HELMY: Wachezaji kukimbizwa ni mazoezi ya kizamani

Sunday November 28 2021
Yanga PIC
By Khatimu Naheka

YANGA kwenye benchi lao kuna raia wa kigeni watano wakitoka mataifa mbalimbali kuna mmoja hajulikani na wala hatajwi sana ila kazi yake imewaongezea ubora mkubwa wachezaji wa timu hiyo kando ya mbinu za kocha mkuu Nesreddine Nabi.

Anaitwa Helmy Gueldich. Huyu hapo kwenye picha. Sio jina linalotajwa sana Yanga ambayo msimu huu imekuwa ikiupiga mwingi huku wachezaji wakiwa fiti lakini huyu ni kocha wa mazoezi ya viungo ambaye kwa mujibu wa Nabi jamaa amefanya kazi kubwa ya kuwajengea msingi bora wachezaji wa timu hiyo.

Ni Mtunisia ambaye alicheza soka kidogo tu na kustaafishwa na majeruhi. Amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti akifunguka kila kitu juu ya kazi yake ndani ya timu hiyo inavyokwenda na mambo mengine ya kikosi hicho.

Alianzia kucheza kisha ukocha

Kama hufahamu Helmy alianza kucheza soka ingawa hakucheza muda mrefu akapata pancha kwenye kifundo cha mguu kisha kufanyiwa upasuaji na baadaye akaamua maisha yake yahamie kusomea ukocha wa viungo ajira ambayo anaitumikia sasa.

“Nilianza kucheza mpira nakumbuka nilianza kucheza soka mwaka 1995 nikianzia klabu ya Sportif Sfaxien ya kwetu Tunisia hawa wamewahi kushinda Kombe la Shirikisho Afrika,nikianzia timu za vijana na nikapanda taratibu mpaka timu ya wakubwa,anaeleza Helmy.

Advertisement

“Nilikuwa nacheza winga ya kushoto lakini kocha wangu mmoja akaona kitu tofauti akanitaka nirudi kucheza kama beki wa kushoto nilitaka kukataa akasema nijaribu atanielekeza na baadaye nikaona inawezekana na nikakubalika sana.

“Bahati mbaya wakati naanza kuchanganya katika kipaji changu niliumia vibaya eneo la kifundo cha mguu hapo ndio ilikuwa mwisho wa kucheza kwangu soka nililazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa mpaka nikakaa sawa,sikuona tena nafasi yangu ya kuendelea kucheza nikaamua kurudi shule na mpaka baadaye kusomea hii kazi ambayo naifanya sasa.

“Nilisomea kazi hii ka miaka minne katika chuo kikubwa cha mambo ya mazoezi ya viungo pale Tunisia,nilipata uzamili (Master of degree) ya mambo ya viungo na utendaji katika michezo badaye nikapata pia na pia nilipata leseni B ya CAF na mwisho nikamalizia kupata shahada ya uzamivu ya mazoezi ya viungo.

“Baada ya masomo niliajiriwa katika klabu ya Sportif Sfaxien nikiwa kocha wa viungo wa timu ya vijana chini ya miaka 19 nikashinda makombe mawili ya ligi ya vijana na FA baadaye nikapandishwa mpaka timu ya chini ya miaka 23 nako tulishinda makombe yote ya mashindano ya umri huo nikaenda timu ya daraja la pili pale Tunisia kupata uzoefu nako sikukaa sana nikachukuliwa na Esperance Sportive nikifanya kazi na kocha Nabil Maaloul.


Nabi ampigia simu

“Wakati nataka kuondoka pale baada ya kocha Maaloul kuondoka nilipokea simu ya kocha Nabi (Nesreddine) akaniambia yuko hapa Tanzania katika klabu kubwa ya hapa iliyoshinda mataji mengi na yenye mashabiki wengi wanaoipenda timu yao na anataka niungane nae kama nitakuwa tayari.

