HISIA ZANGU: Kwanini sasa tuwaondoe langoni kina Djigui Diarra? Hoja dhaifu

Muktasari:

  • Walengwa hapa walikuwa wakubwa wetu wa Kariakoo na rafiki yao Azam. walengwa hapa ni kina Djigui Diarra ambao wamekuwa wakiwakalisha benchi makipa wetu wazawa ambao bado wameendelea kuitwa katika timu ya taifa. Mfano ni Abuutwalib Mshery.

HOJA nyingine dhaifu iliibuka hivi karibuni katika mitandao. Kwamba? Tuwaondoe makipa wa kigeni katika ligi yetu kwa ajili ya kuinua uwezo wa makipa wazawa. Hoja mfu.

Walengwa hapa walikuwa wakubwa wetu wa Kariakoo na rafiki yao Azam. walengwa hapa ni kina Djigui Diarra ambao wamekuwa wakiwakalisha benchi makipa wetu wazawa ambao bado wameendelea kuitwa katika timu ya taifa. Mfano ni Abuutwalib Mshery.

Lakini pia ameibuka kipa Mwarabu Ayoub Lakred ambaye katika siku za hivi karibuni amelifanya lango la Simba kuwa salama. Kuna hoja ilisambaa siku za hivi karibuni kwamba makipa hawa wanaidhoofisha Taifa Stars kwa sababu makipa wazawa wanakosa nafasi ya kucheza katika timu zetu, hasa timu kubwa ambazo zinashiriki mara kwa mara katika michuano ya kimataifa.

Najua ambako hoja hii imeokotwa. Imeokotwa kutoka katika mataifa ya Afrika Kaskazini ambako wamekataza kuwa na makipa wa kigeni. Nchi kama Misri, Morocco na Tunisia zimekataza kuwa na makipa wa kigeni. Tusichojua ni kwamba wamefanya hivi kwa sababu wanajua wana makipa wazuri. Ni kama hawa wengine kina Ayoub ambao wameangukia kwetu.

Sisi tuna makipa wazuri wa kutupa kiburi cha kufanya hivi? Hatuna. Mtu kama Diarra anatuonyesha wazi kwamba hatuna makipa wa hivi. Ayoub pia amekuwa mpinzani wa kwanza wa ukweli wa Aishi Manula baada ya Aishi kuishi kwa amani kwa muda mrefu akiwa na wasaidizi kutoka Tanzania.

Kifupi ni kwamba hatuna makipa wazawa ambao wanaweza kukufanya ujisikie salama wanaposimama langoni. Hakuna makipa wanaoweza kutupa kiburi hiki. Ukiachana na Yanga, Simba na Azam kuna makipa wazawa wapo kwingineko, je wanafanya maajabu gani? kwanini mpaka inafikia makocha wa timu ya taifa wanawachagua makipa wa akiba wa Simba na Yanga? Kwanini wasiende kwa makipa wazawa wanaocheza kwingineko?

Lakini kitu cha msingi zaidi ni kujikumbusha kwamba hizi timu kubwa ni taasisi binafsi. Zinaangalia kwanza maslahi mapana ya klabu zao kabla ya kuangalia maslahi ya taifa. Huu ni ukweli ambao hata sisi wenyewe tunaishi nao katika ofisi zetu. Tunaanza kuangalia kwanza maslahi mapana ya familia zetu kabla ya kuangalia mambo mengine.

Mpaka wamefikia hatua ya kuangalia makipa wa kigeni ni kwa sababu wanataka kilicho bora zaidi. Wanaangalia maslahi yao mapana kabla ya kuangalia mambo ya utaifa. Ni tabia ambayo wameiga kutoka katika timu mbalimbali.

Kipa namba moja wa Arsenal anatoka Hispania. Kipa namba moja wa Manchester United anatoka Cameroon. Kipa namba moja wa Real Madrid anatoka Ubelgiji. Kipa namba moja wa Manchester City anatoka Brazil. Kipa namba moja wa Barcelona anatoka Ujerumani.

Sio kwamba nchi zao hazina makipa. Hapana. Wanaangalia kilicho bora. Katika dunia ya kisasa ya ushindani watu wanaangalia kilicho bora. Watu wanaangalia zaidi ushindani. Kitu muhimu ni kwa makipa wetu kuingia katika ushindani kama ambavyo Aishi alifanya.

Lakini kwanini na sisi tusiwe kwao? Kungekuwa na ubaya gani kwa Mshery kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini? Amezuiwa? Hapana. Kwanini kama tuna makipa bora na wao wasiende kucheza soka la kulipwa kwingineko kama ambavyo kina Novatus Dismas wamefanya?

Tusiwalinde wachezaji wetu kwa kuua ubora wa klabu zetu. Tunajua namna ambavyo mafanikio bora ya klabu zetu yametokana na ujio wa wageni. Hauwezi kumuweka langoni kipa ambaye haumuamini kwa sababu tu unataka kutetea nafasi za wazawa. Waingie katika ushindani. Ni timu gani Fei Toto hawezi kucheza mpaka tunyofoe mgeni katika nafasi yake? hakuna. Kwahiyo kumbe tunamuhitaji Fei Toto wa langoni.

Unapomuondoa Diarra katika lango la Yanga unajaribu kujiuliza, ni kipa gani mzawa ambaye ana miguu bora atasimama katika lango la Yanga? Kipa gani mzawa ambaye ana miguu bora atasimama katika lango la Simba? Mbona katika hizo timu nyingine hatuwaoni wakifanya hivyo? Tunataka wakaanze kujifunzia katika lango lenye presha kama la Yanga au Simba?

Hoja hii ni kama ile ya kupunguza wageni. Ambacho hatujui ni ukweli kwamba tangu timu zetu ziwe na wageni bora ndio ambapo kwa namna moja au nyingine timu yetu ya taifa imeimarika zaidi? Wageni wakifanya vizuri timu inafika mbali na kina Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wanajikuta wamecheza mechi nyingi za kimataifa. Wanapokwenda Taifa Stars hawashangai tena.

Kina Bakari Nondo Mwamunyeto, Dickson Job na Ibrahim Bacca wamekwenda hadi katika mechi mbili za fainali za Shirikisho kutokana na ubora wa kina Fiston Mayele. uzoefu wao katika michuano hiyo ndio uliwafanya wasitetereke katika mechi za Afcon.

Wachezaji ni bidhaa. Tuwaingize katika ushindani. Wajifunze na wajue kwamba soka ni maisha yao. Dunia ya leo hatulindi bidhaa ovyo. Inabidi bidhaa ipambane sokoni kutokana na ubora wake. Ni suala la mteja kuamua kununua kiberiti cha Tanzania au kiberiti cha Kenya.

Hapo hapo najaribu kuwakumbusha waleta hoja kwamba miaka mingi iliyopita makipa wengi wa kigeni wasingeweza kuingia katika soko letu kwa sababu tulikuwa na makipa hodari. Kina Mohamed Mwameja, Idd Pazi, Joseph Fungo, Madata Lubigisa, Ally Bushiri na wengineo wengi. Hatukuhitaji tuwe na kina Diarra.

Tuliinua macho na kutazama kwingine kwa sababu ya kuondoka kwa ubora wa makipa wa Tanzania. Kwanini tuhatarishe malango yetu kwa sababu ya uzawa? Acha ubora wa mchezaji uamue. Mbona nafasi za ndani tuna wachezaji bora ambao hauwezi kudiriki kuleta wachezaji wa kigeni katika nafasi zao?