Hivi ndivyo Kim anavyoipika Taifa Stars ijayo

PENGINE ni kutokana na ubobezi wake kwenye uvumbuzi, kulea na kuendeleza vipaji vya vijana wadogo ndio maana imekuwa rahisi kwake kutoa nafasi kwa makinda kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Huyu ni Mdernmark, Kim Poulsen ambaye anahudumu Tanzania kwa mara ya pili, ya kwanza alikuwa amejikita zaidi kwenye soka la vijana, ndiye aliyekuwa nyuma ya mpango wa kuzalisha vijana waliwatoa kimasomaso Watanzania kwa kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za mataifa ya Afrika chini ya miaka 17 kule Gabon mwaka 2017.
Poulsen kama walivyo makocha wengine wenye kutambua msingi wa mpira ni vijana waliondaliwa vizuri, hata mara baada ya kurejea kwa mara nyingine tena kuhudumu kwenye soka la Tanzania huku safari hii akibebeshwa mikoba ya kukinoa kikosi cha Taifa Stars ameendelea na falsafa zake za miaka saba iliyopita.
Tangu 2021 Poulsen aliporejea nchini ameonekana akiwaamini vijana kwenye kikosi chake cha Taifa Stars kwa vipindi tofauti amekuwa nakiwaita kwenye kikosi chake kwa ajili ya kupata uzoefu mapema kabla ya kuanza kutumika, ilikuwa hivyo kwa Ramadhan Kabwili, Kelvin John, Nickson Kibabage na wengine kibao.
Kadri siku zilivyokuwa zinasogea ndivyo wigo wa vijana ukaendelea kuongezeka kwenye kikosi hicho cha Poulsen na sasa wameanza kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mfano mzuri ni kwa kiungo, Novatus Dismas ambaye anaichezea kwa mkopo Beitar Tel Aviv Bat Yam akitokea Maccabi Tel Aviv zote za Israel.
Akiwemo Novatus hawa hapa makinda wengine sita wenye umri chini ya miaka 20 ambao wamepata nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kipindi hiki cha wiki ya kimataifa ambacho Tanzania imejipa ubavu dhidi ya Afrika ya Kati huku mchezo uliosalia ukiwa dhidi ya Sudan ambao utachezwa kesho, Jumanne.
HAJI MNOGA
Hii ni mara yake ya kwanza kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars na alipata nafasi kwenye mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Afrika ya Kati.
Beki huyo wa kulia mwenye miaka 19, alicheza kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza mara baada ya mchezo huo, tulipata nafasi ya kuzungumza naye, “Kuichezea nchi ambayo naipenda ni jambo kubwa sana kwangu, mambo mengine nadhani yatakaa sawa taratibu,”
“Kwangu ni suala la muda tu kwa sababu naamini kwenye utaratibu, nimefurahishwa sana na ushirikiano kutoka kwa kila mchezaji wenzangu,” anasema.
Katika mchezo huo wa kirafiki ambao Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Afrika ya Kati, Haji hakuonekana kufunguka sana kwa maana yakushambulia kama ambavyo imezoeleka akicheza huko England kwenye klabu ya Weymouth anayoichezea kwa mkopo akitokea Portsmouth.
NOVATUS DISMAS
Tangu pale ameanza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, amekuwa akifanya vizuri kasi cha kutumika mara kwa mara kwenye michezo mbalimbali ya ushindani, alipachika bao la kwanza kwa Taifa Stars kwenye mchezo dhidi ya Afrika Kati.
Umri wake,19, na kiwango ambacho amekuwa akikionyesha ni vitu viwili tofauti, amekuwa akitumika kama kiungo mkabaji, amekuwa akitekeleza vizuri majukumu yake huku muda mwingine akisaidia kusukuma mashambulizi.
Novatus alianza safari yake ya kucheza soka la kulipwa Ulaya, 2021 baada ya kufanya vizuri Israel ambako alienda kwa mualiko maalum kwenye kabu ya Maccabi Tel Aviv kufuatia kufanya makubwa Ligi Kuu Bara akiwa na Biashara United ambayo alikuwa kichezea kwa mkopo wa msimu mzima akitokea Azam FC.
