HISIA ZANGU: Bado simshikii dhamana Kibu, tusubiri na tuone

Muktasari:

MSHAMBULIAJI mpya wa Tanzania anayezungumzwa kwa sasa ni Kibu Dennis wa Mbeya City na timu ya taifa. Naambiwa kwamba wakubwa Simba na Yanga wanakimbizana kusaka saini yake. Sijui nani anaweza kuipata saini yake.

MSHAMBULIAJI mpya wa Tanzania anayezungumzwa kwa sasa ni Kibu Dennis wa Mbeya City na timu ya taifa. Naambiwa kwamba wakubwa Simba na Yanga wanakimbizana kusaka saini yake. Sijui nani anaweza kuipata saini yake.

Ananikumbusha washambuliaji wetu wazawa wa siku za karibuni. Sitaki kumuwekea dhamana. Ingekuwa katika kucheza Kamari ningeweka nafasi ya nusu kwa nusu. Sijui wachezaji wetu wamepatwa na nini katika siku za karibuni.

Kioo cha Ligi yetu ni timu tatu. Simba, Yanga na Azam. Hawa ndio wakubwa wetu na hata msimu ujao wana asilimia kubwa za kutuwakilisha katika michuano ya kimataifa. Wachezaji wazawa wanaotamba katika baadhi ya nafasi katika timu hizo hawatoki eneo la mbele.

John Bocco anabakia kuwa mwakilishi pekee katika eneo la mbele. Halafu pale Azam kuna Idd Nado amekuwa akifanya vizuri. Nani mwingine? Sioni. Kama utamfanya Nado kuwa winga basi mshambuliaji wa kati atabakia kuwa John Bocco pekee.

Kuna pengo kubwa kati ya Bocco na wengineo. Kwa mfano, Yanga walimsajili Ditram Nchimbi baada ya kung’ara akiwa na kikosi cha Polisi Tanzania kisha Taifa Stars. Ditram ndiye aliyetupeleka Cameroon katika michuano ya Chan baada ya kung’ara katika pambano dhidi ya Sudan ugenini.

Unamuonaje Ditram kwa sasa? Ni aibu kusema lakini alikaa mwaka mzima bila ya kufunga bao lolote. Mshambuliaji unawezaje kukaa kipindi kirefu hivi. Wakati Bocco akiwa anabanana na wageni mahiri akina Meddie Kagere na Chris Mugalu, Nchimbi habanwi na yeyote mahiri.

Washambuliaji kama Fiston Abdulrazak na Michael Sarpong wameshindwa kuonyesha makali yao Jangwani na ilikuwa nafasi nzuri kwa Ditram kuonyesha makali yake lakini bahati mbaya ameshindwa kufanya chochote.

Mshambuliaji anayeitwa Waziri Junior alikuwa ana kila sababu ya kusajiliwa Yanga baada ya kufunga mabao 14 akiwa na klabu ya Mbao ya Mwanza ambayo ilishuka daraja. Lakini mpaka sasa Waziri ameifungia Yanga mabao mawili tu.

Hawa wote Waziri na Ditram wamepewa nafasi na wameshindwa kuonyesha makali yao. Wakati mwingine wamekuwa wakikosa mabao ya wazi mpaka yanakuacha mdomo wazi. Hauwezi kuwalaumu Yanga kwa kuwanunua. Waliona dalili za makali yao mahala fulani na wakawachukua.

Kwa mfano, unawalaumu nini Yanga kwa kumchukua mshambuliaji aliyeifungia timu yake mabao 14? Timu ambayo ilikuwa katika maeneo ya chini na unatazamia kwamba endapo akichezea timu yenye wachezaji wengi mahiri zaidi huenda akawa hatari zaidi.

Imeshindikana kwa Waziri kurudia fomu yake. juzi baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Polisi Tanzania, rafiki yake, mshambuliaji mwenzake, Nchimbi aliandika kwa mafumbo katika mtandao wake wa Instagram kwamba wazawa wakipewa nafasi wana nafasi ya kufanya makubwa.

Ukweli ni kwamba nafasi wamepewa sana lakini wameiangusha klabu yao. Wameliangusha pia taifa kwa sababu leo hii Nchimbi haitwi tena katika kikosi cha Taifa Stars ambacho miezi michache iliyopita alikipeleka michuano ya Chan.

