HISIA ZANGU: Mgunda anadumisha falsafa za 'soka letu kivyetuvyetu'

SIMBA imepata kocha mpya kutoka Brazil anaitwa Roberto Oliviere Robertinho na moja kwa moja, Juma Mgunda anakwenda kuwa kocha msaidizi pamoja na Suleiman Matola. Inaendeleza aina fulani ya utamaduni wa soka letu. Wakati mwingine huwa inaitwa ‘soka letu kivyetuvyetu’.

Kuna tamaduni mbili za kushangaza katika soka letu. Huwa zinanichekesha. Kuna hii hapa ya kocha kufikia hadhi ya kuwa kocha mkuu huku akiwa na vyeti kamili lakini kuna wakati anashuka na kuwa msaidizi. Kwanini? Sijui. Na kocha mwenyewe anakuwa na hadhi kubwa.

Imewahi kutokea kwa Charles Boniface Mkwassa ‘Master’. Imewahi kutokea kwa Jamhuri Kihwelo ‘Julio’. Imewahi kutokea kwa Juma Mwambusi.

Kwa sasa inatokea kwa Mgunda. Alikuwa kocha mkuu, Coastal Union, halafu akawa kocha mkuu Simba, halafu ghafla amekuwa kocha msaidizi. Inashangaza kidogo kwa sababu kazi ya kocha msaidizi ni kusapoti mawazo ya kocha mkuu. Kumsaidia kuimarisha mawazo. Vipi kama falsafa zao zinapishana?

Robertinho anaweza kuwa muumini wa falsafa ya 3-5-2 wakati Mgunda anaweza kuwa muumini wa 4-4-2. Wataishije pamoja? Ndio maana wenzetu huwa wanatembea na makocha wao wasaidizi kila wanapokwenda. Sijashangaa kuona huyu kocha ameleta msaidizi wake. Nadhani atakuwa mtu ambaye anaelewa falsafa zake zaidi.

Pale Yanga naambiwa huwa inatokea mikwaruzano kati Cedric Kaze na kocha mkuu, Nasreddine Nabi. Kuna wakati wanakuwa na falsafa tofauti kwa sababu wote ni wasomi wazuri wanaoamini mambo tofauti. Kaze naye kama Mgunda. Kuna wakati alikuwa kocha mkuu Yanga sasa hivi amekuwa msaidizi.

Naambiwa kwamba Kaze huwa hafurahishwi na suala la Nabi kumtumia mlinzi anayetumia mguu wa kulia kucheza upande wa kushoto. Pindi Djuma Shabani na Shomari Kibwana wakiwa fiti wote basi Nabi humpeleka Kibwana upande wa kushoto. Inakuwa ngumu kwake kupiga krosi za upande wa kushoto.

Hata hivyo, hakuna ambacho Kaze anaweza kufanya. Wakati mwingine sio yeye tu. Makocha waliowahi kufikia hadhi ya kuwa makocha wakuu halafu ukawapa usaidizi, pindi makocha wakuu wanapokosekana huwa wanamwaga falsafa zao bila ya kujali kocha mkuu anataka nini. Ni rahisi kuingia katika mgongano.

Ukiongea na makocha wasaidizi unakuta kuna mambo mengi hawasaidiki katika falsafa za makocha wakuu lakini hawana la kufanya. Zaidi ni kwamba licha ya kwamba walikuwa makocha wakuu hapo awali lakini wanajikuta wamekutanishwa tu katika benchi la ufundi na uongozi. Kaze alijuana wapi na Nabi hapo kabla? Lakini Mgunda alijuana wapi na Robertinho hapo awali?

Kwanini tuna utamaduni huu? Nenda kamuulize Juma Mgunda. Atakupa majibu sahihi kwanini amevumilia kushushwa chini na ameendelea kuwa mtiifu katika nafasi yake ya ukocha usaidizi. Ukweli ni kwamba kuna klabu chache zenye uchumi imara katika soka letu. Kwa Mgunda ni afadhali aendelee kuwa kocha msaidizi Simba kuliko kuwa kocha mkuu Coastal Union au Polisi Tanzania.

Kaze alifukuzwa halafu akarudishwa tena klabuni kama msaidizi. Unadhani kwanini hakujisikia aibu? Angeenda wapi zaidi? Ni bora kuwa kocha msaidizi wa Yanga kuliko kuwa kocha mkuu wa Mtibwa Sugar. Ukiwa kocha msaidizi Yanga na Simba una uhakika wa maisha mazuri kuliko kuwa kocha mkuu Prisons.

Ukiwa kocha msaidizi Simba au Yanga una uhakika wa mshahara mzuri, posho nzuri, gari zuri, kambi nzuri lakini pia safari za mara kwa mara za mechi za kimataifa au kambi za ughaibuni. Tatizo kubwa la soka letu ni tofauti kubwa ya kiuchumi kati ya walionacho dhidi ya wasionacho. Wenzetu wameliziba pengo hilo.

Kwa mfano, kocha kama Kaze anaweza kufukuzwa Manchester United lakini akaangukia zake Leicester City kwa sababu mazingira mengi ni yale yale tu ingawa Manchester United ni wakubwa zaidi. Huku ukiondoka Simba ukaenda Kagera Sugar tofauti ni kubwa.

Angalia jinsi wachezaji wa timu nyingine wanavyosota katika mabasi halafu angalia namna ambavyo Simba, Yanga na Azam wanazurura kwa ndege kila uchao. Ni ngumu kwa kocha kufikiria mara mbili kujiunga na timu kubwa kama msaidizi. Hata hivyo, tunafahamu ugumu wa David Moyes kwenda kuwa kocha msaidizi wa Jose Mourinho. Makocha wana majivuno (egoism). Ukiona kocha anakubali ujue hali ya uchumi kwa wengineo sio nzuri.

Tatizo hili halipo kwa makocha tu. Simba na Yanga inamvuta yeyote yule wanayemuhitaji. Sidhani kama Ally Kamwe angeacha kazi ya uchambuzi katika kituo cha Azam TV na kwenda kuwa msemaji wa Coastal Union. Sidhani kama Ahmed Ally angeacha kazi ya utangazaji Azam na kwenda kuwa ofisa habari wa Dodoma City.

Lakini hata wachezaji ipo hivyo hivyo. Nawajua wachezaji ambao huwa wanasikia raha kusugua benchi Simba na Yanga badala ya kwenda timu za mikoani kuonyesha uwezo wao. Wakiwa Simba na Yanga wanapata nafasi ya kupiga picha wakati wanaogelea katika hoteli za kifahari. Ni tofauti kwa timu zetu za mikoani.

Hauwezi kumshangaa sana Mgunda lakini ukweli ni kwamba kama angepata timu nyingine ya kawaida angeweza kwenda kuonyesha uwezo wake vema kuliko kuwa msaidizi wa Robertinho. Alishafanya hivyo na Coastal Union lakini pia alishaonyesha uwezo wake kabla ya kutua kwa Robertinho. Hata hivyo, ni ngumu kwake kuondoka Simba. Labda afukuzwe.

Swali kubwa ambalo tunapaswa kulifanyia kazi ni namna gani tunaweza kuziinua kiuchumi klabu nyingine. Haziwezi kuwafikia Simba, Yanga na Azam lakini inabidi zisogee kidogo ili tuwe na upinzani mzuri katika Ligi yetu. Kuna mambo mengi yanayowafanya watu wajibane pale kwa wakubwa lakini kitu kikubwa zaidi ni uchumi mdogo wa wengineo.