Kitendo cha kufanya vizuri kwenye mazoezi ya timu hiyo ambayo ilimualika kiliifanya miamba hiyo ya soka la Israel kukaa chini na Azam na kumalizana nao hivyo akawa mchezaji rasmi wa Maccabi Tel Aviv, haikumchukua muda kupandishwa kikosi cha kwanza maana alianzia kwenye kikosi cha vijana.
BEN STARKIE
Kwa majina yake kamili anaitwa, Ben Anthony Swakali (alizaliwa Julai 23, 2002), amekuwa akifahamika kama Ben Starkie, ni mchezaji wa kulipwa wa Kitanzania ambaye amekuwa akicheza kama kiungo na muda mwingine kama mshambuliaji.
Kinda huyo amezaliwa na kukulia England, anaichezea Spalding United. Ameanza kuitumikia Tanzania kuanzia ngazi ya chini, kwenye mchezo uliopita dhidi ya Afrika ya Kati alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao walipewa nafasi kwa mara ya kwanza.
Mara baada ya mchezo huo, aliweka wazi hisia zake kwa kusema, “Wakati muhimu sana katika maisha yangu ya soka kucheza kwa mara ya kwanza katika timu ya taifa ya wakubwa kwa Tanzania. Huu ni wakati wa kujivunia sana kwangu na familia yangu.”
KELVIN JOHN
Wapo ambao wamekuwa wakimwona Kelvin John ni kama Mbwana Samatta wa kesho, kutokana na namna ambavyo amekuwa akipita njia za nahodha huyo wa Taifa Stars angali akiwa na umri mdogo kwa sasa kinda huyo wa Kitanzania anaichezea KRC Genk ya Ubelgiji.
Amekuwa akifanya vizuri kwenye kikosi cha vijana hadi benchi la ufundi la wakubwa kuamua kumpandisha huku wakionekana kuwa na hesabu naye kwa msimu ujao.
Kelvin amekuwa na njaa ya mafanikio na ndoto yake kubwa ni kucheza soka la kulipwa kwenye ngazi kubwa zaidi Ulaya kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Samatta ambaye ameweka rekodi kibao ikiwemo kucheza na kufunga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa Ligi na hata kwenye Ligi ya England na kwenye fainali ya Carabao, Wembley.
TEPS EVANCE
Kuna kipindi kinda huyu wa Azam alienda Ufaransa kufanya majaribio kwenye Klabu ya Nantes inayoshiriki Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’, unaweza kusema kwamba haukuwa wakati wake kwani licha ya kufanya vizuri dili hilo liliyeyuka kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
Tepsi alipata nafasi hiyo baada ya kufuzu katika kliniki iliyofanywa Oktoba 29, 2019 kwenye Uwanja wa Uhuru chini ya usimamizi wa kampuni ya Cambiasso Sport Management wakishirikiana na Rainbow Sport.
Kwa sasa kinda huyo amekuwa gumzo Ligi Kuu Bara akiwa na Azam FC kiasi cha Kim kuona kile kilichopo ndani yake hadi kumwita kwenye kikosi cha Taifa Stars, hakucheza kwenye mchezo uliopita pengine ujao dhidi ya Sudan anaweza kupewa nafasi.
ABDULRAZAK HAMZA
Ana miaka 18, lakini amekuwa akipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Namungo, Abdulrazak Hamza anaonekana anaweza kuwa mmoja wa mabeki visiki kwa miaka ya baadae, kuitwa kwake Taifa Stars ni kama kunamfungulia milango ya kheri.
Kwake Namungo ni kama njia ambayo amepanga kuitumia ili kufikia malengo yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kama ilivyo kwa vijana wenzake.
ABOUTWALEEB MSHERY
Amekuwa akitajwa na wadau wa soka la Tanzania tangu akiwa Mtibwa Sugar, ubora wake ndio ulioifanya Yanga kupigana vikumbo kuwania saini yake kufuatia kuondoka kwa kipa namba moja wa timu hiyo, Djigui Diarra ambaye alienda kucheza fainali za mataifa ya Afrika (Afcon 2021) kule Cameroon wiki chache zilizopita. Tangu ajiunga na Wananchi aliendelea kuonyesha makali yake akiwa langoni kiasi cha kumkuna Poulsen na kuona kuwa kipa huyo anaweza kuwa msada kwa taifa miaka michache ijayo licha ya uwepo wa Metacha Mnata na Aishi Manula.