Hukumu ya mwisho Championship

Muktasari:
- Tayari Mtibwa Sugar inayoikaribisha Kiluvya United kwenye Uwanja wa Manungu Complex mjini Morogoro, imesharejea Ligi Kuu Bara msimu ujao, ikiungana na Mbeya City inayohitimisha kwa kucheza na maafande wa Green Warriors, Sokoine jijini Mbeya.
LIGI ya Championship kwa msimu wa 2024-2025, inafikia tamati leo kwa mechi nane kupigwa kwenye viwanja mbalimbali, huku macho na masikio yakielekezwa katika vita ya timu zinazoshuka moja kwa moja na zile zitakazocheza ‘Play-Off’ ya kubakia.
Tayari Mtibwa Sugar inayoikaribisha Kiluvya United kwenye Uwanja wa Manungu Complex mjini Morogoro, imesharejea Ligi Kuu Bara msimu ujao, ikiungana na Mbeya City inayohitimisha kwa kucheza na maafande wa Green Warriors, Sokoine jijini Mbeya.
Stand United iliyo nafasi ya tatu na pointi 60, itakuwa kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga kupambana na wapinzani wao Geita Gold, ambapo timu hizo zitamaliza ya tatu na ya nne na zitapambana katika vita ya ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu.
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mara, wenyeji Biashara United iliyoshuka daraja ikiwa na pointi 15, itakamilisha ratiba kwa kupambana na Polisi Tanzania ambayo mechi ya mwisho ilitoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Stand United.
TMA iliyolazimishwa suluhu mechi ya mwisho na Mbeya Kwanza, itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, kucheza na Bigman FC, yenye kumbukumbu pia ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, uwanjani hapo dhidi ya kikosi cha Mbuni.
Kwenye Uwanja wa Black Rhino Academy uliopo karatu jijini Arusha, Mbuni itaikaribisha Mbeya Kwanza, huku Songea United iliyoichapa Green Warriors mabao 2-1, itakuwa Uwanja wa Majimaji kucheza na Cosmopolitan iliyochapwa 5-0 na Mbeya City.
African Sports iliyo nafasi ya 15 na pointi 19, itakuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga kucheza na maafande wa Transit Camp, inayoshika nafasi ya 13 na pointi 21, ambapo endapo itapoteza itaaga rasmi Ligi ya Championship kwa msimu ujao.
Kikosi hicho kutoka jijini Tanga, kinahitaji kushinda ili kufikisha pointi 22 ambazo zitaiwezesha kumaliza nafasi ya 13 na kucheza ‘Play-Off’ ya kubakia, japo tofauti na ushindi itashuka moja kwa moja na kuungana na timu ya Biashara United.
Wakati zikisubiriwa timu hizo zitakazoshuka moja kwa moja msimu ujao, tayari timu ya Gunners ya mkoani Dodoma ambao ndio mabingwa wa First League, wamekata tiketi ya kucheza Championship msimu ujao, ikiungana na Hausung FC ya mkoani Njombe. Hausung ilikuwa ya kwanza kupanda kutoka kundi A ikikusanya pointi 25 baada ya kushinda mechi saba, sare minne na kupoteza mitatu, huku Gunners iliyokuwa kundi B ikimaliza na pointi 35, ikishinda 11, sare miwili na kupoteza mmoja.

VITA YA UFUNGAJI
Sehemu nyingine yenye mvuto ni ya vita ya ufungaji bora ambapo anayeongoza hadi sasa ni Andrew Simchimba wa Geita Gold mwenye 18, huku nyota wa TMA, Abdulaziz Shahame akifunga 17 na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh akiwa na 16.
Vita kwa nyota hao watatu ndio inayoonekana nzito zaidi ingawa wengine wanaofuatia ni Naku James wa Mbuni FC ya jijini Arusha aliyefunga mabao 11 sawa na Eliud Ambokile wa Mbeya City, huku Yusuph Mhilu wa Geita Gold akitupia nyavuni 10.
Licha ya kasi yao nzuri, ila rekodi inayosubiriwa kuvunjwa ni ya Edgar William ya msimu uliopita wa 2023-2024, wakati akiwa na kikosi cha KenGold alichokipandisha Ligi Kuu msimu huu, ambacho alikifungia mabao 21, ya Ligi ya Championship.
Nyota huyo anayeichezea Fountain Gate msimu huu, mabao hayo 21 aliyofunga, yanamfanya kushikilia rekodi ya mshambuliaji aliyefunga mengi zaidi katika Ligi ya Championship, kwani tangu msimu wa 2017-2018, hakuna aliyefunga idadi kama hiyo.
REKODI YA HAT-TRICK
Msimu huu zimefungwa ‘hat-trick’ tano, akianza mshambuliaji wa Mbeya City, Faraji Kilaza Mazoea, katika mechi baina ya timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania, walioshinda kwa mabao 4-0, Desemba 13, 2024.
Andrew Simchimba wa Geita Gold akafunga pia wakati timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Transit Camp, Februari 10, 2025, huku Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza akifunga katika ushindi wa 5-0, mbele ya Biashara United, Februari 23, 2025.
Nyota mwingine ni William Thobias wa Mbeya City aliyefunga pia wakati kikosi hicho kilichorejea Ligi Kuu Bara sambamba na Mtibwa Sugar, kilipoichapa Kiluvya United mabao 4-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Machi 17, 2025.
Emmanuel Manyanda wa Stand United akaifungia pia timu hiyo iliyo katika nafasi ya ‘Play-Off’ ya kusaka kurejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, wakati kikosi hicho cha ‘Chama la Wana’, kilipoichapa Green Warriors mabao 5-1, Aprili 20, 2025. Msimu uliopita, zilifungwa pia ‘Hat-Trick’ tano huku nyota wa zamani wa Biashara United, Mganda Boban Zirintusa akifunga mbili, wakati Kika Salum (Pan Africans), Abdulaziz Shahame (TMA FC) na Oscar Mwajanga aliyekuwa Mbeya Kwanza wakifunga moja.

KILUVYA KUITIBUA?
Ushindi wa mabao 2-1, ilioupata Mtibwa Sugar dhidi ya Mbuni Aprili 12, 2025, umeifanya timu hiyo kuweka rekodi ya kibabe kwa sababu tangu msimu umeanza, haijawahi kupoteza au kutoka sare mechi yoyote iliocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Mtibwa iliyoshuka daraja msimu uliopita kisha kurejea tena, imecheza mechi 14, kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro kati ya 29 na kushinda pia yote, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 36 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.
Kinachosubiriwa leo ni kuona kama Kiluvya United itakayokuwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro itaivunja rekodi hiyo au Mtibwa Sugar iliyoshinda mechi ya kwanza bao 1-0, Januari 12, 2025, itaendelea umwamba ikicheza nyumbani kwake.
Kocha wa Transit Camp, Ramadhan Ahmada Idd alisema wanatambua mechi itakuwa ni ngumu kutokana na mahitaji ya kila timu, ingawa amewataka wachezaji kucheza kwa tahadhari kubwa na kuepuka makosa yanayoweza kuwagharimu na kuwashusha daraja.
“Wenzetu wanaingia kwa lengo moja tu la kushinda ili waepuke kushuka daraja, sisi tunalijua hilo ndio maana tumejipanga kukabiliana nao kwa sababu sare inatubeba, ingawa tunataka kuepuka ‘Play-Off’ ya kubaki ikitegemea matokeo ya wengine.”