Ifahamu asili ya hat trick

Muktasari:

Hawa wawili wameifanya idadi ya wachezaji kufunga hizo hat trick kufikia 54 katika michezo zaidi ya 800 tangu mashindano hayo yaanze 1930 nchini Uruguay.

KATIKA fainali za 22 za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar mwaka juzi, wachezaji wawili Concalo Ramos wa Ureno na  Kyllian Mbape wa Ufaransa ndio walioibuka na kile ambacho kwa kimombo kinaitwa hat trick yaani kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja.

Hawa wawili wameifanya idadi ya wachezaji kufunga hizo hat trick kufikia 54 katika michezo zaidi ya 800 tangu mashindano hayo yaanze 1930 nchini Uruguay.

Kwa bahati mbaya sikumbuki katika miaka ya karibuni kusoma au kusikia maelezo ya kina ya nini hasa hat trick na historia yake ili kumuwezesha shabiki wa kandanda kuelewa kwa undani suala hili.

Kinachoandikwa au kuelezwa ni kwa mchezaji kupata “hat- trick” na sio zaidi.

Leo nitazungumzia chanzo cha hili neno hat trick. Nilipoanza kuandika habari za michezo katika miaka ya 1960 neno “ hat- trick” lilinikanganya kwa vile neno hat kwa Kiingereza ni kofia na hio trick ina maana ujanja au hadaa. Nlijiuliza upo uhusiano gani wa kofia na ujanja katika kufunga hayo mabao matatu?

Wakati ule zilitolewa tafsiri tofauti na  mashirika ya soka ya kimaifa na wataalamu wa kandanda.

Utata uliongezeka juu ya historia na asili ya neno hili hat-trick. Vyama vya michezo vingi hadi leo vipo katika mvutano wa kila mmoja kudai asili yake inatokana na mchezo wao.

Wachambuzi wa kandanda wengi hupenda kusema nchi zao ndio ziliobuni neno hili.

Ninakumbuka utata uliozuka juu ya “hat trick” katika mkutano uliofanyika chumba cha habari cha Tanganyika Standard (sasa Daily News) katika barabara ya Maktaba jijini Dar es Salaam mwaka 1967.

Mhariri wetu, Ken Ridley (Mwingerea) alituuliza nini maana ya hat trick. Tulikuwa watu zaidi ya 20 katika mkutano, theluthi wakiwa Wazungu kutoka Uingereza, Ireland, New Zealand na Australia.

Miongoni mwao tulikuwepo waandishi wa michezo kama watano. Pamoja nami pia alikuwepo Hadji Konde, mwandishi wa kujitegemea Chris Ndakaba na John Gardener (wote marehemu).

Kila mmoja alitoa tafsiri yake na hatimaye tulikubaliana hakuna aliyeelewa maana halisi ya neno hili na historia yake, isipokuwa tulilitumia tu kila alipotokea mchezaji kufunga mabao matatu.

Kila nilipokwenda kwenye michezo ya kimataifa nje ya nchi niliwauliza waandishi wa michezo waliobobea maana ya “hat-trick”. Kila mmoja alinipa maelezo tofauti, kama nilivyoona katika kile kikao cha ofisini.

Tokea mwanzoni wa karne hii nilijitahidi kumaliza kiu yangu ya kuelewa  maana na historia ya neno hili, lakini bado sijapata jawabu iliyoniridhisha.

Nilichobaini kupitia niliyoelezewa kwa mdomo, niliosoma kwenye vitabu, niliyokuta katika mitandano na njia nyengine ni utata, hasa juu ya asili na tafsiri ya hat-trick.

Wapo wanaosema chanzo ni katika mpira wa magongo kwenye uwanja wa barafu, lakini wapo wanaodai ilitokana na mchezo wa kriketi.

Lipo kundi linalosema chanzo ni katika kandanda na wengine wanadai ni kutokana na mchezo wa mpira wa kikapu.