“Wakati huo nilikuwa nimewahi kusikia habari nzuri kuhusu Tanzania hasa Zanzibar walikuja kule wakati fulani kupumzika lakini pia Simba walikuwa na kocha wa viungo Adel Zrane niliwahi kusoma naye akaniambia nisiachie hiyo nafasi nitapata uzoefu mzuri nikasema acha nije niungane naye lakini bahati mbaya sasa ameondoka.


Awekwa karantini

Wakati Helmy anakubali kutua Yanga kikosi cha timu hiyo kilikuwa kimeweka kambi nchini Morocco na alipofika kule kuungana nao akakutana na kizuizi cha kukaa karantini kwa wiki mbili

“Nilitakiwa kuungana na timu nilipofika Casablanca wakasema kama natokea Tunisia natakiwa kukaa karantini kwa wiki mbili,”anasema Helmy.

“Nilitamani nigeuze wakasema siwezi kutoka ikabidi nikae karantini hotelini siruhusiwi kwenda kokote ,ikabidi nianze maisha ya kufanya kazi kwa simu kwa kumwelekeza vitu kocha Nabi na hata hivyo haikusaidia kwa kuwa sikuwa najua uhalisia wa viwango vya wachezaji


Mashabiki wamshangaza

Helmy anasema baada ya kufika Tanzania kitu kilichomshangaza ni watu wanavyopenda mpira kuanzia watoto mpaka watu wazima huku pia wakiwa watu wema wanaopenda wageni kukiwa hakuna ubaguzi.

“Nilipofika hapa nilishangazwa sana nikakuta watu wa hapa wanapenda mpira na wanaujua mpira,nilishangaa timu moja inaujaza uwanja wa mashabiki 60000 ilikuwa ni wakati mzuri kitu cha ajabu zaidi unakutana na watoto wadogo nao wanazijua timu zao lakini kikubwa ni watu walivyowaungana na wakarimu kila unapopita watu wanafurahia kukuona hakuna anayekutukana wala kukunyanyasa hapa ni sehemu nzuri kuishi.


Kutolewa Ligi ya Mabingwa

“Nilianzia kufanya kazi hapa Tanzania baada ya timu kurudi na siku za kuandaa timu hazikuwa nyingi tukiwa na ratiba ya kuanza kwa Ligi ya mabingwa Afrika bahati mbaya sana tukatolewa hatua ya awali na sababu ilikuwa moja tu tulikua hatujapata muda wa kutosha wa kuandaa timu ni vigumu kufanikiwa pia kuna wachezaji bora nao wakakosa usajili hili liliniumiza sana nilikuwa na malengo makubwa,”anasema Helmy.


Alivyoanza kazi aliwakutaje wachezaji Yanga

“Wakati naanza kazi sikukuta wachezaji katika kiwango duni sana ilikuwa ni kama wako katikati unajua kazi hii huwezi kufanya ikawa nzuri kwa wachezaji wote kwa pamoja unatakiwa kuwapima ubora mmoja mmoja na baadaye kwa makundi na unamalizi kwa timu nzima hii inakusaidia kujua ubora wa mchezaji mmoja na kipi kinamtatiza.

“Kitu kizuri hapa Yanga wachezaji wanaheshimu makocha wao, wanaheshimu na kupokea kila tunachiwaelekeza kufanya, wanajituma na wana kiu ya kutaka kufanikiwa hii inafanya kazi kuwa rahisi kidogo kuliko kukuta wachezaji hawataki kufanya mazoezi.


Hataki mazoezi ya mbio sana

“Nilipoanza hapa kitu kikubwa kigumu kilikuwa kuwakataza wachezaji kukimbia sana mbio inaonekana hiki kilikuwa vichwani kwao kwamba ili uwe fiti unatakiwa kukimbia sana lakini mazoezi ya kisasa hayataki mbio hizo bila mpira mchezaji wa soka anatakiwa kufanya mazoezi ya kukimbia akiwa na mpira.

