HISIA ZANGU: Tujikumbushe Ajibu ni mfanyakazi sio mwanachama

NIMECHUNGUZA nimegundua kwamba watu wa Yanga wana hasira kweli kweli na mchezaji anayeitwa Ibrahim Ajibu. Sijui kwanini? Majuzi ilichomekewa habari za uhamisho wake kwenda Yanga akitokea Simba. kuna watu wa Yanga wamechukia.

Kwanini wamechukia? Wanadai kwamba walijaribu kupambana Ajibu abakie klabuni kwao miaka miwili iliyopita lakini ilishindikana. Sina uhakika kama walifikia dau la tajiri wa Simba, Mohamed Dewji ambaye inadaiwa alitoa kiasi cha Shilingi 80 milioni kumnasa Ajibu.

Inadaiwa kwamba kule Simba nako wakati Ajibu anarudi watu walikuwa na hasira naye. Walikuwa wamechukia kwanini alikuwa ameenda Yanga na wao alikuwa amewatosa licha ya kwamba walimlea kwa muda mrefu tangu akiwa kinda.

Hawakumbuki kwamba maslahi ya kwanza makubwa ya pesa Ajibu aliyapata kwa uhamisho wake wa kutoka Simba kwenda Yanga. Kabla ya hapo alikuwa na mkataba wa kitoto wa miaka minne akiwa na Simba ambao alipewa akiwa kama mchezaji wa timu ya vijana.

Naambiwa kwamba Dewji mwenyewe ndiye ambaye alimkingia kifua na mwishowe akafanikiwa kumnasa. Watu ambao hawakumtaka Ajibu wameendelea kununa mpaka sasa. Kitu kizuri ni kwamba Ajibu mwenyewe hajafanya maajabu sana na eneo lake wageni wamekuwa wakitamba.

Hasira zile zile ambazo kuna watu wa Simba walikuwa nazo dhidi ya Ajibu ni hasira zile zile ambazo kuna watu wa Yanga wanazo dhidi yake. nimewachunguza watu wa Yanga huwa hawaongei sana sababu za kisoka.

Sababu kubwa ni ile kwamba Ajibu aliwaacha wakati wakimtegemea. Sikumbuki kama alitoa maneno machafu kuhusu Yanga lakini ninachojua ni kwamba dau la Simba lilikuwa kubwa kuliko la Yanga. Hili ndio jambo la msingi.

Wenye hasira zaidi wanamkumbusha Ajibu jinsi alivyokuwa staa lakini sasa amekuwa hana kitu na hatambi mbele ya kina Clatous Chama na wengineo. Sioni kama hasira hizi zina tija. Kitu cha msingi ambacho ninawakumbusha watu wa Yanga na hata wale wa Simba ambao walimchukia Ajibu wakati ule kwamba Ajibu ni mfanyakazi sio mwanachama.

Mara nyingi huwa tunawaweka wachezaji hawa katika nafsi zetu. Tunataka wazitumikie timu hizi kama wanachama au mashabiki. Ni kitu ambacho kimewapoteza mastaa wengi wa zamani ambao waliwahi kuhofia kuondoka katika klabu hizi kwa sababu walikuwa wanabembelezwa kukumbuka mapenzi na timu hizi kuliko maslahi.

Endapo Ajibu hatarudi Yanga basi iwe kwa sababu za kisoka zaidi lakini sio kukumbushana kwamba aliikimbia Yanga na kwenda kusaini Simba. Aliikimbia kwa sababu za maslahi zaidi. Na hata kama alisema kwamba Yanga kuna njaa alikuwa sahihi.

Ule ulikuwa wakati wa giza kabisa wakati nahodha wa klabu ambaye alikuwa Ajibu mwenyewe akiongoza michango ya pesa kupitia namba fulani za simu kwa ajili ya kuiendesha klabu. Kwa ukubwa wa klabu kama Yanga ilikuwa aibu.

Shukrani kwa ujio wa GSM kadhia ile ilitoweka lakini yeyote ambaye aliondoka Yanga kwa sababu za kimaslahi alikuwa sahihi. Hawa wachezaji na watu wa benchi la ufundi ni binadamu wanaoka maslahi kama sisi. Kuwachukia kwa sababu walikimbia shida sidhani kama ni kitu sahihi.

Ni kweli Yanga haikuwa na njaa? Sio kweli. Ilikuwa na njaa. Kama mchezaji ulikuwa huru na kupata maslahi makubwa zaidi kwingine usingeondoka? Ungeondoka. Angekuwa mdogo wako ungemshauri nini? Aondoke.

Tukiachana na suala hilo turudi katika ukweli wa Yanga kumuhitaji Ajibu ndani ya uwanja. Ambacho hauwezi kumshikia dhamana Ajibu ni ukweli kwamba anaweza kukuangusha muda wowote ule. Walio karibu naye wanadai kwamba hapendi kujituma.

Bahati mbaya kwake ni kwamba pale Simba amewakuta wachezaji wa maana alioshindwa kuwang’oa katika nafasi zao. Amewakuta kina Clatous Chama, Rally Bwalya na Luis Miquissone ambao wanazitendea haki sana nafasi zao kikosini.

Linapokuja suala la kipaji nadhani Ajibu ana kipaji kizuri kama hao wengine. Tatizo la msingi wote tunalifahamu na ndilo ambalo limesababisha hao wengine wawe mbele yake katika vikosi vya makocha mbalimbali.

Pale Yanga Ajibu ana nafasi. Yanga wana tatizo kubwa la kimsingi katika kutengeneza nafasi ndani ya uwanja. Ajibu wakati anaondoka alikuwa na rekodi ya kucheza mechi 59 akifunga mabao 14 huku akipika mabao 22. Sidhani kama kuna wachezaji wengi wa Yanga wa sasa wanaoweza kuipiku rekodi yake.

Yanga wanaweza wasimuhitaji Ajibu kwa sasa lakini wanachopaswa kufanya ni kuleta wachezaji wa maana zaidi yake, wachezaji ambao watakuwa na viwango sawa na kina Chama na Miquissone ambao wanamuweka Ajibu benchi Simba.

Vinginevyo kama hawataweza kuleta wachezaji hao ni bora kumchukua Ajibu ambaye licha ya kuwekwa benchi Simba lakini bado anaweza kuwa na mchango mkubwa kuliko wachezaji wengi wa sasa wa Yanga. Namba zake hazidanganyi.

Na wala hakuna uongo tukisema kwamba Ajibu alicheza soka la uhakika zaidi akiwa na Yanga kuliko Simba na kuliko wakati mwingine wowote wa maisha yake ya soka. Kama akichukuliwa na kuifanyia kazi Yanga kama vile alivyofanya kabla ya kuondoka basi mchango wake utakuwa mkubwa kuliko wachezaji wengi wa sasa.

Tatizo nadhani mashabiki hawana imani naye. Lakini pia kinachosemwa kingine ni kwamba amekuwa akikaa benchi Simba. Sidhani kama hii ni hoja ya msingi kwa sababu Patrick Vieira alikuwa anakaa benchi AC Milan lakini Arsene Wenger akaagiza apelekwe Highbury ambako aliibuka kuwa mmoja kati ya viungo bora duniani.

Kitu pekee cha kuwaza kwa Ajibu mwenyewe ni kama Simba ikimuacha halafu Yanga na Azam zikamchunia nadhani kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi ataonja machungu ya kucheza soka nchini kwa sababu timu nyingine zote hazitamuhakikishia maslahi mazuri ambayo ameyazoea miaka ya karibuni.