Kila upande unayo maelezo ya kuvutia yenye tarehe na maelezo mengi kutaka kuthibitisha msimamo wao.

Katika kitabu kiitwacho Cricketers Annual kilichoandikwa mwaka 1877 na James Lilly inaelezwa kuwa chanzo chake  kilitokana na siku moja mchezaji kuchukuwa 'wicket' sita kwa kurusha mipira saba. Baada ya mafanikio hayo mchezaji huyo alivua kofia yake (hat) mara tatu na kuivaa.

Lakini pia inaelezwa kuwa miaka 10 kabla ya hapo mchawi mmoja aliyekuwepo uwanjani katika mchezo wa kandanda alivua na kuivaa tena mara tatu kofia yake aliposhangilia hayo magoli matatu yaliyofungwa na mchezo mmoja.

Falsafa nyingine ni kuwa matumizi yake yalianza katika mchezo wa mpira wa magongo mwaka 1858 katika uwanja wa Hude Park, Uingereza .

Kwa mujibu wa simulizi, mchezaji aitwaye Stephenson alipopewa zawadi ya kofia kwa kuwatoa wachezaji watatu, mmoja baada ya mwengine kwa kuwarushia mipira mitatu na kila mmoja kugonga vile vijiti vitatu.

Wengine wanadai lilitokana na mchezo wa mpira wa magongo kwenye barafu ilipokuwa kawaida (hailezwi wakati) kule Amerika ya Kaskazini kuona mashabiki wanavua kofia  na kuzirusha uwanjani mchezaji alipofunga mabao matatu.

Vile vile yapo maelezo kuwa mfanya biashara wa duka la kuuza kofia katika mji wa Toronto, Canada, alikuwa na kawaida katika miaka ya 1940 kumzawadia kofia mchezaji aliyefunga mabao matatu katika mchezo mmoja.

Hadithi nyengine ni ya  klabu moja ya Canada ya kiwanda cha kutengenezea kofia iligawa kofia kwa mashabiki katika mwaka 1946 kila alipotokea mchezaji kufunga mabao matatu.

Kubwa zaidi ni kwamba upo utatanishi wa hat-trick” inapatikana vipi. Wapo wanaosema mabao yote matatu katika soka au mpira wa magongo lazima yafungwe katika kipindi kimoja, cha kwanza au cha pili na sio mawili kipindi kimoja na kipindi chengine au katika muda wa nyongeza.

Katika kriketi wengine wanasema hat-trick hupatikana katika mzunguko mmoja wa kurusha mipira sita na wengine katika mchezo mzima, uwe wa muda wa siku moja au tatu.

Katika kandanda ndio upo mkorogo. Wapo wanaosema hat-trick hupatikana kwa mchezaji kufunga mabao matatu mfululizo bila ya wapinzani kupata bao wakati amefunga hayo mabao matatu. Lakini wapo wanodai ni kwa muda wote wa mchezo, ikiwa pamoja na wakati wa nyongeza au panapokuwepo mpira wa adhabu. Hili goli la mpira wa adhabu lina utata kutokana na wapo wanaosema linahesabika na wengine wanaosisitiza kuwa halistahiki kuhesabiwa.

Huu mvutano katika kandanda  unakwenda mbali zaidi. Lipo kundi linalosema hizi hat-trick zipo za dhahabu, fedha na shaba.

Hii ya shaba wanasema ni ya magoli matatu yaliofungwa kwa njia yoyote ile, iwe yote kwa mguu au kwa kichwa. Ile ya fedha ni  mchezaji anapopata magoli mawili kwa mguu wa kulia au kushoto na moja kwa kichwa.

Hat trick ya dhahabu ni ya mchezaji kufunga bao moja kwa mguu wa kulia, moja mguu wa kushoto na jingine kwa kichwa.

Katika sakata hii ninakumbuka sokomoko aliozusha mwaka 1969 aliyekuwa kocha wa kikosi cha Uingereza kilichobeba Kombe la Dunia 1966, Alf Ramsey mwaka 1969..

