Huyu Mayele achana naye kabisa

WAKATI dunia ikiendelea kushangaa utupiaji wa mabao wa mshambuliaji mpya wa Manchester City, Erling Haaland aliyefunga mara 14 katika mechi 10 alizoichezea timu hiyo hadi sasa, hapa Bongo habari ya mjini ni mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele.

Msimu huu nyota huyo wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara ameanza kwa kasi akitupia jumla ya mabao 11 katika mechi saba alizocheza kwenye mashindano rasmi.

Mayele alifungua akaunti ya mabao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba akitupia mara mbili na kuifanya Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 huku bao pekee la Simba likifungwa na Pape Sakho.

Baada ya hapo alifunga bao moja kwenye mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Polisi Tanzania waliposhinda 2-1, akafunga tena moja katika mchezo uliofuata mbele ya Coastal Union walioshinda 2-0, kisha kuwachapa Zalan ya Sudan Kusini mabao matatu (hat-trick) mechi ya kwanza ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo walishinda 4-0 na kuifunga Mtibwa Sugar moja - ushindi wa mabao 3-0 kwenye ligi kabla ya kukutana na Zalan tena kwenye marudiano na kufunga hat-trick nyingine ushindi wa mabao 5-0. Mechi dhidi ya Azam waliyotoka sare ya 2-2 ndiyo pekee hajafunga.


REKODI YA NGASSA

Hat-trick mbili alizofunga Mayele mfululizo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya CAF hatua ya kwanza ya mtoano dhidi ya Zalan ilimfanya kufikia rekodi ya Mrisho Ngassa kufunga hat-trick mbili mfululizo katika mechi za CAF kwa mchezaji kutoka Ligi Kuu Bara.

Mayele alifunga hat-trick mechi ya kwanza wiki iliyopita Yanga ikiwa ugenini - kwa Mkapa- chama lake likishinda 4-0 na kurudia tena kufanya hivyo ikishinda 5-0 na kuifikia rekodi ya Ngassa aliyoiweka 2014 akiwa Yanga akiifunga Komorozine de Domoni ya Comoro katika ushindi wa 5-2 ugenini na kutupia tena mabao matatu katika ushindi wa 7-0 mechi ya marudiano nyumbani.

Vilevile hat-trick ya Mayele imeonekana kuwa ya muda mfupi zaidi kufungwa na mchezaji wa klabu ya Tanzania kwenye michuano ya CAF kwani alifanya hivyo ndani ya dakika sita tu akifunga dakika ya 60, 63 na 66.

Wachezaji wengine kutoka klabu za Tanzania waliowahi kufunga hat trick kwenye michuano ya CAF ni Boniface Ambani 2009 akiwa Yanga dhidi ya Etoile d’or ya Comoro katika ushindi wa mabao 8-1, Hamis Mcha pia akiwa Azam 2013 alipiga hat trick dhidi ya El Nasr ya Sudan Kusini ugenini katika ushindi wa mabao 5-0 na Kipre Tchetche wa Azam alifanya hivyo mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika 2016 dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini ushindi wa mabao 4-3.


MABAO 30 YANGA

Tangu amejiunga Yanga msimu uliopita, Mayele ameifungia mabao 30 hadi sasa katika mechi rasmi - kwa maana ya Ligi Kuu, michuano ya CAF, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya jamii.

Katika mabao hayo, matatu ni ya Ngao ya Jamii yote akiifunga Simba kwenye ushindi wa 1-0 msimu uliopita na msimu huu akifunga mawili katika kipigo cha mabao 2-1.

Mengine 19 ni ya Ligi Kuu kwa maana ya 16 ya msimu uliopita akishika nafasi ya pili nyuma ya kinara ufungaji bora Ligi Kuu Bara, George Mpole wa Geita Gold (17) na matatu ya msimu huu aliyofunga moja moja kwenye kila mechi dhidi ya Polisi, Coastal na Kagera.

Mawili ni ya ASFC aliyofunga msimu uliopita na kuipa taji hilo Yanga, na mengine sita ni yale ya Ligi ya Mabingwa akiichapa Zalan mabao sita - matatu kwenye kila mechi katika mbili walizocheza.


BADO SITA TU LIGI KUU

Mayele tangu ajiunge Yanga msimu uliopita ametembeza dozi kwa kuzifunga timu 12 kati ya 16 zilizoshiriki Ligi Kuu Bara msimu uliopita na msimu huu akiwa hajazifunga sita pekee.

Timu ambazo hazikuonja bao la Mayele kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita ni nne pekee ambazo ni Mbeya City, Tanzania Prisons, Ruvu Shooting na Simba licha ya kwamba ameifunga Simba mara tatu kwenye Ngao ya Jamii.

Hata hivyo ongezeko la Ihefu na Singida Big Stars zilizopanda Ligi Kuu Bara msimu huu limefanya idadi ya timu ambazo Mayele hajazifunga mechi ya ligi hadi sasa kuwa sita na huenda lolote likatokea kwani bado ana mechi mbili na kila timu kati ya hizo kwa msimu huu.


MWENYEWE ANASEMAJE?

Akizungumzia mwanzo wake bora msimu huu, Mayele anasema ana shauku ya kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

“Nashukuru nimeanza vizuri msimu kwenye ligi na CAF, ndoto yangu ni kufanya vizuri zaidi msimu huu na kuifanya Yanga ifikie malengo,” alisema nyota huyo wa zamani wa AS Vita ya DR Congo.

“Nawapongeza wachezaji wenzangu kwa ushirikiano wanaonipa kwani bila wao siwezi kuwa bora hivi, lakini pia nawashukuru mashabiki wa Yanga na nawaahidi tutafanya vizuri msimu huu na kuhakikisha tunafika hatua ya makundi ( Ligi ya Mabingwa) na kusonga mbele zaidi kimataifa sambamba na kutetea mataji ya msimu uliopita.”

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay anamuelezea Mayele kama mshambuliaji anayejitambua na yuko kwenye kiwango bora zaidi kwa sasa.

“Kwa sasa kila kocha Tanzania inatamani kuwa na mshambuliaji mwenye kariba ya Mayele, kwani anajua kukaa kwenye nafasi, analijua goli na ana uamuzi wa haraka anaofanya kufunga mara kwa mara. Nadhani ataendelea kufunga zaidi na zaidi,” anasema Mayay aliyekuwa kiungo hatari zaidi enzi zake.

Kocha wa Zalan, Mawein Deng aliyechapwa hat-trick mbili mfululizo na Mayele anasema kuwa jamaa ni mshambuliaji hatari ambaye ni ngumu kwa mabeki kumzuia.

“Mayele ana kasi, nguvu na akili kubwa ya kufunga. Unaweza kuwalaumu mabeki kushindwa kumzuia lakini kuna kiwango kikubwa cha ubora kinachofanya kuwa kazi ngumu kumkaba,” anasema Deng.