“Mchezaji wa kisasa anatakiwa kitu cha kwanza kikubwa afanye mazoezi ya gym haya hayaepukiki ni lazima yafanyike,kitu cha pili unatakiwa kufanya mazoezi ya fiziki na sio kukimbia hawa sio watu wa riadha,kwahiyo kama mnakimbia kwa mbio fupi wanatakiwa kukimbia na mpira sio bila mpira,baadaye mtapiga mashuti au mtafanya mazoezi ya kupiga vichwa mpira,hili lilikuwa gumu sana kukubalika kwa kuwa ilikuwa mpya ila sasa kila mtu ameelewa.


Changamoto ya wachezaji wa Stars ni hii

“Kuna changamoto ya mawasiliano,kuna wakati wachezaji wanatakiwa timu za taifa na huko wanakwenda kukutana na makocha wao wengine,sina shida na wachezaji wanje huwa wakifika timu za taifa ninaongea na walimu wao shida iko hapa kwa wachezaji wa Tanzania tunatakiwa kuwasiliana ili kuwajengea ubora wachezaji hizi ni kazi ambazo tunatakiwa kufanya kwa ukaribu ila bado sijaweza kuwasiliana na wenzetu wa hapa nimekuwa nikijaribu kuwatafuta lakini hawapokei simu hii inafanya wachezaji kukosa unyoofu wa kuwajengea ubora katika mazoezi.

“Sijakata tamaa bado nitaendelea kuwatafuta wenzetu ili tuweze kuwapa ubora sahihi ambao utawasaidia huku klabuni na timu ya taifa lakini pia wachezaji nao ni binadamu kama watakuwa wanakutana na mizigo mikubwa na tofauti ya mazoezi tutakuwa tunawaumiza,”anasema Helmy.


WACHEZAJI YANGA ASILIMIA 65 TU

“Ukiniuliza mimi mpaka sasa naona vijana wako sawa kwa asilimia 65 tu, shida ni wachezaji ambao wanakuwa fiti wanaondoka kwenda timu za taifa wengi wakirudi wanakuta wenzao wako juu yao kumekuwa na hiyo tofauti,inatulazimu wote wakirejea tunafanya kazi nyingine ya kuwapa uwiano sahihi,kitu kizuri sasa nimepewa mamlaka ya matumizi ya gym muda wowote ninaotaka hii itatusaidia sana

“Lipo kundi lingine la wachezaji ambao walikuwa wameumia nao wanakuwa na mazoezi yao ya kuwapa mfano kama Yassin (Mustapha) ameanza kurejea nafikiri mlimuona kule Zanzibar bado tunampandisha ubora wake taratibu,kuna Balama Mapinduzi hii wiki amerejea na kuanza mazoezi kamili na wenzake wote akichezea pia mpira kila mtu amefarijika kumuona (Balama) akicheza jana (juzi) kwa muda sasa alikuwa akifanya mazoezi maalum katika programu aliyokuwa anapewa lakini sasa ameanza kufanya mazoezi na timu nzima

“Wengi tulisubiri kuona hili nadhani daktari Youssef (Mohamed) amefanya kazi nzuri ambayo sasa itamfanya Balama kurejea kuitumikia klabu kwa wakati mwingine changamoto ni moja unajua amekaa nje muda mrefu anaona kama anaweza kuumia tena anacheza kwa hofu lakini ni kitu ambacho kitaondoka taratibu kwa kuwa anafanya mazoezi huku tukimfuatilia kwa karibu mwingine ni Yacouba Sogne ambaye bado atakuwa nje kwa muda mrefu na Ambundo (Dickson) ambaye naye nimekabidhiwa sasa kwa ratiba ya awali lakini daktari kama ataniambia anaona yuko sawa nafikiri tunaweza kutumia siku 15 kumfanya ajiunge na wenzake katika mazoezi kamili.”

Unajua ni mchezaji gani ana kasi zaidi ndani ya Yanga lakini kuna vitu gani amehitaji ili kuwaongezea ubora fuatulia sehemu ya pili ya mahojiano haya.

LEO JUMAPILI KWENYE GAZETI LA MWANASPOTI PEKEE. USIKUBALI KUKOSA NAKALA YAKO JAMAA AMEONGEA MADINI SANA.


Advertisement