Ramsey aliuliza: “Je kama mchezaji atafunga bao moja kwa mguu, la pili kwa kichwa na la tatu kwa kifua itakuwa hat -trick ya almasi?"

Wapo waliouliza panapotokea mabao yote matatu kufungwa haraka haraka kama alivyofanya Alex Torr wa Uingereza katika ligi ya Jumapili ya nchi hiyo kwa kutumia sekunde 70 itakuwa hat - trick ya aina gani? Torr alikuwa akiichezea Ross County ilipokutana na Narin County tarehe 28 Novemba, 1964.

Uholanzi iliwahi kusema inahesabu mchezaji kupata hat-trick kama amefunga mabao yote matatu katika nusu moja ya mchezo. Bao la tatu linalofungwa Ujerumani katika muda wa nyongeza huhesabiwa, tofauti na ilivyo katika nchi nyingi za Ulaya.

Ni kawaida katika nchi nyingi  mchezaji anayefunga mabao matatu katika mchezo mmoja kukabidhiwa mpira uliotumika kuuchukua nyumbani kama kumbukumbu.

Katika miaka ya karibuni zimekuwepo hat- trick nyingi, lakini zipo ziliohesabika kuwa za kiufundi na kutolewa  mfano kama uwezo mkubwa wa mchezaji.

Miongoni mwao ni ya Sydney Leroux wa timu ya wanawake ya Marekani wakati walipoifunga Mexico 7-0 mwezi Januari , mwaka 2013. Dada huyu alifunga bao la kwanza kwa  kichwa, la pili kwa mguu wa kulia na la tatu kwa mguu wa kushoto. Alifunga mabao yote matatu katika dakika 19 za kipindi cha kwanza.

Karibu na mpira kumalizika aliongeza bao la nne na kusema hakutaka liingie katika hesabu kwa vile alikuwa anafanya mazoezi.

Christiano Ronaldo alipokuwa na Real Madrid alifunga “hat trick“ yake ya 19 katika Ligi ya Hispania walipocheza na klabu ya Getafe karibu miaka minne iliopita. Bao moja lilikuwa kwa mguu wa kulia, jingine kwa  mguu wa kushoto na moja kwa kichwa.

Edinson Cvani wa Uruguay alifunga mabao matatu, kila mguu bao moja na jengine kwa kichwa timu yake ya Napoli ilioicharaza AS Roma 4-1 katika Ligi ya Italia.

Kwa wachezaji wa Kiafrika wanaocheza Ulaya, mafanikio ya Ayegbeni Yakubu wa Nigeria katika mwaka 2007 hayashauliki.

Alikuwa anaichezea Everton ilipopambana na West Ham mara tu baada ya kutoka  Middlesbrough. Aliyafunga mabao hayo kwa mguu wa kulia,  kushoto na kichwa.

Baadaye alisema alitamani sheria ingeliruhusu kufunga bao kwa mkono.

Zipo simulizi nyingi za kuvutia juu ya hiki kinachoitwa hat trick. Miongoni mwao ni :

Pedro Zurita wa Argentina (alizaliwa tarehe 3, Novemba 1997[) anahesabika kuwa mmoja wa mabingwa wa hat trick. Akiwa na klabu ya Larbatata aliweka historia ya kufunga zaidi ya mabao 1,000, kati ya hayo 128 kwa timu ya Argentina na kuwa na hat trick zaidi ya 50.

Mchezaji anayehasabika kufunga hat trick kwa mwendo kasi zaidi ni Tommy Ross wa Uingereza.

Jina lake limeingia katika kitabu cha rekodi za dunia cha Guiness kutokana na kudunga mabao matatu katika kipindi cha sekunde 90 (dakika moja na nusu) wakati akiwa na miaka 18 alipolichezea Ross lilipokutana na Nairn 1964 katika mashindano ya majimbo Uingereza.

Mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero aliifungia mabao matano  Manchester City katika ushindi wake wa 6-1 ilipokuta na Newcastle 6-1 katika ligi ya mwaka 2015.

Timu yake ikiwa imepachikwa bao moja mapema Sergio alichacharuka na kufunga mabao matano katika kipindi cha dakika 20 na kushangiliwa kwa nderemo na vifijo.

Hii ni pamoja na mabao matatu ya moja baada ya jengine katika kipindi cha dakika 8.

Sergio ameungana na Andy Cole, Alan Shearer, Jermain Defoe, na  Dimitar Berbatov kuwa wachezaji pekee kuwahi kufunga mabao matano katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Katika ligi ya Bundesliga ya Ujerumani, Robert Lewandowski wa Bayern Munich alifanya maajabu timu yake ilipokutana na Wolfsburg.

Akiwa amekaa katika ubao wa wachezaji wa akiba aliingia kipndi cha pili na ulipoanza mchezo tu alihangaika kila pembe ya uwanja kama kuku tembe aliyekuwa anataga kutaga.

Katika kipindi cha dakika 9 alifunga mabao matano, kati ya hayo matatu ya kwanza katika muda wa dakika nne.

Wachambuzi wa mchezo waliuliza : Hali igekuwaje kama alikuwemo tokea mwanzo wa mchezo?

 Jimmy O'Connor wa Uingereza alipokuwa aikichezea klabu ya Scotland ya Shelburne ilipopambana na Bohemians katika ligi ya Scotland mwaka 1967 alifunga mabao matatu katika dakika moja na sekunde, 13.

Eduardo Maglioni wa Argentina alipoichrzea Independiente ilipokutana na Gimnasia La Plata, katika mwaka1973 alifunga hat trick kwa dakika 1 na sekunde 51.

Magnus Arvidsson wa Sweden alipoichezea Hassleholms ilipokutana na Landskrona 1995 alifunga mabao matatu katika muda wa dakika 1 na sekunde 29.

Alex Torr wa Uingereza wakati akiwa na Rawson Spring ilipokutana na kabu ya Winn Gardens katika mwaka  2013 alifunga hat trick katika kipindi cha dakika 1 na sekunde 39.

Katika fainali za Kombe la Dunia za 1966 Geoff Hurst wa England ndiye mchezaji pekee aliyejipaia hat trick katika fainali hizoambapo England iliifunga Ujerumani Magharibi Magharibi 4-2 katika mchezo wa fainali.

Katika kumbukumbu za kupatikana hat-trick katika mchezo wa kandanda yapo maelezo mengi juu ya namna wachezaji hao walivyopata mafanikio hayo.

Lakini ipo hat-trick moja ambayo imekuwa ikizungumziwa sana na unaweza kusema ni ya aina yake na sijuwi kama itakuwa rahisi kupatikana nyengine ya aina hio.

Hii ni ile iliyoshuhudiwa tarehe 21 Aprili mwaka 1986 katika uwanja wa Upton Park, Uingereza, na kubakia kuwa ya kipekee.

Hat-trick hii ambayo imepewa maelezo mengi na vyombo vya habari ni ile iliyopatikana katika mchezo ambao West Ham iliichapa Newcastle 8-1.

Wakati karibu hat-trick zote huwa ni za wachezaji wa kiungo au washambulizi hii ilikuwa ni ya mlinzi.

Mfungaji alikuwa mlinzi wa klabu ya West Ham kwa miaka 21 na ambaye pia aliwahi kuichezea timu ya Uingereza kutoka 1981 hadi 1986, Alvin Edward Martin.

Martin alifanya maajabu haya yaliyowashangaza na kuwafurahishi mashabiki wengi wa kandanda kwa kufunga mbao yake hayo matatu kwa magolikipa watatu tafauti katika mchezo huo.

Kwanza alimfunga katika dakika ya nne tu baada ya mchezo kuanza golikipa mwenye jina la kwanza kama la kwake, Martin Thomas.