Mshambuliaji ambaye walau unaweza kusema alikosa nafasi ni Charles Imlafya wa Simba. Baadaye alitolewa kwa mkopo kwenda KMC lakini ukweli ni kwamba yalikuwa maji mazito kwa Ilamfya kutamba Simba mbele ya Bocco, Mugalu na Kagere. Alikuwa mshambuliaji chaguo la nne na maisha yalikuwa magumu.

Mshambuliaji mwingine ambaye amekuwa akifunga sana katika timu za nje ya Simba, Yanga na Azam na Yusuph Mhilu. Huyu amewahi kucheza Yanga lakini hakuwa nyota sana ingawa kipaji kilikuwepo. Mpaka sasa ameifungia Kagera Sugar mabao mengi.

Unajiuliza, anaweza kurudi timu kubwa ukamshikia dhamana? Sina uhakika sana. Kumbuka kwamba Waziri Junior alishindwa kung’ara na kikosi cha Azam halafu akaenda Mbao akang’ara halafu akarudi timu kubwa Yanga. Anachofanya tunakiona mpaka sasa.

Tuna uhakika gani kwamba Mhilu anaweza kwenda Simba au Azam au akarudi Yanga na kuendeleza makali yake ya Kagera Sugar? Inakuwa ngumu kumshikia dhamana kila unapokumbuka kilichomtokea Waziri Junior.

Nadhani hawa vijana wanakosa nguvu ya kiakili ya kuhimili presha ya kucheza timu hizi kubwa. Wanakuwa wazuri wakicheza katika timu za kawaida ambazo wao ni mastaa huku presha ikiwa sio kubwa kama ilivyo kwa timu kubwa.

Kwanini wanashindwa kuwa huru na kuonyesha uwezo wao katika nafasi hii ya ushambuliaji? Limekuwa fumbo kubwa kwetu. Wachezaji wa nafasi nyingine wameendelea kucheza ingawa wanakabiliana na wakati mgumu kutoka kwa wageni.

Kwa mfano wachezaji wanaocheza nafasi za pembeni katika eneo la ulinzi wamekuwa wakicheza mara nyingi na kumiliki nafasi hizo. Hawa ni akina Mohamed Hussein Tshabalala, Shomari Kibwana, Shomari Kapombe na Yassin Mustapha.

Lakini pia kumekuwa na walinzi tumaini katika maeneo mengine ingawa Simba imeanza kuwa ya moto kwa sababu kombinesheni kubwa imekuwa ya Josh Onyango na Sergi Wawa Paschal. Pale Yanga wanacheza zaidi wazawa kwa sasa na hawana matatizo sana. Labda kama michuano ijayo ya kimataifa itawaumbua kwa sababu hawashiriki kwa muda mrefu.

Eneo la kiungo wapo akina Jonas Mkude, Fey Toto, Salum Aboubakar, Gift Mauya, Mzamiru Yassin na wengineo. Eneo la ushambuliaji ndilo pekee ambalo linaonekana kuwatesa washambuliaji wazawa. Huwa wanang’ara zaidi katika timu za kawaida lakini wanashindwa kung’ara katika timu kubwa.

Presha katika timu hizi hazijaanza juzi wala jana. Zimeanza enzi na enzi lakini leo unajiuliza, akina Mohamed Hussein wangeshindwa kung’ara katika zama hizi? Akina Abeid Mziba na Makumbi Juma wangeshindwa kung’ara katika zama hizi?

Mohamed Hussein alitokea timu ndogo ya Bandari Mtwara lakini alipofika mjini alifanikiwa kuhimili presha pale Jangwani na kuibuka kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora nchini. Kifupi sio yeye, washambuliaji mahiri wa zamani walikuwa wanatokea timu kama hizi ambazo akina Waziri Junior walikuwa wanatokea lakini waliweza kuhimili presha.

Au wachezaji wetu wa sasa wanabadili sana mifumo yao ya maisha baada ya kutua jiji la Dar es salaam? Na sasa tuna Kibu Dennis mkononi. Nafahamu kwamba anaweza kwenda Yanga au Simba. Je ataweza kufuta gundu hili na kumkaribia Bocco katika matawi ya juu? Bado simshikii dhamana. Ni suala la kusubiri na kuona