uliopitishwa kabla ya kuanza kwa ligi ukaharibika baada ya mechi tatu tu kiasi cha uamuzi mwingine kuchukuliwa wa kuuzuia?

Pia, hata kama Gwambina Complex ina upungufu, bado TFF na Bodi ya Ligi ndio waliotakiwa wawe mstari wa mbele kuwatafuta wamiliki kujadiliana nao kuhusu mahitaji na mambo mengine ya msingi kuondoa upungufu huo. Sidhani kama Mnyeti angechukua hatua, hata ya kuongea na vyombo vya habari, kama viongozi wa juu wa Bodi ya Ligi na TFF wangekutana naye na kujadiliana kwa kina suala hilo.

Tunaelekeza hayo yote kwenye kanuni za Leseni za Klabu, lakini hivi Bodi ya Ligi imeshakaa na klabu kujadiliana nazo utekelezaji wa masharti yaliyomo kwenye kanuni hizo?

Kujadiliana ni mambo gani wayape kipaumbele sasa na yapi yaje baadaye? Washajadiliana viwango vya chini kwa viwanja vinavyotakiwa kutumika kwa Ligi Kuu, Championship, Ligi Daraja la Kwanza na nyingine?

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) linafundisha viongozi wa soka kujenga uhusiano mzuri na wamiliki wa viwanja ili mchezo uendeshwe katika mazingira mazuri. Kama uhusiano utakuwa ni huo wa kusomeana kanuni, sijui tunatengeneza nini huko mbele!

Ni muhimu sana, tena nasema sana, kwa viongozi wa soka kutoendekeza hii tabia ya kujibishana na wadau wa soka kuhusu mambo ya msingi. Wakati mwingine busara ni muhimu sana ikatangulizwa ili kutengeneza mazingira mazuri kwa kanuni kufanya kazi bila misuguano. Tukitaka kanuni zifanye kazi kwanza, ni lazima utekelezaji wake utakumbana na vikwazo ambavyo kimsingi havikutakiwa kuwepo.

Naamini marekebisho ya Uwanja wa Gwambina Complex si hoja pekee iliyosababisha mmiliki aiondoe timu, bali ni malimbikizo ya matukio mengi kuanzia kama yale ya uendeshaji kama yaliyoikumba Arusha FC, au ya ukaguzi wa viwanja kama yale niliyohadithiwa au kiburi.

Haya yote yanaweza kulainishwa na vikao vya pamoja vya kujadili kwa kina matatizo na pale ambapo kutaonekana kweli kuna tatizo, uchunguzi wa kina ufanyike ili suluhisho la kweli lipatikane.