Golikipa huyu aliiingia uwanjani akiwa na maumivu ya bega kwa vile mlinda mlango wa akiba namba mbili kucheza.

Kwahivyo, Martin Thomas ikamlazimu kuteremka uwanjani kuokoa jahazi ya Newcastle huku akiwa na maumivu.

Lakini dakika chache baada ya mchezo kuanza na kufungwa bao moja maumivu yalizidi na kulazimika kutoka nje.

Kijana mdogo Peter Beardsley ambaye ndio kwanza alikuwa amejiunga na Newcastle alikuwa tayari kwenda kulinda nyavu , lakini kocha wa Newcastle ,Willie McFaul, alikataa kwa vile alikuwa mdogo na bado hakuwa na uzoefu wa kutosha wa kuweza kuhimili vishindo.

Badala yake mchezaji wa kiungo, Chris Hedworth, akaenda kulilinda goli na baada ya dakika 15 hakuweza kuzuwia mpira wa kichwa uliopigwa na Alvin Martin.

Huyu kipa alipokuwa anajaribu kuokoa mchomo mkali uliokuwa unaelekea golini naye akaumia bega na kutoweza kuendelea na mchezo akiwa kipa. Hapo tena ndipo Beardsley alipopewa nafasi aliyokuwa anaisubiri kwa hamu na kuingia uwanjani kuzuia maafa yasizidi kuwa makubwa na Hedworth akarudi kucheza katikati.

Beardsley naye alifungwa mabao matatu ya haraka haraka na lile la mwisho lilipachikwa kimiani na Martin na matokeo kuwa 8-1 na hivyo Martin kuweka historia ya aina yake katika kandanda.

Alvin Edward Martin aliyezaliwa Lancashire mwaka 1958 alitumia muda mrefu wa uchezaji wake wa kandanda na kabu ya West Ham ambayo aliteremka nayo uwanjani katika michezo 598 ndani na nje Uingereza. Akiwa na West Ham kwa miaka 21 mfululizo alifanikiwa kuisaidia klabu hio kubeba Kombe la FA katika mwaka 1980. Aliihama klabu ya West Ham 1966 na kuichezea msimu mmoja Leyton Orient na baadaye akawa kocha wa klabu ya Southern United kwa miaka miwili.

Aliichezea England michezo 17  na alikuwemo katika kikosi cha ncho hio kiliocheza fainali za Kombe la Dunia za 1986.

Mchezo wake wa kwanza na timu ya Enland ni pale ilipomenyana na Brazil katika uwanja wa Wembley mwezi Mei, 1981.

Baada ya hapo alikuwa mchambuzi maaarufu wa kandanda wa kituo cha radio cha Talk Sport na vipindi vya mihezo vya kituo cha runinga cha Skynews.

Baada ya kustaafu Martin alibaki kuwa mwanachama mtiifu kwa West Ham na mara chache amekuwa akikosekana uwanjani timu hio ikicheza.

Jambo moja ambalo halifai kulipuuza ni kwamba kuoata hat-trick katika michezo, hasa ya kimataifa kama Kombe la Dunia, sio kazi rahisi.

Hii inadhiirika wazi kwa kupatika hat-trick54 katika michezo zaidi ya 800 tokea mashindano haya makubwa kabisa ya kandanda kuanza mwaka 1930 kule Uruguay.

Kwa vyovyote vile hizi hat trick zitaendelea kuwa mada muhimu ya kujadiliwa na kuchambuliwa katika mchezo wa kandanda kwa miaka mingi ijayo.

Wachezaji hao wataendelea kujituma ili kuzipata, hasa katika mashindano ya kimataifa, ili majina yao kama ya Concalo Ramos wa  Ureno na kijana mwenye asili ya Bara la Afrika,  Kyllian Mbape wa

Ufaransa yalivyoingia katika rekodi za fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika kule Qatar hivi karibuni.