Hizi hapa maskani salama za kukuza vipaji vya soka kwa vijana
Muktasari:
- The Blues wamejijengea sifa kubwa kutokana na akademi yao iliyojaa wachezaji vijana wenye vipaji, huku wakipata mafanikio ya kiwango tofauti katika kuingia kikosi cha kwanza.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA wamethibitishwa rasmi kuwa timu bora zaidi ya Ligi Kuu England katika kulea vipaji vya vijana.
The Blues wamejijengea sifa kubwa kutokana na akademi yao iliyojaa wachezaji vijana wenye vipaji, huku wakipata mafanikio ya kiwango tofauti katika kuingia kikosi cha kwanza.
Utafiti umeonyesha sifa hiyo ni ya kweli, kulingana na viwango vya "training clubs" vya mtandao wa CIES Football Observatory.
Football Observatory inafafanua “training clubs” kama klabu ambazo wachezaji walikaa kwa angalau misimu mitatu kati ya umri wa miaka 15 na 21.
Kwa sasa, kuna wachezaji 25 waliopitia Chelsea ambao wanacheza katika Ligi Kuu tano bora barani Ulaya.
Kundi hilo limecheza jumla ya dakika 17,723 za mechi za ligi za ndani msimu wa 2025–26.
Kati ya wachezaji hao 25, wanne wamecheza kwa timu ya kwanza ya Chelsea msimu huu. Baadhi ya wachezaji hao ni Reece James, Trevoh Chalobah, Josh Acheampong na Tyrique George. Cha kushangaza zaidi, wote wanne wamekuwa na klabu hiyo tangu ngazi ya Under-8.
Levi Colwill pia angekuwa kwenye orodha hiyo na kufanya jumla iwe 26, lakini hajaichezea Chelsea kwenye Ligi Kuu England msimu huu kutokana na jeraha la misuli ya goti.
Barcelona wanaongoza orodha kwa ujumla wakiwa na wachezaji 40 waliotoka akademi ya La Masia, wakiwemo 10 waliopo kwenye kikosi cha kwanza kwa sasa.
Wapinzani wao Real Madrid (35) na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa PSG (31) wanakamilisha nafasi tatu za juu, huku kila moja ikiwa na nyota sita waliokuzwa nyumbani wanaocheza kwenye vikosi vya timu hiyo msimu huu.
Stade Rennais (29) na Ajax (27) pia wako juu ya Chelsea. Cha kushangaza, hata hivyo, hakuna hata mmoja kati ya wale 27 wa Ajax aliyeichezea timu ya kwanza msimu huu. Jorrel Hato, yumo miongoni mwa wale 27, akiwa Chelsea, pamoja na wachezaji waliotoka Barcelona, Marc Guiu na Marc Cucurella.
Real Sociedad iko nafasi ya saba na sehemu iliyobaki ya kumi bora inaundwa na vigogo wa Ligi Kuu England; Manchester United, Manchester City na Arsenal. Kila moja ya timu hizi tatu za England ina wachezaji 22 waliokuzwa kwenye akademi zao wanaocheza sasa katika ligi za juu barani Ulaya.
Man City ina wachezaji sita kwenye kikosi chao cha kwanza, akiwemo Phil Foden na Nico O’Reilly; Man United ina watano, kama Kobbie Mainoo; na Arsenal ina wanne wakiongozwa na Bukayo Saka, huku Cole Palmer akiwa alikulia Etihad kabla ya kuhamia Stamford Bridge.
Cha kuvutia, timu inayofuata ya England ni Liverpool, waliopo chini kabisa nafasi ya 48, wakiwa na wachezaji 10 pekee, mmoja pungufu kuliko klabu ya Senegal, AS Generation Foot, ambayo inajivunia nyota wa Ligi Kuu England kama Pape Matar Sarr na Ismaila Sarr, pamoja na mshambuliaji wa Al-Nassr, Sadio Mané miongoni mwa wahitimu wao.
Tottenham hawapo kabisa kwenye orodha. Lyon, Toulouse na Le Havre, pamoja na Athletic Bilbao, Valencia, Villarreal na Espanyol, zinahakikisha kuwa kuna timu saba za Ufaransa na Hispania kati ya nafasi ya 11 hadi 17.
Juventus ina wachezaji 17 waliokuzwa wanaocheza kwenye ligi tano bora Ulaya, mmoja zaidi ya Inter Milan, Bayern Munich, Borussia Dortmund na Benfica.
River Plate ndio klabu iliyofanikiwa zaidi nje ya Ulaya, ikiwa na vipaji 12 vya vijana vilivyocheza zaidi ya dakika 10,000 kwa jumla katika Ligi Kuu England, La Liga, Ligue 1, Serie A na Bundesliga.
Real Sociedad (15) na Athletic Bilbao (12) zina idadi kubwa zaidi ya wachezaji waliokuzwa bado wakicheza kwa klabu zao, huku klabu zote mbili za Basque zikiwa na sera kali za kuchagua vipaji vya eneo lao.